Wednesday, March 25, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOANDIKWA MAGAZETINI LEO MARCH 25 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Wapo Tanga mkbala na Bank ya CRDB, simu 0715 772746

nyuuuNIPASHE
Jeshi la Polisi mkoani Kagera,  limewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na mifupa ya viungo vya mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Zeulia Justus, aliyefariki dunia mwaka 2006 baada ya kujifungua mtoto katika kijiji cha Rushwa Kata Mshabago Tarafa ya Nshamba Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Lutozi (66) na Emmanuel Karoli (50), wakazi wa Kijiji cha Kyota Tarafa Kimwani wilayani humo.
Mwaibambe alisema kuwa  watuhumiwa hao walikamatwa na mifupa mitatu ya mwanamke huyo   baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kijijini humo kuwa kuna watu wanauza viungo vya  albino kwa Sh. milioni tatu.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 20, mwaka huu, wakiwa na mfupa mmoja na walipopekuliwa kwenye makazi yao, walikutwa na mifupa mingine miwili.
Katika mahojiano, watuhumiwa hawa walikiri kwamba, mifupa hiyo ni ya albino aliyefariki mwaka 2006 katika Kijiji cha Rushwa, Kata Mshabago,Tarafa Nshamba, wilayani Muleba,” Mwaibambe.
Alisema watuhumiwa hao walidai kuwa mifupa hiyo waliipata baada ya kufukua kaburi alimozikwa albino huyo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi, Mutalemwa Revocatus.
Mwaibambe alisema polisi waliiomba mahakama mkoani hapa kibali cha kufukua kaburi na kupewa.
Alisema polisi walikwenda kwenye kaburi hilo Machi 23, mwaka huu na kulifukua na kujiridhisha kuwa mifupa hiyo ilikuwa ni ya viungo vya albino huyo.
NIPASHE
Serikali imewasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya ambao unawabana wauza ‘unga’ ukipendekeza kuwa watakaobainika kufanya biashara hiyo haramu watozwe faini ya Sh. bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30, huku wabunge wakitaka watakaobainika wapigwe risasi hadharani au wanyongwe.
Aidha, atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha, kuzalisha au kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi, mirungi na cocaine atatozwa faini isiyopungua Sh. milioni 20, kifungo kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.
Wakichangia muswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MKuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama, wabunge walipendekeza kufutwa kwa kipengele cha faini kwa kuwa kinatengeneza mazingira ya rushwa kwa watendaji wa serikali wanaohusika na kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya, kwa kuwa wanaofanyabiashara hiyo ni watu wenye mabilioni ya fedha.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inakuwa ngumu kutokana na tabia ya serikali kulinda watuhumiwa hata pale ushahidi unapokuwa wazi.
Alisema ili kukomesha tabia hiyo, sheria hiyo inapaswa kutamka kwamba watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo adhabu ndogo iwe kifungo cha maisha, kunyongwa hadi kufa au kupigwa risasi hadharani na kwamba adhabu ya faini iondolewe.
 “Bila hivyo, tutakuwa tunabadilisha chupa, lakini mvinyo ni ule ule. Tatizo tulilonalo ni kulindana siyo vyombo vya usimamizi. Polisi wakikamata mfanyabiashara wa dawa hizi, simu za wakubwa zinapigwa wanawaachia, kwa hiyo mimi sikubaliani na hili la kuanzisha mamlaka kama hatutaondoa tatizo la kulindana,” alisema.
Alisema wafanyabishara wa dawa za kulevya wanajulikana kwa majina hadi nyumba wanazoishi lakini hawachukuliwi hatua badala yake vyombo vya dola vinahangaika kukamata wasafirishaji wadogo wadogo.
Aidha, alikiri kuwa na orodha ya majina na namba za nyumba wanakoishi wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, lakini hawezi kuwataja bungeni hapo kutokana na hali ya sasa kuonyesha kuwa mfumo mzima unawalinda wafanyabiashara hao.
Naye mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, pamoja na kutaka watakaokutwa na dawa za kulevya kunyongwa au kupigwa risasi hadharani wiki mbili baada ya kuhukumiwa, pia aliitaka Serikali itafute mbinu ya kuondoa dhana kuwa wafanyabiashara wakub
NIPASHE
Ofisi za jengo la tawi la Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Dimani, mkoa wa Mjini Magharibi, limeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa ya vitu vilivyokuwamo humo ingawa thamani ya vitu hivyo haijajulikana.
Tukio hilo lilitokea mtaa wa Kisauni usiku wa kuamkia jana saa nane usiku.
Mashuhuda walisema watu wasiojulikana walifika na gari aina ya Pick-up na kuvunja mlango wa ofisi hizo na kulilipua jengo hilo kwa petroli.
Majira ya saa nane usiku ilikuja gari na watu wawili walishuka katika gari hiyo na kuingia ndani huku wakisikika wakisema tayari tuondoke na baada ya kuondoka tu jengo hilo lililipuka,” alisema shuhuda mmoja aliyekuwapo katika eneo hilo.
Alisema baada ya kuona moto na moshi mkubwa ukiwa umetanda ndipo walipowapigia watu wa Zima Moto na walifika kuuzima.
Diwani wa wadi ya Tomondo, Hassan Hussen Yussuf, alisema hali inasikitisha katika harakati za kisiasa kuona Zanzibar inarejea katika siasa za chuki na uhasama.
Matukio kama haya hutokea karibu na uchaguzi kwa kweli inasikitisha sana na kama halii itaendelea itakuwa hatari katika nchi,Yussuf.
Alisema katika jengo hilo kulikuwa na vifaa mbalimbali vya thamani na fedha taslimu za malipo ya uchukuaji wa fomu za wagombea walizolipia zimeteketea.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema CUF kinalihusisha tukio hilo kuwa ni joto la uchaguzi na kuwashutumu waliofanya waliofanya tukio hilo kwani matukio kama hayo yamekuwa yakifanywa inapokaribia kipindi cha uchaguzi mkuu.
Hujuma hizi zimepangwa na ni za makusudi kuchafua amani ya nchi,na hali kama hii hutokea zaidi karibu na uchaguzi na CUF hufanyiwa hujuma mbalimbali ikiwamo kuchomwa moto ofisi zetu,” Bimani.
NIPASHE
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) John Mnyika, ameibua upya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), baada ya kuhoji sababu za vigogo waliopewa mgawo wa Sh. bilioni 73 kutoka Benki ya Stanbic kutohojiwa wala kuchukuliwa hatua hadi sasa.
Alisema hayo jana bungeni wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Mifumo ya Taifa wa Mwaka 2015.
Mnyika alisema kutungwa kwa sheria hiyo kunatia mashaka kama itaweza kufanya kazi vizuri kwa sababu mwaka 2006 zilitungwa sheria mbili muhimu, ambazo hata hivyo hazijasaidia kukomesha vitendo vya ufisadi.
Alizitaja sheria hizo zilizotungwa mwaka huo kuwa ni sheria ya mabenki na taasisi za fedha na sheria ya BoT ya mwaka 2006, ambazo kama zingeweza kufanya kazi vizuri zingesidia kutatua matatizo yanayojitokeza kwenye miamala.
“Kutungwa kwa sheria kunaweza kusiwe suluhisho la matatizo haya kwenye miamala, mfano ilikuwaje ikaruhusiwa kutolewa fedha katika Benki ya Stanbic dola za Marekani milioni 122 kwenda katika akaunti zisizoeleweka kwenda Austaria na Afrika Kusini,”Mnyika.
Alisema pia Sh. bilioni 73 zilichotwa katika benki hiyo na kuingizwa kwenye akaunti za watu, ambao hawaeleweki na hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa na kumekuwa na usiri mkubwa wa suala hilo.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema uchunguzi wa kashfa ya Escrow bado unaendelea na kwamba, taarifa zitatolewa utakapokamilika.
MWANANCHI
Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Warioba, ametaja sifa za rais ajaye kuwa ni uzalendo, uadilifu na dira katika kuliongoza taifa.
Jaji Warioba alisema hayo juzi, katika Kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa hewani na ITV.
Rais anapaswa pia kujua matatizo ya Watanzania, awe mzalendo, mwadilifu na aone mbali. Anapaswa pia kujua  atafanya nini kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta za afya na uchumi,” alisema.
Kwa kauli hiyo, Jaji Warioba anaungana na viongozi wengine kadhaa waliowahi kuzungumzia sifa za rais ajaye, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine; Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye; Mwanasiasa mkongwe, Cleopa Msuya; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba;  na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walitaja sifa hizo za rais ajaye kuwa ni uadilifu, busara, uzalendo, uwezo wa kufanya uamuzi na kuyasimamia, weledi wa masuala ya maendeleo, kutokuwa na makundi, kuwa na nguvu ya mwili na akili na uwezo wa kusimamia Katiba na sheria za nchi.
Walisema yeyote asiyekuwa na sifa hizo, hafai kuwa rais na kuwaongoza Watanzania.
Mtu anayetangaza (mwenyewe) kuwa anataka kuwa rais anakuwa hajui anachokisema…, anakuwa hajui matatizo ya urais. Mtu asiyejua matatizo ya urais anaweza kujisemea tu kwa sababu haelewi urais maana yake ni nini,” alisema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Waziri wa kwanza wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk Hassy Kitine.
MWANANCHI
Licha ya Serikali kusisitiza kuwa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa mfumo wa BVR utakamilika Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa kuwianisha siku zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na zinazotarajiwa kuwasili.
Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36 kabla ya Kura ya Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa wadau kuhusu uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita kuanzia leo na kusisitiza kuwa Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo katika tarehe iliyopangwa unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa BVR unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari 23, mwaka huu kutokamilika hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye wapigakura 392,634 kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini kote.
Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja inaandikisha kati ya wapigakura 80 hadi 100 kwa siku endapo hakuna tatizo lolote, hivyo kwa kadirio la chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa na NEC zitawasili nchini kwa mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha wapigakura milioni 24 wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.
Hata hivyo, katika uandikishaji wa majaribio na baadaye katika Mkoa wa Njombe mashine hizo zimeripotiwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali ama za kukwama, weledi mdogo wa watumiaji na hali ya hewa, hivyo kufanya idadi iliyokusudiwa kutokamilika.
Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya aliyekuwa Makambako, Njombe wakati wa uandikishaji hivi karibuni amesema kwa wastani alishuhudia mashine moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60 kwa siku, idadi hiyo ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa kuandikishwa kwa BVR 7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52, wakati siku zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.
Jambo jingine linalofanya hesabu hizo kukataa ni kitendo cha mashine hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa, kutokuwapo zote nchini hadi sasa, licha ya NEC kusema mara kwa mara kwamba zitawasili wakati wowote.
Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.
MTANZANIA
Hali ya siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kuwa tete baada ya makundi mbalimbali ya jamii kwenda kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa achukue fomu ya kugombea urais.
Hali hiyo imedhihirika baada ya makada wa chama hicho kuanza kuvurugana kwa kutoa kauli zinazopingana juu ya wanaomtembelea Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, kuwataka wajumbe wa Baraza la Wazazi la chama hicho kuomba radhi kwa kitendo chao cha kwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma na kumtaka agombee urais.
Pamoja na Bulembo kutoa kauli hiyo, wajumbe hao wamesema hawako tayari kuomba radhi kwa sababu hawaoni sababu ya kufanya hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, wajumbe hao wa Baraza la Wazazi wa CCM, walisema hawataomba radhi kama walivyotakiwa na Bulembo kwa vile walikwenda kwa Lowassa kwa hiyari yao na kwa mapenzi yao binafsi.
Katika mazungumzo yake, Lupenza alisema viongozi walioratibu ziara hiyo ni pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang, Vioroka Kajoro na Mjumbe wa baraza hilo Mkoa wa Morogoro, Jackline Ngonyani pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mkoa wa Dodoma, Dk. Damas Mukassa.
Alisema yeye hakushawishiwa na mtu yeyote kwenda kwa Lowassa ila aliwasikia viongozi hao wakizungumzia juu ya ziara hiyo na kuwataka waweke jina lake kwenye orodha ya watakaokwenda kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Niliwasikia wakisema kwa mzee ni saa tatu, nikawauliza mnataka kwenda wapi, wakaniambia wanataka kwenda kumsalimia Lowassa, nikawaambia waniandike na mimi jina.
“Kwa hiyo hakuna mtu aliyenishinikiza na hata siku hiyo ya safari, hakuna aliyenikumbusha, kwanza waliniacha nikaenda kwa pikipiki nikiwa nimechelewa,Lupenza
Ngonyani ambaye amekaririwa na vyombo vya habari akisema alishinikizwa kwenda kwa Lowassa, nilimkuta akiwa nyumbani kwa Lowassa akiwa amekaa kwenye viti vya mbele kabisa.
“Hata wakati wa kupiga picha ulipofika, Ngonyani huyo huyo ambaye sasa ametugeuka, aliwataka wajumbe wengine wote wakae mbali aweze kupiga picha yeye na Lowassa peke yao.
“Yaani hata wakati tunajitambulisha huyo huyo Ngonyani alisema ametumwa na watu wa Ruvuma kumletea salamu Lowassa, kwamba wanamsalimia, sasa anageukaje tena?”
Kwa upande wake, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani ambaye ni maarufu kwa jina la Prof. Maji Marefu, alikana kuratibu safari hiyo kama ilivyodaiwa na kueleza kuwa alishirikishwa katika dakika za mwisho na akaamua kwenda.
Wanaojitoa katika ziara hiyo hivi sasa nadhani walifikiri wakienda pale watapewa fedha ama magari. Mimi nimekaa kwenye hii jumuiya kwa miaka 15 sasa, siko tayari kuchaguliwa kiongozi, marafiki wala maadui. Siko tayari kuomba radhi kwa sababu sina kosa nililotenda, nasema sitaomba radhi,Ngonyani.
Naye Dk. Mukassa alisema yeye aliratibu ziara hiyo kama mwenyeji wa Mkoa wa Dodoma ambaye anapafahamu nyumbani kwa Lowassa.
Alisema Sh 600,000 walizozitoa kwa ajili ya Lowassa kuchukulia fomu ya kugombea urais, zimetokana na michango yao wenyewe kama wanachama wa kikundi cha kusaidia wajumbe wa jumuiya hiyo.
MTANZANIA
Rais Jakaya Kikwete ameamuru kubomolewa baadhi ya nyumba zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani, Ilala Dar es Salaam.
Akihutubia wananchi wa eneo hilo jana, Rais Kikwete alisema nyumba hizo zitabomolewa pamoja na karavati hilo kupisha maji kupita na kulijenga upya.
Kwa sasa tunaendelea kuvuta maji yaliyojaa kwenye makazi ya watu kwa kutumia pampu lakini baadaye itabidi tuvunje nyumba zilizoko juu ya karavati kupisha ujenzi wa karavati jipya,” alisema.
Rais Kikwete ambaye alitembelea maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo jana, alisema wananchi wote watakaobomolewa nyumba zao watalipwa fidia huku akitoa rai kwao kuacha tabia ya kujenga holela bila kuzingatia matumizi ya eneo husika.
Katika hatua hiyo, alisema zipo taarifa za kuwapo uhitaji wa chakula kwa waathirika na tayari uongozi wa wilaya na kamati ya maafa zimeanza kushughulikia tatizo hilo.
Wananchi walioathirika na mafuriko hayo waliiomba serikali kuharakisha hatua ya kutoa maji yaliyojaa kwenye makazi yao na kutoa misaada inayohitajika.
Mvua inayoendelea kunyesha Dar es Salaam imesababisha madhara makubwa vikiwamo vifo vya watu saba na nyumba zaidi ya 200 kuzingirwa na maji katika maeneo mbalimbali ya jiji.
HABARILEO
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) amekutana na wadau mbalimbali, kujadiliana jinsi ya kuanza kazi ya kutengeneza andiko la kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya njia sita ya Dar es Salaam­ Chalinze.
Mkutano huo umeshirikisha wahandisi , wanasheria na wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Akifungua mkutano huo jana jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Andiko linaloandaliwa na Kampuni ya Ushauri M/S Cheil Engeneering ya Korea, linatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu na litatumika kuingia mkataba kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi.
Alisema andiko litakuwa ni kielelezo cha kusaidia Serikali kujipanga ni jinsi gani itashirikiana na sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya barabara, ambapo mkutano huo utawapa wadau hao nafasi ya kupendekeza nini kiwepo na kisiwepo katika andiko hilo.
Andiko hilo litasaidia kuonyesha madhara ya kimazingira, fedha zinazohitajika, masuala ya sheria na mahitaji yote ambayo yatatakiwa katika utekelezaji wa mradi wakati ukifika,” alisema.
Kwa mujibu wake, utafiti uliofanyika mwaka 2011, ulionesha barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze inapitisha zaidi ya magari 67,000 kwa siku hivyo ikifika 2017 hali itakuwa mbaya zaidi.
Alisema utekelezaji wa mradi huo hautagusa barabara iliyopo na itakapokamilika itakuwa ikilipiwa, hivyo ambao hawatakuwa na uwezo watalazimika kuendelea kutumia barabara hiyo ya zamani na ndiyo sababu Serikali imeamua kushirikisha sekta binafsi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment