SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 17
ILIPOISHIA
Pakapita ukimya wa
sekunde kadhaa. Bibi alikuwa akiendelea kusuka ukili wake na mimi nilikuwa
nikiumiza kichwa kwa kuwaza. hatimaye nikauondoa ule ukimya.
“Kwa mfano mimi nikipata mke
wa kijini, unanishaurije nioane naye?” nikamuuliza.
Bibi akacheka.
“Bibi mbona unanicheka?”
“Unanichekesha. Huyo mke wa
kijini utampata wapi?”
“Kwani babu alimpata wapi?”
“Yule ni mpaka akuchunuke
mwenyewe”
“Sawa. Je akinichunuka na
kuniambia anataka tuoane, nikubaliane naye?”
“Hayo ni mawazo yako sasa,
mimi nikushauri nini?”
“Unaweza kunishauri kwamba
nioane naye au la”
“Hilo
sio jambo la kushauriwa, ni uamuzi wako na huyo jini kama
utampata. Kwani na wewe unataka kupata utajiri?”
“Hakuna asiyetaka utajiri
bibi”
“Angalia sana, utajiri mwingine una matatizo. Ni bora
uishi masikini hivyo hivyo”
Baada ya kimya kingine kifupi
nikamuaga bibi. Wakati nataka kuondoka nikampa shilingi elfu ishirini. Bibi
akanishukuru.
“Haya bibi nakwenda” nikamuaga
bibi na kupanda pikipiki yangu.
“Uende salama, nisalimie wenzako”
“Nitakusalimia”
SASA SONGA NAYO
Nikawasha pikipiki yangu na
kuondoka. Wakati narudi mjini mawazo yalikuwa yamesonga katika kichwa changu
kuhusu yale maneno aliyonieleza bibi.
Sikuwa nikijua kama babu yangu alimuacha mke wake na kuoa mke wa kijini.
Kwa vile babu mwenyewe alikufa zamani habari zake zilikuwa zimeshahaulika.
Lakini nilijiuliza Zena
alijuaje habari ile? Nikawa na shaka sana
kwamba huyo Zena aliyetajwa na bibi ndiye Zena yule yule.
Nikakumbuka kwamba aliniambia
alikuwa na mimi kwa miaka mingi isipokuwa hakuwa amejitokeza kwangu hivyo
nilikuwa sijui kama nina jini aliyenichunuka.
Pamoja na kufahamu ukweli wote huo bado nilikuwa na mtihani mgumu
mbele yangu, mtihani wa kukubali kuoana na Zena kama
alivyoniambia au kumkataa.
Mpaka muda ule naondoka kwa
bibi sikuwa na uamuzi wowote. Nilitegemea kupata ushauri kwa kaka yangu na kwa
mama yangu.
Nilikwenda moja kwa moja
nyumbani kwa kaka. Nikamwambia.
“Ninatoka Mwambani kwa bibi”
“Umezungumza
naye?” akaniuliza kwa shauku.
“Nimezungumza naye na
anawasalimia”
“Amekuelezaje kuhusu madai ya
babu kuoa mke wa kijini?”
“Amesema ni kweli, babu alioa mke wa kijini
baada ya kumuacha yeye”
Kaka akashituka.
“Kumbe babu alioa mke wa
kijini!”
“Tena alikuwa anaitwa Zena,
jina lile lile la huyu anayenifuata mimi”
Kaka alikuwa amepigwa na
butwaa.
Nikamueleza kwa kirefu
maelezo ya bibi ambayo yalimshangaza sana.
“Isije kuwa jini huyo ndiye
huyu huyu amejitokeza tena”
“Hata mimi nimekuwa
nikijiuliza swali hilo hilo”
“Huyo bibi alikwambia aliwahi
kumuona?’
“Ameniambia hakuwahi kumuona”
“Mimi nadhani jini mwenyewe
ndiye huyo huyo, amejitokeza kwako”
“Inawezekana lakini nitakuja
kumuuliza tupate uhakika”
“Sasa umeamua nini?”
“Bado ninakabiliwa na maswali
mengi. Ninahitaji ushauri wenu ili niweze kuamua”
“Nenda nyumbani umueleze
mama, usikilize atakwambia nini”
“Kwa upande wako unanishauri
nini?”
“Hili ni suala la kujadiliana
sote kwa pamoja lakini kwanza nenda kamueleze mama tusikie kauli yake”
“Sawa. Nitakwenda kumueleza
mama”
Baada ya kuzungumza kirefu na
kaka nikaondoka nyumbani kwake na kwenda nyumbani kwa mama.
Wakati nafika nyumbani, mama
alikuwa amelala. Mjukuu wake alikwenda kumuamsha chumbani. Alipoamka akaja
sebuleni.
“Shikamoo” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari za huko?”
Mama akaniuliza.
“Huko ni kwema. Natoka
Mwambani kwa bibi?”
“Ndio ulikwenda kumuuliza
kuhusu babu yako?”
“Nimemuuliza ameniambia
kwamba babu yetu alimuacha yeye akaoa mke wa kijini”
“Unaniambia ukweli
mwanangu?” Mama akaniuliza kwa mshituko.
“Ameniambia bibi mwenyewe”
“Kumbe babu yako alioa mke wa
kijini?”
“Alioa, na bibi anasema
waliishi pamoja hadi babu alipofikiwa na umauti, yaani wiki moja kabla ya babu
kufariki jini huyo alitoweka”
“Kama ni hivyo inaelekea babu
yenu alikuwa mtu hatari sana!”
“Bibi ameniambia babu
alipomuoa jini huyo alipata utajiri mkubwa, yaani yule jini alimpa utajiri
lakini alipokufa utajiri wake ukapotea”
“Hata kama alipata utajiri,
si jambo la kukubaliana nalo kirahisi”
“Sasa kitu ambacho
kimenitisha ni kuwa huyo jini alikuwa anaitwa Zena kama
jini huyu anayenifuata mimi!”
“Isije kuwa ndiye jini huyo
huyo. Kwanini alikuwambia uende ukamuulize
bibi yako”
“Inawezekana ndiye jini huyo
huyo”
“Sasa sikiliza mwanangu, huyo
jini epukana naye mara moja!”
“Kwanini mama?”
“Atakuharibia maisha yako, kama ni kuoa oa binaadamu mwenzako si jini”
“Kwa hiyo unanishauri hivyo?”
“Inawezekana ni ushauri au ni
amri yangu na naomba unisikilize”
“Sawa, nitakusikiliza.
Nilitaka tu nijue una maoni gani”
“Atakapokufuata tena mwambie
mimi siwezi kukuoa wewe, nitaoa binaadamu mwenzangu. Kwani majini madume hakuna
mpaka akufuate wewe!”
“Ndio nashangaa!”
“Huyo mke wa kijini kweli
utamuonesha kwa wa watu, uwambie mke wangu huyu!”
“Hiwezekani”
“Kwanza
watu watakushangaa na hawatakuja kwako. Mimi pia sitakuja”
Mama alikuwa amekasirika,
sikutaka tena kumjibu kitu. Nikanyamaza kimya.
“Upuuzi mtupu! Amekutia
katika misuko suko chungu nzima halafu uje uishi naye kama
mke wako, kwanza hao watoto mtakaozaa watakuwa ni watoto wa aina gani...epukama
na huyo shetani asikuletee mikosi. Kama ndiye
huyo aliyeolewa na babu yako atokomee huko huko alikokuwa. Mimi simtaki!” Mama
aliendelea kuniambia kwa hasira.
“Sawa mama nimekusikia”
Nilipoondoka kwa mama
nikarudi nyumbani kwangu. Kusema kweli nilikuwa na mawazo mengi sana. Maneno ya mama
yalikuwa yameingia akilini mwangu na wakati huo huo nilikuwa nafikiria endapo
nitamueleza yule jini kwamba siwezi kuoana naye atanifanya nini.
Wakati naendelea kutafakari
nikasikia mlango wangu wa mbele unabishwa. Nikanyanyuka na kwenda kuufungua.
Nilimuona mzee mmoja
aliyekuwa amevaa koti jeusi na kanzu ya darizi pamoja na baraghashia.
Nikamuamkia.
“Shikamoo mzee?”
“Marahaba, waonaje hali
yako?”
“Nzuri, karibu”
“Asante. Nadhani hunifahamu?”
akaniuliza.
“Ndiyo sikufahamu mzee wangu”
“Ninaishi mtaa wa pili. Kuna
mwanangu mmoja ndiye aliyenielekeza hapa kwako”
“Una tatizo gani?”
nikamuuliza kistaarabu.
“Unakumbuka jana majira ya
saa nne asubuhi mpaka tano ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa maeneo ya mjini”
“Bila shaka ulikuwa umekaa
katika Bustani ya Uhuru na msichana mmoja?”
“Ndio nilikuwa nimekaa hapo”
“Nimeambiwa kwamba wakati
yule msichana uliyekuwa naye anaondoka, kuna vijana wawili waliokuwa na
baiskeli walimpora yule msichana mkoba wake na kukimbia nao, ni kweli?’
“Ni kweli’
“Yule mzee alinyamaza kimya akitafakari kwa sekunde zisizopungua tano kisha akaniuliza.
“Huyo msichana ni nani wako?”
“Tunafahamiana tu, tulikuwa
tumekaa tunazungumza”
“Sasa nataka kukueleza kitu
kimoja. Mmoja wa wale vijana waliompora huyo msichana ni mwanangu. Jana usiku
aliporudi nyumbani hatukulala”
“Kwanini?”
“Yule kijana alipoingia
chumbani mwake tulisikia anapiga kelele. Mimi nikaenda kumuuliza ana matatizo
gani, akaniambia kwamba kila anapopitiwa na usingizi anamuona mwanamke anampiga
bakora. Nikamuuliza ni mwanamke gani huyo, ndio akanieleza kwamba kuna mwanamke
walimpora mkoba wake na ndiye huyo anayemuona anampiga bakora.
“Hiyo hali iliendelea hadi
asubuhi, kila akifumba macho tu anamuona, anamtandika. Bakora zimeota mgongoni
mwake. Huyo mwanamke haonekani, anamuona yeye tu pale anapolala.
“Hii asubuhi tukaenda kwa
huyo mwenzake, kumbe na yeye hali ni hiyo hiyo. Amepigwa bakora usiku kucha.
Bakora zimeota kwenye mgongo wake. Kwa kweli nimewagombesha sana wale vijana kwa kututia aibu sisi wazazi
wao kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu wakiwa bado wadogo, kuibia watu,
kupiga watu na kuvuta bangi. Imebidi niwaulize ni mwanamke gani huyo
waliyempora mkoba wake ndipo mwanangu aliponielekeza kwako. Kumbe alikuwa
anakufahamu.
“Sasa mwanangu nimekuja,
nakuomba unioneshe yule mwanamke nimlipe ule mkoba wake na nimuombe radhi ili
wale vijana waondokewe na ile hali”
Yale maneno aliyonieleza yule
mzee yalinishangaza na kunishitua. Wakati yule mzee ananieleza mimi nilikuwa
natokwa na jasho.
“Kwani mpaka hii asubuhi
wanaendelea kuchapwa bakora?’ nikamuuliza.
“Labda wakae bila kusinzia au
kulala. Wanapolala kidogo tu tayari wanapiga kelele wanasema wanachapwa. Ni
mpaka hii asubuhi hawajalala tangu jana wako macho tu. Wameshadhoofika. Kama hii hali itaendelea watakufa”
“Mzee wangu nikwambie ukweli, yule
mwanamke tulikutana pale pale. Sijui anapoishi na sidhani kama
nitamuona tena”
MMMH! MAMBO HAYO!!! LOH KUMBE
YULE MWANAMKE BALAA!!! KWAKWELI ANATISHA!!! HAYA HAWA VIJANA WA WATU ITAKUWAJE
JAMANI!!! MIMI MWENYEWE NIMESHIINGIA UOGA.
No comments:
Post a Comment