RIDHIWAN KIKWETE AVUNJA UKIMYA, AZUNGUMZIA KUHUSU MAKONTENA NA MALI ANAZODAIWA KUMILIKI.
Ndugu zangu waandishi
wa habari, nimeamua kuwaita ili kuzungumza nanyi kuhusu baadhi ya mambo
yaliyokuwa yanasemwa katika vyombo vya habari kuhusu mimi.
Awali ya yote napenda
kusema kuwa habari hizo ni UONGO mtupu, ni mambo yanayozushwa na
waandishi wa habari hizo kwa nia ya kuchafua jina langu kwa sababu
wanazozijua wanaoandika. UKWELI ni kwamba haya ni mambo yenye kufanywa
kwa nia na dhamira mbaya dhidi yangu na hata familia yangu.
Hivi karibuni, kwa
mfano, lipo gazeti moja liliandika na kutoa picha yangu na mtu mmoja
waliyedai ni Mhe. Paul Makonda eti akinifunga kamba za viatu. Katika
maelezo yake mwandishi akadai kuwa Mhe. Makonda alipata uteuzi kuwa Mkuu
wa wilaya ya Kinondoni kwa sababu hiyo. Huu ni uongo usiokuwa na hata
chembe ya ukweli. Napenda watanzania wajue kuwa hakuna wakati wowote
Baba yangu alipokuwa Rais wa nchi yetu alinihusisha kwa namna yeyote ile
katika uteuzi wa mtu yeyote katika Serikali. Hivyo basi kujaribu
kunihusisha na uteuzi wa Mhe. Paul Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya wa
Kinondoni ni jambo lisilokuwa na ukweli wowote.
Pili, Yule mtu anae
onekana katika ile picha siyo Mhe. Paulo Makonda bali ni Bwana
Deogratius Kessy anayefanya kazi katika kampuni ya ushonaji na mavazi ya
Bwana Sheria Ngowi. Nilishona safari suti kwenye kampuni hiyo.
Nilipokwenda kuchukua nguo yangu na nilipovaa ili kuona kama imeshonwa
vizuri, Bwana Sheria Ngowi alitaka nivae viatu vya ngozi. Bahati mbaya
nilikuwa nimevaa sandals hivyo akaamua kunipa viatu vya dukani kwake
nivae. Wakati bwana Deogratius Kessy akinisaidia kuvaa viatu ndipo ile
picha ikapigwa nampiga picha wa kampuni ya Bwana Sheria Ngowi ,
inashangaza na kusikitisha kuona picha hiyo inatumiwa kupotosha ukweli
kwa kutoa maelezo ya uongo. Ni dhahiri kwamba mwandishi aliamua kufanya
hivyo kwa maksudi mazima ya kutoa sifa mbaya kwangu na kwa Mheshimiwa
Paul Makonda. Hivi ndivyo uhuru wa habari unavyostahili kutumika ?
Siku za nyuma gazeti
lingine liliandika eti kuwa nilihojiwa kuhusu sakata la makontena
bandarini. Napenda kuwaambia ndugu waandishi wa habari kuwa sijawahi
kuhojiwa na mtu yeyote, chombo chochote au kamati yeyote kuhusu madai
hayo. Ni uongo usiokuwa na ukweli wowote. Ni mambo ya kugushi na uzushi
kabisa, Ninayasema maneno haya kwa kujiamini na kama mwandishi ana
uthibitisho wa madai yake autoe hadharani watu wauone. Aidha, nasema
kama yupo mtu aliyenihoji ajitokeze kukanusha ninayoyasema, Namtaka
aseme wazi. Nawahakikishia kuwa mtu huyo hayupo na wala hatakuwepo.
Ndugu waandishi na
watanzania wenzangu, inaelekea kuna mtu au genge la watu mahali Fulani
ambao wameamua na kudhamiria kuchafua jina langu na la familia yangu kwa
kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Tangu Serikali ya
awamu ya tano ianze jitihada za kuwabana watu wanaokwepa kulipa kodi za
Serikali bandarini wapo watu wamekuwa wakifanya jitihada za kunihusisha
na watu Fulani wanaotuhumiwa kuhusika na ukwepaji huo. Wapo baadhi ya
watu wamekuwa wakidai eti baadhi ya makontena hayo ni yangu. Na, wapo
waliodai eti kuwa nimekuwa nawasaidia baadhi ya wafanyabiashara hao
kukwepa kodi kwa kutoa maagizo kwa maofisa wa forodha wasiwatoze kodi
inayostahili kulipwa.
Napenda
kuwafahamisha kuwa sijawahi kuagiza bidhaa zozote kutoka nje hivyo
sijawahi kuwa na kontena lolote ambalo nililowahi kutakiwa kulipia
ushuru nikakwepa.Aidha,
sijawahi kumuombea msamaha wa kutokulipa au hata kupunguziwa kodi
mfanyabiashara yeyote au mtu yeyote aliyeingiza kontena nchini kutoka
nchi za nje.Kama mtu ana ushahidi autoe hadharani mimi niuone na
dunia iuone. Nawahakikishia ushahidi huo haupo na wala hautokuwepo.
Labda uwe wa kugushi na wakifanya hivyo wataumbuka.
Napenda pia kutumia
nafasi hii kusema kuwa sina na wala sijawahi kumiliki lori au basi
wakati wowote katika maisha yangu. Aidha, sina hisa au ubia na mtu
yeyote au kampuni yeyote ya malori au mabasi. Nayasema haya kwa sababu
wapo wabaya wangu wanaoeneza maneno ya kunihusisha na kumiliki malori na
mabasi. Pia kunihusisha na baadhi ya makampuni yanayomiliki na
kuendesha biashara ya malori na mabasi.
Ndugu wanahabari,
napenda kusema kwa kurudia na kusisitiza kuwa sina lori wala basi hata
moja na sina ubia na wafanyabiashara ama makampuni yoyote yanayofanya
shughuli hizo. kama yupo mtu yeyote ana ushahidi wa kuhusika kwangu
auweke hadharani watu wauone. Napenda ieleweke kuwa kama ningekuwa na
ubia wa namna hiyo nisingekuwa na sababu ya kuficha. Niogope kitu gani ?
Ukweli ni kwamba sizuiliwi kufanya biashara kama nikipenda kufanya
hivyo , Hata kwa nafasi yangu ya sasa ya uongozi yaani mbunge bado sina
kizuizi. Mbona Bungeni wapo wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo.
Isingekuwa ajabu kwangu kufanya biashara hivi sasa mimi pamoja na kuwa
mbunge ni mwanasheria wa kujitegemea na nimeiweka katika TAMKO langu la
mali na madeni la viongozi kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi.
Nimewavumilia sana
lakini sasa nimechoka, nimeona leo nivunje ukimya. Nimeona niseme kidogo
kwani bila ya kufanya hivyo nitaliacha genge la watu wenye nia mbaya na
mimi waonekane wanasema kweli. Wahenga wanasema msema pweke hushinda!
Nikiendelea kukaa kimya uongo wao utageuka kuwa ukweli dhidi yangu.
Naambiwa hapa nchini
siku hizi kila jengo jipya linalojengwa linasemekana ni la Ridhiwani,
kituo kipya cha petrol ni cha Ridhiwan.
Nimeanza kuona athari
za uongo huo, Siku moja kuna mtu alikuja kuniomba nimpangishe katika
lile jengo la PSPF pale stesheni. Nilipomuuliza nitampangishaje akasema
mbona watu wamemwambia ni jengo langu!? Siku nyingine nikakutana na
jamaa mmoja mwenye asili ya kiasia akiwa anahema. Akasema ananiomba sana
niache kutaka kupora kampuni yake,nikamuuliza kampuni gani hiyo? Na
kwanini anasema hivyo? Akanijibu, anasikia wakisema kampuni yake ni ya
ridhiwani wakati kampuni hiyo hata yeye kairithi kwa baba yake na yeye
alirithi kwa baba yake zaidi ya miaka hamsini iliyopita, Nikamwambia
kuwa habari hiyo si kweli, sina mpango huo na wala sina sababu ya
kufanya hivyo. Hayo ni maneno yanayoenezwa na wabaya wangu walioamua
kunipakazia kwa sababu wazijuazo wao. Tukaachana ,sijui kama ameamini
kama sina mpango wa kumpora kampuni yake. Siku moja Mzee wangu mmoja wa
kwetu kijijini alinilalamikia kuwa nina roho mbaya kwa vile sitaki kumpa
kazi mwanae kwenye kampuni yangu ya malori wakati yeye ni dereva mzuri,
Nilipomueleza Yule mzee kuwa sina lori hata moja akashangaa na kusema
mbona watu wanasema nina malori mengi. Ndugu zangu mnaiona fitina kubwa
inavyotengenezwa katika jamii kuhusu maneno haya, Wapo wanaoniona mimi FISADI, Wapo wanaoniana mimi nina Roho mbaya, Wapo wanao niona mie nataka kupora mali zao.
Baada ya Baba kustaafu maneno yamekuwa mengi na yanazidi kupata kasi.
kila kukicha wanazua jambo jipya. Nimeoa niyaseme haya ili watu wajue
ukweli wa upande wangu.
Naomba nimalize kama
nilivyoanza kwamba yanasemwa mengi lakini ni maneno ya uzandiki, uzushi
na ni uongo mtupu usiokuwa na chembe ya ukweli. Wale wanaosema,
kuandika, na kueneza maneno hayo wanajua kuwa wanasema UONGO, ila
wanafanya hivyo kwa vile wana nia mbaya dhidi yangu na familia yangu ,
Naomba watanzania muyapuuze maneno hayo, naomba watanzania wenzangu
muupuuze uongo huo.
siko hivyo, sina mali hizo na wala sifanyi hayo wanayodai nafanya na wala sina mpango wa kuyafanya.
Imetolewa na:-
Ridhiwan J. Kikwete
Mbunge wa Jimbo la Chalinze.
chanzo:Michuziblog
No comments:
Post a Comment