Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
amechukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuahidi
kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo watuhumiwa wa ufisadi
waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo
kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),
kupeperusha bendera ya umoja huo atahakikisha anaunda Katiba yenye
maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuwaunganisha
Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani
aliwaambia wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa
jana kuwa ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya
viongozi wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi,
uwajibikaji wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na
ufisadi uliokithiri nchini.
Profesa Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo
na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana,
alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kujenga misingi ya kuhakikisha watoto
wanapata fursa sawa ya maendeleo, ajira, afya, kulinda rasilimali za
umma na kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba aliyeanza hotuba yake ya
takriban dakika 45 kwa kutoa wasifu wa usomi na kazi mbalimbali za
kiuchumi alizozifanya kwa takriban miaka 40, alisema anafahamu bayana
matatizo mengi ya Watanzania kwa kuwa amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema matatizo hayo yamesababishwa na
“siasa mbovu za chama cha mapinduzi” ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo
atapatiwa ridhaa ya kuwania kiti hicho cha juu, atakuwa na kazi kubwa ya
kuleta uongozi makini utakaohakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa
maendeleo ya watu wote.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais,
hatakuwa na msalie mtume na mafisadi na wote wanaohusika watawajibika
kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Inatisha sana kuona mafisadi wakubwa,
wala rushwa wakubwa badala ya kuwa ndani ya jela, wanachukua fomu za
urais. Tunahitaji kwa kufuata taratibu na haki, mafisadi hao watumikie
vifungo na mali zilirudishwe kwa umma walikofisadi,” alisema Profesa
Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Iwapo atapatiwa nafasi ya urais, alisema
katika utawala wake atahakikisha watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya
maendeleo kwa kutoa huduma bora afya, lishe na elimu.
Alisema suala la ukuaji imara kwa watoto
halijapatiwa kipaumbele na kusababisha udumavu unaowanyima uwezo mkubwa
wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Mwanasiasa huyo alisema anachukua fomu
nchi ikiwa njia panda baada ya Katiba Inayopendekezwa kuacha masuala ya
msingi ya uadilifu na uwajibikaji na kusababisha wachache kujinufaisha
kwa rushwa.
MWANANCHI
Chama cha ACT – Wazalendo kinatarajia kumtagaza mgombea wake wa urais wa Agosti 10, imefahamika.
Chama hicho kimesema mtia nia
atakayepeperusha bendera ya ACT – Wazalendo atawajibika kutangaza mali
binafsi na vyanzo vyake kwa kufuata utaratibu ulioanishwa katika katiba
ya chama hicho.
Hayo yalisemwa jana mjini Geita na Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe wakati akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Stand mjini hapa.
Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya
chama hicho iliyokutana juzi mjini Tabora, imepitisha ratiba kamili ya
kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi mbalimbali za chama hicho kuanzia
Julai Mosi.
“Kuanzia
Julai Mosi mpaka Julai 17 ni kuchukua fomu kwa ngazi ya udiwani kwa ada
ya Sh10,000, Julai 1-26 kuchukua fomu kwa ngazi ya ubunge na uwakilishi
na ada yake ni Sh20,000 na kwa ngazi ya urais shughuli hiyo itakuwa
kati ya Julai 1-26 na ada yake ni Sh100,000,” Zitto
“Vikao
vya ngazi mbalimbali ya uteuzi vitaanza kuanzia Julai 27 hadi Agosti 10
mkutano mkuu wa chama utakapopitisha jina la mgombea urais.”
Zitto alisema lazima mgombea huyo awe
amethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT –
Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi, awe ni mtu
anayejitegemea kutokana na chanzo halali cha kipato kutokana na shughuli
halali.
Alisema pia atakayetaka kukiwakilisha
chama hicho kwa nafasi ya urais, itampasa kuwa mwenye haiba na taswira
ya kuiwakilisha na kuipa heshima stahiki Tanzania katika Jumuiya za
Kimataifa.
Chama hicho kinaendelea na ziara yake ya
kulinadi azimio la Tabora lililozinduliwa juzi Mjini Tabora likilenga
kuhuisha Azimio la Arusha. Leo watakuwa katika Mkoa wa Kagera.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
jana alikamilisha mchakato wa kusaka wadhamini wa maombi yake ya
kuwania urais kupitia CCM na leo anatarajia kuwa wa kwanza kurejesha
fomu hizo makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.
Sitta ambaye ni miongoni mwa wanaCCM 32
waliokwishachukua fomu kuwania nafasi hiyo, atarejesha fomu hizo baada
ya kupata saini za wanaCCM katika mikoa 21 nchini. Kila mgombea
anatakiwa kupata wadhamini 450 katika mikoa 15, kati ya hiyo mitatu ya
Zanzibar.
Akizungumza na wakazi wa Itundu na mjini
Urambo alikomalizia mzunguko huo, Sitta alisema kazi ya urais si
lelemama ila ataimudu kwani anaifahamu vizuri nchi.
Alisema endapo atateuliwa na chama chake
kugombea urais na kushinda ataimarisha Muungano na kupambana na ufisadi
na uonevu kwa wananchi ili kila mtu afurahie maisha yake.
Aliahidi kuiimarisha CCM kiuchumi ili isiyumbishwe na matajiri.
NIPASHE
Wakati makada wa Chama Cha Mapindizi
(CCM) wakiendelea kumiminika kuchukua fomu ya kuomba chama chao kiwateue
kuwania urais, imebainika kuwa mawaziri 12 wa serikali ya sasa ya Rais Jakaya Kikwete wamejitosa kuwania nafasi hiyo na kuipiku rekodi ya mawaziri wa serikali ya Rais Benjamin Mkapa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Idadi hiyo (ya mawaziri 12) imefikiwa baada ya kujitokeza pia kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro, ambaye ratiba inaonyesha kuwa atachukua fomu leo makao makuu ya CCM mjini Dodoma.
Ofisa Habari CCM makao makuu, Gabriel Athuman,
jana alisema Dk. Migiro atachukua fomu saa 4:00 asubuhi, sawa na kada
mwingine aitwaye Salum Maluku na hivyo kufanya idadi ya makada wote
waliojitokeza kuwania urais kufikia 33.
Idadi iliyofikiwa sasa ya mawaziri
wanaowania kuteuliwa na CCM ili wachuane na wapinzani katika Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kwa nia ya kumrithi Rais Kikwete
inaipiku idadi ya mawaziri waliojitokeza kumrithi Mkapa katika uchaguzi
mkuu uliofanyika mwaka 2005, ambao mawaziri waliochuana zaidi na kufika
mbali katika harakati za kuwania nafasi hiyo walikuwa wanne tu.
Mawaziri waliochukua fomu ya urais mwaka
2005 na kuchuana vikali ndani ya mchujo wa CCM walikuwa ni Rais Kikwete
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri
Mkuu (mstaafu), Frederick Sumaye.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, Dk. Abdallah Kigoda (sasa
Waziri wa Viwanda na Biashara) na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,
Prof. Mark Mwandosya (sasa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalum).
Mbali na Migiro, mawaziri wengine
waliochukua fomu kutaka kumrithi Rais Kikwete hadi kufikia leo ni Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Stephen Wassira na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus
Kamani.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Kazi Maalum, Prof. Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias
Chikawe; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe.
Mawaziri wengine ni Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa
Kamati Kuu ya Chama hicho itakayokutana Julai 12 itakuwa na kibarua cha
ziada katika kuwachuja wagombea na kubaki na majina ya kuyapeleka mbele
ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutokana na ukweli kuwa
baadhi ya waliojitokeza ni wajumbe pia wa CC, baadhi wakitokana na
nyadhifa zao.
Hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk.
Mohamed Gharib Bilal ambaye pia ameshachukua fomu kuwania urais, Waziri
Mkuu Pinda, Wasira na Migiro.
NIPASHE
Wakati utoaji huduma za afya ukizidi
kuzorota katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ukosefu wa damu
umekuwa tatizo sugu linalosababisha mateso na vifo kwa wagonjwa.
Hospitali hiyo inahitaji wastani wa
chupa za damu 70 hadi 100 kwa siku kwa ajili ya kuwawekea wagonjwa
mbalimbali, lakini imekuwa na uwezo wa kupata chupa 20 hadi 30 pekee kwa
siku.
Baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo
waliliambia NIPASHE kuwa ukosefu wa damu MNH ni wa muda mrefu, hivyo
`kujenga’ mazingira ya kuamini kuwa uongozi wake umeshindwa kulipatia
ufumbuzi wa kudumu.
Daktari bingwa wa watoto hospitalini
hapo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ni kawaida kwa
wagonjwa wanaohitaji damu kukaa wodini hadi siku tatu na wengine kufa
kutokana na kukosa damu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya
wagonjwa wanawekewa damu kidogo ya mahitaji kama sharti la
kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki kuchangia, na inapotokea
wasijitokeze kufanya hivyo, madaktari wanasitisha kumuongezea (mgonjwa)
damu iliyobaki.
Lengo la hatua hiyo linaelezwa kuwa ni
hamasa kwa walio karibu na mgonjwa kuchangia ili irejeshwe kwenye benki
ya damu kwa vile wakati mwingine, damu inayotolewa inaweza isiwe kundi
la ile inayohitajika kwa mgonjwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa
inapotokea dharura kwa mgonjwa kuhitaji damu, MNH inamkopesha (mgonjwa)
kiasi kidogo cha damu kuokoa maisha kwa wakati husika, huku ndugu
wakitakiwa kuchangia ili kufidia kiasi halisi kinachohitajika.
“Kama mtu amezidiwa wakaona anaweza
kufa, wanamkopesha damu kidogo kama unit moja ambayo ni nusu lita na
haitoshi, lakini lengo ni kuwalazimisha ndugu wa mgonjwa kuchangia kiasi
cha damu inayohitajika,” kilieleza chanzo kingine katika wodi ya
wanawake.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa
zinaeleza kuwa baadhi ya vifo vikiwamo vinavyotokea kwenye wodi
vinahusishwa na ukosefu wa damu.
Taarifa za kitabibu kutoka kwa
madaktari wakiwamo wa MNH zinaeleza kuwa mgonjwa anayehitaji kuongezewa
damu akikaa muda mrefu bila kupata huduma hiyo, moyo unashindwa kufanya
kazi na hivyo kusababisha kifo.
Vyanzo tofauti vimebaini kuwa uongozi
wa MNH unalaumiwa kwa hali hiyo kutokana na kushindwa kukusanya damu kwa
wingi kwani hakuna jitihada zozote zinazofanyika kama vile kuhamasisha
wananchi kujitolea damu kwenye kitengo cha damu.
Watu wanaoathirika kutokana na ukosefu
wa damu ni wanaofanyiwa upasuaji, wenye matatizo yanayohusiana na
tumbo, wanaoharisha na kutapika damu, wenye saratani ya damu, upungufu
wa damu na magonjwa ya kuambukiza.
Daktari anayezungumza na NIPASHE kwa
sharti la kutotajwa jina gazetini, alisema upungufu wa damu
unasababishwa na uzembe wa kitengo cha damu kushindwa kufanya kazi yake
ipasavyo kama kuhakikisha kunakuwa na akiba ya damu ya kutosha, hivyo
kuweka rehani maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.
Wakati MNH ikidaiwa kushindwa
kufanikisha upatikanaji damu, mwamko wa umma bado ni mdogo katika kutoa
damu inayohitajika kwa maisha ya wagonjwa.
HABARILEO
Shule ya Msingi Saadani Chumvi iliyopo
Kata ya Mkange wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, imefungwa baada ya wazazi
kuwa na hofu baada ya watu wawili na mbuzi 70 kuliwa na Simba kutoka
kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Shule hiyo ambayo iko jirani na hifadhi
hiyo ilifungwa mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matukio hayo hali
ambayo ilisababisha wazazi kuogopa watoto wao kudhuriwa na wanyama hao
hivyo kuwahamishia watoto wao kwenye shule ya Msingi ya Saadani.
Akizungumza jana, Mtendaji wa Kijiji cha
Saadani, Hussein Msilu alisema mara baada ya matukio hayo wazazi wa
watoto hao waliingia hofu na kuwaondoa watoto wao wapatao 67 na
kuwahamishia kwenye shule hiyo ya Saadani ambayo iko umbali wa kilomita
kati ya sita na saba.
Msilu alisema kutokana na hali hiyo
uongozi wa kata na kamati ya shule kwa pamoja walikubaliana wanafunzi
hao kuhamishiwa kwenye Shule ya Msingi Saadani kutokana na hofu
iliyotanda kuwa wanafunzi wanaweza kuliwa na simba hao.
Alisema wanaushukuru uongozi wa kiwanda
cha chumvi kwa kutoa usafiri kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi kwenda
na kurudi kutoka kwenye Kitongoji hicho cha Saadani Chumvi hadi shuleni
Saadani, kwani umbali ulikuwa mrefu sana pia ni hatari kwani wanapita
ndani ya hifadhi hiyo ambayo ina wanyama mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani
Kikwete alisema alipata taarifa hiyo na kuwasiliana na mamlaka husika na
kwamba tayari zilichukuliwa za kuwaondoa simba hao, lakini kilichobaki
kwa sasa ni hofu ya wananchi.
Aidha, aliwatoa hofu wazazi na kuwaambia
wawarejeshe watoto hao shuleni hapo ili waendelee kusoma hapo kwani ni
karibu na makazi yao tofauti na Saadani ambako ni mbali pia ni usumbufu
mkubwa kwao, kwani hali hiyo imedhibitiwa.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete,
amesema mara baada ya kung’atuka madarakani baadaye mwaka huu,
ataanzisha taasisi yake itakayojikita zaidi katika kushughulikia masuala
yanayowagusa watoto, wanawake na maendeleo ya kilimo.
Aidha, amesema angependa kutumia muda
wake mwingi kufanya kazi ya kuwasaidia Watanzania kuinuka kiuchumi,
badala ya majukumu mengine ya kimataifa, yakiwemo ya usuluhisho wa
migogoro.
Akiwa katika Hoteli ya Crownie Plaza,
alisema anakusudia kuanzisha taasisi itakayosaidia makundi mbalimbali,
hasa watoto na wanawake na pia kundi la wakulima ambao kutokana na wingi
wa karibu asilimia 80 ya Watanzania wote, wakiinuliwa watakuwa na
nafasi kubwa ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na
taifa kwa ujumla.
Rais Kikwete aliyekuwa katika siku ya
pili ya ziara yake Uholanzi, baada ya kuwa amefanya hivyo Finland na
Sweden, alilazimika kuyasema hayo muda mfupi baada ya umoja wa
Watanzania hao kumzawadia begi la kubeba makabrasha, huku wakisema
wanaamini baada ya muda wake wa uongozi kwisha, atakabidhiwa majukumu
mengi ya kimataifa kutokana na heshima kubwa aliyojijengea duniani.
Walitolea mfano kukabidhiwa jukumu la
kusuluhisha migogoro ya kisiasa, ikiwemo ya Kenya, kuwa ni uthibitisho
wa kuaminiwa kwake na jumuiya ya kimataifa.
Alikabidhiwa pia ngao maalumu ya
ushupavu katika uongozi, na kitenge kwa ajili ya mke wa Rais, Mama
Salma, lakini akizungumzia zawadi hizo, alishukuru na kusema hilo la
jukumu la kusuluhisha migogoro ya kimataifa si kipaumbele chake, kwani
anafikiria zaidi kuwatumikia Watanzania kwa mrengo mwingine.
Aidha, alisema mara kadhaa amekuwa
akipenda kuwatumikia Watanzania, ndiyo maana kabla ya kuwa Rais wa Awamu
ya Nne wa Tanzania, aliwahi kupewa heshima ya kufanya kazi ya kimataifa
huko Algiers, Algeria lakini alikataa.
MTANZANIA
Mahakama Kuu yaAfrika Kusini imetoa amri ya muda ya kumzuia Rais wa Sudan, Omar al Bashir anayehudhuria kikao kilichoanza jana cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) kutoondoka nchini humo.
Mahakama hiyo imemuagiza al-Bashir
abakie hadi leo wakati itakaposikiliza kesi inayoitaka iiamrishe
Serikali ya Afrika Kusini kumkamata kiongozi huyo akajibu mashitaka
yanayomkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya
mjini Hague, Uholanzi.
Mapema jana, Rais Bashir alikaribishwa na maofisa wa Afrika Kusini wakati akiwasili mjini Johannesburg.
Licha ya a mahakama kutangaza uamuzi
huo, kiongozi huyo wa Sudan alipiga picha ya pamoja na viongozi wengine
wa Afrika akiwa amevalia suti ya bluu, tai na akitabasamu wakati picha
ikichukuliwa.
Rais al Bashir anasakwa na mahakama hiyo kwa uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
AU inakutana chini ya uenyekiti wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano unaoonekana kughubikwa na mzozo wa Burundi na migogoro ya uhamiaji, ugaidi na mihula mitatu ya urais.
AU inakutana chini ya uenyekiti wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano unaoonekana kughubikwa na mzozo wa Burundi na migogoro ya uhamiaji, ugaidi na mihula mitatu ya urais.
AU imekuwa ikikiuka maombi kadhaa ya kuitaka imkamate al- Bashir tangu amri hiyo mkamata ilipotolewa mwaka 2009.
Hali hiyo imezusha mvutano baina ya ICC
na AU huku baadhi barani Afrika wakiituhumu mahakama hiyo kuwa chombo
cha kuwalenga Waafrika tu.
Hata kabla ya matukio ya jana, AU
imekuwa ikiitaka ICC iache kuwaandama marais walio madarakani na kwamba
haitalazimisha wanachama wake kumkamata kiongozi yeyote kwa niaba ya
mahakama hiyo.
Chama tawala cha African National
Congress (ANC), kilisema Serikali ya Afrika Kusini ilitoa msamaha ‘kwa
washiriki wote wa mkutano wa wa AU kama sehemu ya taratibu za kimataifa
kwa nchi wenyeji wakati wa mikusanyiko ya AU au hata Umoja wa Mataifa
(UN).
“Ni
katika msingi huu, pamoja na mambo mengine ANC inatoa mwito kwa Serikali
ya Afrika Kusini kupinga agizo hilo lililoletwa kuilazimisha kumkamata
Rais al-Bashir,” taarifa ya ANC ilisema na kuongeza kuwa
mataifa ya Afrika na Ulaya Mashariki yanaendelea kukandamizwa kwa
kulengwa isivyo halali na uamuzi wa ICC.
Lakini kwenye taarifa yake , ICC ilisema
kuwa waranti mbili za kumkamata Bashir bado zipo. Mwendesha Mashitaka
wa ICC, Fatou Bensouda amesema Afrika Kusini ina wajibu wa kumkamata
al-Bashir na kumkabidhi kwa mahakama hiyo.
Ofisi yake imekuwa ikiwasiliana na
mamlaka za Afrika Kusini tangu iliporipotiwa kuwa rais huyo wa Sudan
atazuru nchi hiyo kuhudhuria mkutano wa AU.
Kwa habari matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment