Saturday, March 28, 2015

NILIJUA NIMEUWA SEHEMU YA (4)

Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Mkombozi Sanitarium Clinic. Mabingwa wa magonjwa yaliyoshindikana yakiwemo ya wanawake na ugonjwa wa baasiri na mengine mengineo. Wapo Chuda Tanga na simu 0654 361333
 
ILIPOISHIA
 
Kwa vile nilikuwa kwenye mwendo wa kasi nililipita gari hilo na kwenda kusimama mbele. Hapo hapo mawazo yangu yakabadilika. Niliwaza kwamba huenda gari hilo liliegeshwa kwa hila lionekane limeharibika kumbe ni majambazi wanaosubiri magari yasimame waanze kupora watu.
 
Nilikuwa nimechelewa kufikiria hilo. Nilikuwa nimeshasimamisha teksi na jamaa aliyenisimamisha alikuwa ameshafika kwenye dirisha la teksi yangu!
 
Chini ya siti yangu ya dereva, siku zote huweka parange (sime ya kimasai) kwa ajili ya kujihami endapo kutatokea tatizo la kuvamiwa na mtu au watu wenye nia mbaya.
 
Kwa vile sikuwa na uhakika kuwa mtu huyo aliyenisimamisha alikuwa na nia mbaya au nzuri, tayari nilishapeleke mkono wangu wa kulia kuushika mpini wa parange iliyokuawa chini ya siti niliyokalia.
 
Nilikuwa nimejiweka tayari, kama atakuwa na nia mbaya niweze kukabiliana naye.
 
SASA ENDELEA
 
“Samahani bwana” Mtu huyo akaniambia. Ingawa sauti yake ilikuwa tulivu nay a kibinaadamu, ilikuwa imeficha taharuki.
 
“Unasemaje?” nikamuuliza nikiwa nimemkazia macho kusoma mawazo yake.
 
“Mimi ni daktari wa hospitali ya Bombo. Nimepigiwa simu kuitwa   hospitali, kuna mama mjamzito anahitaji kufanyiwa operesheni ya dharura sasa hivi. Kwa bahati mbaya gari langu limeharibika njiani. Naomba unipeke Bombo haraka” akaniambia.
 
“Kusema kweli nilimuelewa. Nikamuuliza.
 
“Na hilo gari lako je?”
 
“Ningeomba kama itawezekana unisaidie kulivuta niliondoe mahali hapa”
 
“Hiyo itakuwa ni kazi nyingine” nikamwambia.
 
“Naomba msaad wako kaka, sina jinsi na siwezi kuliacha hapa”
 
“Unataka nilivute hadi wapi?”
 
“Hadi Bombo. Nitaliegesha sehemu. Kutakapokucha nitajua la kufanya”
 
“Utanilipa kiasi gain?”
 
“Sema wewe”
 
“Kulivuta hilo gari lako pamoja na kukufikisha wewe Bombo utanilipa elfu ishirini”
 
“Sawa. Nitakulipa”
 
Alipokubali kima changu nilifungua mwa gari nikashuka.
 
“Una kamba?” nikamuuliza.
 
“Kamba sina’
 
Nilikuwa na kamba ya akiba kwenye boneti la teksi yangu. Nilikwenda nyuma ya gari, nikafungua boneti na kutoa kamba. Nikaiweka chini.
 
Kisha niliisogeza teksi mbele ya gari la mtu huyo lililokuwa pembeni. Nikashuka tena na kufunga ncha moja ya kamba nyuma ya gari langu na ncha nyingine nikaifunga mbele ya lile gari. Nilipomaliza nilimwambia mtu huyo ajipakie kwenye gari lake.
 
Wakati anajipakia na mimi nilikwenda kwenye mlango wa teksi nikaufungua na kujipakia. Nilitia gea na kuiondo teksi taratibu. Kamba ilinyooka na kukaza kabla ya kuanza kulivuta gari la nyuma.
 
Niliingia barabarani nikawa naendesha taratibu. Kwa vile niliendesha kwa mwendo mdogo tulifika Bombo saa kumi na mbili asubuhi.
 
Nilishuka kwenye teksi nikaifungua ile kamba na kuiweka kwenye boneti.
 
“Nakushukuru sana” Mtu huyo akaniambia baada ya kushuka kwenye gari lake.
 
Alitoa pochi mfukoni akaifungua na kutoa noti mbili za elfu kumi kumi akanipa.
 
“Sasa nipe namba yako, naweza kukuhitaji tena” Mtu huyo akaniambia.
 
Nikampa namba yangu ya simu akaiandika kwenye simu yake kasha akaniuliza.
 
“Unaitwa nani?”
 
“Andika Majomba Teksi”
 
Baada ya kuandika jina hilo aliniambia.
 
“Vizuri, nitakutafuta”
 
“Sawa” nikamjibu. Nilijipakia kwenye teksi yangu nikaiwasha na kuondoka.
 
Wakati naendesha nilijikuta nikumuwaza huyo mwanamke mjamzito aliyetakiwa kufanyiwa operesheni. Sikuwa na hakika kwamba alikuwa katika hali gani muda ule kwani kwa vyovyote vile yule daktari alikuwa amechelewa sana kufika pale hospitali kutokana na gari lake kuharibika.
 
ITAENDELEA na usiache kuperuz www.tangakumekucha.blogspot.com kwa habari kedekede ni hapa hapa kumekuchablog

No comments:

Post a Comment