Wednesday, December 16, 2015

TANESCO MUHEZA YAENDESHA MSAKO WA NYUMBA KWA NYUMBA WEZI WA UMEME



Tangakumekuchablog
Muheza,SHIRIKA la umeme Tanzania Tanesco Wilaya ya Muheza imendesha operesheni ya nyumba kwa nyumba kubaini watu wanaotumia umeme wa wizi na kufanikiwa kuwakamta watu kumi waliokuwa wamejiunganishia umeme kinyume na taratibu.
Operesheni hiyo iliyofanyika kata ya Genge, Mbaramo, Majengo na Misozwe na kusimamiwa na Menejea wa Tanesco Wilaya ya Muheza, Edward Mwakapuja na Mhandisi na mdhibiti wa upotevu wa umeme Mkoa wa Tanga, Kassim Rajabu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya operesheni hiyo, Meneja wa Shirika la umeme Tanzania Tanesco Wilaya ya Muheza, Edward Mwakapuja, aliwataka wateja wote wanaotumia umeme wa wizi kujisalimisha kabla wakaguzi kuwafikia.
Alisema msako huo utakuwa wa nyumba kwa nyumba na kuwa endelevu hivyo kuwataka wateja wanaotumia umeme wa wizi kujisalimisha wenyewe kwa shirika hilo na kupata msamaha kwa kutopelekwa mahakamani.
“Leo tumefanya operesheni ya nyumba kwa nyumba na kuwakamata wateja kumi wakitumia umeme wa wizi-----tunasema kama kuna wengine  wajisalimishe wenyewe kabla sisi kuwafikia” alisema Mwakapuja
Kwa upande wake Mhandisi wa Shirika la Umeme Mkoa wa Tanga, Kassim Rajab, aliwataka wateja wa shirika hilokuacha kurubuniwa na vishoka kwa madai kuwa mwisho wake  atakaeathirika ni mteja.
Alisema kuwa mafundi vishoka ambao huwarubuni wateja kuwaunganishia umeme kwa njia za wizi na kujipatia kitu kidogo na mwisho wa siku mteja ndie muathirika.
“Nawaomba wateja wetu kuacha kurubuniwa na mafundi vishoka kwani mwisho wa siku itakuja kubainika tu------umeme wa wizi hauna mwisho mwema” alisema Rajab
Alisema ili kuepuka sheria ni vyema mteja wa shirika hilo kutoa tarifa pale anapobaini kuwa na tatizo nyumbani kwake na kuacha kulikalia ikiwa na pamoja na kutoa taarifa za nyumba zitumiazo umeme wa wizi.
                                                  Mwisho




 Mkaguzi wa mita za umeme shirika la umeme Tanzania Tanesco Mkoa wa Tanga, Omari Abdi akikagua mita za umeme wakati wa operesheni Wilayani Muheza  kukagua mita ambazo zimeunganishwa kinyemela na kuibia Tanesco operesheni iliyofanyika jana


No comments:

Post a Comment