Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita kwa wale wanaorisiti. Pia wanatoa kozi za Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha
uangalizi maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi
kurudisha bastola hiyo, akisema ni mali na aliiagiza ipelekwe
hospitalini kwa sababu ya kujilinda.
Akizungumza na waandishi wa habari
hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu
akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa
kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata hivyo, katika kwa upande mwingine,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema
bunduki hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa wachungaji 15
waliokamatwa lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima, alitoa
taarifa akisema bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo.
Pia alisema kuhusu risasi 17 za bunduki
aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo lakini akasema
uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika
tumbo, Gwajima alisema alipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya
kijamii kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa
ajili ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa
kutaka kumtorosha.
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya
ambao wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na
polisi kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao.
“Usiku
wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa
namna ile unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani,
nikaamua kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili
likitokea lolote niweze kujilinda,” Gwajima.
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji
wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa
ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla
sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka
kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa
Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka
ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika
vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi
kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa
kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma,
akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu
ambacho hakikufanyika kwa wakati.
MWANANCHI
Vyombo vya usalama nchini Kenya,
vinawashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa
kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
Taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia, Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.
Mtanzania huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.
Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.
“Hawa
wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata
mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” Kamishna Marwa.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema: “Tunafuatilia hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”
Kamishna Marwa alisema raia hao wawili
wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo
Thika, Jimbo Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania,
iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali
imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki
ili wakajiunge na makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa
usalama wamepata taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana
hao,” alisema Kamishana Marwa.
Hivi karibuni, tovuti ya al-Jazeera
ilitoa taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video ulioonyesha mwakilishi
wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Levant (ISIL)
akimtaka kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya
mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Kamishna Marwa alisema ingawa nyaraka za
wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni wanafunzi, lakini bado
walibanwa kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka nchini Somalia.
Aliongeza zaidi kuwa chanzo cha habari
cha kiusalama kilieleza kuwa nyaraka za wasichana hao zilionyesha kuwa
walikuwa wakienda kuolewa na wanajeshi wa kundi la al-Shabaab.
MWANANCHI
Wachambuzi wa soka wamesema timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ haina kiwango cha kuvutia uwanjani na imepoteza mvuto.
Wakizungumza baada ya kuishuhudia Taifa
Stars ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Malawi katika mchezo wa kirafiki
wa kimataifa uliofanyika Mwanza juzi, walisema wanauona mwisho mbaya wa
kocha Mholanzi, Mart Nooij.
Kocha Joseph Kanakamfumu aliliambia gazeti hili kuwa Nooij hajaibadilisha Stars na inacheza ili mradi tu tofauti na mtangulizi wake, Kim Poulsen.
Kanakamfumu alisema jambo kubwa
analokosea Mholanzi huyo ni uteuzi wa kikosi chake, hasa aina ya
wachezaji anaowaita kwani wengi wao hawako fiti.
“Nikiangalia
hajaibadilisha timu tofauti na wakati wa Kim kwani timu ilikuwa unaona
kabisa inacheza mpira mzuri, lakini kwa huyu timu haichezi kwa
mpangilio, hatuoni mtiririko mzuri uwanjani, kila mchezaji anajichezea
anavyojua yeye,” alisema Kanakamfumu.
Aliongeza: “Tatizo
kubwa anapokosea ni kwenye uteuzi wa timu yake, inatakiwa aangalie
wachezaji anaowaita wapo vizuri namna gani kulingana na mfumo
anaoutumia, kwani wachezaji wengi aliowaita hawaendani na mfumo wake wa
kujilinda.”
Naye Eugine Mwasamaki alisema tatizo liko kwa kocha na hata wachezaji wake kwani kiwango cha timu hiyo si kizuri na kinasikitisha.
Mwasamaki alisema anachoshangaa ni Nooij
kuwaita kikosini wachezaji ambao hata kwenye klabu zao hawachezi na
kuwacha wengi wanaoonyesha viwango vizuri kwenye mechi Ligi Kuu Bara.
Wachezaji ambao hawana namba ya kudumu katika klabu zao kwa sasa, lakini wapo Stars ni pamoja na Mwadin Ally, Amri Kiemba, Deo Munishi na John Bocco.
NIPASHE
Wafuasi 11 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamevamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati wakitokea katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Fuoni Jitimai, wakati wakirudi nyumbani baada ya mkutano huo, uliofanyika Makunduchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja,
Juma Sadi, alisema watu wasiojulikana waliwajeruhi wafuasi hao, ambao
walikuwa katika gari na majeruhi hao kukimbizwa katika Hospitali ya
Mnazi Mmoja na baadhi yao wamepewa ruhusa na wengine wamelazwa.
Kamanda Sadi alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kuwatia mbaroni waliohusika.
Wakati huo huo, Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim,
jana alilitaka Bunge lijadili kwa dharura hali ya amani visiwani
Zanzibar kwa maelezo kuwa wanachama wa CUF, wamepigwa na kujeruhiwa.
Alisema kupigwa kwa wafuasi na wanachama
wa CUF kunahatarisha amani visiwani humo na Tanzania kwa ujumla hivyo,
akaliomba Bunge lijadili hali hiyo. Akijibu mwongozo huo, Spika wa
Bunge, Anne Makinda, alimtaka aandike hoja yake na aiwasilishe kwa Katibu wa Bunge kwa njia ya maandishi.
NIPASHE
Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi,
jana alitoa ushahidi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es
Salaam, kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Khalid Kagenzi, za kutaka
kumdhuru mumewe.
Kutokana na hatua hiyo ya Mushumbusi,
Dk. Slaa alisema tayari wamefunga ushahidi kwa upande wake. Mushumbusi
ambaye aliongozana na mumewe, Dk. Slaa walifika katika kituo hicho saa
4:00 asubuhi na kutoka saa 7:25 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, Dk. Slaa alisema alimsindikiza mkewe kituoni hapo kutoa maelezo akiwa shahidi yake.
“Leo mke wangu alikuja kutoa ushahidi.
Na maelezo yote aliyoyatoa yameandikwa. Ameyapitia na mimi nimeyapitia.
Hivyo, kwa upande wangu ushahidi nimekamilisha. Imebaki kwao tu kwa
hatua zaidi pamoja na faili letu kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP),” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza: “Ninaomba
ieleweke kwamba mke wangu ni shahidi na siyo mtuhumiwa kama ambavyo
nimekwisha kueleza. Naomba msipotoshe kama ilivyotokea awali.”
Kwa upande wake, Mushumbuzi alisema
wakati tukio linatokea, alishindwa kutoa ushahidi alipoitwa na Jeshi la
Polisi kwa sababu alikuwa safarini, lakini baada ya kurudi alitoa
taarifa kwa jeshi hilo.
“Wakati
tukio linatokea, niliitwa kutoa ushahidi wangu, lakini sikufanya hivyo
kwa sababu nilikuwa safari. Niliporudi niliwaambia, kwa hiyo wakaniambia
nije leo,” Mushumbusi.
Aliongeza: “Maelezo ambayo nimeyatoa ni
yale yale niliyosema kwenye vyombo vya habari. Kwa hiyo yameandikwa na
nimeyapitia nikajiridhisha.”
Awali, akizungumza na waandishi wa
habari juu ya wito wa mke wa Dk. Slaa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hakuwa na taarifa na jambo hilo
na kwamba suala hilo linawezekana kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa
utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Sina
taarifa juu ya jambo hilo. Lakini hilo ni jambo la kawaida. Siyo jambo
kubwa sana na ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi wa polisi. Na
kama amekuja kuhojiwa ni wito, ambao anaweza kuitwa mtu mwingine
yeyote,” Kova.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya
habari, Mushumbusi alidai alibaini njama za Kagenzi ambaye alikuwa
mlinzi wa Dk. Slaa, kutaka kumuua mumewe baada kukutwa na msaidizi wake
wa ndani akiwa katika meza ya chakula, ambayo hutumika kwa ajili ya
kuandalia chai ya mumewe japokuwa haikuwa kawaida yake kunywa chai
katika meza hiyo.
Alisema hata hivyo, baada ya kukutwa na
msaidizi wake wa kazi za ndani, Kagenzi alishtuka na kumwaga chai na
hata alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, hakutoa sababu za msingi.
Taarifa za awali za Kagenzi kutaka
kumdhuru Dk. Slaa zilitolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere
Marando, mbele ya waandishi wa habari, ambaye alieleza kuwa amekuwa
akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili
iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.
Alidai Kagenzi amekuwa akitumiwa na
maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na
kuziwasilisha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete ametunukiwa tuzo
kubwa zaidi zinazotolewa na Umoja wa Vijana wa Afrika, kwa kutambua
uongozi bora na mchango wake katika kuendeleza vijana.
Tuzo hiyo iitwayo “The African Youth Peace Award”,
hutolewa na umoja huo kwa wakuu wa nchi na viongozi wa Afrika, ambao
wamethibitika kuchangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa Waafrika.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, ilisema jana kuwa , Rais Kikwete alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa
Umoja huo, Francine Muyumba, wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alikabidhiwa tuzo hiyo aliposimama kwa
dakika chache kuwasalimia vijana wanaohudhuria mkutano wa tatu wa
viongozi vijana wa Afrika na China, mkoani Arusha.
Muyumba alimweleza Rais Kikwete kama
kiongozi mfano wa kuigwa kwa mchango wake katika kuwatambua na
kuwaendeleza vijana katika nafasi za uongozi.
Rais Kikwete alikutana kwa mazungumzo na
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe,
Robert Mugabe, aliyekuwa jijini Arusha kufungua mkutano huo.
Alimshukuru Rais Mugabe kwa kukubali mwaliko wake wa kutembelea Tanzania ili kufungua mkutano huo.
Rais Kikwete pia alikutana kwa
mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti
cha China, Wang Jiariu, ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa vijana
kutoka China kwa ajili ya mkutano huo.
HABARILEO
Wizara ya Nishati na Madini iko kwenye
mchakato wa kukamilisha uandaaji wa sheria tatu, zitakazowasilishwa
bungeni wakati wowote, zenye lengo la kuweka uwazi katika maeneo yote
yanayohusu mikataba ya uchimbaji wa madini na gesi.
Aidha, wizara hiyo imetangaza
kugunduliwa kwa gesi asilia ya futi za ujazo trilioni 1.0 hadi 1.8
katika kisima cha Mdalasini 1 mkoani Mtwara. Ugunduzi huo unaongeza
kiwango cha gesi asilia iliyopatikana kwenye kitalu namba mbili na
kufikia futi za ujazo trilioni 22.
Unafanya gesi asilia iliyopatikana
nchini hadi sasa kufikia futi za ujazo trilioni 55.08. Akizungumza mjini
hapa, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alitaja sheria
zinazofanyiwa kazi kwa sasa ni ya uchimbaji, usambazaji na utafutaji.
Sheria nyingine ni ya Uwazi na Uwajibikaji katika masuala ya madini na
inayofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Petroli ya mwaka 1984.
Alisema sheria hizo zote zina lengo la
kuhakikisha kila kitu kuhusu madini kuanzia uchimbaji, utafutaji wake na
mikataba kinakuwa wazi, tofauti na ilivyo sasa ambapo kwa mujibu wa
Sheria ya Petroli mikataba yote ni ya siri.
“Najua
watu wamekuwa wakipigia kelele uwazi wa mikataba, sasa hili tunataka
tulifanyie marekebisho ya kisheria, kwa kuwa mimi kama waziri nimefungwa
mikono siwezi kuweka hadharani kutokana na sheria kukataza hilo,
nikiiweka wazi kampuni hizi zina uwezo wa kunishitaki na nitalipa
mamilioni ya fedha,” Simbachawene.
Alisema ili kuendana na wakati na kasi
ya ugunduzi wa gesi asilia nchini na nchi nyingine za jirani, ikiwa ni
pamoja na ushindani wa soko la gesi, wizara hiyo inataka kuomba Bunge
lifanyie kazi haraka sheria hizo, ikiwezekana kabla ya Bunge la bajeti.
“Wenzetu
Msumbiji wamegundua gesi nyingi kuliko sisi, sasa tukiendelea kusuasua
na jambo hili la sheria kwa mwaka mmoja pekee, tutaachwa sana nyuma,
tunataka suala hili liishe muda si mrefu,” alisisitiza.
Hata hivyo, Simbachawene alisema si
kweli kwamba mikataba iliyopo ilikuwa na usiri mkubwa, kama
ilivyodhaniwa kwani mingi, ilikuwa ikiwasilishwa kwenye Kamati za Bunge
na kupitiwa na wabunge.
Akizungumzia ugunduzi mpya wa gesi
asilia, waziri huyo alisema kisima kilichogunduliwa gesi hiyo cha
Mdalasini 1, kimechimbwa katika urefu wa meta za maji ya bahari 2,296
Kusini mwa Kitalu namba mbili chenye miamba yenye umri miaka 66 hadi
145.
HABARILEO
Utekelezwaji wa adhabu ya kifo kwa watu
10 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, kutokana na kuhusika katika mauaji
ya watu wenye ulemavu (albino), unasubiri saini ya Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF).
Katika swali lake, Barwany, alitaka
kufahamu ni lini utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu 10, waliokwisha
hukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama kutokana na kuhusika na mauaji ya
albino, itatekelezwa. Silima, alisema kwa mujibu wa taratibu za
kisheria, adhabu ya kifo inapotolewa, utekelezaji wake husubiri saini ya
Rais.
“Sijapata taarifa kama hukumu hizi tayari Rais ameziwekea saini ili zitekelezwe ila nitafuatilia ili Sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Katika swali la msingi la mbunge huyo,
alitaka kufahamu hadi sasa kuna kesi ngapi za mauaji ya walemavu wa
ngozi zilizokwishatolewa hukumu baada ya kufikishwa mahakamani na kesi
ngapi bado zinasubiri huku na ni kwanini zimechelewa kutolewa maamuzi.
Waziri alisema kati ya mwaka 2006 na
2015, jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa
ngozi yaliripotiwa nchini na kati ya matukio hayo 41 yalihusisha vifo
43, matukio 13 yahusisha majeruhi na mawili ya kupotea watu hao albino.
Alisema kesi 46 kati ya matukio 56
zilifikishwa mahakamani na kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu
ya kifo na kesi 10 badi ziko chini ya upelelezi.
Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa
huru kwa kukosa ushahidi. Silima alisema pia kesi 10 bado zinaendelea
kusikilizwa mahakamani na ziko katika hatua mbalimbali.
“Kuhusu
kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi, kunachangiwa na
sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA)
kutoka mamlaka za uchunguzi na mashahidi kutopatikana kwa urahisi na
wakati”.
Katika swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Al Shamaar Kwegyir (CCM), alitaka kujua Serikali imefikia wapi katika kumtafuta mtoto Pendo Emmanuel mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa Kwimba, aliyechukuliwa mikononi mwa mama yake mzazi na mpaka sasa hajulikani alipo.
Akijibu swali hilo, Silima alikiri kuwa
mpaka sasa Polisi inamtafuta na katika upelelezi unaoendelea jumla ya
watu 14 wanashikiliwa na kuhojiwa kwa kuhusika kwa namna moja ama
nyingine na tukio hilo, akiwemo.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment