Tuesday, June 2, 2015

WAKAZI WA KIVULENI KATA YA KIOMONI TANGA WAONYESHA NJIA


Tangakumekuchablog

Tanga,WAKAZI wa kijiji cha Kivuleni kata ya Kiomoni halmashauri ya jiji la Tanga, wamechangia zaidi ya shilingi milioni ishirini kwa ujenzi wa  kituo cha afya ili kuondokana na kero ya kufuata matibabu masafa ya umbali zaidi ya kilometa 15.

Wakizungumza  na waandishi wa habari mapema leo, wakati wa hatua za awali za ujenzi wa kituo hicho, walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya kufuata matibabu ambapo baadhi ya wakati wanawake wajawaziti hujifungua njiani.

Walisema kituo hicho mara baada ya kukamilika kwake itakuwa msaada kwa wakazi wengi wakiwemo wa vijiji vya jirani ambapo mbali ya masafa hayo wamekuwa wakikumbana na adha ya miundombinu mibovu ya barabara .

“Kwanza tunamshukuru diwani wetu kwa kujitolea eneo lake kujengwa kituo cha afya na ndio sisi tukashawishika kuchanga pesa tuanze ujenzi----tunaimani ndani ya mwaka mmoja huduma itaanza” alisema Rehema Hassan

“Wahanga wakubwa wa mambo ya afya ni wanawake wajawazito na wazee na mara nyingi wanawake wakati wanapotaka kujifungua hupata shida baada ya miundombinu ya barabara mibovu na wengine hujifungulia njiani” alisema

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Kauli Makame, amewataka wananchi kuendeleza na moyo wao wa kuchangia na wa kujitolea hadi kituo hicho kitakaposimama na kutoa ahadi ya kuwa nao bega kwa bega.

Alisema wakati wa vikao vya mabaraza ya Udiwani amekuwa akilipigia kelele kero ya wananchi wa kata hiyo kwa kukosa huduma ya matibabu jambo ambalo hufuata matibabu masafa marefu.

“Kwa kuona kero ya wananchi wangu na mimi mwenyewe kama diwani nimetoa eneo langu ili kujengwa kituo----nimelitoa kabla ya kuwa diwani hii ni kuonyesha kuwa nimeguswa na kero za wananchi wenzangu” alisema  Makame

“Kwa jitihada zangu na za viongozi wenzangu leo tumeanza kwa kulisafisha eneo ambalo tutajenga kituo na kesho tutaanza kulipima ili kuanza ujenzi mara moja kwa pesa za wananchi ambazo wamechanga wao wenyewe” alisema

Aliwataka wananchi hao kuendeleza moyo wao wa kujitolea hadi ambapo kituo hicho kitakaposimama na kuahidi kuwa nao bega kwa bega hadi kitakapokamilika na kuahidi kusaidia kila ambapo kutahitajika msaada.

                                           Mwisho

 Katapila likisafisha eneo ambalo kitajengwa kituo cha afya kijiji cha Kivuleni kata ya Kiomoni halmashauri ya jiji la Tanga  baada ya kukusanya zaidi ya shilingi milioni 21 kwa nguvu zao. Eneo hilo limetolewa na Diwani kaya ya Kiomoni , Kauli Makame ikiwa ni jitihada za kuondosha kero ya kufuata huduma za matibabu zaidi ya kilometa 15 kutoka kijijini hapo.




No comments:

Post a Comment