Friday, December 18, 2015

UCHAMBUZI WA MAGAZETI NA CANDLE EDUCATION CENTRE TANGA

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita, Candle inaendelea kupokea wanafunzi wanaojiandaa na masomo ya Form 1 hadi Form Six, Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema afya yake ni njema na anaendelea na majukumu yake ya kila siku kama kawaida.
Amesema hivi sasa yuko India alikokwenda kufanya uchunguzi wa afya yake katika Hospital ya Apollo na kwamba madaktari wake bado wanaendelea kumfanyia uchunguzi wa macho.
Akizungumza  jana kupitia simu yake ya kuganjani kutokea nchini India, Spika Ndugai alizungumzia afya yake, aliondoka nchini Desemba 3, mwaka huu kwenda kuwaona madaktari wake ili kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Alisema, mara ya kwanza alikwenda India mwezi Machi mwaka huu kwa ajili ya uchunguzi wa afya na madaktari walimtaka arejee tena mwezi Septemba lakini alishindwa kutekeleza matakwa hayo ya kitabibu kwa sababu ya kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Spika Ndugai alisema baada ya kumaliza uchaguzi mkuu na mkutano wa kwanza wa Bunge la 11, madaktari wake walimshauri aende kwenye uchunguzi jambo ambalo amelitekeleza.
“Niko ngangari, nadhani unanisikia ninavyoongea. Nimekuja India kwa uchunguzi wa afya yangu kama daktari wangu alivyonitaka lakini majukumu yangu yote muhimu nayatekeleza huku nilipo, kila kitu niko vizuri isipokuwa nimeshauriwa pia nifanyiwe uchunguzi wa macho na huo unaenda taratibu kidogo lakini ukikamilika tu narejea nyumbani na nina hakika sikukuu ya krismass nitaisherehekea nyumbani,” alisema Spika Ndugai.
Akizungumzia taarifa kuwa anasumbuliwa na figo na kwamba kabla hajaondoka kwenda India alianguka baada ya kuishiwa nguvu na kukimbizwa uwanja wa ndege akiwa hajitambui, alisema jambo hilo si la kweli.
“Nimeondoka nikiwa natembea mwenyewe na wasaidizi wangu wa Bunge waulizeni watawaambia hilo. Nimefika hapa India nikiwa na nguvu zangu, nahudhuria uchunguzi kwa mujibu wa ratiba kisha narejea hapa nilipofikia na nimekuwa nikiwatembea Watanzania wenzangu waliolazwa hapa kila mara. Hao wanaoeza uongo huo wana lengo la kupotosha wananchi tu,” alisema Spika Ndugai.
Awali Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Spika Ndugai aliondoka nchini kwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kwamba hali ya afya yake ni njema.
MTANZANIA
Jaji mstaafu Mark Bomani, amesema ili kumaliza dosari zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu kisiwani Zanzibar, njia pekee ni kuunda jopo litakaloweza kumaliza mgogoro uliopo.
Jaji Bomani alisema dosari zinazosemekana zilitokea wakati wa uchaguzi  zinatakiwa zibainike kwa kutumia jopo la wataalamu ambao wanaaminika na ikiwezekana liwe chini ya mmoja wa majaji wakuu wastaafu.
Alisema yaliyotokea Zanzibar ni utata mtupu, hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,  kufuta matokeo ya uchaguzi katika mazingira ya kutatanisha.
Jaji Bomani alisema si vibaya kama ZEC itashirikina na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kupata wataalamu wa mambo ya uchaguzi kutoka taasisi za kimataifa.
“Jopo hili likibaini na kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza, daftari la kudumu la wapigakura lipitiwe kwa umakini ili uchaguzi urudiwe mara moja,” alisema.
Aidha alimwomba mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad  asijitangaze mshindi wala asiogope uchaguzi kurudiwa.
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Jaji Bomani alisema jitihada zilizoanzishwa mwaka 2012 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete zinapaswa kuendelezwa baada ya kugonga mwamba.
Alisema mchakato huo, ulitumia mamilioni ya fedha, kamwe hauwezi kuachwa hivi hivi kwa sababu utakuwa ni uharibifu wa fedha za walipakodi wa nchi hii.
“Nina imani jambo hili litafanikiwa kwani uzoefu wa masuala hayo tunao wa kutosha kuhitimisha mchakato huo,” alisema.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuachia kwa dhamana aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Tiagi Masamaki na vigogo wengine wawili wa mamlaka hiyo, baada ya Kamishna huyo kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika ya Sh bilioni 2.12 kama moja ya masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha aliwaachia washitakiwa hao kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, yaliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanane ambao ni wafanyakazi wa TRA pamoja na wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kwa kula njama za kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Washitakiwa walioachiwa kwa dhamana ni Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja TRA, Habibu Mponezya na Meneja Udhibiti wa Forodha na Ufuatiliaji, Burton Mponezya, ambao waliwasilisha ombi la dhamana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Waliachiwa baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kutoa mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni mbili, kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika waliosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 20 na mmoja kati ya wadhamini hao ni mfanyakazi wa serikali.
Katika dhamana yake, Masamaki aliwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni 2.129 mali hiyo ipo katika eneo la Mikocheni na inamilikiwa na Sospeter Machunge ambaye aliwasilisha mahakamani hati ya kukubali, hati yake itumike kumdhamini Masamaki.
Habibu aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.129, ambapo hati moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 574 inamilikiwa na Salum Said, na nyingine ya Sh bilioni 1.55 inamilikiwa na Wakifu Abdallah.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, alipinga hati hizo kupokelewa na kuhoji Abdallah amepata wapi mali zenye thamani hiyo akiwa na miaka 30. Abdallah alidai amerithi kutoka kwa baba yake na pia anajishughulisha na biashara ndogo ndogo.
Burton aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.3, moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 373 inayomilikiwa na Kampuni ya Theokratia Ltd, pamoja na hati ya mali yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 inayomilikiwa na Sabah Salum, pia waliwasilisha hati za tathmini ya mali hizo.
Wamiliki wa mali hizo walikuwepo mahakamani na kuridhia hati zao zitumike kuwadhamini washtakiwa hao, pia washtakiwa hao walikuwa na wadhamini wawili ambao kila mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 20 na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.
Katika masharti mengine yaliyotolewa na Jaji Winifrida Korosso wa Mahakama Kuu, washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama ya Kisutu na pia kila baada ya wiki mbili wanatakiwa kuripoti ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa.
Baada ya washitakiwa hao, wanaowakilishwa na Wakili Alex Mgongolwa na Majura Magafu, kukamilisha masharti ya dhamana, Wakili Msigwa alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mkeha alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana na washitakiwa wengine, wataendelea kuwa rumande hadi Desemba 30, mwaka huu itakapotajwa tena.
Desemba 4, mwaka huu, Masamaki na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Novemba 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika, walikula njama za kuidanganya Serikali kuhusu Sh bilioni 12.7, kwa madai kuwa makontena 329 yaliyokuwa kwenye Bandari Kavu ya Azam (AICD), yametolewa baada ya kodi zote kufanyika, jambo ambalo si kweli.
Katika mashtaka mengine, inadaiwa kati ya siku hizo, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, washtakiwa waliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7. Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
HABARILEO
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ameamuru kusitishwa mara moja malipo yanayofanywa kwa makandarasi waliojenga barabara tano za ndani ya wilaya hiyo.
Amefanya hivyo kwa maelezo kuwa watendaji wa Manispaa hiyo, wameshirikiana na makandarasi hao kuiibia serikali Sh bilioni 5.7.
Fedha hizo ni ongezeko ambalo makandarasi hao, wanatakiwa kulipwa baada ya kujenga barabara hizo, ambazo thamani halisi ya ujenzi huo ni Sh bilioni tano.
Lakini, katika hali isiyo ya kawaida, makandarasi hao wanatakiwa kulipwa Sh bilioni 10, ongezeko ambalo ni zaidi ya asilimia 100.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Makonda alisema taratibu za Serikali zinataka kama barabara haikukamilika ndani ya muda uliowekwa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo mvua na sababu zinginezo, mkandarasi anatakiwa kulipwa fedha zaidi ambazo ni asilimia 15 ya thamani ya fedha za mradi.
“Lakini kinachostaajabisha katika miradi hii ya barabara, fedha ambazo zimeongezeka ni zaidi ya asilimia 15, kiasi hiki ni zaidi pia ya asilimia 100, wametumia utaratibu gani kulipa fedha hizi za ziada kwa makandarasi hawa?” Alihoji Makonda.
Alizitaja barabara ambazo watendaji wamezitumia kufisadi fedha za umma kuwa ni ujenzi wa barabara ya Lion kwa kiwango cha lami yenye thamani ya Sh milioni 592.1, lakini nyongeza ya fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 860.1 na hivyo kufanya mradi huo kugharimu Sh bilioni 1.4.
Barabara ya kutoka Biafra hadi Embassy, matengenezo yalikuwa ni Sh milioni 507.9 na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 487.5 jumla ya malipo kwa mkandarasi ni Sh milioni 994, barabara ya Mabatini thamani ya mradi ilikuwa Sh milioni 655.5 na fedha zilizoongezeka ni Sh milioni 777.8 na jumla ya mradi kugharimu Sh bilioni 1.4.
Makonda alitaja barabara nyingine zilizojengwa kwa kiwango cha lami zenye ufisadi ni ya Journalism, ambayo ujenzi wake ulikuwa ugharimu Sh bilioni mbili, nyongeza ya fedha katika mradi huo ni Sh bilioni 1.8 na hiyo kufanya mradi huo hugharimu Sh bilioni 3.8, Barabara ya Maandazi ambayo thamani ya mradi ni Sh milioni 799 imeongezwa kiasi cha fedha Sh bilioni 1.2 na hivyo kufanya mradi wote kugharimu Sh bilioni 2.
“Nyongeza hizi zinatia shaka na ni jambo la kushangaza, nimeamuru makandarasi wasiendelee kulipwa fedha hizi na nimetoa siku tano kwa ofisi ya uchunguzi ya mkoa ichunguze malipo haya na mafaili ya miradi hiyo yaletwe ofisini kwangu mara moja,” alisema Makonda.
Alisema ili malipo ya ziada yalipwe, lazima Bodi ya Zabuni ya Wilaya na Bodi ya Mfuko wa Barabara, ziidhinishe malipo hayo. “Lakini cha kushangaza katika malipo haya, yanayoendelea kufanywa na Manispaa, makandarasi wamelipwa kabla hata bodi hazijatoa ukubali wa malipo haya kufanyika,” alisema.
Alisema Bodi ya Mfuko wa Barabara katika ripoti yao, walikataa fedha hizo za malipo ya zaida zisitolewe. Lakini, alisema fedha hizo zilitolewa na Manispaa kwa makandarasi hao na hiyo inaonesha kwamba kuna mchezo mchafu, umefanywa kati ya watumishi wa Manispaa na makarandasi wenyewe.
Alisema wahusika wakuu katika malipo hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Kitengo cha Manunuzi, Mhandisi wa Barabara wa Manispaa ambao ndio wanatakiwa kutoa maelezo ya kuwepo kwa nyongeza hiyo ya malipo kinyume cha taratibu za Serikali.
“Watu wanadai naingilia kazi za watu, nisipobaini uozo huu kwenye wilaya yangu sifai kuwa mkuu wa wilaya, haiwezekani watu wafisadi fedha za umma kiasi hiki wakati tunakosa hata pesa ya kujenga wodi ya wazazi pale Hospitali ya Mwananyamala,” alisema Makonda.
Alisema ataendelea kupambana, kuhakikisha kwamba kila mwananchi anafaidika na keki ya Serikali ;na sio watu wachache ambao wamepewa dhamana ya kufanya kazi kwenye ofisi za umma wafaidike na keki hiyo.
Barabara hizo ni nje ya barabara zingine, ambazo Makonda mwanzoni mwa mwaka huu aliziundia tume kuchunguza ujenzi wake, ambao walidai ulikuwa chini ya kiwango hali inayofanya mvua zikinyesha barabara hizo zinageuka mahandaki.
Tume hiyo ilibaini ujenzi kuwa chini ya kiwango, lakini mabilioni ya fedha zimetumika katika ujenzi huo. Ilipendekeza hatua kuchukuliwa kwa wahusika waliohusika kujenga barabara hizo, ambazo mvua ikinyesha zinageuka mashimo.
HABARILEO
Taasis ya Utafiti ya Twaweza imezindua matokeo ya utafiti walioufanya hivi karibuni ukionesha asilimia 88 ya Watanzania wanaiona Tanzania iko salama. Matokeo ya utafiti huo wenye jina ‘Itikadi kali inavuma Tanzania’, yametokana na takwimu za sauti za watu 1,879 zilizopatikana kwa njia ya simu za mkononi kati ya Septemba 2 na Oktoba 11, mwaka huu .
Akizungumzia utafiti huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema utafiti huo ni wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa. Alisema licha ya hisia kwamba kwa sasa Tanzania iko salama, asilimia tano watu bado wana wasiwasi juu ya vitisho vya mashambulizi katika siku zijazo.
Alisema matokeo ya utafiti yanaonesha wananchi wanaamini kuwa ukosefu wa ajira, utawala mbovu pamoja na kukatishwa tamaa na mifumo ya serikali ndio vitu vinavyochangia kuibuka kwa makundi yenye itikadi kali, Afrika Mashariki .
Asilimia 21 ya wananchi wanadhani kuwa dini inaweza kuwa sababu. “Kwa picha hii na hali halisi ya nchi yetu hatushangai kuona kwamba wananchi wanahofia uwezekano wa mashambulizi kutokea lazima tuangalie jambo hili kwa makini zaidi,” alisema Eyakuze.
Alisema utafiti huo umeonesha asilimia 46 ya wananchi wana wasiwasi juu ya vikundi vyenye itikadi kali kujaribu kuwashawishi wanafamilia kujiunga. Wengine wanahofia wanafamilia wao kushawishika kujiunga navyo na asilimia tano ya wananchi wanamjua mtu ambaye amejiunga au aliyeshawishiwa kujiunga na vikundi hivyo.
Aliongeza kuwa utafiti huo pia umeonesha asilimia 48 ya wananchi wanapendelea ufumbuzi wa kijeshi kupambana na vikundi vyenye itikadi kali na asilimia 20 wanapendekeza mazungumzo na vikundi hivyo kama njia bora katika kusonga mbele.
Hata hivyo, asilimia 96 ya wananchi wana imani kubwa na jeshi wakiliona imara huku asilimia 90 wakiwa na imani kwamba linaweza kuwalinda dhidi ya shambulizi lolote. “Imani hii kwa vyombo vya usalama vya nchi imechangiwa na hisia za wananchi kuhusu serikali kufanikisha kudumisha usalama wakati wa uchaguzi inaonesha asilimia 61 walifikiri serikali ilifanya kazi kubwa kudumisha usalama katika kipindi hicho,” aliongeza Eyakuze.
Alisema kihistoria polisi siku zote wamekuwa wakitazamwa vibaya na wananchi, kwani asilimia 61 ya wananchi waliitaja kama taasisi kinara wa rushwa nchini na dosari zao kadhaa ndio sababu kuu zinazofanya uhalifu kutoripotiwa Polisi.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkuu wa Usalama Jeshini, Meja Jenerali Venance Mabeyo alisema suala la itikadi kali ni pana, hivyo jamii inatakiwa kuondoa tofauti zao. Alisema tishio la mashambulizi si kubwa kama nchi nyingine na linaweza kumalizika kabla halijaleta madhara.
“Tanzania bado haina makundi ya kigaidi, mengi ni ya kijamii wananchi wasiwe waoga, hali inadhibitiwa na wananchi wanatakiwa kuwa watoa taarifa za matukio hayo ili isaidie jeshi,” alisema Meja Jenerali Mabeyo.
HABARILEO
Vilio vimetawala baada ya wakazi waishio katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam kukumbwa na bomoabomoa ambapo nyumba zaidi ya 100 zimebomolewa katika siku ya kwanza katika eneo la Mkwajuni na Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni.
Jana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam, zilianza kazi ya kubomoa nyumba zote zilizo katika maeneo oevu, kando ya mito na bahari.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Manchale Heche alisema bomoabomoa hiyo inalenga kuzibomoa nyumba zaidi ya 4,000 zilizojengwa katika maeneo hayo huku nyingi zikiwa ni katika Bonde la mto Msimbazi.
“Leo hapa Jangwani tumeanza kwa kubomoa nyumba zaidi ya 100, lakini nyumba zaidi ya 4,000 zinatarajiwa kubomolewa na hizi ni zile zote ambazo zimejengwa katika maeneo ambayo yanakatazwa kisheria,” alisema Heche.
Heche alisema serikali ilishatoa tangazo la mwisho juu ya kuwataka wakazi wote waliojenga katika maeneo ya mabondeni, na maeneo yote hatarishi wahame, lakini watu wameendelea kukaidi.
“Tumekuwa tukiwasihi kuhama maeneo ya mabondeni kila mara, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete ilishawatangazia wananchi wa mabondeni wahame na aliwapa viwanja huko Mabwepande, lakini wameviuza na kuendelea kujenga na kuishi mabondeni kinyume cha sheria za mazingira na mipango miji,” alifafanua Mwanasheria Heche.
Nyumba zitakazokumbwa na bomoabomoa hiyo ni zile zilizojengwa maeneo yote ya bondeni katika Bonde la Mto Msimbazi, kando ya mito na katika maeneo ya hifadhi ya bahari ndani ya mita 60.
Aidha, Mwanasheria huyo alisema bomoabomoa hiyo ni endelevu, hivyo kuwataka wananchi wote wanaoishi maeneo ya miundombinu na maeneo yote hatarishi, iki wemo katika fukwe za bahari, kingo za mito na mikondo ya bahari kuhamisha mali zao mapema kabla hawajafikiwa.
Wakazi wote waliopo katika Bonde la Mto Msimbazi, ikiwa ni kuanzia Jangwani hadi maeneo ya Gongo la Mboto, katika Manispaa ya Kinondoni, na kwingineko, wanapaswa kuhama.
Wakazi waliokutwa na kadhia hiyo, kwa nyakati tofauti wamesikika wakilalamika kutokuwa na taarifa japo mara kadhaa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwatangazia kuhama kwa hiyari.
Heche alisema ubomoaji huo, haulengi Dar es Salaam pekee, bali ni kazi inayofanyika nchi nzima na wote waliojenga mabondeni na katika maeneo oevu, wahame.
Alisema wao wanalenga kulinda usalama wa wananchi kimazingira na kiafya kwa ujumla kwa maeneo hayo ni hatari na wenyewe ni mashuhuda pindi patokeapo mvua wanakumbwa na mafuriko.
Mwezi uliopita, Manispaa ya Kinondoni iliendesha bomoabomoa kwa watu waliojenga katika maeneo ya wazi na ilieleza kuwa kazi hiyo itakuwa endelevu
MWANANCHI
Jumla ya wanafunzi 503,914 kati ya 518,034 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa kupata alama A, B na C, wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za Serikali katika awamu ya kwanza. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 97.3 ya wanafunzi waliofaulu na wenye sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza.
Hata hivyo, wanafunzi 12,847 kati ya hao waliofaulu kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara, wameshindwa kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Akitangaza matokeo hayo jana Dar es Salaam, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jaffo alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2016 ni 503,914 kati yao, wasichana ni 255,843 sawa na asilimia 99.2 na wavulana 248,071 sawa na asilimia 97.7.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza imeongezeka kwa asilimia 0.7 ikilinganishwa na asilimia 97.23 ya wanafunzi waliochaguliwa awamu ya kwanza kuingia kidato cha kwanza mwaka 2015.
“Wanafunzi 610 sawa na asilimia 61.2 ya wanafunzi 997 wenye ulemavu waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wamefaulu na wote wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari na ufaulu wao ni sawa na ongezeko la asilimia 0.6 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2014,” alisema Jaffo.
“Naagiza mikoa na halmashauri zenye wanafunzi hawa 12,847 ambao wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza kuhakikisha kuwa wanakamilisha vyumba vya madarasa kabla ya Machi mwakani ili kuwezesha wanafunzi hawa kujiunga na kidato cha kwanza,” alisema Jaffo.
Sh18.7 bilioni kila mwezi Katika hatua nyingine; Jaffo alisema Serikali imetenga Sh18.77 bilioni kwa kila mwezi kuanzia mwezi huu hadi Juni 2016 kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa shule za Serikali kuanzia ngazi ya msingi hadi kidato cha nne ikiwa ni pamoja na chakula cha wanafunzi kwa shule za bweni na ada.
MWANANCHI
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Teknolojia na Tiba (IMTU), kimeingia katika sakata jipya la kuamriwa kuhama ndani ya siku 14 kutokana na kushindwa kulipa kodi ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Amri hiyo imekuja baada ya mpangishaji wa IMTU ambaye ni Shirika la Maendeleo la Taifa(NDC) kupeleka notisi kupitia kwa kampuni ya mnada ya Fosters Auctioneers & General Traders, ya kuondoka katika ploti namba 2348 iliyopo Mbezi Beach jijini hapa.
Jerome Msemwa, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uwakili ya Msemwa & Advocates inayoiwakilisha NDC, alisema jana kuwa IMTU ilisainiana mkataba wa upangishaji na shirika hilo kwa Sh100 kwa mwaka kuanzia mwaka 1996 kwa miaka 15 hadi Agosti, 2011 na tangu hapo chuo hicho hakikulipa kodi yoyote kwa mpangishaji wake.
“Hadi sasa NDC inadai jumla ya Sh3.06 bilioni kama deni la kodi ya kuanzia Agosti, 2011 hadi Septemba, 2015 kwa kodi ya Sh73 milioni kwa mwezi,” alisema Msemwa akieleza kuwa nakala za notisi hiyo imesambazwa katika taasisi mbalimbali zikiwemo Ikulu na vyombo vya habari.
Agizo hilo ni pigo jingine kwa uongozi wa IMTU ambao utalazimika kutafuta eneo mbadala kuendeleza masomo kwa wanafunzi wa chuo hicho, ambao tangu Julai mwaka jana wamejikuta wakisoma katika mazingira magumu.
Itakumbukwa kuwa Serikali iliwahi kuifungia hospitali ya chuo hicho Julai, 2015 kutokana na kutotimiza masharti na taratibu za uendeshaji. Sakata hilo ilikuwa ni sehemu ya mfululizo wa balaa zilizokuwa zikiikumba IMTU, baada ya viungo vya binadamu ambavyo hutumika kufundishia madaktari kukutwa vimetupwa eneo la katika msitu uliopo Bunju wakati huo.
Notisi hiyo ilisema kuwa IMTU tangu Septemba 2012 ilikuwa ikipeleka mashauri mahakamani ya kupinga kuondolewa katika eneo hilo, lakini Septemba 2014 Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotoa amri ya mpangaji huyo kuondoka, ambaye hata hivyo hakutekeleza.
“Unatakiwa kuondoka katika eneo hilo linalomilikiwa na NDC na kulipa madeni yote haraka iwezekanavyo. “Zingatia kuwa ukishindwa kuhama ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya notisi hii, tumepatiwa maagizo ya kukuondoa kwa nguvu bila taarifa yoyote na kushikilia mali zako zote ili kuweza kulipia madeni hayo,” ilisomeka notisi hiyo.
Mkurugenzi wa hospitali ya IMTU, Profesa Yassin Mgonda alisema hajapata notisi hiyo na kueleza kuwa huenda imeufikia uongozi wa juu hasa mmliki na mwenyekiti wa chuo hicho, Katuri Subbarao. “Siwezi kusema nimejiandaeje kuondolewa wakati sina taarifa yoyote na mtu aliyeachiwa madaraka yupo likizo.
Ila nafahamu kuwa kulikuwa na mgogoro wa muda mrefu wa masuala ya kulipana na mambo yalikuwa hayajakaa vizuri,” alisema Profesa Mgonda.
MWANANCHI
Mkazi wa Kijiji cha Malolo Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Chipunguli Mkisi (30) anadaiwa kumuua mkewe Neva Mwaweza (24) kwa kumcharanga mapanga kichwani kutokana na wivu wa mapenzi, kisha kujiua kujinyonga kwa kamba.
Akizungumzia jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana. Msangi alifafanua kuwa inadaiwa kuwa Mkisi alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa ana uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine. “Baada ya kuua, naye akaamua kujitundika kwenye mti umbali wa mita 100 kutoka nyumbani kwake,” alisema Msangi.
Alisema mwili wa Mkisi ulikutwa na majeraha kwenye vidole vya mikono na kando ya mti aliojinyongea kulikuwa na panga na karatasi iliyoandikwa kuwa ameamua kumuua mkewe na yeye kujinyonga kwa sababu alikuwa na uhusiano mwanaume aliyemtaja jina.
Msangi alisema maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi Vwawa.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment