Sunday, December 6, 2015

NEW AGE IMEKULETEA UCHAMBUZI WA MAGAZETI LEO DECE 06

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha NEW AGE Tanga, New Age ni mabingwa wa kupasisha wanafunzi wa kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, New Age iko na walimu mahiri wenye weledi wa kumjenga mtoto kielimu na kupasi alama za juu, Kituo kipo Tanga mkabala na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) simu 0717 713866
TANZANIA DAIMA
Mahakama ya Bunda amemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Changwe Changige mwenye miaka 54 kwa kosa la kumuoa na kumbaka mtoto wa miaka minane.
Wakati huo huo mahakama hiyo imemhukumu baba wa mtoto huyo kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kuruhusu mtoto huyo kuolewa.
Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Junuari mwaka jana katika kijiji cha Nyaburundu.
Akitoa hukumu hiyo hakimu wa mahakama hiyo alisema watuhumiwa hao watakwenda jela pamoja na adhabu hizo zitakwenda pamoja.
Mwendesha mashtaka alieleza kuwa washtakiwa hao walikula njama na kumuoza mtoto huyo kwa siri huku muhusika akitumia nafasi ya kumuoa mtoto huyo kwa kumbaka na kumsababishia maumivu makali.
HABARILEO
Serikali imesema idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, imeendelea kuongezeka kutoka laini za simu za viganjani milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32.1 Desemba mwaka jana.
Msemaji wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prisca Ulomo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kanuni mpya za Huduma za Ziada za mwaka 2015 za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.
Aidha, alisema watumiaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka milioni 3.56 mwaka 2008 hadi milioni 11.34 mwaka 2014.
Alisema mafanikio hayo, yamerahisisha kutoa na kupata huduma kwa haraka na kwa wakati na wananchi hawalazimiki tena kusafiri sambamba na kupunguza urasimu katika huduma za kutuma na kupokea fedha.
“Huduma hii imesaidia mengi ikiwemo kulipia ankara za maji, umeme, ada na ukusanyaji wa mapato ambapo takwimu zinaonesha kwamba kuna watumiaji 12,330,962 wa miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki,” alisema.
Alisema mafanikio hayo, pia yameleta changamoto kwenye sekta na katika jamii, ikiwemo utoaji wa huduma za ziada kwa watumiaji wa huduma za ziada bila kuwa na utaratibu unaoeleweka kati ya mtoa huduma na mpokea huduma au mlaji.
Baada ya kujitokeza kwa changamoto katika utoaji wa huduma za ziada, serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilitunga kanuni mpya za Huduma za Ziada za Mwaka 2015 ambayo tayari imeshaanza kutumika,” alisema.
Alisema lengo kuu la kanuni hizo ni kuweka utaratibu mahususi, unaoeleweka wa utoaji na upokeaji wa huduma za ziada, ambazo ni huduma za mawasiliano za kielektroniki zinazotolewa kupitia mitandao zaidi ya huduma za msingi za mawasiliano, mfano kupokea ujumbe
HABARILEO
Wanyama pori aina ya mbogo ‘ nyati’ wanane wenye thamani ya Sh milioni 32.6, wamekufa papo hapo kutokana na kugongwa na gari la mizigo, wakivuka barabara kuu ya Morogoro – Iringa.
Barabara hiyo inakatisha Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, iliyopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Tukio la kugongwa kwa wanyamapori hao , lilitokea kati ya saa tatu na nne usiku Desemba 3, mwaka huu ;na askari wa Tanapa wa doria walifika kwenye eneo la tukio muda mfupi baada ya gari hilo kuwagonga na kuwaua mbogo hao.
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Dattomax Sellanyika alisema jana kuwa tukio la kuuawa kwa idadi kubwa ya wanyamapori wakiwemo mbogo hao, halijawahi kutokea na ni hasara kubwa kwa hifadhi na taifa.
Alisema tukio la kugongwa na kuuawa kwa wanyama hayo, lilisababishwa na gari lenye namba za usajili T 363 CVF aina ya Fuso, lililokuwa ikiendeshwa na Said Omary, likitokea Mang’ula wilayani Kilombero likiwa na shehena ya magunia ya mchele kwenda Dar es Salaam.
Sellanyika alisema mbogo hao wanane waliouawa, wameisababisha hifadhi hiyo hasara kubwa ya jumla ya Sh 32,680,000 ambapo kila mbogo mmoja ni Dola za Marekani 1,900 sawa na Sh milioni nne.
“Tukio hili ni la kusikitisha na linahuzunisha nikiwa mhifadhi wa Mikumi. Hifadhi imepata hasara kubwa na inatuuma sana kuona wanyamapori wamekufa kwa kugongwa na gari ndani ya hifadhi “, Sellanyika.
Alisema wanyamapori hao ndio wanaovutia watalii kutembelea hifadhi ya Mikumi na kulipatia taifa fedha za kigeni , hivyo kuendelea kuuawa kwa kugongwa na magari kunawavunja moyo hata watalii wanapoona wanyama wakiuawa bila hatia.
Dereva wa gari hilo, Omary alijitetea kuwa wanyamapori hao walikatisha barabara kwenye kona na alipojaribu kuwakwepa, alishtukia akiwaparamia na kuwaua wanane papo hapo.
Alisema alipokuwa anajitahidi kufunga breki, ghafla mipira ya kupitisha upepo ilishindwa kufanya kazi, hivyo kwenda moja kwa moja kuwagonga mbogo hao kwa bahati mbaya na bila gari kupinduka.
HABARILEO
Majina ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), waliohusika kutoa makontena 2,431 bila kulipa ushuru kati ya Machi hadi Septemba 2014 katika Bandari ya Dar es Salaam, yamepatikana na kufikishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Taarifa zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa wahusika wote walioshiriki katika hujuma hiyo, majina yao yameshafikishwa kwa Waziri Mkuu na kinachoendelea ni uchunguzi wa kila mmoja wao.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufanya ziara ya ghafla wiki hii katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo alisema makontena hayo 2,431, yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu (ICD) nne ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.
Kutokana na taarifa hiyo, Waziri Mkuu alimtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga, ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo, ambapo jana ilithibitishwa kuwa kazi hiyo imekamilika na kinachofanyika ni uchunguzi wa watuhumiwa.
Mbali na kupeleka majina hayo, Mhanga pia alipewa wiki moja inayoisha Alhamisi ya wiki ijayo, kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo wa sasa bandarini na kuweka mfumo mpya wa malipo wa kielektroniki (e-payment). Uchunguzi Ingawa haijajulikana aina ya uchunguzi unaofanyika dhidi yao, lakini ni wazi moja ya hatua hizo za kiuchunguzi, itahusu namna walivyohusika na ukaguzi wa mali zao.
Tayari uchunguzi wa aina hiyo, umeshaanza kufanyika kwa watuhumiwa wa utoaji wa makontena 329 yaliyokuwa kwenye ICD ya Azam, ambayo yanakadiriwa kuipotezea Serikali zaidi ya Sh bilioni 80, ambapo taarifa zimeonesha kuwa baadhi walikaguliwa mpaka katika majumba yao.
Waziri Mkuu Majaliwa alipokwenda bandarini kwa mara ya kwanza kupitia ziara ya kushtukiza na kuibua upotevu wa mapato katika makontena hayo 329, aliagiza mali za watuhumiwa hao zichunguzwe, kama zinalingana na mapato ya mtumishi wa umma.
Aidha wiki hii katika utekelezaji wa agizo hilo, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango, aliagiza watumishi wote wa mamlaka hiyo, kuwasilisha taarifa sahihi ya orodha ya mali zote wanazomiliki kwa ajili ya uhakiki wa kina. Watumishi hao wametakiwa kuwasilisha taarifa hizo kwa uongozi wa juu wa mamlaka hiyo ifikapo Desemba 15 mwaka huu.
Agizo hilo limeambatana na onyo kuwa mtumishi yeyote, atakayebainika kuhusika na vitendo vyovyote vya ubadhirifu, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi, kulingana na makosa atakayokutwa nayo.
Wengi kupoteza kazi Hatua hiyo inazidisha wasiwasi wa kuongezeka watumishi wa Serikali walio katika hatari ya kusimamishwa kazi, baada ya wenzao 36 kusimamishwa kazi wiki hii na wiki iliyopita.
Walioanza kusimamishwa kazi Ijumaa ya wiki iliyopita walikuwa Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande; Hamisi Ali Omari (hakutajwa ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
Siku hiyo hiyo waliyosimamishwa kazi vigogo hao, Rais John Magufuli, akamsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kesho yake wakaongezwa watumishi wengine watatu; ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
Kabla hali haijatulia, Alhamisi ya wiki hii watumishi wengine 27 wa TRA, walikamatwa katika geti namba tano na kusimamishwa kazi, kisha wakawekwa rumande kupisha uchunguzi wao.
Kortini Wakati uchunguzi huo ukiendelea, juzi maofisa waliosimamishwa kazi Ijumaa ya wiki iliyopita kwa upotevu wa mapato katika makontena hayo 329, akiwemo Masamaki (56), Mponezya (45), Mpande (28), Omari (48) na Eliachi (31), walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.
Washtakiwa hao pamoja na wafanyakazi wengine wa ICD ya Azam, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.
Mbali na hao watumishi wa TRA, wengine waliopanda kizimbani kwa makosa hayo ni wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam, akiwemo Mkuu wa Ulinzi na Usalama, Raymond Louis (39) na Meneja Ashraf Khan (59).
HABARILEO
Mmkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba mmiliki wa Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sadiki alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake imeiamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q Consult kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo Manispaa ya Kinondoni imekata rufaa.
“Kampuni ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali kurudisha ufukwe huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza ufukwe huo kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa manufaa ya mtu mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.
Alisema wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa, kama watu wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata rufaa.
Akielezea sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na Manji mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya Kinondoni kuendeleza ufukwe huo.
Alisema, hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba huo baada ya Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya kuendeleza ufukwe huo.
“Kama nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata rufaa katika uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo mwekezaji huyo namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi hiyo na kuamua kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania wote,” alisema Sadiki.
Kwa kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji huyo endapo ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena, kama wanavyoutumia sasa.
Sadiki alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na benki hapa nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo hilo ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na watu wote.
NIPASHE
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), jana ilifanya ukaguzi wa kushtukiza wa kupima ulevi madereva wa mabasi makubwa ya abiria yaendayo mikoani na nchi jirani ya Uganda na kubaini mambo yanaenda vizuri.
Sumatra, katika ukaguzi huo iligundua kiwango cha ulevi miongoni mwa madereva kimepungua.
Sumatra ilishirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani kufanya ukaguzi huo ambao hufanyika mara kwa mara kwa kushitukiza.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema nia ya ukaguzi huo ni kuwaelimisha madereva na abiria wanaosafiri na mabasi hayo kutambua sheria na wajibu wa kila mmoja awapo safarini.
Hapa tumekuja kwa ajili ya ukaguzi wa magari na madereva wapo ambao hawazingatii sheria wala kutumia video za mamlaka ambazo tumetoa kwa kila basi liendalo masafa marefu,รถ alisema Ngewe.
Ngewe alisema wanatoa elimu hiyo hususani kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka, kutokana na madereva wengi kutozingatia sheria, kanuni na wajibu wao wawapo barabarani.
Alisema kila mmoja anatakiwa kutambua wajibu wake na haki wanapokuwa ndani ya chombo cha usafiri, ili kutovunja sheria za usalama barabarani.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa chama cha madereva mkoani Mwanza, Shaban Wandiba, alipongeza zoezi hilo linalofanywa mara kwa mara na Sumatra, lakini alisema iwapo dereva atapatikana na kosa la kutumia kilevi, sheria kali imfuate.
Zoezi hilo la kupima ulevi kwa madereva lilifanyika katika kituo kikuu cha mabasi Nyegezi jijini Mwanza jana kuanzia saa 11:30 asubuhi na kumalizika saa 1:00, lakini hakuna dereva aliyekamatwa anatumia kilevi chochote.
NIPASHE
Wakati Rais John Magufuli akitimiza siku 31 akiwa amejifungia Ikulu kutatua kero za nchi bila kusafiri nje ya nchi, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ameendelea kujumuika katika hafla za kimataifa baada ya kuonekana nchini Afrika Kusini juzi akiwa mwalikwa wa Mkutano wa China na Afrika.
Tangu aingie madarakani Novemba 5, Rais Magufuli amepiga marufuku safari za nje kwa watendaji wa serikali bila ya kibali maalumu cha Ikulu.
Alifikia uamuzi huo baada ya kubainisha katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 11 mwezi uliopita kuwa safari za kimataifa zinatafuna mabilioni ya fedha za walipa kodi.
Rais Magufuli hajasafiri kwenda nje ya nchi mbali na kwenda Dodoma kwa ajili ya kumwapisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuzindua Bunge.
Picha zilizotumwa na Ofisi ya Makamu wa Rais jana, zilimwonyesha JK akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyemwakilisha Rais Magufuli kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na China, uliomalizika jana jijini Johannesburg.
JK ameonekana katika picha hizo akitembelea mabanda ya maonyesho ya mkutano huo ulioandaliwa na China ili kujadili mikakati ya ushirikiano baina yake na Afrika.
Ni mara ya pili kwa Kikwete kwenda nje ya nchi tangu Rais Magufuli aingie madarakani. Novemba alionekana katika Jiji la Addis Ababa Ethiopia.
Kwenye utawala wake wa miaka 10, Rais mstaafu huyo alilaumiwa kusafiri mara nyingi nje ya nchi akiwa na msururu wa viongozi na wasaidizi wake hivyo kutumia gharama kubwa, lakini alijitetea kuwa huenda nje kutafuta fedha za maendeleo.
Wakati akihutubia Bunge mjini Dodoma mwezi uliopita Rais Magufuli alisema safari za nje ziliigharamu nchi Sh. bilioni 356 kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.
Alisema kati ya kiasi hicho karibu Shilingi bilioni 200 zilitumiwa kwa tiketi za ndege, kadhalika bilioni 68 zilitumiwa kwa mafunzo ya nje wakati bilioni 104 ziliishia kwenye mifuko ya vigogo na maofisa kwa ajili ya posho.
Rais Magufuli alisema mabilioni hayo ya safari yangejenga kilometa 400 za barabara kwa kiwango cha lami akitaja ile inayotoka Urambo Tabora hadi Kigoma mjini.
Katika kutimiza azma ya kupinga safari za nje , Rais Magufuli alikacha kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola, uliofanyika visiwa vya Malta wiki mbili zilizopita.
Aliagiza Balozi wa Tanzania jijini London Uingereza na maofisa wengine wanne kuiwakilisha nchi kwenye mkutano huo hatua iliyookoa karibu Shilingi milioni 700 ambazo zingegharamia safari hiyo.
NIPASHE
Sakata la makontena 329 yaliyotoroshwa kinyemela bandarini  na kukwepa kodi ya zaidi ya Sh. bilioni 80 limezidi kuchukua sura mpya baada ya watu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kuongezeka na kufikia 47.
Miongoni mwa waliokamatwa wamo wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao mali zao zinachunguzwa ili kujua walizipataje pamoja na baadhi ya wamiliki wa makontena hayo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani, alisema idadi  ya waliokamatwa imeongezeka ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo  walikuwa wanawashikilia watuhumiwa 12 ambapo watano wanatokea TRA, watano kutoka Bandari Kavu ya Azam na wawili wamiliki wa makontena, hivyo kuongezeka kwa idadi hiyo kunatokana na msako ambao bado unaoendelea.
DCI alisema katika awamu ya pili ya msako huo wamefanikiwa kuwakamata wafanyakazi wa TRA  27 na wanane wakiwa ni wamiliki wa makontena hivyo kufanya idadi ya watuhumiwa wanaoshikiliwa mpaka sasa kufikia 47.
Alisema kati ya watuhumiwa hao wanane walifikishwa mahakamani juzi na wengine wanaendelea na uchunguzi  kubaini wahusika katika tukio hilo ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
DCI alisema kadri ushahidi utakapotolewa kwa wakati utafanikisha watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani mara moja.
Alitoa wito kwa wananchi ambao wana taarifa za mali zinazomilikiwa na watuhumiwa hao kutoa taarifa ili ziwasaidie katika uchunguzi wao.
Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ya awamu tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ilibaini ubadhilifu wa ukwepaji wa kodi kwa makontena 329 ambayo yameisababishia hasara serikali kiasi cha sh. bilioni 80.
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ambaye alifanya ziara ya kushutukiza bandarini hapo alibaini makontena hayo kupitishwa bila kulipia kodi tangu Julai mwaka huu.
Kutokana na ubadhirifu huo, Jeshi la polisi liliagizwa kuchukua hatua kwa wale wote ambao wamehusika katika suala hilo la ukwepaji wa kodi.
Kufuatia sakata hilo Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade alisimamishwa kazi huku jeshi la polisi likiwashikilia na maafisa kadhaa waandamizi wa mamlaka hiyo akiwemo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Hadi sasa tayari makampuni 43 yamebainika kuhusika katika kupitisha makontena hayo na makampuni manne yamelipa kodi ya Sh. Bilioni 5.2 kwa TRA.
NIPASHE
Kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli, imeibua upya sakata la ubomoaji wa jengo la ghorofa 16 ambalo serikali iliamuru libomolewe baada ya kutokidhi viwango lakini viongozi walionekana kulega lega katika utekelezaji wa agizo hilo.
Azma ya kubomolewa kwa jengo hilo lililopo mtaa wa Indira Ghand na Kisutu, kunafuatia tukio la Machi 29 mwaka 2013 baada kuporomoka kwa jengo pacha lililosababisha vifo vya watu 36, na kujeruhi wengine 18.
Hata hivyo, kazi ya kubomoa imeonekana ikisuasua kwa miaka mitatu kutokana na wakandarasi wanaopewa kazi hiyo kujitoa katika hatua ya mwisho wakitoa sababu mbalimbali.
Manispaa ya Ilala sasa imetangaza kufanya kazi hiyo haraka na tayari kampuni tatu za kimataifa zimejitokeza kufanya kazi hiyo.
Akizungumza na Nipashe, Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, David Langa alisema Halmashauri hiyo ipo katika hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi wa kufanya kazi hiyo.
Alisema mpaka sasa katika zabuni iliyotangazwa kuna kampuni tatu zilizojitokeza kutaka kazi hiyo na wako katika hatua za mwisho mwisho kumpata mshidi wa zabuni hiyo.
“Kuna mambo mengi ya kuangalia kabla ya kubomoa jengo, lazima tujiridhishe athari zitakazojitokeza katika usalama wa watu, mazingira na mali zingine,” alisema Langa.
“Muda si mrefu tutataja jina la kampuni itakayopewa kazi, ” aliongeza Langa.
Jengo hilo linamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la la Nyumba la Taifa (NHC) na Ali Raza Investment, awali lilitakiwa kuvunjwa na kampuni ya kichina ya CRJ lakini ilishindikana.
Mtaalam mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema ubomoaji wa jengo la aina hiyo ni kazi ngumu na hapa nchini kuna kampuni na taasisi chache zenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Alisema kuna aina mbalimbali za ubomoaji salama wa majengo ya aina hiyo, lakini ina gharama kubwa.
Mtaalam huyo alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha jengo hilo linaporomoshwa kwa kushuka chini na si vinginevyo kwa ajili ya kuepuka madhara.
Alizitaja njia hizo kuwa ni kubomoa kwa kuondoa ghorofa moja moja kutoka juu, lakini alionya njia hiyo ina hatari ya kukosea kisha sehemu ya ghorofa kuangukia makazi ya watu.
Alisema njia nyingine ni kutumia vyombo maalum vya kukatia na kuondoa vifusi.
“Kwa kutumia njia hii inakuwa rahisi kidogo, lakini mara nyingi kunahitajika vyombo na utaalamu wa hali ya juu ambao kwa nchi yetu ni vigumu kupata,” alisema mtaalam huyo.
Alitaja njia inayofaa na yenye madhara kidogo ni ubomoaji wa mabomu ambayo inapolipuka inaporomosha jengo kwa kulishusha chini.
Alisema mabomu hayo yanategwa kulingana na urefu wa jengo, kisha yanalipuliwa kufuata mtitiriko maalum ambao hautasababisha jengo kukatika na kuanguka.
“Mabomu haya yanategwa katika nguzo za kila ghorofa, halafu yanalipuliwa kuanzia juu kushuka chini, hivyo jengo litashuka chini na halitatawanyika,” alisema mtaalam huyo.
Hata hivyo alieleza kwamba njia hiyo inawezekana pale kazi hiyo itafanywa na vikosi vya Jeshi la Ulinzi au kampuni iliyothibitika inaweza kutumia utaalam huo.
MWANANCHI
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), limeanza rasmi kutumia bei mpya za ankara za maji, ikiwa ni siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) kupitisha mapendekezo ya kupandisha bei kama walivyoomba.
Awali, Dawasco iliomba kuongeza bei ya utoaji wa huduma hiyo ili kuboresha huduma zake katika Jiji la Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.
Bei hizo mpya ambazo zimeanza rasmi kutumika Desemba Mosi, zimepanda kutoka kiasi cha Sh1,098 kwa lita 1,000 hadi kufikia Sh1,663 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 51.
Ofisa Habari wa Dawasco, Everlisting Lyaro alisema kupitishwa kwa mapendekezo hayo kutaongeza uwezo wa shirika hilo kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wateja wao.
Lakini pia huduma zitaboreshwa zaidi baada ya kukamilisha miradi yote mikubwa ya maji ambayo tayari ipo katika hatua zake za mwisho,”“ alisema Eva.
Wakazi wa jijini Dar es salaam, wameiomba Dawasco kuhakikisha inawapatia huduma hiyo kulingana na mahitaji yao huku ikiendana na gharama iliyoongezwa.
“Sisi hatuna shida na ongezeko la bei, tunachotaka ni huduma bora ya maji, Dawasco wahakikishe wananchi tunapata huduma hiyo bila usumbufu, siyo wanaongeza bei halafu maji yenyewe hatuyapati, hapo hatutakubali kabisa,” alisema Penieli Tenga, mkazi wa Mwananyamala Manispaa ya Kinondoni.
MWANANCHI
Ili kudhibiti upotevu wa mapato na kuboresha huduma, Hospitali ya Wilaya ya Ilala Amana, imeanza kutoa huduma zake kwa njia ya mtandao kuanzia kujisajili hadi mgonjwa anapolipia gharama za matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema teknolojia hiyo imeisaidia hospitali kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kusimamia huduma kwa karibu kati ya mgonjwa na watoa huduma.
Alisema mgonjwa yeyote hivi sasa haruhusiwi kumkabidhi fedha taslimu muhudumu wa hospitali bali mpokea malipo ambaye huichanja kadi yake kuonyesha kuwa amelipa fedha halali aliyotozwa kwa matibabu.
Mwananchi lililofika hospitalini hapo na kuzungumza na baadhi ya wagonjwa ambao walionyesha kufurahishwa na utaratibu huo. Walisema umesaidia pia kupunguza foleni hospitalini hapo.
Mmoja wa wagonjwa waliofika kutibiwa katika hospitali hiyo, Yeledi Livingstone, alisema huduma hiyo imesaidia mgonjwa kupata matibabu kwa haraka tofauti na awali.
Mgonjwa mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema lifika hospitalini hapo kwa ajili ya vipimo na kupiga picha X ­ Ray, na alitakiwa kulipa gharama ya Sh3,000, aliilipa kwa kutumia kadi yake ya benki.
“Jana nilikuwa sijaingiziwa fedha ofisini, zikaingizwa jioni ndiyo maana nimekuja leo nimelipa kwa kadi yangu ya benki na nimefika dirishani nikajieleza taarifa zangu zikatumwa huku imefika zamu yangu nimeitwa kwenda kumuona daktari kwa matibabu zaidi,” alisema.
Mgonjwa mwingine, Zamda Athumani alisema: “Hii narudi mara ya pili, wasipoingiza taarifa vizuri utaganda kwa daktari, kwenye vipimo na ukiuliza wahusika wakikuangalia kama haupo hupati huduma, nimerudi wamerekebisha ndiyo nakwenda kumuona daktari sasa,” alisema Zamda.
MWANANCHI
Tanzania imetangazwa rasmi kuwa ni mojwapo ya nchi isiyokuwa na ugonjwa wa polio katika nchi za Afrika katika mkutano wa Tume ya Afrika ya kuthibitishwa kutokomezwa kwa polio(Afrika Regional Certification Commission for Polio Eradication).
Kutangazwa kulifanyika katika mkutano huo uliofanyika nchini Madagascar, Novemba 26, mwaka huu. Kauli hiyo ilitolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.
Donan Mmbando wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam.
“Hii inamaanisha kuwa kwa sasa hatuna ugonjwa wa polio tena nchini kwa sababu tumeweza kuwafikia watoto wengi zaidi kwa kuwapatia chanjo ya polio na hivyo kuongeza kinga kwenye jamii.
Kutokana na mafanikio hayo, tunatakiwa bado kuendelea na kutoa chanjo ya polio kwa watoto wote stahiki ili kuongeza kinga kwa jamii pamoja kuimarisha mfumo wa ufutiliaji wa mgonjwa yoyote mwenye ulemavu wa ghafla,” alisema Dkt. Mmbando.
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba mgonjwa wa mwisho wa polio alipatikana Julai mwaka 1996 hapa nchini. Aliongeza kuwa ufuatiliaji wa magonjwa yanayokingwa na chanjo uliimarishwa na kufikia viwango vinavyo kukubalika kimataifa na kuthibitisha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 waliopata ulemavu wa ghafla wanapatikana na sampuli zao kuchukuliwa mara moja.
Hivyo kuanzia mwaka 1997 mpaka Oktoba 2015 jumla ya sampuli 6,249 za watoto waliopata ulemavu zilipelekwa kwenye maabara za kimataifa na kuthibitishwa kuwa hakuna sampuli iliyoonesha uwepo wa ugonjwa wa polio.
Dkt. Mmbando aliongeza kwamba wizara yake kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imekuwa ikihakikisha kwamba watoto wote Tanzania wanapata chanjo zenye ubora ili kuwakinga dhidi ya magonjwa ya milipuko ikiwemo ugonjwa wa polio.
“ Mwitikio wa wananchi kwa huduma za chanjo umeendelea kuwa mkubwa kwa takribani miaka kumi iliyopita na kufikia viwango vya zaidi ya asilimia 90 kwa kila chanjo kitaifa na wilaya zaidi ya asilimia 80 kufanya vizuri katika kutoa huduma za chanjo,” alisema Dkt. Mmbando. Ugonjwa wa polio ni ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na virusi vya polio, unaathiri misuli na mfumo wa fahamu hivyo kusababisha kupooza kwa viungo hasa na miguu na wakati mwingine kusababisha hata kifo .
Alisema ulemavu huo ukishajitokeza huwa ni wa kudumu, waathirika wakuu wa ugonjwa huo ni watoto hasa waliaochini ya umri wa miaka mitano. Aliongeza kwamba ugonjwa huo unazuilika kwa chanjo ya polio ambayo ni salama na inatolewa bure na Serikali katika vituo vyote vya huduma ya afya. Dkt.
Mmbando alitoa pongezi kwa wananchi wote wakiwemo viongozi na watendaji wa ngazi zote kwa ushirikiano wao ambao umeifikisha Tanzania kwenye ramani ya dunia ya kutokuwa na ugonjwa huo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi nne ambazo zimepata cheti hicho mwaka huu, katika bara hilo.Pia ni nchi ya 33 kati ya nchi 47 za bara hilo ziliowahi kupata cheti hicho. Katika bara hilo bado nchi 14 ambazo hazijawahi kupata cheti hicho.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment