NIPASHE
Serikali imesema kuwa inafanya utaratibu
wa kuwalipa fedha takribani Sh. bilioni 19 za waliokuwa wanachama wa
Taasisi ya Development Entrepreneurship Community Initiative (Deci).
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu,
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema fedha hizo zimehifadhiwa katika
akaunti ya Benki Kuu (BoT) na kwamba kinachofanyika sasa ni uangalizi wa
kiasi cha michango iliyochangwa na wanachama ili waweze kulipwa kwa
usahihi.
“Bado fedha zinashikiliwa BoT uchambuzi
unaendelea kufanywa kwa umakini wa hali ya juu, utakapokamilika
wanachama wote waliochanga fedha watalipwa,” alisema Mkuya.
Aidha, Waziri Mkuya alisema siyo jambo
litakaloweza kuchukua muda mfupi kukamilisha mchakato wa malipo ya
wanachama hao, kwani linahitaji muda wa kutosha kufanyiwa kazi
kikamilifu, ingawa hakutaja kiasi kilichopo.
Mwaka 2009 serikali ilisitisha shughuli
za Deci na kuwafungulia mashtaka wakurugenzi watano wa taasisi hiyo
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na Agosti
19, mwaka 2013, walihukumiwa.
NIPASHE
Wabunge wamefichua ufisadi katika
Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, ambayo watendaji wakuu
wa hospitali hiyo wameuziana magari mapya ya serikali kwa bei ya kutupa
ya Sh. milioni 8 kila moja.
Ubadhirifu huo ni wa kutisha uliibuliwa
jana Bungeni wakati mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Mbunge wa Viti Maaalum Chadema, Suzan
Lyimo, alisema viongozi wakuu KCMC wameuziana magari aina ya Prado na
Nissani Patro kwa bei ya Sh. milioni 8 kila moja mwaka 2013, ambayo
yalipelekwa katika hospitali hiyo kwa shughuli mbalimbali.
Alisema kutokana na ubadhirifu huo
Mhasibu wa hospitali hiyo, Paulo Muhunya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chama cha Wafanyakazi wa Afya (TUGHE), alimjulisha Rais Jakaya Kikwete,
kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kuhusu ufisadi huo.
Lyimo alisema katika hali ya kushangaza
Mhasibu huyo baada ya kutoa taarifa za ubadhirifu huo, Mei 5, mwaka huu,
alisimamishwa kazi jambo ambalo linatia mashaka.
“Nchi hii inashangaza inakuweje mtu
aliyesaidia kutoa taarifa za kufichua wizi yeye ndiye anaadhibiwa, au
ndio utaratibu wa serikali ya CCM kuwalinda wezi,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Chadema,
Congesta Lwamlaza, alisema Serikali ya CCM ni ya kutumbua tu ndiyo maana
fedha nyingi zinatengwa kwa mambo ya starehe tu.
NIPASHE
Chama Cha Wapangaji Tanzania, kimeiomba
Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kutokubali kuuza nyumba za
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zilizopo katikati ya miji hasa Upanga
jijini Dar es Salaam, kwa kuwa wanaotaka kuzinunua ni matajiri wachache
wenye kiu ya kunufaika na rasilimali za nchi.
Aidha, chama hicho kimeishauri serikali
kusitisha upangaji wa muda mrefu kwa nyumba za NHC, ili Watanzania wengi
hasa wanaoanza kazi waweze kunufaika na nyumba hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndumey Mukama,
alisema utafiti wao umebaini kuwa kuna wapangaji wa kudumu NHC ambao
sasa wanataka kuuziwa nyumba hizo kwa bei ya kutupa wakati tayari
wameshajenga nyumba maeneo mengine.
Alisema wapangaji wa muda mrefu wa NHC
hasa maeneo ya mjini kama Dar es Salaam ni watu wenye uwezo ambao
wengine wamejenga nyumba nzuri na wanazipangisha kwa dola za Marekani,
huku wakiendelea kulipa kodi ndogo NHC. Alisema wapo wanasiasa wachache
na baadhi ya wapangaji wa muda mrefu wanaong’ang’ania kuuziwa nyumba
hizo kinyume cha utaratibu.
Aliishauri Serikali iweke sheria ya
ukomo wa upangaji wa nyumba za serikali angalau miaka mitano ili kutoa
nafasi kwa Watanzania wengi hasa wanaoanza maisha kuweza kupanga nyumba
hizo.
Mukama alisema: “Utaratibu wa sasa wa
wapangaji kukaa kwa muda mrefu katika nyumba hizo umewajengea kiburi
wapangaji hawa na wamefikia hatua ya kutaka kuuziwa nyumba hizi kwa bei
chee wakati ni rasilimali ya Watanzania wote. Hawa wanaouwezo wa kununua
nyumba zinazojengwa sasa katika maeneo mengine na NHC wakanunue huko.”
Alisema jambo lingine linalowapa kiburi
wapangaji wa NHC ni kusikilizwa ‘sana’ na serikali hata pale ambapo
wanakiuka masharti ya upangaji.
Chama hicho pia kimeishauri serikali
itengeneze sera ya nyumba ambayo itawabana pia wenye nyumba binafsi na
kuweka usawa kwenye sekta hiyo.
MWANANCHI
Tofauti na makada wengine wa CCM ambao
walianza kwa kutangaza nia kisha baada ya kuchukua fomu kuzungumza na
waandishi wa habari, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, jana alichukua
fomu kimyakimya bila kutaka kuzungumza lolote.
Badala yake akasema atatafuta muda muafaka wa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kusoma fomu alizopewa na chama chake.
Hata hivyo, kwa kifupi kabisa alisema
endapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi atatekeleza Ilani ya CCM na
kuwaomba Watanzania wamuombee.
Dk Magufuli ambaye alikuwa amevalia
suruali nyeusi na shati la kijani, hakuwa na mbwembwe za wapambe wengi
kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine.
Alisindikizwa na watu watatu akiwamo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama na wapambe wawili walioshuka katika gari lake.
Kada huyo alichukua fomu yake saa 11.30 jioni na kisha kuondoka zake katika eneo hilo kimyakimya.
John Magufuli ni nani?
Alizaliwa Oktoba 29, 1959 huko wilayani Chato, Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya Mkoa wa Geita).
Alianza elimu ya msingi katika Shule ya
Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule
ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma kidato cha kwanza na cha
pili mwaka 1975 – 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza
ambako alisoma kidato cha tatu na nne mwaka 1977 – 1978.
Alisoma kidato cha tano na sita mkoani
Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981.
Halafu akarudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya
Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa
mwaka 1981 – 1982.
Alipopata stashahada yake, moja kwa moja
alikwenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema,
akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya
mwaka 1982 na 1983.
Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai –
Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi
Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi –
Juni 1984).
MWANANCHI
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akiahidi kupambana na
mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi ambayo ni umaskini, ujinga,
maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Akitangaza nia hiyo kwenye Ukumbi wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mwanza jana, Ngeleja alisema anatambua
kwamba Watanzania wa leo wanatamani kumpata rais ambaye atapambana kwa
dhati na vitendo na maadui hao.
“Nina mikakati madhubuti ya kujibu swali
la kiutafiti linaloonyesha kwamba mamlaka, idara na taasisi za umma
zenye dhamana kubwa ya maisha ya Watanzania mfano, Polisi, Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) na watendaji wakuu wa taasisi za biashara (CEO) ndiyo
wanaoongoza kwa tuhuma za kupokea rushwa,” alisema.
Ngeleja akiwa ameambatana na mkewe,
Blandina na Mwenyekiti wa Kamati yake ya Maandalizi, Mbunge wa Magu, Dk
Festus Limbu waliingia ukumbini saa sita mchana na kupokewa na makada wa
CCM waliohudhuria ambao walitoka maeneo mbalimbali ikiwamo vyuo vikuu,
wajumbe wa halmashauri kuu kutoka bara na visiwani, wawakilishi wa
wamachinga na wavuvi.
Alisema Watanzania wanatamani kuwa na
rais ambaye atasimamia kwa dhati umoja na mshikamano wa kitaifa,
Muungano, kulinda amani, kukemea kwa nguvu zote ubaguzi wa dini, kabila,
rangi na aina nyingine yoyote ya ubaguzi inayoweza kujitokeza nchini na
kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.
“Historia ya nchi yetu ni ndefu na imepita misukosuko mingi lakini kwa umoja, udugu na mshikamano wetu tumefanikiwa,” alisema.
Hata hivyo alisema hivi sasa rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili ni maadui wengine walioongezeka kwa kasi.
“Kadri Watanzania tunavyozidi kuongezeka
kwa idadi na maadui zetu hawa nao wanazidi kujitanua. Hivyo mbinu,
mikakati na silaha za kupambana na maadui hawa lazima zibadilike,”
alisema.
Ngeleja alisema baada ya kushauriwa na
baadhi ya Watanzania kutoka pande zote za nchi tena wa kada mbalimbali
amejitafakari, kujitathmini na kujiridhisha kuwa anayo dhamira ya kweli
kuwatumikia Watanzania.
“Nimejitafakari, nimejitathmini na
kujiridhisha kwamba ninayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania
kupitia nafasi ya urais. Mbali ya dhamira ya kweli nimejipima kwamba
ninao uwezo wa kubeba matarajio ya Watanzania, kupitia utekelezaji wa
kaulimbiu yangu isemayo: “Maono Sahihi, Mikakati Thabiti, Matokeo Halisi
(MMM),” alisema.
MTANZANIA
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), huku akisema hana mpango wa kushindwa.
Lowassa aliwasili katika Makao Makuu ya
CCM mjini hapa jana saa 10:20 jioni akiambatana na mkewe, Regina huku
akisindikizwa na wabunge mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari
pamoja na wanachama waliokuwapo katika Ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mara
baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema hawezi kuzungumzia upande wa
kushindwa katika safari yake.
“Swali rahisi sana, sina mpango wa
kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na
waandishi wa habari kama atashindwa katika kinyang’anyoro hicho.
Alipoulizwa kuhusu hali ya nchi kuwa na
watu wanaoshambuliwa, Lowassa alisema atajenga Serikali itakayojali utu
na uhuru wa vyombo vya habari.
“Kwanza nimpe pole yule mwandishi wa
MTANZANIA aliyeteswa. Sikubaliani na mambo ya kuingilia uhuru wa watu
kuteswa. Serikali yangu itaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” alisema
Lowassa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM waliokuwa wamefurika
ndani na nje ya ukumbi huo.
Alipoulizwa kwanini anahusishwa na
vitendo vya ufisadi, Lowassa aliyekuwa akijibu maswali kwa ufupi,
alisema kama kuna mtu ana ushahidi na tuhuma hizo amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu
anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi
viongozi kwa rekodi za matusi ila tutawapima kwa matendo yao,” alisema.
Kada huyo wa CCM alivitaka vyombo vya
habari kutoshabikia tuhuma zisizo na ushahidi, huku akisisitiza kuwa
kila mtu apimwe kwa rekodi yake.
Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Lowassa hakutaka kulizungumzia akisema bado hajavuka daraja.
“Nitavuka daraja nitakapolifikia,” alisema.
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
alisema ni sera ya CCM iliyotekelezwa baada ya kutokea mgogoro kati ya
vyama vya CCM na CUF.
“Angalieni kule Marekani, vyama vya
Democrat na Republican, vinashindana kwa kura chache sana. Hata sisi
tunapishana kwa kura chache, mimi nadhani kama hatupishani sana hivyo
hilo ndilo suluhisho,” alisema.
Awali Lowassa aliwashukuru wana CCM
waliofurika katika ukumbi huo akisema anajua kero za chama hicho na
atakapokuwa rais atazishughulikia.
“Nawashukuru kwa kunileta nyumbani, nimeitumikia CCM kwa muda mrefu. Nilieleza Dodoma na Arusha nia yangu.
Naelewa matatizo wanayopata watumishi wa
CCM, nayaelewa. Mishahara midogo, hawakopesheki, hawana fedha za likizo
na hawana uchumi mzuri. Wakati wengine wanajengewa nyumba na mikopo
wenyewe hawapati,” alisema Lowassa.
Hata hivyo, alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha uchumi ndani ya chama hicho, lakini akasema akiwa rais atafanya zaidi.
“Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” alisema.
“Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” alisema.
Baada ya mkutano huo, Lowassa alikwenda
kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma kupata udhamini wa chama hicho
ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi
alikuwa miongoni mwa wanachama waliomdhamini, akiwamo mlemavu wa miguu,
Idd Omari.
Baadhi ya vigogo waliokuwa ukumbini ni
pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter
Serukamba na Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah.
Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya
Dodoma Mjini baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema vigelele na makofi
anavyopigiwa sasa haviwezi kumpeleka Ikulu isipokuwa wananchi wanapaswa
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili iwe njia rahisi ya yeye
kuwa mkuu wa nchi.
“Naomba watu wajiandikishe, hakikisheni
watoto wenu, wajomba na hata washikaji zetu wanajiandikisha katika
Daftari la Wapigakura na nitarudi tena kwenu kuomba kura,” alisema.
Huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa
Dodoma, Lowassa aliwaambia amekwenda kuomba wadhamini na si kuomba
kura, kwani amebanwa na sheria na utaratibu wa chama chao.
Alisema ameguswa na mapokezi waliyompa na kuwashukuru wadhamini wake kwa kumwamini na kusisitiza kuwa atarudi tena kuomba kura.
“Leo siombi kura, naweka akiba ya maneno
hata wakihesabu nina kampeni potelea mbali, lakini nilipokuwa waziri
mkuu nilianza kuijenga Ikulu mnayoiona mpaka leo haijakamilika, nitakuja
kuikamilisha, maana yake nini, nahamia Ikulu Dodoma,” alisema mbunge
huyo wa Monduli huku akishangiliwa na mamia ya wananchi hao.
MTANZANIA
UPELELEZI wa kesi inayomkabili Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima na wenzake watatu
umekamilika na kesi inatarajiwa kuanza usikilizwaji wa awali Julai 2,
mwaka huu.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack
Kimaro aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana wakati kesi
hiyo ilipokuwa inatajwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa,
Kimaro alidai kesi ilikuwa inatajwa, lakini upelelezi wa kesi hiyo
umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa
maelezo ya awali.
Hakimu Riwa aliyakubali maombi ya upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hadi Julai 2, mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni
msaidizi wa askofu huyo, Yekonia Bihagaze (39), mfanyabiashara George
Mzava (43) na mkazi wa Kimara Baruti, Geofrey Milulu (31).
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima
anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika
Packers Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi
ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwamba
ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu
wa amani.
Katika kesi ya pili namba 84, Gwajima
anakabiliwa na shtaka moja la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi
kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kwamba kati ya Machi 27 na 29,
mwaka huu ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi
silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 , risasi tatu za pisto na risasi
17 za shotgun.
Shtaka la pili na la tatu linawakabili
washtakiwa waliobaki ambao wanadaiwa kwamba Machi 29 mwaka huu katika
Hospitali ya TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi
hizo bila ruhusa kutoka mamlaka husika.
HABARILEO
BARAZA Kuu la uongozi la Chama cha
Wananchi (CUF) limemchagua kwa kura zote 56 Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari hapo
katika ofisi ndogo ya CUF Shangani mjini hapa, Mkurugenzi wa Mipango na
Uchaguzi wa chama hicho, Omar Ali Shehe alisema maalim amepita bila ya
mpinzani katika kinyang’anyiro cha nafasi ya urais wa Zanzibar kutokana
na imani kubwa ya wanachama wa chama hicho dhidi yake.
Alisema uamuzi huo sasa utamfanya Maalim
Seif kumsubiri mgombea kutoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
ajili ya kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
“Chama cha CUF kimebadilisha utaratibu
zamani jina la mgombea wa nafasi ya urais linaamuliwa na mkutano mkuu wa
chama, lakini tumebadilisha maamuzi hayo kutokana na gharama kubwa za
kuitisha mkutano katika chama kichanga kama hiki,” alisema.
Mapema Shehe alitangaza majina ya mwisho
ya wagombea wa nafasi ya Uwakilishi na Ubunge katika chama cha CUF
katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba.
Katika majina hayo yanaonesha kwamba
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa ambaye aliangushwa katika kura
za maoni amerudishwa kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Mji Mkongwe
kwa tiketi ya CUF, Mohamed Ibrahim Sanya ameondolewa katika
kinyang’anyiro hicho na nafasi yake kuchukuliwa na mwandishi mkongwe
aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
Ali Saleh.
Sanya aliibuka nafasi ya kwanza katika
mchakato wa kura za maoni huku akimuangusha vibaya kwa kupata kura 21
Ali Saleh ambaye alishika nafasi ya tatu.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi
alipoulizwa kuhusu maamuzi ya Baraza la Kuu la Uongozi wa CUF, alisema
baadhi ya vigezo muhimu vilipewa kipaumbele cha kwanza ikiwemo suala
zima la matokeo ya kura za maoni kutoka katika majimbo ya uchaguzi kwa
wanachama.
Aidha, alisema suala la utekelezaji na
kukubalika katika jamii ni suala la pili ambalo lilizingatiwa kwa lengo
la kuona mgombea anafanikiwa na kukivusha chama hadi kupata ushindi.
“Vipo vigezo tulivipa kipaumbele cha
kwanza ikiwemo matokeo ya awali ya kura za maoni za wanachama katika
majimbo ya uchaguzi, lakini pia suala zima la utekelezaji na kukubalika
katika jamii,” alisema.
Kwa habari na matukio mbalimbali yanayojiri ndani na nje ya nchi , ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment