Mama Sumaye kunyang’anywa mashamba, Gwajima kushtakiwa, wanahabari kufungwa jela? Hizi nimezitoa MAGAZETINI LEO
NIPASHE
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani
Pwani, imewataja vigogo wanaohodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya
kuyaendeleza na kuwapa siku 90 kuhakikisha wanayaendeleza, kinyume
chake yatachukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tatu Suleiman,
ilisema vigogo hao walinunua mashamba katika eneo hilo na kuyaacha muda
mrefu bila kuyaendeleza akiwamo mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mama Ester Sumaye ambaye anamiliki mashamba mawili yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 240 eneo la Misufini, Kibaha vijijini.
Taarifa hiyo inawataja watu wengine maarufu ambao wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo kuwa ni, Phillipo Marmo ambaye ni Balozi wa Tanzania Ujerumani anayemiliki shambamaeneo ya Kikongo, Nicodemus Banduka
ambaye ni mkuu wa mkoa mstaafu wa mikoa ya Pwani, Iringa na Mtwara
anayemiliki shamba eneo la Vikuge ambalo alilipata mwaka 2000 na Kipi Warioba aliyewahi kuteuliwa kugombea Ubunge Jimbo la Kawe ambaye anamiliki eneo Mperamumbi lenye ukubwa wa heka 4000.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa watu wengi
walichukua mashamba katika eneo hilo kuanzia miaka ya 1986 na kushindwa
kuyaendeleza na kusababisha kuwa mapori hali iliyopelekea halmashauri
hiyo kufuata sheria na kanuni zinazohusiana na umiliki wa ardhi.
Kufuatia mashamba hayo kutelekezwa,
halmashuri ya wilaya hiyo inapanga kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara
husika ili miliki zake zifutwe endapo wahusika watashindwa kuyaendeleza
kwa muda waliopewa.
Tatu, alisema mwaka jana waliwataka watu
wote waliochukua mashamba hayo kuyaendeleza baada ya kufanyiwa uhakiki
na baadhi ya watu walijitokeza kuyaendeleza, lakini watu zaidi ya 40
hawajitokeza.
“Kutokana
na kukahidi kuyaendeleza mashamba hayo, tumeshapeleka majina ya
wamiliki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara
imetutaka tutoe tena siku 90 kama hawatatekeleza kwa kipindi hicho,
watajua nini cha kufanya,’’ alisema.
Gazeti hili lilipowasiliana na Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye
kwa njia ya simu ili kuzungumzia taarifa za mkewe kushindwa
kuyaendeleza mashamba hayo kwa kipindi kirefu, alisema hana taarifa
zozote za mkewe kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo anayomiliki.
‘‘Wewe
ndiyo nakusikia, sisi hatujaliona hilo tangazo, wala mke wangu hana
hizo taarifa ila baadaye tutakapoziona tutakupigia simu tuwasiliane,’’ Sumaye.
NIPASHE
Marais wa nchi za ukanda wa Kati,
wamewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuangalia miradi 23 ya
miundombinu iliyopitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa reli, barabara na
bandari huku wakitaka ushiriki wa sekta binafsi.
Wamewataka wawekezaji hao kujiwekeza na kujenga miradi hiyo kwa ubia na sekta binafsi za ndani na nje.
Wito huo uliyotolewa jana na marais wa
Tanzania, Rwanda, Burundi, na wawakilishi wa Uganda, Kenya na DRC
katika mkutano wa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje,
kujadili namna ya kushirikiana katika uboreshaji wa miradi iliyopitishwa
kwa ajili ya utekelezaji.
Akimkaribisha Rais Paul Kagame wa Rwanda kufungua mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete ,
alisema Rwanda na Tanzania mwaka 2003 zilisaini makubaliano ya ujenzi
wa reli ya Dar Isaka hadi Rwanda, lakini kutokana na umuhimu wake
Burundi iliunga mkono na baadaye Benki ya Afrika iligharimia upembuzi
yakinifu na sasa mradi huo ni miongoni mwa miradi ya ukanda wa kati ya
kipaumbele.
“Nawahakikishia
wawekezaji na wafanyabiashara mliopo hapa, ukichagua kuwekeza katika
ukanda wa kati, hakuna cha kupoteza bali utapata faida nyingi,” alibainisha.
Katika mjadala wa maswali na majibu
kutoka kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa wakuu hao wa nchi, baadhi
ya wawekezaji aliwaomba viongozi hao kuangalia kwa mapana uwepo wa
kitega uchumi kimoja kama Bandari ya Dar es Salaam ambayo inatumiwa na
nchi zote kuingia fedha katika uboreshaji na uimarishaji.
Kwa upande mwingine, Rais Kikwete,
alisema suala la Bandari ya Dar es Salaam inayotumiwa na nchi zote
litaangaliwa na wakuu wa nchi husika, hasa katika utashi wa kisiasa, ili
usiachwe kuwa mzigo kwa Tanzania huku manufaa yakiwa kwa wote.
Aidha, Rais Kikwete alisema moja ya
mipango mikubwa ya serikali ya Tanzania ni kuwekeza katika reli ili watu
binafsi waruhusiwe kuwa na treni zao kama ilivyo kwa usafiri wa mabasi
kuwa barabara ni za serikali, lakini wasafirishaji ni sekta binafsi.
“Tunataka
iwe kama uwanja wa ndege kwamba ndege ya nchi yoyote na mtu binafsi
inaweza kutua alimradi ilipe gharama za kutua na kufuata sheria
nyingine…Uganda wana treni zao nasi tunafungua milango kwa watu binafsi
kuwekeza kwenye treni,” alisema.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amewateua wabunge
wawili wapya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku ikiwa
imesalia miezi minne kabla ya Bunge hilo kuvunjwa.
Walioteuliwa ni Dk. Grace Khwaya Puja na Innocent Sebba, ambao uteuzi wao umeanza Machi 20, mwaka huu.
“Rais
amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ibara ya 66 (I) (e), ambapo amepewa mamlaka ya
kuteua wabunge wasiozidi 10,” ilieleza sehemu ya taarifa ya
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.
Uteuzi huo umekamilisha idadi ya wabunge, ambao Rais Kikwete amepewa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo kikatiba.
Wabunge, ambao wameshateuliwa na Rais ni pamoja na Prof. Makame Mnyaa Mbarawa; Prof. Sospeter Muhongo na Dk. Asha-Rose Migiro.
Wengine ni Janet Mbene (Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara); Saada Salum Mkuya (Waziri wa Fedha), Zakhia Meghji, Shamsi Vuai Nahodha na James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi).
Uteuzi wa wabunge hao wapya uliofanywa
na Rais Kikwete kipindi hiki, utawafanya wafanye kazi ya ubunge kwa
miezi minne tu kabla ya Bunge la 10, lililoanza Novemba, 2010, kuvunjwa
Julai, mwaka huu.
Kwa sasa Bunge hilo linaendelea na
mkutano wake wa 19, mjini Dodoma kabla ya kuhitimisha wa 20 na wa
mwisho, unaotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili mfululizo, kuanzia ama
mwezi ujao au Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Elimu na
Ushirikiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alifafanua jana
kuwa, jumla ya mikutano ya Bunge moja huwa 20 katika kipindi cha miaka
mitano ya uhai wake.
NIPASHE
Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha makundi yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.
Nape amesema hatua hiyo ya Lowassa
ambaye ni Mbunge wa Monduli ni nzuri kwa kuamua kusitisha makundi kwenda
kumshawishi agombee urais, ambayo kwa siku chache mfululizo yalikwenda
nyumbani kwake Monduli na mjini Dodoma kwa nia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana
wilayani Same, Kilimanjaro, Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa
amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo
inatakiwa kufuatwa na kila mwanachama wa CCM.
Jumanne wiki hii, Nape alimuonya Lowassa
kujiepusha na makundi hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na
taratibu za chama na kwamba, hali hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa
kugombea urais kupitia CCM.
Nape alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya CCM azuie makundi yanayokwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumtaka
agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya
wakati.
“Kilichokuwa
kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama
chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi
kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo nimpongeze Lowassa kwa
kutii agizo la chama,” Nape.
Kuhusu shutuma kuwa kauli anazozitoa
siyo za chama bali zake binafsi, Nape alisema yeye ndiye msemaji pekee
wa chama na hakuna msemaji mwingine, hivyo kauli zinazotolewa ni za
chama na siyo zake.
“Kanuni
na taratibu ambazo nazisimamia zipo miaka mingi kabla ya mimi kuzaliwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu, hivyo
lazima nisimamie misingi ya itikadi pamoja na kanuni na katiba ya chama
chetu. Kwa nafasi yangu siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea,” Nape.
Akizungumzia kuhusu wapambe wa makada wanaotaka urais, Nape aliwataka kuwa makini wasije wakawaharibia sifa wagombea wao.
“Ni
vizuri wataka urais wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao
kwani wanaweza kuwasababishia kukosa sifa ndani ya chama, nawashauri
wote wanaotaka kugombea urais kupitia CCM kutowasikiliza wapambe wao kwa
kila wanachoambiwa, maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha
sifa za kugombea urais,” Nape.
Alisisitiza kwamba, kwenye hilo si kwa
wapambe wa Lowassa tu, bali ni kwa wapambe wote waliopo nyuma ya makada
wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
“Ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha
wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya chama ili wawe salama, kinyume
cha hapo watajipoteza sifa,” alisisitiza Nape.
Zaidi ya vijana 100 wakiwamo wanafunzi
wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, wamekutana
mjini Moshi na kutoa tamko linalodai kwamba, iwapo Lowassa atapoteza
sifa za kugombea urais, CCM kijiandae kisaikolojia kwa sababu kinaweza
kupasuka na kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Vijana hao kutoka Jumuiya za Vyuo Vikuu
vya Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sekta binafsi, walitoa angalizo
hilo jana mjini Moshi kwa waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu
Lowassa ajibu kauli ya Nape aliyoitoa Jumanne akidai hawezi kuzuia
mafuriko kwa mkono.
MWANANCHI
Wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar kutafuta suluhu
kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, kuna
uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka Chadema.
Tovuti hii inaweza kuripoti kwa uhakika
kuwa uwezekano huo unatokana na vigezo vinavyotumiwa na vyama hivyo
kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na kwenye nafasi ya urais
ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya vyama vingine katika umoja
huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo hivyo ni matokeo ya uchaguzi
2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali
za Mitaa wa Desemba mwaka jana, mtandao wa chama nchini na nguvu ya
mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka
ndani ya kamati ya ufundi ya Ukawa zinasema pamoja na kuwapo mvutano
katika baadhi majimbo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar hakuna
tatizo hilo, jambo linaloipa CUF nafasi ya moja kwa moja kwenye ubunge,
uwakilishi na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri
ya CUF kupita moja kwa moja Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa,
inatoa fursa kwa upande wa Bara, kwa vyama vilivyosalia kupitishwa
kuwania urais wa Muungano.
Hata hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo
juu, Chadema ndiyo inakuwa na nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na
rekodi vyama vilivyosalia Bara.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema
kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete
akiwa na kura 2,271,941 (asilimia 26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim
Lipumba aliyepata kura 695,667 (asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa
NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388 (asilimia 0.31). NLD haikusimamisha
mgombea urais.
Kwa upande wa majimbo yaliyotokana na
uchaguzi wa 2010, Chadema kiliongoza kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka
Bara), CUF 23 (wawili kutoka Bara, 21 Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne
(wote wa Bara).
Katika rekodi za uchaguzi wa mitaa
zilitolewa na Tamisemi kabla ya chaguzi za marudio, Chadema ilipata
mitaa 980, ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR Mageuzi (28) na NLD
mtaa mmoja. Kwa upande wa vijiji, Chadema kilishinda vijiji 1,754, CUF
(516), NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema
kiliviongoza vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF
(2,561), NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
MWANANCHI
Mvutano mkali uliibuka jana bungeni
wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha Muswada wa Takwimu wa mwaka
2013, baada ya wabunge kuupinga.
Muswada huo una kipengele kinachotoa
adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini isiyopungua Sh10
milioni kwa mtu au chombo cha habari kitakachofanya makosa ya kutoa
takwimu zisizokuwa sahihi.
Wabunge hao waliufananisha muswada huo
na miswada miwili ya habari ya mwaka 2015 ambayo itawasilishwa bungeni
Jumanne chini ya hati ya dharura kwa usiri uliopo na mpango wa
kuiwasilisha bila wadau kushirikishwa.
Awali, muswada wa Takwimu uliwasilishwa
kwenye mkutano wa 17 wa Bunge uliofanyika Novemba mwaka jana na wabunge
wakapinga vifungu vinavyobana waandishi wa habari kuhusu eneo la
takwimu, ndipo Serikali ilipoamua kuutoa kwa maelezo kuwa inakwenda
kuurekebisha hadi ilipourejesha jana na ukapitishwa kwa mbinde.
Jana, Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu kali na Serikali kujibu kuwa imeshakifanyia marekebisho.
Hata hivyo, Mnyika hakukubaliana na
maelezo hayo, bali alisema kifungu hicho hakijafanyiwa marekebisho
yoyote na Serikali na adhabu bado inaendelea kuwa kali.
Mnyika aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyehoji, “Iweje
Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa taarifa zisizo
sahihi lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa hizo zisizo
sahihi na ofisa huyo wa Serikali?”
Maelezo ya Bulaya yalimfanya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kusimama na kusema kwa kifupi kuwa
“mwandishi atakwenda kujieleza mahakamani au polisi.”
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba 2014
muswada huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipendekeza faini ya Sh10
milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari
kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
“Mtu
yeyote, kwa kujifanya anatimiza majukumu yake, iwapo anapata au anaomba
kupatiwa taarifa ambayo haijaidhinishwa kuipata na kuichapisha au
kuisambaza atakuwa amefanya kosa ambalo adhabu yake ni kifungo
kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua shilingi milioni mbili au
vyote kwa pamoja,” ilisema ibara ya 37 (d) cha muswada huo.
MWANANCHI
Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa sasa
ndiyo habari ya mjini, Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na
ongezeko kubwa la watu wanaotumia mitandao ya kijamii sehemu mbalimbali
duniani.
Hii inatokana na wengi kutumia simu za kisasa maarufu kama smartphone ambazo zina uwezo mkubwa wa mawasiliano ya intaneti.
Inakadiliwa kuwa kwa sasa mtu mmoja kati ya watu wanne duniani kote, anatumia mojawapo ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApps.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya
watumiaji wa mitandao hii, ni vijana wenye umri chini ya miaka 30. Na
wengi hutumia simu za mkononi zenye mtandao wa intaneti na wengine
hutumia kompyuta kutembelea mitandao hiyo.
Pamoja na faida kadhaa za matumizi ya
mitandao hiyo, baadhi ya watafiti wa maswala ya afya ya jamii
wanabainisha kuwa matumizi ya mitandao hii yana athari kwa afya ya
kisaikolojia na ubora wa maisha kwa watumiaji.
Jambo la kuvutia ni kwamba watafiti
wamegundua kuwa watu wengi wanaotumia mitandao ya kijamii hawana utulivu
wa kihisia na wengi wanakabiliwa na wasiwasi.
Katika utafiti ulioongozwa na Dar Meshi wa Chuo Kikuu cha Freie
cha Ujerumani, inaonekana kuwa watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii
wanapata uraibu fulani. Uraibu huo ni wa kutaka kuendelea kuwasiliana na
hata kuona fahari kuzidi kuongeza idadi ya wale anaowasiliana nao.
Wengi wao huhangaika ili kuinua kiwango chao cha kujisikia vizuri kihisia.
Mwaka 2012, shirika linalojihusisha na maswala ya hali ya wasiwasi nchini Uingereza (Anxiety UK)
lilifanya utafiti kuhusu athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na
kubaini kuwa asilimia 53 ya washiriki wa utafiti huo walikuwa
wamebadilika kitabia kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Na asilimia 51 ya watu wote waliokiri kuwa walibadilika kitabia. Mabadiliko yao yalikuwa yameegemea kuwa hasi kuliko chanya.
Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia
66 ya washiriki wa utafiti walikosa usingizi na utulivu wa kihisia kila
walipomaliza kutumia mitandao ya kijamii.
Asilimia 55 walisema kuwa walihisi
wasiwasi na kukosa furaha pale waliposhindwa kupata mtandao ili
kuunganishwa na mitandao ya kijamii wanayoipenda.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Dk Linda Blair, mtaalamu wa saikolojia anasema kuwa watu wengi hupata athari za kisaikolojia kwa sababu wanashindwa kudhibiti matakwa yao,” anasema akisisitiza: afikiri jambo kubwa ni watu kuanza kutawaliwa na teknolojia, badala ya wao kuitawala,” Dk Blair.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,limemtaka Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kujisalimisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Hatua hiyo ya polisi imekuja baada ya
jeshi hilo kupokea malalamiko, ambapo inadaiwa Mchungaji Gwajima alitoa
lugha ya kashfa dhidi ya Kardinali Pengo ambaye alipinga tamko
lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) la kuipigia kura ya Hapana Katiba Inayopendekezwa.
Taarifa iliyotolewa janana Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi, Kamishna Suleiman Kova,
imemtaka Mchungaji Gwajima kujisalimisha haraka katika Kituo cha Polisi
cha Kati kwenye Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda kwa mahojiano kuhusu
tuhuma za kashfa na matusi.
Kova alisema jeshi hilo limepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani Kardinali Pengo.
Alisema matusi hayo yameonekana kupitia
mitandao mbalimbali ya kijamii ya WhatsApp na mingineyo, ambapo kuna
sauti iliyorekodiwa na picha za video zikimuonyesha Mchungaji Gwajima
akimkashifu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo katika hali
ambayo pia imewaudhi watu wengine.
Kova alisema baada ya tukio hilo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kumpata Mchungaji Gwajima bila mafanikio.
“Ni
muhimu sana kwa Mchungaji Josephat Gwajima aripoti mwenyewe badala ya
kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake
katika jamii.“Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hili unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake,” aKamanda Kova.
Hivi karibuni sauti iliyorekodiwa na
picha za video zilionekana katika mitandao ya kijamii ambazo zilikuwa
zikimtukana Kardinali Pengo.
Sehemu ya maneno hayo ambayo yanamwonyesha Gwajima akizungumza kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ni;“Pengo
unaaibisha kama mtoto mdogo aliyevaa pampasi aliyebebwa na mama yake,
Pengo ni mjinga asiyefaa, juzi aliokoka kwa kula chakula chake ovyo
ovyo, sijui kala maharage ya wapi?
“Pengo awe Mkatoliki amejishushia heshima yake mwenyewe, aache uaskofu
awe mkulima wa kawaida, hafai mzee ametudhalilisha kabisa na amewageuka
maaskofu wote kwa kile walichopatana .
“Amewadhalilisha maaskofu wote, amedhalilisha CCT, amedhalilisha CPCT, pia amewadhalilisha Watanzania wote.”.
“Amewadhalilisha maaskofu wote, amedhalilisha CCT, amedhalilisha CPCT, pia amewadhalilisha Watanzania wote.”.
UHURU
Rais Jakaya Kikwete,
amesema siku chache zijazo mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za Afrika
Mashariki na Kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam, itabebwa kwa treni na
kusafirishwa kwa reli na kuachana na usafirishaji mizigo kwa malori.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa treni
za mizigo kwenda nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda,
Burundi na Rwanda, alisema kwa sasa mizigo itasafirishwa kuanzia makao
makuu ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwenda nchi husika.
Alisema kwa sasa wataalamu wa TRL wamebuni
utaratibu mzuri wa mabehewa yanayotoka nchi moja kwenda nyingine moja
kwa moja tofauti na utaratibu wa awali wa kukata bogi ili kushusha
mizigo.
“Pamoja
na treni za nje ya nchi, lakini kutakuwa na treni za kubeba mizigo ya
ndani…utaratibu huu utapunguza ucheleweshaji wa mizigo uliokuwapo, hivyo
nchi zenye bandari kuona kama adhabu kusafirisha mizigo kupitia
Tanzania,” alisema.
Rais Kikwete alisema mkutano uliowaleta
pamoja marais wa nchi za Afrika Mashariki na Kati una lengo la
kuimarisha miundombinu ya barabara, reli na bandari ili Tanzania itimize
wajibu wake wa kuzisaidia nchi zisizo na bahari.
Rais alieleza kuwa alikwenda Burundi na
kuzungumza na wafanyabiashara ambao kilio chao kikubwa kilikuwa ni
ucheleweshaji wa mizigo unaoanzia bandarini na vikwazo vingine zikiwamo
barabarani kiasi cha nchi hiyo kujilaumu kupakana na Tanzania.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta,
alisema kwa sasa inachukua siku mbili kwa mizigo kufika Kigoma kwa
ajili ya kusafirishwa kwenda Burundi, DRC na Rwanda na kwamba kwa sasa
kutakuwa na mabehewa kati ya 15 na 20 kwa kila safari.
Alisema mizigo ya kwenda Rwanda
itashushwa Bandari Kavu ya Isaka na ya Uganda itashushwa feri ya Mwanza
na kuvushwa kwa meli kwa haraka.
“Utaratibu
huu ni endelevu, utakuwa kila mfanyabiashara atafuatilia mzigo wake
ulipo na atapata kwa muda mfupi…tunawashukuru mafundi wa Tanzania na
Malaysia ambao wamezifufua Injini za miaka 40 iliyopita kufanya kazi
upya,” alisema.
Rais wa Burundi, Pierre Nkrunzinza,
aliishukuru Tanzania kwa jitihada za kuisaidia nchi hiyo katika masuala
ya kupata Uhuru, kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe na sasa kuwa na
amani ya kudumu.
Alisema wakati wa vita Warundi milioni
moja walipata hifadhi ya muda Tanzania na kwamba kwa sasa wanazisaidia
nchi zenye vita zikiwamo Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment