Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
Abiria waliotaka kusafiri kwenda
wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, nusura wachapane ngumi wakigombea
foleni ya kukata tiketi katika Kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo (UBT).
Gazeti hili lilishuhudia abiria hao
wakiwa kwenye foleni wakisubiri kukata tiketi katika mabasi ya Kampuni
ya Meridian yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Rombo
mkoani Kilimanjaro.
Katika tukio hilo, baadhi ya abiria
walivuruga utaratibu wa foleni kwa kuwavuka wenzao na kujisogeza mbele
ili wakate tiketi, hali iliyosababisha kutoelewana miongoni mwao, huku
wengine wakitoleana matusi wengine wakitaka kurusha ngumi.
“Msituchanganye bwana, kama vipi hapa
ngumi zitapigwa, sisi tumepanga foleni wao wanataka kujifanya wana
haraka sana wanavuruga foleni kwa kujipeleka mbele,” alisikika dada
mmoja akilalamika huku wakatishaji wa tiketi za kwenda mikoa ya Kanda ya
Ziwa wakichukizwa na hali hiyo wakida inawazuia kufanya kazi zao kwa
uhuru.
Mfanyakazi wa Kampuni ya mabasi ya Osaka
yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Musoma, aliwalaumu
abiria wanaokwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuwa wamekuwa kero
kutokana na kung’ang’ania katika kituo hicho licha ya kuambiwa tiketi za
kwenda katika mikoa hiyo zimekwisha.
“Yani hawa abiria wa Rombo wamekuwa kero
sana, wanatufanya sisi tushindwe kufanya kazi kwani hawaamini kuwa
tiketi zimekwisha wao wanang’ang’ania maofisini tu,” alisisikika
akilalamika.
Abiria mmoja aliyejitambulisha kwa jina
la Elisha Ngowi, alisema kuwa tangu juzi alifika kituoni hapo kwa ajili
ya kukata tiketi kwenda Rombo, lakini mawakala wa basi la Meridian
walimtaka aondoke arudi siku iliyofuata.
Upatikanaji wa tiketi katika kituo hicho
umekuwa kama donda ndugu kwani kila mwaka kuelekea Sikukuu ya Krismasi
watu wengi hutaabika kutokana na usafiri wa kwenda katika maeneo
mbalimbali nchini.
MTANZANIA
Salome Lukumay ambaye ni mke wa
aliyekuwa kachero mkuu wa kitengo cha intelijensia cha Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa (TANAPA), marehemu Emily Kisamo, anashikiliwa na Jeshi
la Polisi Mkoa wa Arusha kwa ajili ya mahojiano.
Mbali na Salome, taarifa zinasema jeshi hilo linawashikilia watu wengine wawili kwa ajili ya mahojiano juu ya kifo cha Kisamo.
Vyanzo mbalimbali vya habari jijini hapa
wakiwamo baadhi ya marafiki wa marehemu Kisamo, waliiambia MTANZANIA
kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, kwamba Salome na watu hao
wawili wanashikiliwa kwa kuwa kuna dalili za wao kuwa na mawasiliano na
kachero huyo kabla hajauawa kwa kuchinjwa.
Kisamo anadaiwa kuuawa Desemba 18, mwaka
huu kwa kuchinjwa na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili kisha mwili
wake kuwekwa ndani ya buti ya gari yake iliyotelekezwa eneo la
Kikwarukwaru, lililopo Kata ya Lemara jijini hapa.
Taarifa za mke huyo wa marehemu
zilionekana kuwa za kweli baada ya MTANZANIA kufika nyumbani kwa
marehemu jana na kukuta waombolezaji wakiwa peke yao bila yeye kuwapo.
Hata MTANZANIA lilipotaka kuonana na mke
huyo wa marehemu, mmoja wa ndugu zake wa karibu alisema hakuwapo
nyumbani tangu mumewe alipouawa wiki iliyopita.
“Tangu jana watu wanakuja msibani kutoa
pole, mama mwenye nyumba hayupo. Taarifa zilizopo zinadai bado
anaendelea kulisaidia Jeshi la Polisi kwenye upelelezi wa mauaji ya muwe
wake,” alisema rafiki wa marehemu akiomba asitajwe jina gazetini kwa
kile alichosema yeye si msemaji wa familia.
Naye msemaji wa familia ya marehemu
Kisamo, Wakili Mwandamizi wa Kujitegemea Colman Ngallo, alisema hana
taarifa za mke wa marehemu kukamatwa.
“Hatuna taarifa yoyote mpaka sasa, polisi wanaendelea na uchunguzi wao,” alisema Wakili Ngallo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Liberatus Sabas, alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo jana, aliwaambia
waandishi wa habari kwamba tukio hilo ni la kesi ya mauaji, hivyo
analazimika kujiridhisha katika utoaji wa taarifa.
Kisamo aliuawa wiki iliyopita na watu
wasiojulikana, na polisi waligundua maiti yake ikiwa ndani ya gari baada
ya kuendesha msako mkali wa kumtafuta.
MTANZANIA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Charles Kitwanga, amepata kigugumizi kuweka hadharani orodha ya majina
ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, licha ya kuliagiza Jeshi la
Polisi limpatie.
Amesema hata akiwa na orodha hiyo,
haitasaidia kukomesha biashara ya dawa za kulevya na badala yake
wameunda mfumo utakaosaidia kudhibiti dawa hizo kuingizwa nchini.
Waziri Kitwanga, alitoa kauli hiyo Dar
es Salaam jana, muda mfupi baada ya kumalizika kikao chake na maofisa
wakuu wa Jeshi la Polisi Makao Makuu kilicholenga kumpatia taarifa na
maelezo ya mambo mbalimbali aliyoagiza, baada ya kufanya ziara ya
kutembelea maeneo mbalimbali ya jeshi hilo wiki iliyopita.
“Mtakumbuka hivi karibuni nilitoa
maelekezo kwa Jeshi la Polisi kunipatia taarifa za mambo mbalimbali na
leo (jana), nimekutana nao, wamenipatia maelezo ya kutosha na
tumejadiliana namna watakavyounda mfumo mzuri wa kuhakikisha dawa za
kulevya haziingii nchini, na hata zile zilizokamatwa zinateketezwa,”
alisema Waziri Kitwanga.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama
amepatiwa orodha hiyo alisema: “Kuwa na orodha haiwezi kusaidia,
tumejadiliana namna ya kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti uingizwaji na
uuzwaji wa dawa za kulevya.
“Mimi sina ‘list’ (orodha) na sijui kama
Rais anayo, nashangaa nyie (waandishi wa habari) mnaandika tu na hata
ningekuwa nayo haisaidii kitu maana hatuwezi kwenda kumkamata mtu na
kumshtaki bila kuwa na ushahidi.”
Itakumbukwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete
katika utawala wake, aliwahi kuuambia umma wa Tanzania kuwa ana orodha
ya wauza dawa za kulevya wakubwa.
Hadi anaondoka madarakani Novemba 5, mwaka huu, hakuwahi kuwataja kwa majina wahusika wakuu wa biashara hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Kitwanga alisema
mfumo wa sasa wa kudhibiti biashara hiyo hautajali hadhi ya mtu, na
kwamba atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kama watu
wengine.
“Mfumo hautajali ni mkubwa, mdogo,
mwembamba au mnene, atakayekamatwa anachukuliwa hatua mara moja bila
kujali cheo chake,” alisema Kitwanga.
Alisema mfumo huo pia umelenga kuzuia vitendo vya kigaidi na wizi katika bandari nchini.
Alisema kikao hicho pia kilizungumzia
suala la ubambikaji wa kesi kwa wananchi, ambapo watahakikisha kabla ya
mashtaka mtu aliyekamatwa anashtakiwa kwa kosa alilokamatwa nalo ni si
vinginevyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP) Ernest Mangu, amekanusha taarifa zilizosambaa kuwa jeshi
hilo limewasimamisha kazi askari 300, baada ya kubainika kughushi vyeti
kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Taarifa hizi hazina ukweli wowote,
tunategemea mtu aliyesambaza atasakwa na atafikishwa mbele ya vyombo vya
sheria,” alisema IGP Mangu.
MTANZANIA
Wakati shinikizo la kimataifa juu ya
hali ya Zanzibar likipamba moto, Rais Dk. John Magufuli, amekutana na
aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu
jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo kwa saa 2.
Hali ya kisiasa ya Zanzibar, tayari
inatajwa kuiathiri Tanzania kwa kusababisha ikose zaidi ya Sh trilioni 1
zilizokuwa zitolewe na Marekani, ikiwa ni sehemu ya fedha za msaada wa
Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).
Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es
Salaam jana, ilisema mazungumzo hayo yametokana na maombi ya Maalim Seif
ya siku nyingi na kuwa yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan.
“Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili
hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu
inayoendelea. Rais Dk. Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein, Maalim Seif na viongozi wote wanaoshiriki katika
mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.
“Rais Magufuli pia amewapongeza na
kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu, wakati
mazungumzo baina ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), yakiendelea huko Zanzibar,” ilisema taarifa ya Ikulu.
Taarifa hiyo, ilisema Maalim Seif
amemweleza Dk. Magufuli juu ya hali ya siasa Zanzibar, huku kiongozi
huyo wa Jamhuri ya Muungano akimshukuru kwa taarifa yake aliyosema ni
nzuri na akamsihi waendelee na mazungumzo hadi mwafaka upatikane.
Ilisema majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya Tanzania.
“Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi
waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea
kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF
haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo,” ilisema taarifa hiyo.
Maalim Seif pia amekutana takribani mara saba na Dk. Shein, huku mazungumzo yao yakiwa ni siri kubwa.
Baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi visiwani humo, Serikali ya
Uingereza na ile ya Ireland Kaskazini zilipinga uamuzi huo.
Serikali hizo zilisema hazioni sababu ya
kufutwa matokeo hayo, baada ya waangalizi wa kimataifa kufurahishwa na
uchaguzi ulivyofanyika kwa amani.
HABARILEO
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea
kutamba katika chaguzi ndogo baada ya kushinda katika Jimbo la Masasi
mkoani Mtwara huku ikiwa na kila dalili ya kutangazwa mshindi Ludewa
mkoani Njombe.
Katika chaguzi saba zilizofanyika baada
ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, CCM imezoa viti sita huku
kimoja cha Kijitoupele mjini Unguja kikisubiri tarehe mpya ya uchaguzi.
CCM imeshinda katika majimbo ya Lushoto,
Handeni Mjini, Lulindi, Ulanga Mashariki, Masasi na Ludewa ambayo
ingawa matokeo rasmi yalikuwa hayajatangazwa wakati tukienda mitamboni,
lakini CCM ilikuwa ikiongoza kata 20 na zilikuwa zimebaki kata sita.
CCM imepoteza tena Jimbo la Arusha
Mjini. Mgombea ubunge Jimbo la Masasi kupitia CCM, Rashid Chuachua
ameibuka kidedea kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo mdogo juzi kwa
kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Uchaguzi huo mdogo wa ubunge ulifanyika
kutokana na kushindwa kufanyika Oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa
jimbo hilo wa chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi kufariki dunia Oktoba
15, mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi
kutokana na tatizo la shinikizo la damu.
Akitangaza matokeo hayo usiku wa kuamkia
jana, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Masasi ambaye pia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Fortunatus Kagoro alisema
wananchi 60,598 waliandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,
huku Chuachua akipata kura 16,597 na mpinzani wake wa karibu kutoka CUF,
Ismail Makombe (Kundambanda) akipata kura 14,069.
Wagombea wengine ni Mustapha Swalehe wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipata kura 512, Dk Peter
Mrope wa ACT- Wazalendo kura 347 huku mgombea wa NLD akiambulia kura 70
pekee.
Wakala wa CUF ambaye ni Mbunge wa Jimbo
la Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma alisema mgombea wao ameshindwa kwa kura
na kwamba Tume ya Uchaguzi imetenda haki kwa kuendesha uchaguzi wa
uwazi na ukweli kuanzia kwenye vituo vya upigaji kura hadi kwenye
majumuisho ya matokeo.
Katika Jimbo la Ludewa, mgombea wa CCM,
Deo Ngalawa amewaacha kwa mbali wagombea wengine katika matokeo ya kata
20 zilizokuwa matokeo yake yamepatikana.
HABARILEO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hana
kinyongo na mtu yeyote kwa sababu alitangaza msamaha siku
aliyokabidhiwa cheti kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na kusisitiza kuwa
siasa ziliisha tangu Oktoba 25, mwaka huu.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati
akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani
Ruangwa mkoani Lindi. “Sina kinyongo na mtu yeyote na roho yangu iko
huru, hivi ndiyo nilivyo.
Nilikwishatangaza msamaha kwa hiyo
ninawaomba wale niliowakwaza nao pia wanisamehe… lakini ninawasihi kuwa
milango iko wazi, wawe huru kurudi wakati wowote,” alisema huku
akishangiliwa na wananchi hao.
Aliwaeleza wakazi hao wa Ruangwa na
vitongoji vyake kwamba amekuja kuwashukuru kwa kumchagua na kumpa kura
nyingi la sivyo asingefanikiwa kuwa mbunge wao. “Kipekee ninamshukuru
Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais na kutupa sisi wana Ruangwa
tusaidiane kulibeba jukumu hili.
Ninawahakikishia kuwa pamoja na jukumu
hili la kitaifa, sitawaacha wala sitawaangusha. Nitakwenda mikoa mingine
hapa nchini ili kuwasikiliza na kuwahudumia Watanzania huku nikijua
kwamba mpo salama.”
HABARILEO
Rais Paul Kagame wa Rwanda amefurahishwa
na hatua ambazo Rais John Magufuli anazichukua, hasa katika usimamizi
na utendaji kazi wa bandari huku akimhakikishia kuwa Rwanda iko tayari
kushirikiana na Tanzania, hasa katika kuitumia Bandari ya Dar es Salaam.
Siku chache baada ya kuingia madarakani,
Rais Magufuli akimtumia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya
ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako alifichua ufisadi wa
mabilioni ya shilingi kutokana na upotevu wa makontena, ambayuo
hayakulipiwa kodi stahili kwa serikali.
Kutokana na ufisadi huo, Rais aliivunja
Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), alitengua
uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe na kusimamisha maofisa
kadhaa wa bandari hiyo na wengine wanaohusika na usimamizi wa bandari
kavu.
Aidha, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na maofisa wengine wa
mamlaka hiyo, ambao miongoni mwao tayari wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutokana na ubadhirifu
huo.
Kutokana na hilo, Rais Kagame kupitia
kwa Balozi wake nchini, Uegene Kayihura, amempongeza Rais Magufuli kwa
hatua alizochukua kusafisha uozo katika bandari hiyo, ambayo Rwanda
inapitisha asilimia 70 ya mizigo yake. Dk Magufuli jana alikutana na
kufanya mazungumzo na Balozi Kayihura Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Kayihura
aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Kagame ambaye alimpongeza
Dk Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Kayihura, Rais
Kagame amefurahishwa na hatua ambazo Rais Magufuli anazichukua hasa
katika usimamizi na utendaji kazi wa bandari na kumhakikishia kuwa
Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania hasa kuitumia Bandari ya Dar
es salaam ambayo hupitisha asilimia zaidi ya 70 ya mizigo ya Rwanda.
Aliongeza kuwa Rwanda na Tanzania ni
nchi marafiki na majirani, hivyo kuna kila sababu ya kujenga ushirikiano
madhubuti katika sekta ya uchumi. Rais Magufuli alimuomba Balozi
Kayihura, kumfikishia Rais Kagame salamu za shukrani kwa kumpongeza
kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania na kwamba amedhamiria kuimarisha zaidi
ushirikiano na Rwanda.
Alimhakikishia Balozi Kayihura kuwa
Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendelea kushirikiana na Rwanda ili
wananchi wa nchi zote mbili wanufaike kimaendeleo. Katika hatua
nyingine, Dk Magufuli amemhakikishia Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Dk Tonia Kandiero kuwa Serikali yake itaendelea
kushirikiana na benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Dk Magufuli alisema hayo jana Ikulu
jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi
huyo. Pamoja na kumhakikishia ushirikiano, Rais Magufuli alitoa mwito
kwa benki hiyo kupunguza michakato ya kuelekea katika utekelezaji wa
miradi na badala yake ameshauri uwepo utaratibu wa haraka unaowezesha
kuanza kwa miradi katika kipindi kifupi baada ya fedha kutolewa.
Kwa upande wake, Dk Kandiero pamoja na
kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano, amemhakikishia kuwa benki iko
tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ambavyo
imekuwa ikifanya na kwamba kwa sasa imetenga dola bilioni 2.3 kwa ajili
ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema katika mipango yake, ADB
imelenga kujielekeza katika utoaji wa mikopo katika sekta ya nishati na
usafiri. Naye Dk Magufuli aliipongeza ADB kwa kuamua kujielekeza katika
sekta hizo za nishati na usafiri na pia aliisisitiza kuangalia namna
itakavyounga mkono mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
kisasa.
HABARILEO
Serikali imesema itachukua hatua kali
kwa baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za
sekondari, wanaoendelea kutoza fedha za uandikishaji wa wanafunzi wa
darasa la kwanza na kutoza michango mbalimbali kwa wazazi kwa muhula
unaoanzia Januari 2016.
Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali
imekwishatenga kiasi cha Sh bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji
wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni mwakani, huku akionya kuwa
atakayezitumia vibaya, atatumbuliwa jipu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Stella Manyanya alisema wamepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa elimu
kwamba kuna baadhi ya shule bado zinatoza michango.
“Wanaofanya hivi wanakiuka maagizo ya
serikali kwa makusudi, ikumbukwe kwamba Rais Dk John Magufuli
alikwishatamka wazi kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2016, elimu itatolewa
bure bila malipo kwa shule zote za umma nchini. Agizo hilo liko wazi na
halina mjadala,” alisema Manyanya.
Alisema kutokana na tamko hilo, wizara
ilitoa Waraka Namba Tano wa Mwaka 2015 kuhusu utoaji wa elimu pasipo
malipo na Waraka Namba Sita wa Mwaka 2015 uliotoa ufafanuzi na maelekezo
ya utekelezaji wa jambo hilo.
“Nasisitiza wakuu wa wilaya na
wakurugenzi wa halmashauri wa wilaya, miji na manispaa zote nchini
wafuatilie kwa karibu utekelezaji wa maagizo haya. Aidha watoe taarifa
pale ambapo walimu wakuu na wakuu wa shule wanakwenda kinyume ili hatua
stahiki zichukuliwe mara moja,” alifafanua Naibu Waziri.
Pia alitoa mwito kwa jamii kutoa
ushirikiano kwa kutoa taarifa katika ofisi za elimu za Kata, Wilaya,
Mkoa, Kanda au Makao Makuu ya wizara pale wanapobaini kuna shule
zinazokiuka maagizo hayo. Katika hatua nyingine, Manyanya alisema
serikali itaendelea na utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wote hasa wale
wanaotoka kwenye familia duni na yatima waliotimiza vigezo.
“Nasisitiza wanafunzi wote waliopatiwa
mikopo waitumie vizuri ili iweze kuleta tija ili wanafunzi wanaonufaika
waweze kujisaidia wao wenyewe, familia zao na waweze kuchangia maendeleo
ya nchi,” alisema na kuongeza kuwa watachukua hatua kwa vyuo vikuu
vitakavyobainika kuchelewesha mikopo kwa wanafunzi wake baada ya
kuipokea kutoka Bodi ya Mikopo kwani ni kinyume cha maagizo ya Rais na
linaleta usumbufu usio wa lazima.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akiwa mjini Ruangwa juzi, alisema; “Kazi ya utumbuaji majipu
imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugharimia elimu ya bure,
ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa
kampeni.
Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza
kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari 2016 watoto
waanze kufaidika.” “Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni
lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo wakurugenzi wa halmashauri
pamoja na maafisa elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,”
alisema.
“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela
ya mitihani, na zile shilingi 10,000 kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma
sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao
haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika
kuziombea kibali,” alisema.
Alisema Serikali imekwishafanya hesabu
za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa
wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa
tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa.
“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na
sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi
tutaitekeleza.” Imeandikwa na Hellen Mlacky, Dar na Mwandishi Maalumu,
Ruangwa.
MWANANCHI
Kasi ya Rais John Magufuli kuitaka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewalazimu kufuta likizo kwa
wafanyakazi wake wote ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa
kiwango cha juu.
Wakati uongozi wa mamlaka hiyo ukifuta
likizo hizo, tayari Rais Magufuli ameipongeza kwa kukusanya mapato ya
zaidi ya Sh1.3 trilioni mwezi huu.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, Richard Kayombo alisema lengo ni kuhakikisha kuwa mapato zaidi yanakusanywa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kufutwa kwa
likizo hizo kutokana na mtikisiko ulioikumba mamlaka hiyo ukiwamo wa
kuibuliwa kwa ufisadi katika ukusanyaji wa mapato uliosababisha
watumishi 35 kuchukuliwa hatua mbalimbali, wanane kati yao wakifikishwa
mahakamani akiwamo Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Wafanyakazi wa TRA wataungana na wenzao
wa Tanesco ambao pia likizo zao zilifutwa na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa lengo la kushughulikia tatizo la
umeme nchini huku akisisitiza kuwa hataki kusikia kukatika katika kwa
nishati hiyo nchini.
Mkoani Kilimanjaro nako, mkuu wa mkoa
huo, Amos Makalla alipiga marufuku likizo za wakuu wa wilaya,
wakurugenzi na wakuu wa idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza kwa
vitendo hotuba na maagizo ya Rais Magufuli. Msimamo wa Tucta.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam Desemba 2, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi (Tucta), Hezron Kaaya alitaka ieleweke kuwa likizo ni haki
ya mfanyakazi na kama kuna mwajiri anataka kuzuia likizo hiyo, anapaswa
kufanya majadiliano na mwajiriwa ili wakubaliane kulingana na taratibu
za sheria zilizopo.
MWANANCHI
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo amesema ataanza kuwatimua wafanyakazi wazembe, wavivu
na wasiokuwa na tija kwenye Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika
muda wa siku 90 zijazo.
Pamoja na kuwataka watendaji wake kwenda
na kasi yake ili asiwepo atakayeshindwa hivyo kulazimika kuachia ngazi,
Profesa Muhongo ametoa maagizo matatu kwa Tanesco.
Akizungumza juzi katika Kituo cha
Somanga, Lindi wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tano ya
kutembelea vituo vya kuzalisha umeme kuanzia Hale mkoani Tanga, Nyumba
ya Mungu mkoani Kilimanjaro Mtera (Dodoma), Kihansi (Iringa), Kidatu
(Morogoro), Mamlaka ya Bodi ya Maji ya Mto Rufiji (Rubada), Somanga
(Lindi) na mitambo ya gesi ya Madimba ya kuchakata gesi mkoani Mtwara,
Profesa Muhongo alisema: “Siko tayari kubaki na wazembe.
Afadhali nibaki na watumishi wachache
wanaojituma. Sasa ifikapo Februari mwakani, mfanyakazi atakayebainika
kashindwa kwenda na kasi yangu atalazimika kuitema nafasi ili ichukuliwe
na vijana.
Maagizo matatu Akiwa Somanga Profesa
Muhongo aliamuru Tanesco kuwasha mashine zote zilizokuwa zimezimwa kwa
ajili ya dharura ili zipeleke umeme katika maeneo yenye uhaba akisema
wizara yake imedhamiria kumaliza tatizo hilo. Agizo hilo lilitolewa
baada ya kupewa taarifa na Meneja wa Somanga, Mhandisi Job Leonard kuwa
kati ya mashine tatu za kituo hicho, moja ndiyo inafanya kazi, ya pili
imepumzishwa; ya tatu inasubiri kufanyiwa matengenezo mwakani.
“Kila mara nawaambia Tanesco mmekosa
ubunifu, mnajifanya mnabana matumizi huku Watanzania wanalalamikia
umeme. Endapo mngewasha mashine iliyobaki si ingeweza kupeleka umeme
katika gridi ya taifa ili tupunguze adha kwa wananchi?” alisema. “Suala
hili halipo hapa Somanga nimetaarifiwa hadi Biharamulo lipo. Huko nako
nitakwenda kuangalia mitambo iliyowekwa bila kufanya kazi,” alisema
Profesa Muhongo na akataka tatizo la mashine kutowashwa litatuliwe
kuanzia wiki hii na waache visingizio vya kukauka kwa Bwawa la Mtera.
Agizo jingine alilolitoa ni kwa wakulima wenye mashamba makubwa
kufungiwa maji ili yaelekezwe katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Agizo hilo linatarajiwa kuathiri
mashamba makubwa ya mpunga ya wawekezaji wa Kapunga na Mbarali, na
wakulima wadogo wadogo wa Madibira.
Shamba la Kapunga linachukua asilimia 70
ya maji ya Mto Ruaha na Mbarali limechukua maji ya Mto Balali wakati
Madibira wanatumia maji ya Mto Lyandembela, mito ambayo hutiririsha maji
katika Bwawa la Mtera.
Katika agizo la tatu, Profesa Muhongo
ametaka Tanesco na Shirika la Mandeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukaa
pamoja kujadiliana namna ya kumpatia umeme mwekezaji wa kiwanda cha
saruji, Alhaji Aliko Dangote.
Alisema kiwanda hicho kimeshaanza
uzalishaji wa sarujii lakini kimelazimika kukodi mitambo nje kwa ajili
ya kuzalisha umeme, mbali na kuwa na mitambo inayohitaji gesi asilia na
makaa ya mawe ili kujizalishia umeme wa megawati 75. “Wakipatiwa makaa
ya mawe au gesi watazalisha megawati 75, ambazo wataipa Tanesco 35 na
wao kubaki na 45 kama wanavyohitaji,” alisema Profesa
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment