Sunday, June 7, 2015

MWENGE WAINGIA NA KUKIMBIZWA WILAYANI MUHEZA, TANGA


Tangakumekuchablog

Muheza, KIONGOZI wa mbio za Mwenge kitaifa, Juma Khatib Chumu, amewataka wananchi kuacha kuchagua viongozi wala rushwa na badala yake waangalie watu wenye uchungu wa maendeleo kwa wananchi wake.

Akizungumza na wananchi kijiji cha Mkuzi Wilayani hapa jana wakati wa mbio za mwenge, Chumu aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wenye tamaa ya kuongoza nchi wakati hawana uwezo wa kuongoza.

Alisema kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu amedai  kujitokeza makundi ya watu na kujinadi kwa wananchi wakati uwezo huo hawako nao na hivyo kuwataka kuwa makini na watu hao.

“Ndugu zangu wa kijiji cha Mkuzi na Muheza kwa ujumla nawatabanaisha na viongozi watakaoibuka kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kujinadi kuomba kura ya urais wakati hawana uwezo huo” alisema Chumu na kuongeza

“Tujihadhari na viongozi wala rushwa na ambao hawana uchungu na nchi yao ndugu zanguni------kila mmoja anatambua kiongozi bora kwa wananchi mwenye uwezo” alisema

Akizungumzia kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya, kiongozi huyo aliwataka vijana kufanya kazi ya kujipatia kipato kwa njia za halali na kuacha kutumiliwa na matajiri kwenda nje kubeba unga.

Alisema kuna baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha wamekuwa wakirubuni vijana kwenda ng’ambo kubeba unga jambo ambalo amesema ni hatari na mwisho wake ni mbaya katika maisha.

Alisema ili kuweza kutokomeza matumizi ya madawa ya kulevya ni wajibu wa kila kijana kujibidiisha kwa kufanya kazi na kudai kuwa kazi ziko nyingi za kufanya zikiwemo za kujiajiri.

Alisema Wilaya ya Muheza iko na fursa nyingi za kimaendeleo kikiwemo kilimo cha machungwa, ndizi  na miwa ambacho Serikali iko na dhamira ya dhati ya kujenga kiwanda cha kusindika matunda.

Alisema kwa ujio huo ni fahari kwa wana Muheza kila mmoja kutambua wajibu wake kwa kuwekeza katika kilimo na kuacha kusubiri hadi wageni kuhodhi maeneo yao na kushika hatamu ya kilimo.

                                                      Mwisho
 Wakimbiza mwenge wa Uhuru wakiutembeza mwenge mchakamcha kijiji cha Mkuzi Wilayani  Muheza mapema leo asubuhi




  Mkuu wa Wilaya ya Muheza Tanga, Estarina  Kirasi (kulia) akikabidhiwa mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Regina Chonjo mapema leo asubuhi katika kijiji cha Mkuzi Wilayani Muheza Tanga.


No comments:

Post a Comment