Kumekucha Blog
Tanga,WAHITIMU wa mafunzo chuo cha Ufundi Ustadi (Veta) Tanga wameitaka Serikali
kulegeza masharti ya leseni kufungua kampuni lengo likiwa ni kuweza kujiajiri ili
ujuzi wao usiwe wa mifukoni na makabatini.
Wakizungumza wakati wa mahafali ya 38 chuoni hapo jana,
wahitimu hao wamesema kwa sasa ni vigumu kupata ajira Serikalini na hivyo
kutaka ujuzi wao kuweza kuutumilia kwa kufungua makampuni yao na kuweza
kuisaidia Serikali katika kutoa ajira.
Wamesema kufanya hivyo kutawawezesha kutoa ajira kwa wengine
wasio na kazi jambo ambalo litasaidia kupunguza vijana wasio na kazi mitaani
pamoja na watumiaji wa madawa ya kulevya na waporaji wa kutumia nguvu.
“Tuko na furaha ya kuhitimu kozi zetu ila changamoto kubwa
iko katika kupata ajira iwe serikalini ama taasisi binafsi----hii ni kutokana
na kuwa na wasomi wengi wasio na kazi” alisema Devid Elias
“Jambo zuri ambalo Serikali inatakiwa kufanya hasa sisi ambao
tumetokea katika vyuo ni kutulegezea masharti ya upatikanaji wa leseni za
kampuni----itakuwa msaada kwetu na vijana wasio na kazi”alisema Elias
Kwa upande wake mhitimu wa kunyoosha bodi za magari, Rose
John, amewataka wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari kuacha
kukata tamaa na badala yake wajiunge na vyuo vya ufundi.
Alisema kuna wanafunzi wengi ambao humaliza elimu ya
sekondari wamekuwa wakikata tamaa ya masomo na kusahau kuwa viko vyuo vya
ufundi ambavyo vinaweza kuwatoa kimaisha kama vilivyo vyuo vyengine.
“Tatizo hasa liko kwa wazazi mtoto anapoamaliza naona ndio
mwisho wa masomo na kumuingiza katika biashara au kumuacha akipotea---wanasahu
kuwa viko vyuo vya ufundi” alisema Rose
Aliwataka wazazi kukumbuka kuwa vyuo vya ufundi vinaweza
kuwabadilisha watoto wao katika maisha yao mbeleni pamoja na ya kwao na hivyo
kutambua kuwa elimu na ujuzi sio wa shuleni peke yake.
Aliwakumbusha kuwa kumuacha mtoto wakati yuko na elimu ya
kiwango cha chini ni jambo la hatari linaloweza kuwatumbukiza katika magenge ya
kihuni pamoja na biashara haramu za uuzaji unga na uvutaji bangi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment