HADITHI
MWANAMKE 18
ILIPOISHIA
“Yule mzee alinyamaza kimya akitafakari kwa sekunde zisizopungua tano kisha akaniuliza.
“Huyo msichana ni nani wako?”
“Tunafahamiana tu, tulikuwa tumekaa
tunazungumza”
“Sasa nataka kukueleza kitu
kimoja. Mmoja wa wale vijana waliompora huyo msichana ni mwanangu. Jana usiku
aliporudi nyumbani hatukulala”
“Kwanini?”
“Yule kijana alipoingia
chumbani mwake tulisikia anapiga kelele. Mimi nikaenda kumuuliza ana matatizo
gani, akaniambia kwamba kila anapopitiwa na usingizi anamuona mwanamke anampiga
bakora. Nikamuuliza ni mwanamke gani huyo, ndio akanieleza kwamba kuna mwanamke
walimpora mkoba wake na ndiye huyo anayemuona anampiga bakora.
“Hiyo hali iliendelea hadi
asubuhi, kila akifumba macho tu anamuona, anamtandika. Bakora zimeota mgongoni
mwake. Huyo mwanamke haonekani, anamuona yeye tu pale anapolala.
“Hii asubuhi tukaenda kwa
huyo mwenzake, kumbe na yeye hali ni hiyo hiyo. Amepigwa bakora usiku kucha.
Bakora zimeota kwenye mgongo wake. Kwa kweli nimewagombesha sana wale vijana kwa kututia aibu sisi wazazi
wao kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu wakiwa bado wadogo, kuibia watu,
kupiga watu na kuvuta bangi. Imebidi niwaulize ni mwanamke gani huyo
waliyempora mkoba wake ndipo mwanangu aliponielekeza kwako. Kumbe alikuwa
anakufahamu.
“Sasa mwanangu nimekuja,
nakuomba unioneshe yule mwanamke nimlipe ule mkoba wake na nimuombe radhi ili
wale vijana waondokewe na ile hali”
Yale maneno aliyonieleza yule
mzee yalinishangaza na kunishitua. Wakati yule mzee ananieleza mimi nilikuwa
natokwa na jasho.
“Kwani mpaka hii asubuhi
wanaendelea kuchapwa bakora?’ nikamuuliza.
“Labda wakae bila kusinzia au
kulala. Wanapolala kidogo tu tayari wanapiga kelele wanasema wanachapwa. Ni
mpaka hii asubuhi hawajalala tangu jana wako macho tu. Wameshadhoofika. Kama hii hali itaendelea watakufa”
“Mzee wangu nikwambie ukweli, yule
mwanamke tulikutana pale pale. Sijui anapoishi na sidhani kama
nitamuona tena”
SASA ENDELEA
Mzee akashituka
na kujishika kichwa.
“Mimi nilidhani unajuana na
huyo mwanamke. Basi wale vijana hawatakuwa na maisha tena” Mzee akasema kisha akaniuliza.
“Unasema kweli, hujuani naye
kabisa?’
“Sijuani naye mzee wangu,
siwezi kukudanganya. Tulikutana pale pale, kila mmoja alikuja kivyake na
aliondoka kivyake’
Mzee aliduwaa kwa sekunde
zisizopungua kumi, alipozinduka aliniuliza.
“Hivi mwanangu utanisaidiaje
na balaa hili?”
“Mzee wangu sina namna yoyote
ya kukusaidia”
“Tuseme yule mwanamke
alikwenda kwa mganga kuwaroga wale vijana?”
“Kwa waswahili hilo jambo linawezekana
lakini siwezi kujua”
“Sasa nifanyeje?”
Sikumjibu yule mzee.
Alionesha wazi alikuwa amechanganykiwa. Alipoona nipo kimya, aligeuka bila
kuniaga na kushuka kwenye baraza ya nyumba yangu. Nikamsikia akisema peke yake.
“Kama
hawatakoma, hawatakoma tena!”
Alipofika chini ya baraza
ndipo alipokumbuka kuniaga.
“Haya kwaheri mwanangu”
akaniambia.
Nilimuangalia yule mzee hadi
alipokata kona mtaa wa pili, lakini mawazo yangu yalikuwa kwa Zena. Kitendo
kile cha kuwatandika wale vijana bakora kilionesha kuwa mwanamke yule wa kijini
alikuwa wa hatari.
Nilikumbuka wakati wale
vijana wamempora mkoba wake alionekana mtulivu ingawa alionesha kuwa na hasira.
Aliniambia “Waache tu” kumbe alikuwa na lake alilokuwa
amelipanga.
Japokuwa niliwahurumia hao
vijana lakini sikujua ningempata wapi huyo Zena ili nimwambie awasamehe hao
vijana. Na hata kama ningekutana naye na kumwambia hivyo sikudhani kama angenisikia.
Nilirudi ndani na kuendelea
kujiwazia. Nilihisi kwamba hata mimi maisha yangu yangeweza kuwa katika hatari kama nitakataa kumuoa Zena na kwa kweli hata hapo
nitakapokutana naye nitashindwa kumueleza ukweli
kwamba sikubaliani na matakwa yake ya kumuoa.
Kwa vyovyote vile yule mwanamke
anaweza kunidhuru!
Nilipowaza hivyo nilitoka
tena. Nikafunga mlango wangu na kuondoka na pikipiki yangu, nikaenda nyumbani
kwa mama.
Kitendo cha kurudi tena kwa
mama kilimshitua, akaniuliza.
“Kulikoni?”
“Nimerudi tena” nikamwambia.
“Ndio mana nimekuuliza
kulikoni?”
Nikamueleza mama kile kisa
cha yule jini kuwatandika bakora wale vijana waliomuibia mkoba wake.
“Baba wa mmoja wa wale vijana
ameniambia hao vijana hivi sasa wako taabani wanamtafuta yule msichana wamuombe
msamaha” nikamwambia.
Mama naye alishituka.
“Yaani wanapolala ndio
wanamuona huyo msichana anawatandika bakora?”
“Ndio mama, na inakuwa usiku
kucha na mchana kutwa. Miili ya wale vijana imeota makora migongoni”
“Huyo jini ni mbaya sana”
“Sasa nimefikiri hata mimi
anaweza kuja kuniletea madhara kama nitakataa
kumuoa”
“Ni kweli, sasa nikupeleke
kwa mganga”
“Wapi?”
“Kule Mnyanjani, ni hodari sana kwa majini”
“Ndio maana nimekuja ili
tushauriane kwenda kwa huyo mganga, vinginevyo naweza kupata balaa”
“Sasa nikupeleke lini?”
“Leo, twende leo”
“Saa ngapi?’
“Maliza kazi zako nitakufuata saa
tisa twende”
“Sawa. Basi njoo hapo saa
tisa twende”
Tulipokubaliana na mama
nikaondoka. Wakati nafika nyumbani kwangu nikakutana na yule mzee akiondoka.
“Nimegonga mlango, nimeona
kimya. Nilikuwa naenda zangu” akaniambia.
“Nilitoka kidogo”
“Nimekuja kukujulisha kuwa
yule mwanangu ameshafariki
dunia”
Nikashituka.
“Eh ameshafariki!”
“Amefariki kama nusu saa hivi
iliyopita akiwa kwa mganga. Tulikuwa tumempeleka kwa mganga baada ya mateso kumzidia”
“Poleni sana jamani. Yule mwenzake naye
anaendeleaje?’
“Sijapata habari zake.
Nimekuja kukwambia hivyo, kwaheri mwanangu”
Mzee huyo akaondoka. Nilipata
hofu sana.
Sikuweza hata kuingia ndani. Niliona kama vile
nitakutana na jini huyo, nikageuza pikipiki na kurudi kwa mama.
Nilipofika nilimuhadithia
lile tukio la kufa kwa mmoja wa wale vijana.
“Nimekuja nikusubri hapa
hapa, sikuingia hata nyumbani kwangu” nikamwambia.
Chakula cha mchana nilikula
pale pale kwa mama. Baada ya kula ndipo tulipoondoka. Nilimpakia mama kwenye
pikipiki tukaelekea huko Mnyanjani.
Wakati huo eneo hilo la Mnyanjani lilikuwa kama
kitongoji cha mji huo. Likiwa karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi, lilikuwa
moja ya maeneo ya kiasili ya mji wa Tanga yenye historia iliyosheheni utamaduni
wa jiji hilo.
Eneo hilo
hivi sasa limebadilika na kuwa na nyumba za kisasa na kuwa sehemu ya jiji hilo.
Ili ufike Mnyanjani unapita vitongoji kadhaa pamoja na
viunga vya minazi. Ni mwendo wa karibu kilometa kumi.
Mama alinionesha nyumba ya mganga
huyo iliyokuwa imejengwa kwa miti na udongo na kuezekwa makuti ya minazi.
Tukasimama na kubisha mlango.
“Karibuni” tukasikia sauti ya
kiume ikitukaribisha.
Tukaingia ndani. Ukumbi ulikuwa giza. Kulikuwa na mwanga hafifu uliotokea
kwenye mlango wa nje na wa uani.
Mganga mwenyewe alikuwa
amekaa kwenye jamvi lililokuwa limetandikwa pale ukumbini. Alikuwa akikatakata
mizizi ya dawa.
“Karibuni” akatuambia tena
huku akitutazama.
“Tumeshakaribia” mama
akamwambia na kisha
kumuuliza hali.
Mimi nikamuamkia. “Shikamoo”
“Marahaba. Karibuni mkake
kwenye jamvi”
Tukakaa kwenye jamvi.
“Tumekuja tuna shida” Mama
akaanza kumwambia mzee huyo aliyekuwa amevaa kikoi cha rangi nyeupe.
“Shida gani?”
MAMBO YAMEFIKA KWA WAGANGA.
JE MGANGA HUYO ATAWEZA KUPAMBANA NA MWANAMKE HUYO WA KIJINI AMBAYE AMESHAONESHA
SI WA KUCHEZEA? SUBIRI HADI HAPO KESHO NIKUPE FULL STORY. NAJUA UNA HARAKA
LAKINI FANYA SUBRA.
TUNAKARIBISHA MATANGAZO. KAMA
UNA TANGAZO LAKO TUONE.
No comments:
Post a Comment