Tuesday, June 2, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOJIRI MAGAZETI YA LEO, JUNE 02 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisni kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

HAYAA

MWANANCHI
Hamasa ya wanaCCM kutangaza nia ya kuwania urais imemwibua mwanafunzi Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Maliki Malupu (34).
Malupu alitangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM akiahidi kushughulikia suala la elimu, afya, kilimo na michezo huku akijua kuwa umri wake haujatimia miaka 40 inayotakiwa kikatiba.
Akitangaza nia hiyo mjini Morogoro jana, Malupu alisema kutokana na uaminifu na uadilifu wake, ameamua kuwania nafasi hiyo pamoja na mambo mengine kwa kuwa ni haki yake kikatiba.
Alipoulizwa atatimizaje nia yake hiyo bila kuwa na sifa kikatiba, alisema vifungu vya katiba vinavyotaja umri vina utata, hivyo ameamua kuingia kuvitafutia suluhisho.
“Unajua ibara ya 39 (1) (b) inasema lazima utimize miaka 40, lakini ibara (d) inasema mtu mwenye sifa za kuwa mbunge au mjumbe wa baraza la wawakilishi anaweza kuwania urais,” alisema akifafanua kuwa yeye ana sifa hizo.
Akieleza sababu nyingine zilizomsukuma kuwania urais, Malupu alisema kuwa ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa kikamilifu kwa kuwa muda mrefu imekuwa ikichezewa na baadhi ya viongozi.
Alisema muundo wa sekta hiyo unapaswa kurekebishwa kwa ama kufutwa au kuondoshwa utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu wa GPA kwa wanafunzi wa elimu ya sekondari katika mitihani ya kidato cha sita na cha nne.
Alisema utaratibu huo haufai kwa kuwa hautoi matokeo ya kuboresha maarifa kwa wanafunzi, pia unawaathiri wanafunzi kisaikolojia katika kujitofautisha wao na wanafunzi wa elimu ya juu.
“Nitahakikisha naboresha mitalaa kwa masomo ya kidato cha nne na cha sita ili kuleta weledi wa kina na wa kutosha, nitaboresha mazingira ya watumishi sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na stahiki za walimu wa msingi hadi vyuo,” alisema.
Katika mkutano wake wa saa 1.30, Malupu alisema atahakikisha anadhibiti suala la maprofesa kuacha kazi yao ya weledi na kukimbilia katika siasa na ataboresha stahiki zao na mishahara kwa kuwalipa vizuri wanaofundisha vyuo vya Serikali na binafsi bila ubaguzi wowote ili kuimarisha sekta ya elimu ngazi vyuo vikuu.
Malupu alisema ataitazama sekta ya kilimo kwa kuongeza vyuo vikuu vya kilimo ili kuleta tija ya kilimo katika sekta hiyo na Serikali yake itakuwa na mkakati mahsusi wa kutoa elimu na mitaji kwa wakulima wanaofanya kilimo chenye tija na kilimo cha kujikimu. Katika afya, Malupu alisema kuwa atahakikisha suala la afya linasimamiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja kuwapatia wazee huduma bure na kwamba zahanati, vituo vya afya na hospitali zinapatiwa vifaatiba vya kutosha ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.
Malupu pia alizungumzia wananchi wanaoishi katika visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza na Mafia mkoani Pwani kuwa wamesahaulika, hivyo akiteuliwa na baadaye kuchaguliwa atahakikisha anakifanya kisiwa cha Ukerewe kuwa mkoa unaojitegemea ili kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma Mwanza.
MWANANCHI
 Katibu Mkuu wa Chadema, Dk  Willibrod Slaa amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), mwaka huu, unaingia kwenye uchaguzi ukiwa na safari ya uhakika na siyo ya matumaini kama ilivyotolewa na mmoja wa watangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Dk Slaa alisema, kauli hiyo ni moja kati ya nyingi zinazotolewa na viongozi wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo Watanzania wamechoka kuzisikia na badala yake wanahitaji vitendo.
Alitoa kauli hiyo juzi mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya, alipokuwa akihutubia wakazi wa mji huyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.
Dk Slaa alisema Watanzania wanahitaji safari yenye uhakika wa maendeleo ambayo watayapata Oktoba, mwaka huu, kupitia upinzani lakini siyo  kutoka kwa kiongozi yeyote wa CCM.
“Eti safari ya matumaini, hivi kweli Tanzania iliyojaa kila aina ya madini na utajiri wa kutisha halafu tunasema safari ya matumaini badala ya vitendo? Watanzania tumechoka na kauli za matumaini, tumechoka kuishi kwa matumaini katika nchi yetu,” alisema Dk Slaa.
Mbali na hilo, Dk Slaa  aliwashangaa baadhi ya watangaza nia wa CCM walioiponda Serikali yao kwamba imeshindwa wakati wao ndio walitakiwa kuwa mstari wa mbele kuondoa kero hizo.
Ukawa wajipanga
Akizungumza kuhusu Ukawa walivyojipanga kuingia Ikulu Oktoba mwaka huu, Dk Slaa alisema wana akiba ya kutosha ya viongozi makini wa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Alisema wakishika dola hawatakuwa na sababu yoyote ya kukopa viongozi kutoka kwa CCM.
“Hatuna njaa ya viongozi ndani ya upinzani, tunao wa kutosha. Hatuna haja ya kwenda CCM kuwakopa viongozi, Oktoba tupeni ridhaa upinzani tubadili sura ya nchi,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alisema, licha ya Serikali ya CCM kuamua kugawa majimbo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujiokoa, hawataambulia kitu kwani wamejipanga kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.
“CCM tumewagundua na janja yao, baada ya kuona wabunge wao wamekabwa koo, ndio wanatafuta njia mbadala ya kujiokoa kwa kugawa majimbo, lakini tunasema majimbo yote yaliyopendekezwa kugawanywa Mbeya kama yatapitishwa tunachukua yote,” alisema Silinde.
MTANZANIA
MBIO za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio hizo.
MAKONGORO
Akitangaza nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama jana, Makongoro aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama hicho, Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuendesha makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha juu kwa fedha.
CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho, alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi katika misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni kibaka tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele atabaki kuwa kibaka tu.
“Wananijua vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo wanaotuvurugia chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,” alisema Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM.
Alisema baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na mipasuko isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
“Vibaka waturudishie CCM yetu, watambue wao ni wachache na sisi wazalendo ni wengi, hawatushindi na fedha zao na kitaeleweka tu.
“Leo hii viongozi wetu wa CCM wamekuwa ni watu wa kuendeshwa na vibaka hawa wanahongwa fedha ovyo…wao wana mifugo yao ndani ya NEC basi mimi sijafuga hata kuku, nasema kitaweleweka,” alisema Makongoro.
Alisema yeye hawezi kufanya hivyo kwa sababu rasimu ya ilani ya chama hicho bado haijapitishwa na chama, hofu yake ni kwamba anaweza kutoa ahadi na zikawa kinyuume na ilani ya chama chake.
“Nimewasikia wanajinadi,nawashangaa sana, najiuliza kwani wao ni akina nani watoe ahadi kabla ya ilani ya chama? Ikitokea ahadi yako ikaenda kinyume na ilani si ndiyo mwanzo wa kuwa na rais muongo…sitaki kuwa rais muongo nitaheshimu chama changu kwa kila mchakato na maelekezo,” alisema Makongoro.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu aliyeiomba kazi hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai kukukuongoza maana hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili ajinufaishe,” alisema Makongoro.
Wanawake wananipenda
Makongoro alisema anakerwa na siasa chafu dhidi yake zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya CCM.
Alizitaja siasa hizo kuwa ni tuhuma za kulaaniwa na baba yake, ulevi na mtu anayependa wanawake.
Akijibu tuhuma hizo, Makongoro alihoji umati uliomiminika kumsikiliza kwamba, “jamani naonekana nimelaaniwa? Naelekea kuokota makopo? Jamani mnanionaje, naonekana mlevi? na umati ulikataa kwa kusema, “hapana”.
“Eti wanasema Makongoro anapenda wanawake sasa wanataka nipende wanaume? Wanawake wananipenda na mimi nawapenda, hizi siasa chafu wanazonituhumu hazinisumbuilangu ni moja tu vibaka rudisheni nchi yetu,” alisema.
MTANZANIA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ametegua kitendawili kuhusu hatima ya madai ya wananchi katika mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.
Lukuvi amesema kutokana na hali hiyo kuanzia sasa kila mwananchi mwenye kiwanja au nyumba yake atalazimika kuuza kiwanja chake kwa bei anayoitaka au kujenga nyumba kwa mujibu wa ramani ya mji mpya
Akizungumza na wananchi hao juzi katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam, Lukuvi, alisema sintofahamu iliyokuwapo ilitokana na hapo awali wananchi kutowekwa wazi kuhusu mchakato wa uuzaji wa maeneo yao.
“Wananchi wamekuwa katika sintofahamu juu ya uuzaji wa maeneo yao, wengine mnafikiri Serikali ndiyo itakayonunua ardhi yenu na wengine mnafikiri ardhi inadalaliwa na Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni (KDA),” alisema Lukuvi na kuongeza;
“Hakuna Serikali itakayouza ardhi wala KDA kudalalia ardhi yenu…wananchi wa Kigamboni ndiyo mtakaoamua juu ya uuzaji wa ardhi yenu na serikali itakuwa mwangalizi ili wananchi wasiibiwe kwa kuuza bei ya chini sana,” alisema Lukuvi huku umati huo ukimshangilia.
Alisema wananchi wanachotakiwa ni kuchagua mambo matatu katika mpango huo ambayo ni kuuza ardhi yao wenyewe moja kwa moja kwa wawekezaji, kuingia ubia na wawekezaji na kutafuta fedha za kujenga wenyewe.
Alisema kama mwananchi ataamua kujenga mwenyewe atatakiwa kufuata ramani na mpango wa mji mpya unavyoonyesha.
“Mtu anaweza kuamua kujenga mwenyewe lakini si kwamba unaamua kujenga unachotaka bali utajenga kilichopo kwenye mpango, haiwezekani eneo la kujenga majengo makubwa ya biashara wewe ujenge choo,” alisema Lukuvi.
Alisema ili kuhakikisha wananchi wanatekeleza mambo hayo matatu ni lazima wapatiwe hatimiliki za maeneo yao suala ambalo awali halikuwapo kwa madai kuwa hakuna haja ya kutoa hati kwa eneo ambalo tayari lipo kwenye mpango.
“Katika suala la kutoa hati nilipingana na watu wa Mipango Miji na nikawaambia lazima wananchi wapewe hati zao ili wakati wa kufanya makubaliano na wawekezaji wawe na ushahidi wa kumiliki ardhi hiyo,” alisema Lukuvi.
MTANZANIA
KAMBI Rasmi ya Upinzani bungeni imesema Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiba sera yake ya elimu inayozungumzia elimu bure kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.
Mbali na hilo, wapinzani wameonya makada wa chama hicho wanaotangaza nia ya kuwania urais kuacha kutumia sera hiyo ya upinzani kwa sababu walikuwa Serikalini tangu uhuru na wameshindwa kufanya hivyo.
Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo bungeni jana kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Msemaji Mkuu kwa kambi hiyo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo, alisema elimu haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za CCM kwa awamu zote za utawala wake na ndiyo maana imeshindwa kutekeleza hata Ilani yake ya uchaguzi.
“Sera ambayo CCM imepigia upatu kwa miaka yote 53 ya uhuru na ambayo pia imeshindwa kutekeleza ni kilimo, ndiyo maana tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere sera zilizosikika ni Siasa ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa na sasa Kilimo Kwanza. Hatujawahi kusikia elimu kwanza kwa utawala wa CCM kwa miaka yote 53 ya Uhuru,” alisema.
Suzan ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) alisema sera ya elimu kwanza ni ya upinzani na kwamba ipo katika ilani ya uchaguzi ya Chadema ya mwaka 2005 na 2010 na imepewa kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu.
“Itakumbukwa kwamba Chadema iliposema elimu bure kama ingechaguliwa kuunda serikali mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda chafu ya kuwapotosha wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure.
“Lakini ili kuthibitisha ile methali isamayo kwamba njia ya muongo ni fupi, CCM hivi sasa imekubali kula matapishi yake na kusema katika kipengele cha 3.1.5 cha sera mpya ya elimu ya mwaka 2014 kwamba elimu itakuwa bure,” alisema na kuongeza:
“Huu ni uthibitisho kuwa CCM imebobea katika wizi hadi kufikia hatua ya kuiba sera ya upinzani waziwazi bila aibu. Ukawa ikitwaa madaraka ya dola katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu itakuwa bure.”
Sera mpya ya elimu
Kuhusu sera mpya ya elimu, alisema imekuwa hazitekelezeki kwa kuwa ni sera bainishi na imekuwa ikibainisha upungufu pekee na kuacha sehemu ya utekezaji.
Alisema ili sera hiyo iweze kutekelezeka ni lazima kuwapo na walimu bora, zana bora za kufundishia na walimu wenye motisha.
“Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuandika vizuri sera zake, lakini utekelezaji wake ni shida. Mfano sera hii haielezi ni kwa kiasi gani itaondoa ubaguzi au matabaka ya elimu hasa viwango vya elimu. Pia haielezi nini maana ya kufuta ada ikiwa kuna michango mingi kuliko ada yenyewe,” alisema.
Dk. Kawambwa
Awali akiwasilisha hotuba yake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imetekelezwa.
Alisema sekta ya elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mikakati hiyo.
Dk. Kawambwa aliainisha vipaumbele vya sekta ya elimu vilivyomo katika mwongozo wa taifa wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2015/2016 kuwa ni
pamoja na kuongeza upatikanaji wa fursa ya elimu kwa usawa katika ngazi zote za elimu na mafunzo, kuinua ubora wa elimu na kujenga stadi stahiki, kuimarisha taasisi za usimamizi wa ubora wa elimu na ufuatiliaji na tathmini ili zitekeleze majukumu yake.
NIPASHE
Mbunge wa Vunjo (TLP), (pichani), amemshukia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdularhman Kinana, kwamba anamchonganisha na wapiga kura wake kwa  kudai kuwa serikali imetoa Sh. milioni 400 katika jimbo hilo kupitia Mfuko wa Jimbo wakati siyo kweli.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2015/16 bungeni jana, Mrema alisema ni jambo la kushangaza kwa Kinana kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kumchonganisha na wapiga kura wake, ili CCM ijijengee mazingira mazuri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“CCM kwanini mnaanza kushiriki uongo, mnataka kunichonganisha kwa wapiga kura wangu ili kuning’oa Vunjo, nawahakikishia CCM hang’oki mtu Vunjo, hizo Sh. milioni 400 hazijaletwa jimboni kwangu labda mmepeleka kwa wabunge wa CCM,” alisema.
Mrema alisema mbinu zinazofanywa na CCM kumshambulia katika jimbo lake kama mpira wa kona haziwezi kuzaa matunda.
HABARILEO
SEKTA ya Elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Matokeo ya utekelezaji wa mikakati iliyowekwa na BRN ni kupanda kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (Darasa la Saba) na kupanda ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Sekondari (Kidato cha Nne).
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliyasema hayo bungeni jana wakati alipowasilisha Bajeti ya Mwaka 2015/16.
Dk Kawambwa alisema, “Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka mmoja (2013/14) sekta ya elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mikakati hiyo.”
Aliyajata baadhi ya mafanikio ambayo yamehakikiwa na ‘Presidential Delivery Bureau’ ni kutoa tuzo kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne.
Alisema jumla ya tuzo 3,044 zilitolewa kwa shule zilizopata ufaulu uliotukuka na zile zilizopanda kwa ufaulu ikilinganishwa na mwaka 2013.
Pia alisema walimu 4,103 wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kumudu masomo.
Aidha, alisema ujenzi wa miundombinu ya shule 47 za sekondari kati ya 264 zilizolengwa katika awamu ya kwanza ulikamilika. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule 1,200 katika awamu tatu.
“Madeni ya shilingi 1,852,162,158.21 ya malimbikizo ya mishahara yalilipwa kwa watumishi 916 wa wizara,” aliongeza Dk Kawambwa.
Alisema matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo ni kupanda kwa ufaulu wa darasa la saba kutoka asilimia 50.6 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 56.99 mwaka 2014.
“Na kupanda kwa ufaulu wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Sekondari (Kidato cha Nne) kutoka asilimia 57.09 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 69.76 mwaka 2014,” alieleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Akizungumzia utungaji wa Sera za Elimu, alisema rasimu ya andiko la uanzishwaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu imekamilika, na kuwasilishwa katika mamlaka husika.
Aidha, alisema katika mwaka 2014/15, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitoa mikopo kwa wanafunzi 99,590 wakiwemo 2,117 wa Stashahada ya Elimu ya Ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Alisema Bodi hiyo ilikusanya marejesho ya mikopo kiasi cha Sh 15,978,993,320.04 sawa na asilimia 45.5 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2014/15 na hivyo kufikia Sh 75,575,793,215 sawa na asilimia 45.45 ya Sh 165,008,246,475 za madeni yaliyoiva.
Kuhusu changamoto katika mwaka wa fedha uliopita, ilisema mojawapo ilikuwa ni kulipa madeni ya wazabuni na huduma nyingine sasa yanafikia Sh 45,855,370,632.7.
Alisema kati ya hizo, Sh 25,195,672,974.2 ni deni la wazabuni wa vyuo vya ufundi na Sh 5,148,207,930.00 ni deni la posho za wahadhiri.
Akizungumzia vipaumbele kwa mwaka 2015/16, alisema Wizara itasimamia utungaji na utekelezaji wa Sera za Elimu, ithibati ya shule na udhibiti wa ubora wa elimu.
Kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, alisema itaendelea kuratibu na kusimamia udahili na ukaguzi wa wanafunzi 60,000 ili kufikia lengo la kuwa na wanafunzi 300,000 katika taasisi za elimu ya juu ifikapo mwaka 2016.
Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, alisema itakusanya Sh 51,001,034,808.24 za marejesho ya mikopo iliyotolewa kati ya mwaka 1994/95 na 2014/15.
Kwa habari na matukio na mengi mengineo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment