Tuesday, June 14, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 20

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572

MWANAMKE 20

ILIPOISHIA

Hirizi yenyewe ilikuwa imeshatayarishwa tayari. Mganga akanipatia. Nikaichukua na kuitia mfukoni.

Nikatoka na kupanda pikipiki yangu. Sasa kidogo moyo wangu ulikuwa na matumaini. Ile hofu niliyokuwa nayo ya kukutana na Zena ilikuwa imenitoka.

Wakati nakaribia kulitoka eneo la Mnyanjani, niliona mtu amesiamama pembeni mwa barabara chini ya mti wa mwembe. Nilipoukaribia mwembe huo nilishituka nilipoona mtu mwenyewe alikuwa  Zena. Alikuwa amesimama kama aliyekuwa akisubiri mtu.

Nikaongeza mwendo ili kumkwepa na nikajifanya sikumuona. Wakati pikipiki imeshika kasi nikahisi kama kulikuwa na kitu nyuma yangu. Nikageuza uso wangu kutazama nyuma. Nilishituka tena. Alikuwa ni Zena aliyekuwa amekaa kwenye siti ya nyuma ya pikipiki yangu!

Sikuweza kujua alipakiaje kwenye pikipiki yangu wakati alikuwa amesimama kwenye mti ambao nilikwishaupita, tena nikienda kwa kasi. Kutokana na mshituko nilioupata mikono yangu ilitetereka nikajikuta ninaanguka na pikipiki. Mimi na Zena tukawa chini!

Nikainuka haraka. Lakini Zena alikuwa mwepesi zaidi. Nilimkuta tayari ameshasimama.

SASA ENDELEA,

“Inua pikipiki yako” akaniambia.

Nikiwa nimetahayari nikaushika usukani wa pikipiki na kuiinua.

“Isimamishe” akaniambia tena.

Nikaiwekea standa.

“Unatoka wapi?”

“Mimi?’

“Jamani kwani nazungumza na nani?”

“Natoka kule…”

“Wapi?”

“Mnyanjani”

“Kufanya nini?”

Nikatunga uongo.

“Kumsalimia mjomba wangu”

Zena akanitazama kwa karibu nusu dakika bila kuniambia chochote. Bila shaka aligundua kuwa nilikuwa namdanganya. Wakati Zena akinitazama jasho jembamba lilikuwa linanitoka. Nilikuwa nikilihsi likitiririka kwenye uti wa mgongo wangu.

Nilikuwa najiuliza yule mganga alinipa hirizi akaniambia nikiwa nayo mfukoni Zena hatanifuata, mbona niko naye hapa?

“Humo mfukoni umetia nini?” Sauti ya Zena ikanishitua.

Alikuwa akiutazama mfuko wa suruali yangu ambao nilitia ile hirizi.

“Wapi?” nikamuuliza tena nikijifanya sikumuelewa.

“Nimekuuliza humo mfukoni mwako umetia nini?” Zena akaniuliza tena sasa kwa sauti ya ukali kidogo.

“Sijatia kitu, ni pesa zangu tu” nikamjibu.

“Hebu tia mkono wako mfukoni” akaniambia.

Nikatia mkono kwenye mfuko mwingine.

“Sio huo, tia kwenye mfuko huu”

Zena alinionesha mfuko huo kwa kidole chake.

Nikatia mkono kwenye mfuko huo.

“Hebu toa hicho kitu ulichokigusa”

Bila kupenda niliitoa ile hirizi.

“Hebu nioneshe”

Nikamuonesha, hata haikumshtua.

Akaishika na kuiweka kwenye kiganja chake kisha akanitazama.

“Nini hii?’ akaniuliza kwa dharau.

Sikumjibu. Nilikuwa nimefadhaika sana.

“Wewe unajidanganya sana, sikujua kama unaweza kuwa mpumbavu kiasi hicho. Shika hirizi yako” akaniambia.

Nikaichukua ile hirizi.

“Itupe kule!” akaniambia akinionesha kitu kilichokuwa kando yetu.

Nikaitupa. Ningefanyaje? Sikuwa na la kufanya. Hirizi yenyewe haikumtisha hata kidogo. Bora kuitupa tu.

“Nipakie twende zetu” akaniambia akiwa ameridhika kwa kile kitendo cha kuitupa ile hirizi.

Sikutaka hata kumuuliza twende wapi, nikawasha pikipiki iliyokuwa imezimika kisha nikaipanda. Zena akakaa nyuma yangu. Nikatia gea na kuondoka.

Nilikuwa naendesha pikipiki huku natetemeka mpaka Zena akaniuliza.

“Unatetemeka nini?”

“Sitetemeki” nikamjibu huku nikijua kuwa nilikuwa natetemeka.

Akanyamaza kimya. Hakunisemesha kitu mpaka tulipoingia mjini.

“Nishushe hapa” akaniambia mara tu tulipoipita hospitali ya Makorora.

Nikashukuru kusikia kauli hiyo. Nilikuwa nikihisi kama nimepakia chatu nyuma yangu. Nikaisimamisha pikipiki haraka na kushusha mguu wangu.

Zena akashuka.

“Niache hapa hapa. Wewe nenda zako” akaniambia.

Ingawa sauti yake ilikuwa tulivu lakini uso wake ulikuwa umekasirika. Nikamuona anavuka barabara na kuelekea upande wa hospitali ya Makorora.

Nikatia gea na kuiondoa pikipiki yangu taratibu. Sikutazama nyuma tena. Nilipofika kwenye mzunguko wa barabara ya Pangani nilikata kulia nikaelekea nyumbani kwa mama. Sikutaka kwenda nyumbani kwangu ingawa palikuwa karibu na hapo.

Nilipofika nyumbani kwa mama nikamueleza tukio zima lililokuwa limenitokea. Mama akashituka.

“Sasa huyo shetani amekwenda wapi?” akaniuliza.

“Sijui amekwenda wapi. Nimemuacha karibu na hospitali ya Makorora”

“Ina maana alikufutilia kule kwa mganga”

“Nafikiri. Amejua kuwa nimepewa hirizi na akaona iko mfukoni mwangu”

“Sasa itakuwaje?”

“Hata sijui. Hapa mwili wote unanitetemeka”

“Sasa ungerudi umueleze yule mganga”

“Unanishuri nirudi tena kwa yule mganga?”

“Ndio. Umueleze habari yote. Yeye ndio atajua la kufanya”

“Sasa twende sote. Yule jini asije akanifuata tena”

“Ngoja twende”

Dakika chache baadaye mimi na mama yangu tukawa kwenye pikipiki tukielekea Mnyanjani kwa yule mganga. Tulipofika pale mahali nilipoanguka na pikipiki nilimuonesha mama.

“Mahali tulipoanguka ni hapa” nikamwambia.

“Na huyo jini mwenyewe ulimuona amesimama wapi?”

“Alikuwa amesimama kwenye mti ule pale”

Nikamuonesha mti wa mwembe nilipomuona Zena amesimama.

“Inaonekana alikuwa akikufuatilia wewe” Mama akaniambia.

Tulipofika nyumbani kwa mganga tulikuta vilio vimetawala ndani ya nyumba huku nyumba yenyewe imeja watu hadi nje.

“Kuna nini?” nikamuuliza mama kabla ya kushuka kwenye pikipiki.

“Ngoja tuulize” Mama akaniambia.

Tulishuka kwenye pikipiki. Mtu mmoja alipotuona tulikuwa wageni akatufuata.

“Karibuni” akatuambia.

“Tumeshakaribia” Mama akamjibu.

“Habari za hapa?” nikamuuliza.

“Hapa si kwema, tumepata msiba” yule mtu akatuambia.

“Msiba wa nani?”

“Msiba wa huyu bwana aliyekuwa anaishi katika nyumba hii”

Nikatazamana na mama yangu kisha nikaendelea kumuuliza yule mtu.

“Sisi tunachojua ni kuwa mwenye nyumba hii ni yule mganga wa kienyeji”

“Niye huyo huyo aliyefariki”

Nikatazamana tena na mama yangu, sasa kwa mshituko.

“Dakika chache tu zilizopita si nilikuwa naye hapa?” nikauliza.

“Kufariki kwake kulikuwa kwa miujiza sana. Niliambiwa alikuwa akizungumza na mteja wake mmoja aliyefika na pikipiki, nafikiri ulikuwa wewe”

“Nadhani nilikuwa mimi kwani si muda mrefu sana nilipoondoka hapa”

“Basi mara tu ulipoondoka, yule mganga aliingia chumbani mwake. Mke wake alikuwa jikoni akasikia sauti ya mume wake akipiga kelele kuwa anakabwa na mwanamke. Mpaka mke wake anaingia chumbani alimkuta ameshakufa”

“Nikaguna na kumtazama mama.

“Mama umelisikia hilo tukio?”

“Nimelisikia” Mama akajibu kwa sauti iliyonywea kisha akaniambia.

“Basi twende zetu”

“Nilikuwa nimempa pesa kwa ajili ya kunifanyia kazi yangu ambayo tulipatana aifanye kesho lakini nitamsamehe” nikasema.

“Ulimpa kiasi gani?’ yule mtu akaniuliza.

“Kama laki mbili hivi. Lakini nitasamehe”

“Kama umeamua kuzisamehe ni jambo zuri”

“Poleni sana kwa msiba huo” nikamwambia na kupanda kwenye pikipiki yangu.

“Haya kwaheri baba” Mama akumuaga yule mtu kabla ya kukaa nyuma yangu. Tukaondoka.

WASOMAJI WANGU, MAMBO HAYO! MGANGA AMESHAUAWA! NAFIKIRI JAMAA HATAKUWA NA UJANJA TENA! LAKINI HADITHI INAENDELEA NA BLOGY YETU BADO INAKUALIKA WEWE MSOMAJI WAKE KESHO UTUTEMBELEE TENA, NI TANGA KUMEKUCHA.

HUWEZI KUPATA MAMBO MAKUBWA KAMA HAYA KATIKA BLOG YOYOTE HAPA NCHINI


No comments:

Post a Comment