Tangakumekuchablog
Mlalo, MBUNGE
wa jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi (CCM), ameitaka jamii kuishi kwa upendo na
ushirikiano na kukemea vitendo vya ukatili na migogoro isiyo na tija.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana kufuatia tukio la kukatwa kidole gumba mwelemavu wa ngozi (Albino), Ester
Maganga (69) mkazi wa kijiji cha Bangoi kata ya Pea Mlalo juzi, Shangazi
alisema kitendo hicho kinafaa kulaaniwa na kutoruhusu kutokea tena.
Alisema waliofanya hivyo ni wahuni
ambao wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na kuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia
kama hiyo.
“Tumesikitishwa na wahuni waliomkata
bibi yetu kidole na kutoweka nacho----tukio hili ni la kwanza kutokea kwani
tulikuwa tunayasikia tu kupitia vyombo vya habari” alisema Shangazi na kuongeza
“Nawaomba viongozi wa Serikali na
jeshi la polisi kwa pamoja kuwasaka watu waliofanya kitendo hicho na kukomeshwa
kabisa kwani kimetutia kiwewe---natambua kuwa ni watu wa nje ya hapa” alisema
Shangazi ameitaka jamii kupendana na
kuishi kwa kushirikiana kwa kila jambo na kuacha mitafaruku ambayo haina tija
na kujikita zaidi katika masuala ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu watu kujiunga na
mifuko ya Hifadhi ya jamii, Shangazi
alisema ameitaka mifuko hiyo kufika
katika jimbo lake na kutoa elimu ya upatikanaji wa matibabu bure.
Alisema gharama za matibabu ni kubwa
jambo ambalo kwa kiasi kikubwa inapelekea maisha ya wananchi kuwa magumu siku
hadi siku kutokana na makali ya matibabu.
“Gharama za matibabu ni kubwa sana
kulingana na kipato cha mwananchi kwa siku moja----nitaishawishi mifko ya
hifadhi ya jamii kuja na kutoa elimu ya upatikanaji wa matibabu bure” alisema
Alisema maendeleo yamekuwa yakishuka
siku hadi siku kutokana na pesa nyingi kwenda kwenye matibabu na hivyo kuitaka
mifuko ya hifadhi ya jamii kufika jimboni humo na kutoa elimu kwa makundi
mbalimbali yakiwemo ya wakulima.
Mwisho
No comments:
Post a Comment