MWANANCHI
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, anatarajia
kufanya mkutano wa hadhara kesho jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya ziara
ya kuwashukuru Watanzania waliompigia kura wakati wa uchaguzi mkuu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema katika ziara hiyo Lowassa ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa Ukawa, ikiwa ni mwanzo wa ziara ya nchi nzima.
“Watawashukuru kwa namna walivyounga
mkono upinzani na ajenda ya mabadiliko katika uchaguzi mkuu uliopita na
wanavyoendelea kuweka matumaini yao kwa upinzani kuwa ndiyo nguzo imara
wanayoweza kuitegemea kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa ajili ya
maendeleo yao na ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Itakumbukwa mbali ya Watanzania
kupiga kura za ushindi katika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu
uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana na
Ukawa na kuongeza nguvu kubwa ndani ya Bunge, hususan kupitia Kambi ya
Upinzani Bungeni,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kambi rasmi ya upinzani bungeni itakuwa Serikali mbadala ya wananchi.
“Wameviamini vyama vyetu hivyo
kusimamia na kuongoza halmashauri zipatazo 34 nchi nzima, ikiwa moja ya
misingi imara katika kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa wananchi
wanastahili shukrani kwa imani hiyo ambayo ni ishara ya kuwa matumaini
yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na upinzani imara
kupitia Ukawa.
MTANZANIA
Wakati vita dhidi ya wakwepa kodi katika
Bandari ya Dar es Salaam ikipamba moto, umeibuka utata wa Sh bilioni 80
ambazo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema ni kodi ya makontena 329 kutoka kwa wafanyabiashara 58, walioyatoa bandarini bila kuyalipia kodi.
Akitoa ufafanuzi wa ukusanyaji wa fedha hizo, Desemba 12, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Philip Mpango,
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamekusanya Sh bilioni 10.6 kutoka
kwa wafanyabiashara 28 na kwamba wamebaki 15 wanaodaiwa Sh bilioni 3.7.
Kutokana na takwimu hizo,
wafanyabiashara hao 15 nao wakilipa kodi, zitapatikana jumla ya Sh
bilioni 14.3 kwa makontena yote 329, jambo linalofanya kuwe na upungufu
wa Sh bilioni 65.7, tofauti na kiasi cha Sh bilioni 80 alichosema Waziri
Mkuu Majaliwa.
Juzi Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alipotafutwa
na gazeti hili kufafanua utata huo, alisema: “Sikiliza, usituingize
kwenye ‘issue’ na waziri mkuu, ninachoweza kusema ni kwamba tumekusanya
Sh bilioni 10.6 na zilizo nje bado ni Sh bilioni 3.7.”
Alipotafutwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri
Mkuu, Irine Bwire siku hiyohiyo, alisema waziri mkuu ameshatoka ofisini,
lakini takwimu za Sh bilioni 80 hakuzitoa kichwani bali kwenye ripoti
iliyotoka TRA.
“Mimi nitamuuliza vizuri kesho asubuhi (jana),” alisema Bwire.
Jana alipotafutwa tena, alisema hajafanikiwa kuzungumza na waziri mkuu kwa kuwa alikuwa na vikao vingi.
“Labda baadaye kama atarudi ofisini kwa sababu sasa hivi amekwenda Ikulu kwenye kikao kingine,” alisema Bwire.
Rais Dk. John Magufuli, alipokutana na
wafanyabiashara, alitoa siku saba kwa waliokwepa kulipa kodi kufanya
hivyo na watakaokaidi watachukuliwa hatua.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa
habari, Desemba 12, Dk. Mpango alisema ni kampuni 28 tu ndizo zilizotii
agizo hilo la rais na kufanikisha ukusanyaji wa Sh bilioni 10.6.
Dk. Mpango alisema kuwa muda wa kulipa
kodi kwa hiari uliisha Desemba 11, hivyo wafanyabiashara 15 ambao
wameshindwa kulipa kodi katika kipindi hicho “wasubiri cha moto” kwa
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hata hizo siku saba walizokuwa
wamepatiwa tayari walikuwa wameshavunja sheria, hivyo wale waliolipa kwa
wakati wamesamehewa kupelekwa mahakamani, lakini ambao hawajalipa
watashtakiwa na kupigwa faini,” alisema Dk. Mpango bila kubainisha kiwango cha adhabu.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara hao
walienda “kulalamika”, lakini TRA haitawasamehe kwa kuwa kodi hizo
zinahitajika kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dk. Mpango alibainisha kuwa kati ya
fedha zilizokusanywa katika kipindi hicho, Sh bilioni 4.16 zimetoka
katika kampuni 13 ambazo zimelipa kodi yote iliyokuwa imekadiriwa, huku
Sh bilioni 2.2 zikitoka katika kampuni 15 zilizotoa sehemu ya kodi
wanayodaiwa.
Alisema bandari kavu (ICD) ya Azam
ililipa kiasi cha Sh bilioni 4.17 kama dhamana kati ya Sh bilioni 12.6
ya kodi iliyokuwa imekwepa kulipa katika sakata hilo la upotevu wa
makontena 329.
MTANZANIA
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar
es Salaam, imeridhia kutoa dhamana kwa watuhumiwa watatu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na kuwataka kila mmoja kutoa fedha taslimu Sh
bilioni 2.6.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Winfrida
Koroso, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Tiagi Masamaki (56) ambaye ni
Kamishna wa Forodha wa mamlaka hiyo, Burton Mponezya na Habibu Mponezya ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja.
Alisema kabla ya kutoa dhamana hiyo,
mahakama hiyo imepitia maelezo ya pande zote mbili ambazo ni upande wa
washtakiwa na wa Serikali ili kuangalia kama watuhumiwa hao wana vigezo
vya kupewa dhamana.
Jaji Koroso alisema baada ya kupitia
maelezo hayo, mahakama iliridhia kuwapatia dhamana hiyo, huku ikiwataka
kutimiza masharti sita ili waweze kukidhi vigezo.
Aliyataja masharti hayo kuwa ni kila
mwombaji kulipa fedha taslimu Sh bilioni 2.6 au mali yenye thamani ya
fedha hizo na kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa
Serikali wenye bondi ya Sh 20 kila mmoja.
Alisema, kila mwombaji hatakiwi kusafiri
bila ya kibali cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi hiyo
inaendeshwa, kuwasilisha vibali vya usafiri ikiwamo paspoti katika
mahakama hiyo na kuripoti mahakamani hapo kila baada ya wiki mbili siku
ya Jumatatu.
Alisema masharti mengine ni kila
mwombaji ahakikishe taarifa zote alizowasilisha mahakamani hapo ziwe
zimesainiwa kisheria na kukamilisha taratibu za dhamana ndani ya saa 24
ili waweze kukidhi vigezo vya dhamana hiyo.
Awali, Masamaki na wenzake walifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakituhumiwa kufanya makosa
mawili ya uhujumu uchumi ambapo shtaka la kwanza ni kutoa makontena 329
katika Bandari ya Dar es Salaam bila ya kulipiwa kodi na kuisababishia
Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Novemba 17
mwaka huu, sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam,
watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kuidanganya Serikali kuwa Sh
bilioni 12.7 zimetolewa kwa kutoa makontena 329 katika bandari kavu ya
Azam baada ya kodi zote kutolewa.
Shtaka la pili, inadaiwa kuwa Juni mosi
na Novemba 17, mwaka huu ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walishindwa
kutimiza majukumu yao kwa namna inavyotakiwa na kusababisha Serikali
kupata hasara ya Sh bilioni 12.7.
HABARILEO
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea amepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
akikabiliwa na mashitaka ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Kubenea ambaye ni Mbunge kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alifikishwa mahakamani hapo jana
na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis mbele ya
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba.
Vitalis alidai juzi katika Kiwanda cha
TOOKU Garments kilichoko maeneo ya Mabibo External, Kinondoni, Kubenea
alitumia lugha ya matusi kwa Makonda, jambo ambalo lingeweza kusababisha
uvunjifu wa amani.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Kubenea
alimwambia Makonda; “wewe kibaka, mpumbavu, mjinga na cheo chenyewe cha
kupewa tu.” Kubenea ambaye anatetewa na Wakili Peter Kibatala
akisaidiana na Dk Rugemeleza Nshala, Nyaronyo Kicheere, Geremia
Mtobesia, Omary Msemo na Fredrick Kiwelu, alikana mashitaka hayo.
Wakili Vitalis alidai upelelezi wa kesi
hiyo umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Wakili Kibatala aliomba mshtakiwa apewe dhamana kwa kuwa mashitaka
yanayomkabili yana dhamana kisheria. Upande wa Jamhuri haukuwa na
pingamizi juu ya ombi hilo.
Hakimu Simba alisema mshtakiwa anatakiwa
awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini hati ya
dhamana ya Sh 500,000. Kubenea alitimiza masharti ya dhamana, hivyo
kuachiwa kuwa nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29,
mwaka huu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
HABARILEO
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amesema
diwani anayefikiri ameingia madarakani kwa lengo la kupata utajiri ni
vyema ajiondoe mapema, kwa kuwa serikali haitavumilia mtu atakayebainika
kujihusisha na rushwa, watachukuliwa hatua.
Alisema wapo wanaofikiri udiwani ndiyo
njia ya kujinufaisha kwa kuendekeza vitendo vya rushwa, ufisadi na
kuhujumu miradi ya wananchi. Mwambungu alitoa rai hiyo jana mjini hapa
alipokuwa akizindua Baraza la kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya mji
wa Mbinga.
Akiwasilisha salamu za serikali katika
baraza hilo, aliwataka watendaji wa serikali kushirikiana pamoja na
madiwani hao kufikia malengo ya kimaendeleo, yaliyokusudiwa kwa manufaa
ya jamii.
“Ndugu zangu kiongozi ambaye ni
mpenda rushwa au fisadi aliyekubuhu, tukikubaini tutakuchukulia hatua na
mwisho wa siku tutakuondoa, tafuteni maisha kwa njia zilizo halali
acheni kujihusisha na matendo maovu”, alisisitiza Mwambungu na kuongeza:
“Hapa namaanisha kwamba kila
ngazi itekeleze wajibu wake, mapato yatumike kwa kuzingatia taratibu
zilizowekwa, hatutamsamehe wala kujenga huruma kwa mtu ambaye ni mwizi,
na mwenye lengo la kutaka kuturudisha nyuma kimaendeleo.”
Alisema lengo la serikali ni kutaka
kwenda na kasi ambayo inaendana na weledi, uaminifu na uadilifu wa hali
ya juu katika utendaji kazi.
Awali kabla ya Mkuu huyo wa Mkoa kutoa
salamu hizo kwa baraza hilo la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga,
ulifanyika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti, Makamu wake na kamati
mbalimbali za halmashauri hiyo. Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Diwani wa
Kata ya Myangayanga, Ndunguru Kipwele kutoka CCM aliyepata kura 24.
Alikuwa akishindana na Diwani wa Kata ya
Mbiga Mjini B, Frank Mgeni wa Chadema aliyepata kura mbili. Nafasi ya
Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Diwani wa Kata ya Kikolo, Tasilo
Ndunguru aliyepata kura 23 na kumshinda Aidan Nombo wa Kata ya Utiri,
aliyepata kura tatu.
HABARILEO
Polisi mkoani Singida inamshikilia
Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Itaja na mkewe kwa tuhuma za kumfungia
ndani ya chumba mtoto wao mlemavu wa viungo kwa miaka 12 bila kutoka
nje.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni David Mtipa (59) ambaye ni Mchungaji wa Kanisa
hilo na mkewe Mariam Philipo (45) wote wakazi wa kijiji cha Itaja katika
tarafa ya Mgori wilayani Singida.
Kamanda Sedoyeka alisema tukio hilo
liligundulika juzi katika kijiji hicho baada ya Polisi kupata taarifa za
siri kutoka kwa wasamaria. Akielezea tukio hilo, Kamanda Sedoyeka
alisema watuhumiwa walimfungia ndani ya chumba mtoto huyo, Timotheo David (30) kwa muda wa miaka 12 huku huduma zote za kibinadamu, ikiwemo haja ndogo na kubwa pamoja na chakula zikifanyika humo ndani.
“Baada ya timu ya askari wa
Upelelezi na Ofisa Ustawi wa Jamii kufika eneo hilo wakiwa na viongozi
wa kijiji na kufanya mahojiano, watuhumiwa walikiri kumfungia chumbani
mtoto wao huyo na kwamba ni mlemavu wa miguu na mikono, lakini pia ni
mlemavu wa akili,” alisema Kamanda Sedoyeka na kuongeza:
“Wamesema mtoto wao alizaliwa
mwaka 1984 akiwa mzima, lakini alipofika darasa la sita 2003 alianza
kuugua ugonjwa usiojulikana ikiwa ni pamoja na kuanguka kisha kutoa povu
mdomoni huku mwili wake ukibadilika rangi kuwa ya njano na kutibiwa
bila mafanikio.”
Aidha, alisema mlemavu huyo alitibiwa
maeneo mbalimbali bila mafanikio na ndipo wazazi hao walipoamua
kumfungia ndani baada ya kuona wanafedheheshwa mbele ya jamii huku akila
chakula, kujisaidia humo chumbani na kutoruhusiwa kutoka nje.
Kutokana na hali hiyo, majirani
waliingiwa na hofu kwa kutomwona mtoto huyo kwa kipindi kirefu kiasi
hicho hali iliyozua maswali mengi. Wakati baadhi walijua huenda ameuawa,
wengine walihusisha kitendo hicho na imani za kishirikina huku
Mchungaji akidaiwa kuzidiwa maarifa na mkewe.
Alisema kitendo cha kumfungia mtoto huyo
ndani kwa kipindi chote hicho, kumwacha akiwa uchi na kumlaza kwenye
kitanda cha kamba kisichokuwa na godoro ilikuwa ni ukiukwaji wa misingi
ya binadamu na si cha kiutu.
Alisema amepelekwa Hospitali ya Mkoa wa
Singida kwa matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake wakati wazazi hao
wakishikiliwa na kuhojiwa ili hatimaye wafikishwa mahakamani kwa ukatili
uliovuka mipaka.
HABARILEO
Wafugaji waliovamia maeneo ya wakulima
katika kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero mkoani Mogorogo na
kusababisha mapigano yaliyoua mkulima na ng’ombe 71, wamekimbia kijijini
hapo na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumzia hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Mvomero, Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty
Mkwasa alisema ulinzi bado umeimarishwa eneo hilo, na kwamba wafugaji
waliovamia wamekimbia.
“Wafugaji wamekimbia na sisi
tutateketeza maboma yao, kwa sababu walivamia eneo hili la wakulima na
ng’ombe walioachwa wamepigwa mnada na fedha imeingizwa kwenye mfuko wa
serikali ya kijiji hicho,” alisema Mkwasa.
Aidha, katika msako uliofanywa kwa
ushirikiano wa Serikali ya Wilaya na Polisi silaha moja ya askari
iliyochukuliwa ilipatikana na kwamba wakulima wametolewa hofu na
kusisitizwa kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Alifafanua kwamba hali kwa sasa kijijini
hapo ni shwari na kwamba mifugo iliyouawa kwa kukatwakatwa mapanga yote
imeshafukiwa na uongozi wa serikali ya wilaya umepanga kuingia mkataba
na viongozi wa vijiji na kata ili kudhibiti, migororo baina ya makundi
hayo.
Alisema katika kudhibiti matukio ya
mapigano au uvunjifu wa sheria na mpango wa matumizi bora ya ardhi,
Mvomero itaanza kuingia mkataba na watendaji wa vijiji na kata na iwapo
migogoro itatokea, wao ndio watawajibishwa.
Awali Desemba 12, mwaka huu, kundi la
wafugaji wa jamii ya Kibarbaig waliwavamia wakulima na kuanza
kuwashambulia kutokana na mmoja wa wafugaji ambaye mifugo yake iliharibu
mazao ya mkulima kutakiwa kulipa fidia ya Sh 200,000. Katika tukio
hilo.
HABARILEO
Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri nchini wametakiwa kuhakikisha takataka zote zilizolundikwa
wakati wa kazi ya usafi iliyofanyika Desemba 9, nchini kote
zinaondolewa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene wakati
akizungumza na watumishi wa wizara hiyo mjini hapa, na kuagiza kuwa
ifikapo Desemba 20, mwaka huu takataka zote zilizolundikwa ziwe
zimeondolewa.
“Naagiza wakuu wa mkoa, wilaya
na wakurugenzi kuwa ifikapo tarehe 20 mwezi huu takataka zote ziwe
zimeondolewa katika maeneo yao,” alisema Simbachawene na
kuongeza kuwa hategemei kusikia baada ya tarehe hiyo takataka kuwa bado
zimelundikana kwenye maeneo mbalimbali.
Kumekuwapo na mlundikano wa takataka
katika maeneo mbalimbali ya miji nchini na kuwa uchafu baada ya kazi ya
usafi ya Desemba 9, nchini kote kutokana na agizo la Rais John Magufuli
la kufuta sherehe za sikukuu ya Uhuru na badala yake siku hiyo itumiwe
kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.
NIPASHE
Kwa mara ya saba sasa viongozi wakuu wa kitaifa wa Zanzibar, akiwamo mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohamed Shein na mgombea urais wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad,
wamekutana bila taarifa zozote kwa umma kutolewa juu ya mazungumzo hayo
tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba 25,
mwaka huu.Zikiwa zimetimia siku 47 sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo, vikao hivyo vimekuwa vikifanyika huku umma ukiwa njia panda juu ya kinachozungumzwa kutokana na kugubikwa na usiri mkubwa.
Jana viongozi hao wakuu wa kitaifa walikutana kwa mara ya saba Ikulu mjini hapa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kupata taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo ya kikao hicho.
Viongozi waliokutana jana ni Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Balozi Seif Ali iddi, Makamu wa Pili wa Rais na marais wastaafu, Amani Abeid Karume na Ali Hassan Mwinyi, ambao walikutana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.
Alipoulizwa kuhusiana na mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai (hashiriki mazungumzo hayo), alisema chama chao hakijui chochote kinachozungumzwa katika vikao hivyo kwani havihusiana na chama.
“Vikao vinavyoendelea kufanyika Ikulu ambavyo vinawakutanisha viongozi wa kitaifa havihusiani na vyama na ndio maana hakuna mwakilishi wa CCM wala Cuf, isipokuwa viongozi wa serikali,” alisema Vuai.
Hata hivyo, licha ya kutopatikana kwa taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo hayo, hali ya amani na usalama visiwani hapa imezidi kuimarika, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
NIPASHE
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, amewaonya vikali mawakili wa serikali wanaokula njama za kuhujumu kesi mahakamani kwa kushirikiana na mawakili wa kujitegemea na kusababisha serikali kushindwa kesi na kuingia hasara za mabilioni ya fedha.
Masaju alisema ili kutenda haki kwa Watanzania, mawakili wa serikali wanatakiwa kutojihusisha na mchezo huo mchafu wala kushiriki kwa namna yoyote kesi za mawakili wa kujitegemea.
Alisema wakati mwingine mawakili wa serikali wanakula njama na wateja wao kuharibu kesi mahakamani au wakati mwingine wakili hao anashirikiana na mteja kuvujisha kesi mahakamani.
“Kuapishwa kwenu leo (jana) kusiwe ni sehemu ya uvunjifu wa sheria za mahakama, kwa sababu mtaungana na kundi jingine la maofisa wa mahakama kwa lengo la kupigania utawala wa haki uliothabiti katika sehemu zote,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, alisema mawakili hao wamefikisha idadi ya mawakili 5,176 nchini, lakini kati yao 55 wanakabiliwa na mashtaka ya nidhamu na kuwataka mawakili hao walioapishwa kufanya kazi kwa uadilifu, pamoja na kulinda siri za wateja.
Alisema kila mwaka serikali inawaapisha mawakili wapya 450 hadi 500, hali ambayo imesaidia kutatua changamoto ya uhaba wa mawakili katika mahakama mbalimbali nchini, pamoja na kupunguza mrundikano wa kesi ambazo zingeweza kusikilizwa kwa wakati.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment