Tangakumekuchablog
Handeni,MKUU wa
Mkoa wa Tanga, Said Magalula, amesikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu
kuchoma moto misitu na nyasi na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya Tanga kuwachukulia
hatua za kisheria wote wenye tabia hiyo.
Akizungumza katika maadhimisho ya
siku ya Kutundika Mizinga ya Nyuki kitaifa yaliyofanyika kijiji cha Bogolwa
Wilayani Handeni Mkoani Tanga juzi,
Magalula alisema vitendo vya uchomaji moto misitu na nyasi umekuwa ukiwakimbiza
nyuki na viumbe hai.
Alisema hali hiyo pia imekuwa
ikichangia uhaba wa mvua katika maeneo hayo na kusababisha ukame na
hivyo kuwa chanzo cha kuibuka kwa uhaba wa chakula na njaa kuingia majumbani.
“Uchomaji wa moto misitu na nyasi
umekithiri Tanga na hili sitokubali kuona linaendelea----vitendo hivi vimekuwa
vikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na ukame” alisema Magalula
na kuongeza
“Tumekuwa tukiona baadhi ya maeneo
kukumbwa na balaa la njaa kutokana na kukosa mvua--- tumekuwa tukipata mvua
zaidi ya mara tatu kwa mwaka halafu sisi wenyewe tunaikimbiza kwa kukata miti
na kuchoma moto misitu” alisema
Katika kulikomesha hilo, Magalula
aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya Tanga kuwachukulia hatua kali za kisheria watu
wenye tabia ya kuchoma moto misitu na
nyasi na kuweza kulitokomeza jambo hilo kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza katika sherehe hizo,
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki , Gladness Mkamba, amewaondoa hofu
wafugaji nyuki kuwa soko la Asali liko ndani na nje ya nchi na hivyo kuwataka
kuongeza mizinga ya ufugaji nyuki.
Alisema kwa sasa soko hilo
linaendelea kukua kwa kasi katika masoko
ya Ulaya na Amerika na hivyo ni fursa za wafugaji kuyatumia masoko hayo pamoja
na soko la pamoja la Afrika Mashariki.
“Soko la asali linazidi kukua kwa
kasi kila siku na hii ni fursa kwa wafugaji na vijana kuchangamkia masoko---hii
ni pamoja na hili la kwetu la Afrika Mashariki” alisema Mkamba
Alisema Idara ya Misitu na Nyuki
itafanya makongamano na vijana kuhamasisha ufugaji nyuki kwani watu wengi
hawana elimu hiyo na kuadhimiria kutembelea kila Wilaya.
No comments:
Post a Comment