Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 7727246
MWANANCHI
Mtu mmoja amekamatwa na polisi akiwa katika harakati za kutafuta soko
la kuuza mtoto mdogo wa dada yake ambaye ana ulemavu wa ngozi mwenye
umri wa miaka sita.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa juzi kuwa ni Masanja Mwinamila , mkazi wa Ugembe wilayani Nzega.
Kamanda Bwire alisema polisi walipata taarifa za mtuhumiwa huyo
kutafuta wateja ndipo askari walipoweka mtego kwa kujifanya wanunuzi na
kukubaliana naye kufanya biashara kwa kiwango cha fedha alichohitaji na
kudai kwamba mtuhumiwa alitekeleza makubaliano hayo na kwenda kumchukua
mtoto huyo akiwa na mama yake na ndipo askari walipomtia mbaroni.
Kamanda Bwire alieleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Bwire alieleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Bwire alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni mkakati maalumu
unaoendelea kufanywa na polisi kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Joyce Mwandu alieleza kuwa
kaka yake alifika nyumbani kwake na kudai kuwa amekwenda kumtembelea na
baada ya muda alitokomea na mtoto hadi alipopata taarifa za kukamatwa
kwake.
MWANANCHI
Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala ya Afrika, Linda Thomas-Greenfield amemuuliza Rais Jakaya Kikwete iwapo ana mtu wake katika orodha ndefu ya makada waliojitokeza kuomba kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Waziri huyo aliuliza swali hilo usiku wa
kuamkia Jumatatu mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati anazungumza
na Rais Kikwete kutokana na wanachama wa CCM 35 kujitokeza kuchukua fomu
za kuwania urais.
Viongozi hao walikuwa wanahudhuria
Mkutano wa 25 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika, kwa siku mbili,
kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Convention jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kumalizika jana.
Makada hao wa CCM wameibua upinzani
mkali kwenye mbio za urais na hadi sasa hakuna dalili za mtu yeyote kuwa
ana nafasi kubwa ya kupitishwa, hali ambayo imesababisha vyombo vya
habari kubashiri kuwa mteule wa CCM anajulikana kwa viongozi wa juu wa
chama hicho tawala.
Wakati nchi ikijiandaa kupata kiongozi
mpya atakayeongoza Serikali ya Awamu ya Tano, mbio za urais ndani ya CCM
zimevutia idadi kubwa ya wanachama ambayo haijawahi kutokea kabla na
baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 baada ya
watu 35 kuchukua fomu hadi sasa.
Mwaka 1995, wanaCCM waliojitokeza kutaka
kumrithi Rais Ali Hassan Mwinyi walikuwa 15 na mwaka 2005 waliojitokeza
kutaka kumrithi Rais Benjamin Mkapa walikuwa 11.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, Ikulu ilisema jana kuwa mwanzoni tu mwa mazungumzo baina ya
viongozi hao, Linda alimuuliza Rais Kikwete, “Je, unaye mgombea yeyote ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea”.
Baada ya swali hilo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete alijibu, “Sina
mgombea ninayempendelea. Wagombea wote ni wa kwangu, ni wa chama
changu, isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki
katika chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali”.
Kuhusu utiriri wa wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.
“Hiki
ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani awe
mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu ya
wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka ya
karibuni.
“Vile
vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu katika miaka 10
iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa kujitokeza kugombea
nafasi hiyo.”
Rais Kikwete alisema hana tatizo na
wingi wa wagombea kwa sababu haiwezekani kuwazuia watu kugombea nafasi
hiyo kwa sababu ni haki yao.
MWANANCHI
Umoja wa watendaji wakuu wa kampuni wa CEO RoundTable (CEOrt) umeandaa mdahalo wa kuzungumzia mbio za urais utakaowahusisha viongozi wa vyama vya upinzani, Prof. Ibrahim Lipumba, Dk Willibrod Slaa, Zitto Kabwe na Emmanuel Makaidi, lakini Chadema imesema itakuwa tayari kwa midahalo baada ya mchakato wa ndani kukamilika.
Kauli hiyo ya Chadema inaweza kuwa
kikwazo kingine kwa CEOrt kuendesha midahalo hiyo baada ya wa kwanza
uliokuwa uhusishe makada 10 wa CCM wanaoomba ridhaa ya chama hicho
kuwania urais, kushindwa kufanyika kutokana na viongozi wa sekretarieti
kutoa kauli tofauti siku moja kabla.
Kiongozi wa CEO, Ali Mufuruki
alisema jana kuwa Dk Slaa, Profesa Lipumba, Makaidi na Zitto, ambaye ni
kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, wamethibitisha kushiriki kwenye mdahalo
huo utakaofanyika kesho kuanzia saa 1:00 jioni jijini Dar es Salaam.
Lakini Dk Slaa aliiambia Mwananchi jana
kuwa Chadema itakuwa tayari kushiriki kwenye midahalo baada ya kumaliza
mchakato wa kupata mgombea wake na kukamilisha Ilani ya Uchaguzi, mambo
ambayo alisema hupitishwa na vikao vya juu.
“Kamanda,
sijui kama ni kongamano au mdahalo: 1. Chadema inaendeshwa kwa katiba,
kanuni na taratibu zake. Hadi siku ya leo taratibu zetu hazijafikia
kupata aspirants (watangazania),” alisema katibu huyo mkuu wa Chadema katika ujumbe wake mfupi wa simu.
“2.
Kama kuna waliopata aspirants, Chadema bado mchakato wetu unaendelea.
3. Midahalo inafanywa kwa msingi wa ilani. Chadema ilani yetu haijafika
bado mbele ya vikao vya maamuzi, yaani Baraza Kuu na Mkutano Mkuu. Hivyo
tukienda mdahalo tutakuwa tunazungumzia ilani ipi?
“Hivyo tuko tayari kwa midahalo yote baada ya mchakato wetu wa ndani kukamilika.”
Mufuruku alikuwa ametuma taarifa hiyo
kwenye ukurasa wake wa facebook na alipopigiwa simu na Mwananchi,
alithibitisha kuwapo kwa mdahalo huo ambao alisema utaonyeshwa moja kwa
moja na vituo vya televisheni, redio na intaneti.
Kuhusu ushiriki wa Zitto, ambaye
atagombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mufuruki alisema CEOrt
imemualika kwa kuwa ni kiongozi wa chama ambacho kinaweza kusimamisha
mgombea wa urais.
“Kushiriki
si lazima uwe unachukua fomu za kugombea urais. Yeye ni kiongozi wa
chama ana mawazo yanayoweza kutoa mchango kwenye mdahalo,” Mufuruki.
CEOrt imepanga kufanya midahalo kadhaa
mwezi huu na Juni 25 itaendesha mdahalo utakaoshirikisha wagombea kutoka
CCM baada ya kada mmoja tu, Balozi Amina Salum Ali, kujitokeza kwenye
mdahalo wa kwanza na hivyo kusababisha uahirishwe.
Profesa Lipumba, ambaye amechukua fomu
za kuomba ridhaa ya CUF kupitishwa kugombea urais kwa mara ya tano iwapo
jina lake litapitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
aliiambia Mwananchi jana kuwa atashiriki kwenye mdahalo huo, kama ilivyo
kwa Makaidi ambaye amepitishwa na NLD kuwania nafasi hiyo.
NIPASHE
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
imetoa tahadhari kwa wagombea watakaokiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi
ya mwaka 2010 watakuwa wanajiweka katika hatari ya kutoteuliwa na vyama
vyao.
Hadi sasa vyama ambavyo makada wake
wameanza kuchukua fomu za kuomba kuwania urais ni Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
alitoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi na sheria ya
vyama vya siasa ambazo zinapaswa kuzingatiwa na vyama na wanasiasa
katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
“Natoa
tahadhari au angalizo kwa vyama vya siasa na wanasiasa wasipuuzie utii
wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa sababu kutawaathiri nje na ndani ya
vyama ,” alisema.
Mutungi alisema katika kipindi cha
kuelekea uchaguzi mkuu mgombea yeyote au chama cha siasa asipozingatia
sheria hiyo atakuwa anahatarisha nafasi yake ya kugombea na kutoteuliwa
na chama chake kutokana na kukiuka masharti yaliyopo ndani ya sheria
hiyo.
Alisema chama cha siasa kitakachopuuzia
sheria ya uchaguzi na kikapitisha mgombea ambaye amekiuka masharti
yaliyomo ndani ya sheria hiyo kitakuwa kinapitisha mgombea ambaye
atawekewa pingamizi na atakuwa amejiharibia nafasi hiyo.
“Sitaki
kuamini kuwa sekretarieti ya chama kilichosajiliwa kisizingatie utii
wa sheria ya uchaguzi, kila mtu ni jukumu lake kuzingatia utii wa sehria
bila shututi,” alisema.
Jaji Mutungi alisema kipindi hiki siyo
muda mwafaka wa kufanya tathmini kama vyama vya siasa na wagombea
wamezingatia sheria hiyo kwani hivi sasa ofisi ya msajili na vyombo
vingine vinaendelea kufuatilia suala hilo na muda ukifika matokeo
yatatolewa kwa kuweka wazi vyama na wagombea waliokiuka sheria.
Aliongeza kuwa sheria ya gharama za
uchaguzi madhumuni yake yaliwekwa kwa misingi ya kutaka kudhibiti
matumizi ya gharama katika mchakato wa uchaguzi na kuthibiti vitendo
vinavyokataza na sheria ya nchi.
NIPASHE
Wabunge wamegawanyika katika nyongeza ya
tozo la bei ya mafuta ya taa, petroli na dizeli, huku wengi wakidai
kuwa itapandisha bei ya bidhaa mbalimbali na maisha kuwa magumu na
wengine wakidai itawezesha maeneo ya vijiji kupata umeme na hivyo
kuharakisha maendeleo.
Juni 11, mwaka huu, Waziri wa Fedha
akiwasilisha Bajeti ya mwaka 2015/16, alipendekeza ongezeko la tozo ya
Sh. 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli na kufanya tozo kuwa Sh. 100,
huku mafuta ya taa kutoka Sh. 100 hadi 150.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia,
alisema Tanzania ina ukanda wa bahari wenye urefu wa kilomita za mraba
230,000, serikali ingejikita vizuri katika sekta ya uvuvi mapato makubwa
kwani mwaka juzi ilikuwa ipatikane Sh. trilioni moja.
“Badala
ya kukimbizana na Machinga Kariakoo, tungepanga na kutumia mapato ya
uvuvi, ripoti ya Chenge one iliainisha vyanzo vipya vya mapato vya
kuiwezesha serikali kuacha kutegemea vyanzo vile vile kila mwaka,” alisema.
Alisema sekta ya utalii, Tanzania ni ya
kwanza barani Afrika kwa mazingira ya utalii na ya pili duniani kwa
vivutio vya utalii ni ya 110 kati ya nchi 133 kwenye ushindani wa utalii
au mapato ya utalii.
Mbunge Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa,
alisema serikali haijajikita kukusanya mapato katika kampuni za simu,
jambo ambalo linazua maswali kuwa huenda kuna wachache wanaopata mgawo
na wanamisha dhamira ya serikali kukusanya mapato.
Alisema Tanzania kuna watumiaji wa simu
milioni 32, na serikali ingeweza kutoza Sh. 100 kwa kila vocha ya Sh.
1,000, na kujipati mapato mengi, kwani Kenya imeweza kuzisimamia kampuni
za simu na kukusanya mapato mengi.
Alisema sekta ya uvuvi kuna mapato
makubwa, lakini serikali imeamua kuiachia Kenya kuvua kwa kutumia meli
kubwa katika ukanda wa bahari, na meli pekee iliyokamatwa ni ya Wachina
ambayo haikusaidia kupata mapato.
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo ,
alisema amefurahishwa na bajeti hiyo kwa kuwa imeazimia kujitegemea,
kuweka umeme vijijini kuondokana na matumizi ya vibatari.
“Nimefuraishwa
na mengi kwenye bajeti ila kubwa ni azma ya kupelekea umeme vijijini,
juzi nimetoa hela za mfuko wa jimbo za kuweka umeme wa sola katika
sekondari 21, mambo ya kupata ‘ziro’ hakuna katika wilaya ya Itilima,
miaka 40 iliyopita mtu anaimba wimbo ‘nikununulie taa ya kukanda nikuone
mpenzi wangu ndani ya chumba’ (Kisukuma ni umeme), serikali inayotaka
mambo ya koroboi au kibatari, inarudi nyuma.”
Alisema kwa sasa inatakiwa kuachana na
matumizi ya kibatari au koroboi, na kwamba nyongeza hilo litaumiza,
lakini lina lengo jema la maendeleo.
Cheyo alisema lazima fedha zinazowekewa
wigo kwa ajili ya mfuko wa barabara, maji na umeme ziende kufanya kazi
husika na ijulikane kwa viongozi wote watakaokuja kwenye Wizara siku
zijazo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata,
alisema ni bajeti ya kujenga heshima na ambayo Watanzania wameamua
wenyewe ili kujifanyia mambo wenyewe kwa kutumia fedha za tozo ya
mafuta.
“Mimi na kamati yangu
tulishasema ongezeko hilo liende kwa ajili ya umeme vijijini, makato
yatakayopatikana yatasaidia kuendeleza na kuongeza maeneo mengi ya
vijijini kupata umeme ambao siyo wa kuwasha tu bali maendeleo vijijini,” alisema.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan,
alisema ipo haja kwa serikali kupunguza matumizi yasiyo ya msingi, kama
posho za safari ambazo zimeongezeka kutoka Sh. bilioni 65 hadi 75,
ikiwa ni matumizi yasiyo na tija, hivyo fedha zielekezwe kwenye miradi
ya maendeleo.
“Huwezi
kuacha vijana wasiende Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT) kwa sababu
zimeopungua Sh. bilioni 18, wakati kwenye posho safari za viongozi kuna
nyongeza ya Sh. bilioni 65 hadi 75,” alisema.
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany,
alisema kupanda kwa nishati hiyo ni kuruhusu uharibifu wa mazingira kwa
kuwa sasa wananchi watajikita katika kukata miti kwa ajili ya kupata
nishati, na hivyo kwenda kinyume cha jitihada za utunzaji wa mazingira
zinazofanyika hivi sasa.
HABARILEO
RAIS Jakaya Kikwete ameelezea
kufurahishwa na wingi wa wagombea waliojitokeza kuomba ridhaa ya
kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akisema ni jambo
zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama
hicho.
Aidha, amesema pia msururu wa wagombea
hao ambao sasa wamefikia 36, ni uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania
katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio na kwamba kinyume cha
hapo, wengi wasingependa kujihusisha nacho.
Pamoja na kufurahishwa huko, ameendelea
kusisitiza kuwa, yeye binafsi hana mgombea urais anayempendelea kwa
sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake, isipokuwa anayo kura
moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao mbalimbali kuamua
nani awe mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Rais Kikwete amesema hayo usiku wa
kuamkia juzi mjini Johannesburg, Afrika Kusini wakati akizungumza na
Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza Kitengo cha Masuala
ya Afrika, Linda Thomas- Greenfield.
Viongozi hao wawili walikuwa
wanahudhuria Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Afrika kwenye Kituo cha Mikutano cha Sandton Covention Centre,
Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika jana.
Mwanzoni tu mwa mazungumzo hayo, Linda
alimwuliza Rais Kikwete: “Mheshimiwa Rais, je unaye mgombea yeyote
ambaye unampendelea miongoni mwa utiriri wa wagombea?”
Rais Kikwete alimjibu: “Sina mgombea
ninayempendelea, wagombea wote ni wa kwangu, ni wa Chama changu,
isipokuwa ninayo kura moja ambayo kwa mujibu wa taratibu za haki katika
Chama chetu nitaitumia katika vikao mbalimbali.”
Kuhusu kile kinachoitwa utitiri wa
wagombea, Rais Kikwete alisema wingi wa wagombea ni jambo zuri kwa CCM.
“Hiki ni chama kikubwa. Wingi unatupa nafasi ya kujadili kwa nafasi nani
awe mgombea wetu. Isitoshe, tunaona wagombea wengi zamu hii kwa sababu
ya wigo mkubwa wa uhuru ambao umejengeka katika nchi yetu katika miaka
ya karibuni. Vile vile, wingi wa wagombea unathibitisha mafanikio yetu
katika miaka 10 iliyopita kwa sababu tungeshindwa, watu wangeogopa
kujitokeza kugombea nafasi hiyo.”
Aidha, Rais Kikwete alisema hana tatizo
na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya urais zamu hii kupitia CCM
kwa sababu huwezi kuwazuia watu kugombea nafasi hiyo kwa sababu ni haki
yao.
Alisisitiza wingi wa wagombea zamu hii
ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika
chama hicho na uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10
iliyopita umekuwa wa mafanikio.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete,
jana aliwaongoza maelfu ya wakazi wa Shinyanga na mikoa jirani, viongozi
wa dini, Serikali na wanasiasa kumzika aliyekuwa Mufti na Shehe Mkuu wa
Tanzania, Issa bin Shaaban Simba, aliyeaga dunia juzi jijini Dar es Salaam na kuzikwa jana jioni mjini hapa.
Mbali ya Kikwete aliyeongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe pia alikuwepo, kama ilivyokuwa kwa mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.
Hata hivyo, Rais Kikwete alilazimika
kuwahi kuondoka mara baada ya maziko ili kuwahi majukumu mengine ya
kikazi kitaifa, hivyo kutozungumza lolote.
Lowassa, mmoja wa makada wa CCM
wanaowania kupendekezwa na chama chao kuwania urais wa Tanzania baadaye
mwaka huu akitarajiwa kuchuana na makada zaidi ya 30 wakiwemo Membe na
Sumaye, hakuzungumza lolote na aliondoka muda mfupi baada ya shughuli ya
kuupumzisha mwili wa marehemu.
Hata hivyo, Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu
wa Tanzania wakati Mufti Simba alipochaguliwa kuwa Mufti mwaka 2003
kuziba nafasi iliyokuwa imeachwa na Hemed bin Jumaa aliyeaga dunia mwaka
2002, alizungumza akisema taifa limeondokewa na mmoja wa viongozi
muhimu waliokuwa mstari wa mbele kuunganisha madhehebu yote ya dini.
Alisema wakati wa uhai wake, Mufti Simba
alikuwa ni kiongozi wa watu wa dini zote na alikuwa ni kiungo muhimu
katika suala zima la amani na utulivu.
“Ndugu
zangu leo ni siku ya majonzi makubwa kwaTaifa, tumeondokewa na kiongozi
muhimu, ni mfano wa kuigwa maana katika kipindi chake cha uongozi,
alijitahidi kuhakikisha hakuna migogoro mikubwa ya kidini kwa pande
zote, hali iliyosababisha waumini wa madhehebu mbalimbali ya kidini
kuishi kwa amani na upendo. “Nawaomba viongozi wote wa kisiasa na
kiserikali kuiga mfano wake, kwa kuhakikisha tunadumisha hali ya amani
na utulivu uliopo nchini ili kuliepusha Taifa kuingia katika machafuko,” Sumaye.
Naye Membe, alisema Mufti Simba ameacha
pengo kubwa nchini hasa kwa upande wa madhehebu ya kidini kutokana na
jinsi alivyoweza kuwapatanisha na kutatua migogoro mbalimbali bila ya
kuleta vurugu miongoni mwa madhehebu nchini.
Alisema yeye binafsi anaungana na
familia ya marehemu katika kumuomba Mwenyezi Mungu aipokee na kuilaza
mahala pema roho ya marehemu na kwamba atakuwa pamoja na familia hiyo
katika kipindi chote cha maombolezo.
Mufti Simba alifikwa na mauti asubuhi ya
juzi akiwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa
kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu.
Mufti Simba alijiunga na BAKWATA mwaka
1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ya Mwanza,
Bukoba na Mwaka 1970 alikuwa Shekhe wa Mkoa wa Shinyanga kabla ya
kupanda ngazi na hatimaye kuwa Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania mwaka
2003.
Kwa habari , matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment