Baada ya wiki nzima ya makada wa CCM
kutangaza nia na hatimaye kuchukua fomu za kugombea urais, wapinzani
ndio wanaonekana kunufaika zaidi kutokana na wengi kutumia hotuba zao
kuelezea udhaifu wa kila mmoja.
CCM imepanga mwezi mzima, kuanzia Juni 3
hadi Julai 2 kuwa ni muda wa makada wake kuchukua na kurudisha fomu
kabla ya vikao vya juu vya chama hicho kukutana kuanzia Julai 12 kuchuja
wagombea na baadaye kumpata mmoja atakayesimama kwenye Uchaguzi Mkuu
kupambana na wa vyama vingine.
Tayari makada 15 wameshachukua fomu na
wengine wanaendelea kuchukua, huku waliochukua wakiwa wameshaanza
kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini 30 kila mkoa ili kupata idadi ya
wadhamini 450. Wanatakiwa kupata wadhamini kwenye mikoa 15, kumi ya Bara
na mitano ya Zanzibar.
Karibu wagombea wote walizungumzia nia
yao ya kupambana na rushwa, lakini walilitaja tatizo neno hilo kwa nia
ya kuwashambulia baadhi yao huku maneno ya kuponda umaskini, kujisifu
kwa utajiri, kukaa madarakani muda mrefu, ufisadi na masuala mengine
yakitumika kupondana.
Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyetumia muda mwingi wa hotuba yake kijijini Butiama kuponda makada wote, akiwataja kwa majina kuanzia Edward Lowassa aliyeanza kutangaza nia baada ya kuruhusiwa na chama, Mwigulu Nchemba, hadi Steven Wasira, mwanasiasa mkongwe ambaye alianza kuwa waziri tangu miaka ya sabini.
Makongoro aliwaponda makada watatu
waliojitokeza kwenye maeneo matatu ambayo ni matumizi ya fedha
yaliyopindukia wakati hawana vyanzo vinavyoeleweka, ahadi zao kabla ya
kutoka Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa serikalini kwa muda mrefu bila
ya kufanya chochote.
Makongoro alisema viongozi wengi
wanamyumbisha mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete na kusema kama wanachama wa
CCM wanataka chama hicho kisipotee, wampe nafasi ya kukirudisha kwenye
njia.
Mgombea wa CCM anatarajiwa kukumbana na
upinzani mkubwa zaidi ya mwaka 2010 baada ya vyama vinne-CUF, Chadema,
NLD na NCCR Mageuzi- kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja, huku vyama
vingine nikionekana kujikita zaidi kwenye ubunge.
“Kwanza, kwa chama tawala kuwa na watu wengi wanaojitokeza kutaka urais, inaonyesha kuwa CCM haina mgombea,” alisema katibu mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alipoulizwa maoni yake kuhusu hali hiyo ya kupondana.
Miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza
nia au wanaotajwa kuwa wataingia kwenye mbio za urais wameshatajwa
kwenye kashfa kadhaa zilizoikumba Serikali ya Awamu ya Nne, ambazo ni
pamoja na Operesheni Tokomeza Ujangili, ubadhirifu ulioibuliwa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), mkataba wa umeme wa
dharura na kampuni ya Richmond, uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni
kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na EPA.
Hata hivyo, karibu wagombea wote
wameahidi kupambana na rushwa, wakisema ndilo tatizo kubwa linalosumbua
utekelezaji wa mikakati ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.
MWANANCHI
Spika Anne Makinda amesema endapo Watanzania wataendekeza itikadi za udini na ukabila, Taifa litagawanyika na hakuna atakayenusurika na machafuko.
Makinda alisema kinachosikitisha kwa
sasa ni uongo unaopandikizwa na wanasiasa juu ya tofauti mbalimbali
zinazojitokeza, kama ilivyokuwa kwenye mchakato wa Katiba.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa ibada ya maziko ya mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa aliyefariki dunia siku tano zilizopita kwa shinikizo la damu.
“Kuna kundi la watu wasioitakia mema nchi yetu, lakini hawana hoja. Wanasambaza na kuwapandikizia uongo wananchi, kwa mfano walieneza uongo kwenye Katiba Watanzania wakajigawa. Tusipokuwa makini tutagawanyika, Makinda.
“Ni
ajabu sana mtu mwenye elimu na vyeo vyake akaonekana kuwa sehemu ya
kuleta mpasuko kwenye jamii, lakini huyo ni shetani tu kwani tunaamini
Mungu yupo…ni vyema kila mtu afikirie mchango wake katika jamii.”
Alikuwa akisisitiza maneno yaliyotolewa na Msaidizi wa Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chediel Lwiza
ambaye alimzungumzia Mwaiposa kuwa ni mtu asiye na ubaguzi, muadilifu
na aliyejihusisha na jamii kwa karibu bila kujali makundi yao.
Mwaiposa jana alizikwa nyumbani kwake na
wabunge walioongozwa na Spika Makinda, mameya na wakuu wa wilaya za
Mkoa wa Dar es salaam.
Awali Askofu Lwiza alitoa tahadhari kwa
Watanzania kuchagua kiongozi makini atakayelivusha Taifa kwenye mpasuko
wa udini na ukabila.
Alionyesha masikitiko yake akisema kwa
sasa hatari ukabila na udini, imeshaanza kuonekana kwenye jamii hususani
katika kipindi cha uchaguzi.
JAMBOLEO
Mgombea wa nafasi ya Urais ambaye pia ni Naibu waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba amechukua fomu yay a kugombea Urais na kuweka bayana utajiri wake kwa kusema kwa sasa ana milioni tano kwenye akaunti yake.
Pia alisema Rais Jakaya Kikwete atakuwa
Rais wa mwisho kuongoza Tanzania maskini kwani zipo rasilimali nyingi
zilizogunduliwa nchini na endapo zitatumika vizuri zinatosha kuwaondoa
wananchi kwenye umaskini.
Nchemba alitoa ufafanuzi wa utajiri wake baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari kuhusu mali anazomiliki.
“Wakati
nimeshinda Ubunge wazazi wangu walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya
Tembe, nikawajengea nyumba na hivi sasa ndiyo namalizia nyumba yangu
kule kijijini ambapo fedha za ujenzi wa nyumba hiyo nimekopa kwenye
mafao yangu ya Ubunge” Mwigulu.
“Kwa
upande wa Dar es salaam nina nyumba moja ambayo niliijenga wakati
nafanya kazi BoT , lakini kwenye akaunti yangu hivi juzi juzi nilikuwa
na milioni 5 na nilipunguza kutokana na hizi heka heka za uchaguzi”.
Alisema kwa sasa zimegundulika
rasilimali nyingi ikiwemo gesi pamoja na madini yanayoendelea
kugundulika kila mahali, zinatosha kuifanya nchi kuondokana na umaskini.
NIPASHE
Mnikulu Shabani Gurumo,
aliyepokea asante ya Shilingi milioni 80.8 katika mgawo wa fedha za
kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, ametimuliwa kazi Ikulu.
Taarifa za kuondolewa Gurumo, zilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue , katika mahojiano na gazeti hili ambaye alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa wiki moja iliyopita.
Gurumo aliyekuwa na wadhifa wa Ofisa Mkuu wa Ikulu, alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing James Rugemalira, alipohojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Rugemalira alikuwa mzawa wa kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo pamoja na Tanesco zilifungua akaunti hiyo ya Escrow.
Fedha alizopokea Gurumo zinadaiwa kuwa
ni sehemu ya zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilizochotwa kifisadi katika
akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Balozi Ombeni alisema hawana cha
kumfanya kwa upande wao na kwamba Ofisi ya Utumishi wa Umma ndiyo yenye
jukumu la kuamua kinachofuata dhidi ya mtumishi huyo. “Sisi hatuna cha kufanya zaidi ya kuondolewa Ikulu, Ofisi ya Utumishi itaamua nini kinachofuata.”
Awali Mnikulu huyo alipinga madai ya
yeye kupewa zawadi hiyo ya Escrow na lakini alikiri kuwa alipokea
Shilingi milioni 80.8 kutoka kwa Rugemalira kwa sababu za urafiki
walionao kwa muda wa miaka 10 na hazihusiani na mgawo.
Aliwaambia wajumbe wa Tume ya Maadili kuwa aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alijieleza zaidi kuwa hata siku moja
hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha
na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.
Akasema anahisi pengine Rugemalira
alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa
na maradhi ya saratani.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitoa
taarifa kuwa Shilingi bilioni 301 zilichotwa kwenye akaunti hiyo na
kusababisha vigogo kadhaa akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kujiuzulu.
NIPASHE
Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi, amesema anamuunga mkono, kada wa CCM, Edward Lowassa katika safari ya matumaini.
Aidha amewahimiza Watanzania wanaofikiri wanazo sifa za kuwaongoza wananchi wajitokeze ili wapimwe uwezo wa kuitumikia nchi.
Mbali na hilo ameungana na Lowassa
katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana ambayo mara nyingi
amekuwa anaizungumzia.
Askofu Niwemugizi alitoa msimamo huo
jana kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya seminari ndogo ya
Mtakatifu Karoli Lwanga.
Alisema Watanzania wanajua Lowassa
ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM na wanamuombea na
kumtakia mafanikio katika safari yake hiyo.
“Tunatamani kuiombea nchi yetu iwapate viongozi makini, waadilifu, wakweli, watakaoongoza kwa misingi ya haki na usawa. Watakaoijenga jamii yenye kuaminiana na kuheshimiana, inayojali mema ya wote, watakaolinda amani na kudumisha umoja wa taifa,”
“Nimefurahi
Lowassa kukubali mwaliko wangu, tumekualika wewe maana najua yatasemwa
mengi yasiyo sahihi kwa kuja kwako huku, sote tunajua kuwa sasa ni joto
kubwa la uchaguzi.”
“Wanaweza
kufikiri nimekuita kukupigia kampeni katika safari yako ya matumaini
uliyoitangaza kule Arusha, hayo siyo malengo yangu, ila wanaotaka
kuliona hivyo basi juu yao, na kwanini sikuita mwingine ila wewe,
nafikiri tuna uhuru wa kupanga na kuchagua,”alisisitiza.
Alisema amemualika Lowassa kumshukuru
kwa kumpokea bila miadi, kumsikiliza wakati akiwa Waziri Mkuu mwaka 2007
na kutatua msigano wa ardhi ya Two Biharamulo iliyokabidhiwa na jeshi
kwa askofu mtangulizi wake mwaka 1996.
Alisema alimuagiza Waziri wa Ardhi
kipindi hicho Dk. John Magufuli, kulitatua na jimbo likapewa ardhi yake
na sasa jimbo lina hati ya kumiliki ardhi hiyo hata kama ilipunguzwa
kiasi.
Akizungumzia vijana, elimu na ajira
alimwambia Lowassa:“Ujue kuwa tuko pamoja na wewe ndiwe mwasisi wa shule
za kata, sasa zina wanafunzi wengi sana, lakini wanapomaliza kidato cha
nne wengi wao wanarudi vijijini na wanajikuta hawana ajira, hali hii
inawatesa sana na wana hasira.”
Akizungumza, Lowassa aliwaomba
kuendelea kumuombea kwa sala na maombi ili Mungu akijalia katika safari
yake ya matumaini kazi ya kwanza iwe ni kuunda chombo maalum cha elimu
kwa kushirikisha wadau na wataalam.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, anakusudia kuanzisha Wizara ya Mafuta na Gesi, ikiwa ni vipaumbele vyake akichaguliwa kuiongoza Zanzibar.
Hamad ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar, ambaye CUF imemteua kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar
kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, ameeleza hayo jana.
Sambamba na hilo aliahidi kuwa endapo
atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atahakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na
shirika la ndege ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ili kurahisisha
safari na shughuli za kibiashara ikiwamo utalii.
Aliahidi kuitangaza Zanzibar kuwa
bandari huru, sambamba na kujenga bandari mpya itakayotoa huduma bora
kwa mwambao wa Afrika Mashariki.
Alisema Zanzibar inazo fursa nyingi za
kuweza kunyanyua kipato cha wananchi na kwamba ataweka kipaumbele katika
kuziibua na kuziendeleza.
Alisema katika kujenga mazingira bora ya
uwekezaji, ataisimamia ipasavyo mamlaka ya vitega uchumi ili kuondosha
vizingiti vinavyokwamisha uwekezaji.
Alifahamisha kuwa wapo wafanyabiashara
wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwekeza miradi mikubwa ya
kiuchumi, lakini wamekwamishwa jambo ambalo ameahidi kulishughulikia
mara akiingia madarakani.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipumba,
alisema Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeshawishika kumuidhinisha Hamad
kuwa mgombea urais wa Zanzibar, kutokana na uwezo na nia ya dhati ya
kuwatumikia Wazanzibari.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete
ameendelea kuaga Watanzania kila anapopata fursa ya kukutana nao, huku
mafanikio ya miaka kumi ya uongozi wake yakijidhihirisha katika maeneo
mbalimbali, ikiwemo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ambako Bajeti ya Serikali kupitia wizara mbalimbali imekuwa ikijadiliwa
na kupitishwa.
Mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini
Stockholm nchini Sweden alikokwenda kwa ziara ya siku tatu, ambayo pia
ni ya kwanza ya kuaga nchi wahisani, Rais Kikwete alikutana na
Watanzania waishio nchini humo, ambako kabla ya kuwaaga, alielezea
changamoto anazoziacha.
Rais Kikwete katika mazungumzo hayo,
amesema Rais ajaye anakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha Tanzania
inayoundwa na Muungano wa nchi mbili, inaendelea kuwa moja kwa kudumisha
umoja wa Watanzania na amani.
“Hapa
tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama na
makabila mbalimbali, lakini lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,” Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alielezea matumaini
yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo
Serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na
Rais ajaye.
Uchumi Awali akizungumzia mafanikio
yaliyopatikana katika uchumi alipokutana na Waziri Mkuu wa Sweden,
Stefan Lofven, Rais Kikwete alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa
wastani wa asilimia 7, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Mbali na kukua kwa uchumi wastani, pato
la Taifa limekua kwa zaidi ya mara tatu, kutoka Dola za Kimarekani
bilioni 14.4 hadi kufikia Dola bilioni 49.2 za Marekani.
Aidha, pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka
2005, wakati Rais Kikwete alipokuwa akiingia madarakani lilikuwa Dola
za Marekani 375, lakini mwaka jana lilifikia Dola za Marekani 1,038.
Mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa ya
Ikulu, zilisababisha Waziri Mkuu wa Sweden, Lofven, kuona umuhimu wa
kuanzisha awamu nyingine ya uhusiano katika maendeleo, utakaoleta maana
zaidi.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa
akizungumzia kasi ya kuondoa umasikini, alisema bado juhudi za kuondosha
umaskini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye
kilimo, ambacho ndicho kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi
zaidi hasa wanaoishi vijijini.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hpa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment