Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
amehukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja
baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwangalizi wa Uchaguzi Mkuu
mwaka 2010.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa.
Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa
faini hiyo iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi
wa chama hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Wabunge waliochanga fedha hizo ni, Mustafa Akuney wa Mbulu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Cecilia Pareso, Joyce Mukya, Rose Kalili na Paulin Gekul wote wa Viti Maalumu.
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye
mitandao ya kijamii juu ya uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni
Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwania tena ubunge au urais katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Suala hilo linafanana na lililotokea
katika mchakato wa uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa
mgombea urais wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake, Saidi Soud Said
walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo jela, Mtikila
akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said akitumikia chuo cha
mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa.
Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia shambulio la kawaida, mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, Nassir Yamin katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa
ambaye amehamishiwa Bukoba, alisema kitendo kilichofanywa na Mbowe
hakikubaliki na kinapaswa kukemewa.
MWANANCHI
Kazi ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
ya kusaka wadhamini juzi nusura iingie dosari baada ya wanachama kutaka
kuchana fomu zenye orodha ya wadhamini kwa madai kuwa hawakupewa “nauli” ya kwenda ofisi za CCM kufanya kazi hiyo.
Wakati tafrani hiyo ikitokea mjini Mbeya, Balozi Amina Salum Ali
alisema mjini Tanga kuwa hajawahi kuona nchi ambayo mtu anaiba fedha,
halafu anaambiwa azirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua zozote, akisema
huo ni udhaifu mkubwa katika kudhibiti ufisadi.
Katika sakata la Mbeya, kundi la baadhi
ya wanachama kutoka kata nne waliokabidhi kadi na kuandikwa majina yao
kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Mbeya Mjini, liliambiwa kuwa hakukuwapo
na posho kwa ajili ya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha wanachama hao kupora na kutaka kuchana fomu iliyokuwa na majina yao.
Katibu wa CCM wilaya hiyo, Kulwa Milonge alisema tukio hilo lilikuwa kubwa na kuhatarisha usalama, lakini chama kiliingilia kati na kusawazisha mambo.
Milonge alisema hadi mwisho wa tukio hilo, ofisa aliyetumwa na Sumaye kukusanya saini hizo aliondoka na majina 45 ya wadhamini.
Sumaye ni mmoja kati ya wanachama wengi
waliojinadi kuwa wanachukia rushwa na ameeleza bayana kuwa iwapo CCM
itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Mkoani Tanga, Balozi Amina alisema kwa
kutumia uzoefu wake kimataifa katika masuala ya fedha, amebaini kuwa
kuna tatizo la kushindwa kudhibiti ufisadi uliokithiri nchini.
Alisema iwapo atapewa fursa ya kuwa Rais
wa Serikali ya Awamu ya Tano, atatumia nguvu kubwa kupambana na ufisadi
unaorutubishwa na tabia ya kulindana kwa sababu hata kama kutakuwa na
uzalishaji mkubwa, kama kuna mifereji ya rushwa, uchumi hauwezi kukua.
MWANANCHI
Mjadala wa Bajeti ya Serikali, ambao
umetawaliwa na suala la kushuka kwa thamani ya shilingi, jana ulichukua
sura ya pekee baada ya mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola
kuingia na begi lililojaa bidhaa mbalimbali kutoka nje ambazo
alizitumia kuthibitisha matumizi yasiyostahili ya fedha za kigeni.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, fedha ya
Tanzania imeshuka kwa zaidi ya asilimia 10 kulinganisha na Dola ya
Kimarekani kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu, na sababu kubwa zimekuwa
zikielezwa kuwa ni kuimarika kwa uchumi wa Marekani na nchi kutouza
bidhaa nje.
Jana Lugola, ambaye mara kadhaa amekuwa
na vioja wakati anapochangia bungeni, aliilaumu Serikali kwa kushindwa
kuzuia kuingia bidhaa ambazo zinastahili kuzalishwa nchini.
“Mheshimiwa
Spika, nina bidhaa hapa ambazo hata hazistahili na hizi ndizo
zinashusha shilingi yetu… nimekuja na kontena zima, kama ingewezekana
kuingia nalo hapa, ningeingia,” alisema kabla ya Spika Anne Makinda kumwambia kuwa anachotakiwa kufanya ni kutoa maelezo na si kuonyesha bidhaa.
Hata hivyo, Lugola aliendelea kuonyesha akisema: “Mheshimiwa
Spika hapa nina dodoki za plastiki kutoka China, soksi kutoka Marekani,
leso kutoka China, chaki (Kenya), pipi (Kenya), nyembe (China), na
pamba za kusafisha masikio kutoka China.
“Pia
vijiti vya kuondoa mabaki ya chakula kwenye meno (China), pipi za
kutafuna (chewing gum), kibiriti (Kenya), rula (China), penseli pia
kutoka China.”
Alisema Tanzania kuna rasilimali ambazo
zingeweza kutengeneza bidhaa hizo, lakini inatumia Dola kununua bidhaa
hizo nje halafu inalalamika kuporomoka kwa shilingi.
Akizungumzia posho za polisi, alisema
kuwa walipendekeza posho ya polisi ya Sh 8,000 anapokuwa kazini, lakini
hadi leo hakuna kilichofanyika.
“Tulishasema
hapa, wengine wako wizara hiyo halafu eti leo wanautaka urais,
wanashindwa kushughulikia hili la posho tu wizara moja, sasa wataweza
kushughulikia wizara zote,” alisema.
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekie Maige alisema kuwa katika Halmashauri ya Msalala, kumekuwa na ufisadi mkubwa katika miradi ya maji.
Akiichambua miradi hiyo alisema mradi wa
maji katika Kijiji cha Bulige uliogharimu Sh700 milioni, umekwama
kutokana na kukosa usimamizi wakati katika Kijiji cha Kagongwa
waliwaeleza wataalamu wa maji kuwa eneo hilo halina maji lakini
waliwabeza na kusema wao ni wataalamu na kutumia Sh430milioni, lakini
hadi leo hakuna maji.
NIPASHE
Serikali itaanza kuitumia Bandari ya
Tanga kuingiza mafuta ifikapo Julai Mosi, mwaka huu, kwa lengo la
kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam.
Sababu nyingine ni kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga pamoja na uharakishaji wa usafirishaji.
Aidha, waingizaji wa mafuta watakaotumia
bandari hiyo watatumia gharama ndogo tofauti na kutumia bandari ya Dar
es Salaam huku fedha zitakazopatikana zikiingia kwenye mfuko wa
kuboresha bandari ya Tanga.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA), Felix Ngamlagosi katika mkutano na wadau wa mafuta ambao uliokuwa unajadili namna ya upangaji bei ya nishati hiyo kupitia bandari ya Tanga.
Alisema mwaka 2012 kulikuwa na mfumo wa
uagizaji mafuta kwa pamoja ambao kwa kiasi kikubwa ulisaidia kupunguza
gharama za uingizaji mafuta nchini na ukusanyaji kodi, akisisitiza kuwa
imefikia wakati wa kutumia bandari hiyo kwani meli nyingi zinashusha
mafuta bandari ya Dar es Salaam.
“Serikali
imeamua kufungua bandari ya Tanga ili kupunguza msongamano katika
bandari ya Dar es Salaam pamoja na ucheleweshaji wa kupakua shehena za
mafuta bandarini kwani utakuta mafuta yanachelewa mwezi mzima hivyo
kusababisha gharama,” alisema.
Aidha, alisema haipendezi waagizaji wa
mafuta kutumia bandari moja kuingiza mafuta na kuwa ikiwa Taifa
litatumia bandari zaidi ya moja itasaidia kuharakisha usafirishaji wa
nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi na kukuza uchumi.
Ngamlagosi alisema mfumo huo utasaidia
nchi kushindana vyema kibiashara na bandari za Mombasa (Kenya), Beira
(Msumbiji) na Afrika Kusini na kuliingizia Taifa kipato kupitia
wafanyabiahara wa nje wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa mchakato wa ukusanyaji
maoni ya wadau wa mafuta ulifunguliwa Mei 19, mwaka huu huku ukitarajiwa
kufungwa Juni 19, 2015.
Mwenyekiti wa Baraza la Walaji (Ewura
CC), Prof. Jamidu Katima. alisema kuwa kazi kubwa ya baraza hilo ni
kuwatetea watumiaji wa nishati hiyo.
“Tunaambiwa meli za mafuta zikishusha
katika banadari ya Tanga zitapunguza gharama kwa watumiaji hivyo
tunapaswa kuliona hilo likitendeka,” alisema.
Prof. Katima alisema kwamba ikiwa mafuta
yatakuwa yakishushwa katika bandari hiyo kwa bei nafuu ni wazi kuwa
gharama za mafuta kwa watumiaji wa mikoa ya jirani na mkoa husika
zitakuwa chini.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujenga utamaduni mpya
wa kukubali matokeo na kumuunga mkono mgombea anayeteuliwa na chama
hicho kugombea nafasi ya Urais mwaka huu badala ya kujenga na kuendeleza
makundi yanayoweza kuvuruga umoja na kuhatarisha mustakabali mzima wa
chama hicho.
Pinda ambaye ni miongoni mwa zaidi ya
wanachama 30 wa chama hicho waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa
kugombea urais kupitia CCM mwaka huu, aliyasema hayo jana jijini Mbeya
alipokuwa akitafuta wadhamini.
Alisema kuwa ingawa watu waliojitokeza
kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya urais kwenye
uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni wengi, lakini anayetafutwa ni mmoja,
hivyo haiwezekani wote waliochukua fomu hizo kufanikiwa kupata nafasi ya
kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM.
“Nitoe rai kwa wadau wote, ni kwamba
ilimradi sisi wote tuliomo humu ni wana-CCM, na wote waliojitokeza
kugombea nafasi hii ni wana-CCM, lazima tujenge tabia, tujenge mwenendo
mzuri wa kuona namna gani huyo moja atakayepatikana wengine wote
tuliokuwa kwenye mchakato huo turudi tumuunge mkono maana ndiye atakuwa
mgombea wetu aliyepatikana,” alisema Pinda na kuongeza:
“Ifahamike kuwa hata kama tungekuwa watu
mia tuliochukua fomu, anayetafutwa ni mmoja tu, haiwezekani sote sisi
tukang’ang’ania tuteuliwe, hivyo katika mazingira haya ni muhimu tujenge
utamaduni mpya wa kuridhika na uteuzi kisha tumuunge mkono huyo
atakayeteuliwa,” alisema Pinda.
Aidha aliwataka wagombea wenzake
kutonuna baada ya uteuzi kufanyika na badala yake wavunje makundi yao na
kumuunga mkono mtu atakayeteuliwa kwa manufaa na maslahi ya chama na
Watanzania kwa ujumla.
Pinda lisema kuwa endapo wagombea wote
kila mmoja atang’ang’ania ateuliwe huku wakiendeleza makundi na kupigana
vijembe hata baada ya mtu anayetafutwa kupatikana, ni dhahiri kuwa CCM
itayumba na pengine kudhoofika.
NIPASHE
“Nilirudia
uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa
nao kama Jaji Mkuu… Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa
kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au
kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza…”
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan,
ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza kuwa licha ya kuwapo
kwa utitiri wa wagombea urais, hakuna Mtanzania yeyote anayeweza
kumnyooshea kidole akimtuhumu kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa.
Jaji Ramadhan ambaye ni kada wa 36
kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho,
alisema hakuna mgombea anayemtisha kati ya wote waliomtangulia, kwa kuwa
hakuna mwanajeshi anayeogopa.
Jaji Ramadhani alikuwa akizungumza na
waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma, muda
mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
“Sina
doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania
anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya
rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Mimi ni mwanajeshi,
nimestaafu nikiwa Brigedia Jenerali Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ). Sijui kama kuna mwanajeshi anayeogopa na hakuna mgombea
ninayemuogopa; nikiogopa ina maana mimi si mwanajeshi,” alisema na kuongeza:
“Nina uzoefu wa kutosha, nina uwezo wa kuwatumikia Watanzania twende huko tunakotaka na kuinua uchumi wetu.
Nimejipima na nimeona nina uwezo wa
kugombea urais kwa sababu nakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kisiasa na
kiuongozi; kilichonisukuma kutangaza nia ya kugombea ni uwezo wangu,
sijashinikizwa na mtu yeyote,” alisema Jaji Ramadhani.
Kuhusu utata alijiunga lini na CCCM, wakati amekuwa mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 33, Jaji Ramadhani alisema:
“Nilijiunga
na CCM mwaka 1969 nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu Kitivo cha Sheria
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na niliendelea na uanachama wangu hadi 1992
kipindi mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na kusababisha mabadiliko ya
Katiba ambayo yaliweka masharti kwa mtumishi wa umma kutokuwa
mwanachama.”
Jaji Ramadhani alisema baada ya
mabadiliko hayo, uanachama wake ndani ya CCM ulisimama hadi mwaka 2010
alipostaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania na kulazimika kurejesha
uanachama wake mwaka 2011 kwa ajili ya kuendelea na masuala ya siasa.
“Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu”.
Kuhusu rushwa, alisema ni tatizo kubwa
nchini. “Tatizo la rushwa katika serikali na nchi yetu ni kubwa, nataka
nilimalize kama chama changu kitaniteua na kushinda nafasi hiyo…wakati
nilipokuwa Jaji Mkuu, nilipambana nalo katika mahakama zetu,” alisema na
kuongeza:
“Nawahakikishia
Watanzania nikiwa Rais, ukila rushwa Kilimanjaro, hutahamishiwa Mtwara
maana hata waliopo Mtwara ni Watanzania, hawataki mla rushwa.”
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Jaji Ramadhani alisema: “Kwa
nafasi yangu niliyokuwa nayo kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, kazi yetu ilikwishamalizika, baada ya kumkabidhi
Rais Jakaya Kikwete, Rasimu ya Pili ya Katiba pale kwenye ukumbi wa
Karimjee na Bunge Maalum la Katiba limemaliza kazi yake, hatua iliyobaki
ni wananchi kuamua katika Kura ya Maoni. Na ndiyo itakayoamua hatma ya
Katiba Mpya na si Rais.”
Alisema kwa sasa hawezi kuainisha
vipaumbele vyake lakini iwapo atateuliwa kugombea urais, kazi yake kubwa
itakuwa ni kutekeleza sera na siasa za CCM ambayo itakuwa imeainishwa
ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
NIPASHE
Pamoja na changamoto za ubovu wa mashine
za kielektroniki za BVR zinazotumika kuandikisha wananchi katika
daftari la kudumu la wapigakura imebainika kuwa hazitunzi vizuri.
Katika kituo cha King’ang’a Wilaya ya
Nyamagana, Mwanza mashine nne zinazotumika katika kituo hicho
zilisafirishwa kwa njia ya bodaboda huku wananchi wakihoji iweje NEC
kushindwa kutumia usafiri wa gari ili kushindwa kuzilinda mashine hizo.
Mmoja wa wananchi alisema ni jambo la
kushangaza kwa Serikali kuruhusu mashine hizo kusafirishwa kwa bodaboda
licha ya kuwepo mashine kwenye baadhi ya barabara.
“Kwanza wanachelewa kufika vituoni, pia
mashine zenyewe zimebebwa kwenye bodaboda, huu ji uhuni ambao baadaye
utasababisha mashine kutofanya kazi kutokana na mtikisiko’
Aidha baadhi ya mashine hizo ziligoma kutoa vitambulisho kutokana na ubovu, lakini baada ya muda zilianza kufanya kazi.
MTANZANIA
Naibu waziri wa Mawasialiano, Sayansi na teknolojia January Makamba
amewataka wanachama wenzake kuangalia rekondi za wote wanaoomba
kuteuliwa na chama cha CCM kugombea Urais kwa sababu chama hicho si
daladala la kudandia kuelekea Ikulu.
January amabye pia ni Mbunge wa Bumbuli
alitoa kauli hiyo jana akiwa kisiwani Unguja wakati akiomba wadhamini
ili ateuliwe kugombea Urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.
“Tunaoomba
ridhaa ya kugombea Urais kwa tiketi ya CCM tupo zaidi ya 30 na hii
inapeleka ujumbe duniani kwamba ndani ya chama chetu tuna demokrasia
tofauti na watani wetu wanaosimama majukwaani kuhubiri demokrasia,
lakini ndani ya vyama vyao kuna masultani” Makamba.
Alisema mwaka huu hawachahui mtu atakayegombea Urais tu, bali wanchagua mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa CCM.
Kada huyo wa CCM ambaye katika Mikoa
miwili alipata kura 80 alisema bila chama hicho alipata kura 80, alisema
bila chama hicho Muungano utakuwa shakani.
MTANZANIA
Kiongozi mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewatangaza Wabunge Moses Machali na Said Arfi kuwa ni wagombea wa Ubunge kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu unaokuja.
Zitto aliwataja wagombea hao wakati wa
mkutano wa hadhara Kigoma ambao aliwataqmbulisha watangaza nia
mbalimbali na kusema sasa chama hicho kimejipanga na makucha ya
unyonyaji wa rasilimali za Taifa.
Awali Zitto alisema muswada wa sharia ya
mafuta na sharia ya matumizi ya fedha za mafuta haiwezi kujadiliwa na
wabunge wenye haraka ya uchaguzi.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment