Tanga, MKUU wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula,
amevitaka vituo vya afya Tanga kutumia fursa ya mikopo itolewayo na
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ikiwemo vifaa tiba na madawa na kuweza kuwa
msaada kwa wananchi katika kupata huduma zilizo bora.
Akizungumza katika kikao cha
uhamasishaji mpango wa mikopo ya vifaa tiba
kilichofanyika hospitali ya Mkoa ya Bombo, Magalula aliwaagiza waganga wakuu wa
hospitali Mkoa na Wilayani kuitumia nafasi hiyo itolewayo na Bima ya Afya.
Alisema kelele za wananchi
kulalamikia huduma mbovu zitolewazo katika vituo imezidi wakati ziko
fursa za kupunguza kero hizo kwa kukopa vifaa pamoja na ukarabati wa majengo
jambo ambalo ni nadra kuipata nafasi hiyo.
“Kumbe kuna fursa kama hizi
zitolewazo na wadau wetu wa afya mimi nilikuwa sijui-----kwa nini sasa
hamuzichangamkii na kupunguza kelele za wananchi kulalamikia huduma mbovu
zikiwemo uhaba wa madawa” alisema na kuongeza
“Kwa maana hiyo natoa agizo kwa
waganga wakuu wa hospitali zote za mjini na Wilayani kuhakikisha wanaitumia
ipasavyo fursa hii na kumaliza manung;uniko kutoka kwa wananchi juu ya
hospitali na vituo vyetu vya afya” alisema Magalula
Alisema kuna baadhi ya vituo vya afya
majengo yake yako katika mazingira hatarishi na mengine kufikia hatua ya
kutaka kuanguka na hivyo kuwaagiza kuchangamkia nafasi inayotolewa na
mfuko wa bima ya afya.
Alisema majengo mengi yako katika
hali mbaya ikiwemo miundombinu ya kupitishia maji na uchakavu wa majengo jambo
ambalo linaondoa taswira ya mazingira ya afya kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Taifa Mfuko
wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga, Ali Mwakababu, alisema mbali ya elimu na
matangazo mengi lakini hadi sasa ni vituo vichache ambavyo vimejitokeza kutaka
mikopo.
Alisema elimu bado inahitajika na
hivyo kuitaka Wizara ya Afya Mkoa kutoa elimu kwa Waganga wakuu wa Wilaya
kuomba mikopo ambayo inaweza kusaidia kuimarisha huduma zao zikiwemo matibabu
na ukarabati wa majengo.
“Toka mwaka 2007 Bima ya Afya
ilipoanzisha huduma ya kutoa mikopo ni vituo vichache ambavyo vimeomba
mikopo-----ukiangalia majengo mengi ni chakavu na havina vifaa tiba” alisema
Mwakababu
“Vituo vyetu viko na uhaba wa madawa
wakati mfuko wa bima umeandaa utaratibu wote wa kupata huduma hizo----kuna
hospitali nyingi hazina huduma za Ex ray na hii pia tunatoa” alisema
Meneja huyo aliwataka waganga wakuu
wa Wilaya kuhakikisha wanamaliza changamoto wanazokabiliana nazo katika vituo
vyao lengo likiwa ni kuboresha huduma kwa wananchi.
Mwisho
Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Tanga, Ali Mwakababu akitoa risala wakati wa kikao cha Uhamasishaji Mpango wa Mikopo na Vifaa Tiba kwa watoa huduma kilichofanyika ukumbi wa hospitali ya Mkoa ya Bombo na kuwashirikisha waganga wakuu wa Wilaya na wadau wa Afya Mkoa wa Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, akifungua kikao cha Uhamasishaji mpango wa mikopo na vifaa tiba kwa watoa huduma kilichoandaliwa na Mfuko wa Bima ya Afya Tanga kilichofanyika ukumbi wa hospitali ya Mkoa ya Bombo na kuwashirikisha waganga wakuu wa Wilaya na madaktari pamoja na wadau wa afya.
Washiriki wa kikao cha Uhamasishaji mpango wa mikopo na vifaa tiba kwa watoa huduma kilichoandaliwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF)Tanga na kuwashirikisha waganga wakuu , madaktari na wadau wa Afya kilichofanyika ukumbi wa hospitali ya Mkoa ya Bombo
No comments:
Post a Comment