Monday, March 23, 2015

BARAZA LA UONGOZI CHADEMA MKOA LAWASIMAMISHA VIONGOZI WAKE HANDENI



Tangakumekuchablog

Tanga, BARAZA la Uongozi Chadema Mkoa wa Tanga , limwasimamisha kazi Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wa Chama hicho Wilaya ya Handeni kwa kushindwa kuwajibika ndani ya chama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Chadema Mkoni hapa, Said Mbweto, alisema uongozi wa chama hicho umewasimamisha kazi viongozi hao hadi uchunguzi dhidi yao utakapomalizika.

Alisema tuhuma zinazomkabili mwenyekiti wa Wilaya, Jadi Bamba ni pamoja na kushindwa kukitumikia chama kulingana na nafasi yake na kusababisha makundi ndani ya chama na  kushindwa kupata nafasi za kuongoza na kuongeza  wanachama.

Alisema chama hicho kimeshindwa kuwa na umoja na kuunda timu moja ya ushindi jambo ambalo limesababisha wanachama kuunda makundi ndani ya chama na hivyo ili kukinusuru uongozi umechukua maamuzi ya kumsimamisha nafasi yake.

“Baraza la uongozi Chadema  mkoa limepitisha uamuzi mmoja wa kuwasimamisha kazi mwenyekiti pamoja na katibu na wajumbe wote wa Chadema wilaya kwa tuhuma za kukihujumu chama” alisema

“Kusimamishwa kwao haijulikani hadi lini lakini hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika----kwa sasa kuna taratibu zinafuatwa ila  wataendelea kufanya kazi za chama na sio kwa nafasi zao” alisema Mbweto

Akizungumzia nafasi ya Katibu, Ramia Kisalazo, alisema ameshindwa kuitumia nafasi yake jambo ambalo wanachama na wapenzi wa chama hicho wamekuwa wakilalamika kwa kushindwa kukitumikia chama kwa nafasi yake.

Alisema Kisalazo amesababisha kutoa mwanya kwa vyama pinzani kujiimarisha na kuchukua maeneo ambayo tayari yalikuwa na ushawishi mkubwa wa Chadema na kuwa na uhakika uchaguzi mkuu ujao kufanya vizuri nafasi za Udiwani.

Alisema kwa mantiki hiyo pamoja na wajumbe wa Chadema Wilaya ya Handeni, Baraza la uongozi Mkoa kwa kutumia vifungu vya Katiba yake 6..3..4 (c) imewasimamisha kazi na uchunguzi dhidi yao unafanyika.

Kwa upande wake Katibu wa Chadema Mkoa, Ismail Massoud, alisema Chama hicho kimejipanga kwa kufanya mikutano mfululizo  ya kuhamasisha chama mjini na vijijini na kuwataka wananchi kukiunga mkono Chadema.

Alisema kwa sasa wanaweka nguvu zaidi vijijini ambako kuna kero nyingi za huduma za kijamii ikiwemo maji safi na usafiri na kuwaeleza Chama Cha Mapinduzi kushindwa kutekeleza ahadi yake ya Maisha Bora kila Mtanzania.

Alisema CCM ilitoa ahadi wakati wa kampeni uchaguzi mkuu uliopita ya kuwapatia huduma bora wananchi wake lakini hadi sasa ambapo unakaribia uchaguzi mwengine hakuna kilichotekelezwa zaidi ya wananchi kuteseka.

Alisema wananchi wa vijijini wako na kero nyingi zikiwemo za upatikanaji wa maji safi na miundombinu ya usafiri wa barabara na hivyo Chadema itafika kila kijiji na kuwaeleza ahadi zilizotolewa kama zimetekelezwa.

“Tutatumia mtaji wa ahadi ya CCM wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kama wamezitekeleza kwa wananchi jibu watakalotuambia kwetu ni mtaji kwani hata yale ambayo hawatayasema sisi tutawakumbusha”” alisema Massoud

Alisema kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, Chadema itahakikisha inashinda nafasi za Ubunge na Udiwani katika majimbo ya Mkoa wa Tanga na kuwataka wananchi kukiunga mkono kwa kuzisikiliza sera zao wakati wa mikutano ambayo imeshaanza kwa baadhi ya maeneo.

                                                           Mwisho

No comments:

Post a Comment