Monday, June 13, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 19

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572

MWANAMKE 19

ILIPOISHIA

Wakati huo eneo hilo la Mnyanjani lilikuwa kama kitongoji cha mji huo. Likiwa karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi, lilikuwa moja ya maeneo ya kiasili ya mji wa Tanga yenye historia iliyosheheni utamaduni wa jiji hilo.

Eneo hilo hivi sasa limebadilika na kuwa na nyumba za kisasa na kuwa sehemu ya jiji hilo.

Ili ufike Mnyanjani unapita vitongoji kadhaa pamoja na viunga vya minazi. Ni mwendo wa karibu kilometa kumi.

Mama alinionesha nyumba ya mganga huyo iliyokuwa imejengwa kwa miti na udongo na kuezekwa makuti ya minazi.

Tukasimama na kubisha mlango.

“Karibuni” tukasikia sauti ya kiume ikitukaribisha.

Tukaingia ndani. Ukumbi ulikuwa giza. Kulikuwa na mwanga hafifu uliotokea kwenye mlango wa nje na wa uani.

Mganga mwenyewe alikuwa amekaa kwenye jamvi lililokuwa limetandikwa pale ukumbini. Alikuwa akikatakata mizizi ya dawa.

“Karibuni” akatuambia tena huku akitutazama.

“Tumeshakaribia” mama akamwambia na kisha kumuuliza hali.

Mimi nikamuamkia. “Shikamoo”

“Marahaba. Karibuni mkae kwenye jamvi”

Tukakaa kwenye jamvi.

“Tumekuja tuna shida” Mama akaanza kumwambia mzee huyo aliyekuwa amevaa kikoi cha rangi nyeupe.

“Shida gani?”

SASA ENDELEA

Mama akamueleza mkasa mzima. Yule mganga naye alishangaa akasema.

“Huyo atakuwa Ummi Subian au Kamari wa Subian”

“Tunataka aondoke kwa mwanangu, asimfuate fuate tena”

“Ngoja nimtazame nijue ni jini gani”

Mganga akachukua kitabu akakifungua kisha akatazama saa yake.

“Ni saa nane sasa” alisema peke yake kisha akatazama kwenye kitabu.

“Aliyetawala muda huu ni Zuhra Kadhi Lhawaiju” Mganga aliendelea kujisemea kisha akatutazama.

“Huyu mwanamke wa kijini ni ruhani aliyechanganya na usubian”

“Yeye mwenyewe pia aliniambia hivyo hivyo” nikamkubalia mganga huyo.

“Hawa majini ni ving’ang’anizi sana na ni wabishi, akitaka jambo lake ni mpaka alitimize”

“Lakini ataweza kumuacha huyu mwanangu?” Mama akamuuliza kwa wasiwasi.

“Ni kazi kubwa. Huyu jini ni wa kurithi, zamani aliwahi kuwa na babu yake huyu kijana”

“Ni kweli, bibi yangu alinieleza leo” nikamwambia mganga huyo.

“Alikuelezaje?”

“Aliniambia kuwa babu yangu alikuwa na mke wa kijini, anaitwa Zena”

Mganga akamtazama mama.

“Unasikia. Sasa kumtoa jini wa aina hii inataka kazi kubwa, si kazi ndogo”

“Sasa tufanyeje?” Mama akamuuliza.

“Nitahitaji mbuzi watatu, wa rangi nyeupe, rangi nyeusi na rangi mchanganyiko” Mganga alituambia kisha akatuuliza.

“Mtaweza kuwapata?”

“Watapatikana” nikajibu mimi.

“Mbali na hao mbuzi watatu, mnipatie maji ya bahari lita tatu, mchanga wa pwani unaofikia kilo moja na kipande cha mti kilichotoka katika eneo lililopiganwa vita”

“Hicho kipande cha mti tutakipata wapi?” nikamuuliza.

“Najua hiki kitawapa tabu, nitawapatia mimi”

“Huo mchanga wa pwani na maji ya bahari pia ungetusaidia wewe, tunaona hapa ni karibu na bahari”

“Gharama yake itakuwa shilingi elfu kumi na tano”

“Sawa.Tutatoa”

“Hao mbuzi watatu pia mnaweza kuwapata hapa hapa kama mtataka”

“Watakuwa kiasi gani?”

“Kila mbuzi mmoja ni shilingi elfu arobaini”

“Kwa hiyo kwa mbuzi watatu itakuwa shilingi laki moja na ishirini elfu”

“Ingiza na hizi elfu kumi na tano za vifaa”

“Zitakuwa laki moja na hamsini na tano elfu”

“Na kazi yangu shilingi laki moja”

“Jumla laki mbili na hamsini na tano elfu”

“Hizo pesa zikipatikana, njooni niwafanyie kazi yenu”

“Pesa zipo lakini zipo nyumbani, labda utupe muda nikazichukue” nikamwambia mganga huyo.

“Hizo pesa nikizipata leo, kwanza nitashughulikia kupata hivyo vitu, Kesho saa mbili asubuhi ndio nitakushughulikia wewe mwenyewe”

“Sawa. Sasa acha turudi. Baadaye nitakuja na hizo pesa.

Baada ya kukubaliana na mganga huyo tuliondoka. Nilimpakia mama kwenye pikipiki nikamrudisha nyumbani kwake kisha mimi nikaenda nyumbani kwangu kuchukua hizo pesa. Zilikuwa ni pesa zile zile alizonipa Zena.

Nilitia mfukoni shilingi laki tatu nikaondoka tena na pikipiki kwenda Mnyanjani. Nilipofika nilimpa yule mganga shilingi laki mbili na hamsini na tano elfu.

“Sasa nenda, uje kesho saa mbili asubuhi, utakuta kila kitu kipo tayari” Mganga akaniambia.

“Sasa nilikuwa na ombi moja” nikamwambia.

“Ndio”

“Nina wasiwasi huyo jini anaweza kunifuata hii leo kutokana na hivi ambavyo nataka kumshughulikia, sasa itakuwaje?

“Nitakupa hirizi, kuwa nayo mfukoni hadi hapo kesho”

“Nikiwa na hiyo hirizi hatanifuata?’

“Abadani. Hawezi kukufuata”

“Basi nipatie hiyo hirizi’

Hirizi yenyewe ilikuwa imeshatayarishwa tayari. Mganga akanipatia. Nikaichukua na kuitia mfukoni.

Nikatoka na kupanda pikipiki yangu. Sasa kidogo moyo wangu ulikuwa na matumaini. Ile hofu niliyokuwa nayo ya kukutana na Zena ilikuwa imenitoka.

Wakati nakaribia kulitoka eneo la Mnyanjani, niliona mtu amesiamama pembeni mwa barabara chini ya mti wa mwembe. Nilipoukaribia mwembe huo nilishituka nilipoona mtu mwenyewe alikuwa  Zena. Alikuwa amesimama kama aliyekuwa akisubiri mtu.

Nikaongeza mwendo ili kumkwepa na nikajifanya sikumuona. Wakati pikipiki imeshika kasi nikahisi kama kulikuwa na kitu nyuma yangu. Nikageuza uso wangu kutazama nyuma. Nilishituka tena. Alikuwa ni Zena aliyekuwa amekaa kwenye siti ya nyuma ya pikipiki yangu!

Sikuweza kujua alipakiaje kwenye pikipiki yangu wakati alikuwa amesimama kwenye mti ambao nilikwishaupita, tena nikienda kwa kasi. Kutokana na mshituko nilioupata mikono yangu ilitetereka nikajikuta ninaanguka na pikipiki. Mimi na Zena tukawa chini!

Nikainuka haraka. Lakini Zena alikuwa mwepesi zaidi. Nilimkuta tayari ameshasimama.

DUH! JAMAA AMEKWAMA! KAPEWA HIRIZI LAKINI JINI KAMTOKEA HIVYO HIVYO. Sijui itakuwaje?

Kama kawaida kwa leo tunaishia hapa lakini kesho panapomajaliwa tutakuwa tena uwanjani. Usikose kututembelea. Ni TANGA KUMEKUCHA,

No comments:

Post a Comment