NILIJUA NEMEUA (3)
ILIPOISHIA
Habours ilikuwa klabu ya
starehe ambayo ilikuwa ikitumiwa kwa maonesho ya miziki hasa miziki ya taarab.
“Unataka nikufuate hapo
Habours Club?” nikamuuliza.
“Ndiyo”
“Nikupeleke wapi?”
“Nyumbani”
“Ulikuwa kwenye mziki?”
“Ndiyo”
SASA ENDELEA
Nilisita kumpa jibu. Kwa
upande mmoja sipendi kukatisha usingizi wangu kwani nilihitajika kuamka saa
kumi na mbili asubuhi niingie kazini. Kurudi kwangu nyumbani ni saaa sita au
saba usiku.
Lakini kwa upande mwingine
sikutaka kumkatisha tamaa mteja wangu. Kwa vile ilikuwa ni kazi ya usiku
nilijua ingeniingizia pesa nzuri. Nikaona nimfuate.
“Unasemaje, utanifuata?” Sauti ya Mariam ikakatisha mawazo yangu.
“Mko wangapi?” Nikamuuliza
ili kupanga masilahi yangu.
“Tuko wawili, mimi na rafiki
yangu”
“Nisubirini, nakuja”
“Sasa ukifika nipigie
unishitue kwani tuko ndani”
“Sawa, nitakupigia”
Mariam akakata simu.
Niliondoka kitandani na
kuanza kuvaa. Nilikuwa nikiishi eneo la Msambweni kwenye nyumba yangu mwenyewe.
Ilikuwa nyumba ya urithi. Tuliirithi mimi na mdogo wangu wa kiume baaada ya
baba yetu kufariki dunia.
Mdogo wangu Kabwe naye
hakumaliza hata miaka miwili akafariki. Alifariki Afrika Kusini alikokwenda
kutafuta maisha.
Nilipta habari kuwa alipigwa
na kuuawa na wenzake na kisha kuzikwa huko huko na serikali baada ya ndugu zake
kutoonekana.
Mimi nilikuja kufahamishwa na
marafiki zake walionipigia simu kutoka Capetown. Wakaniambia kuwa Kabwe aliuawa
na kuzikwa huko huko.
Baada ya kifo cha Kabwe
nikaimiliki mimi nyumba yetu. Ilikuwa na vyumba sita vya ndani na vinne vya
uani ambavyo nilikuwa nimevipangisha isipokuwa chumba kimoja ambacho nilikuwa
nikiishi mwenyewe.
Wakati huo sikuwa na mke na
pia sikuwa na mawazo ya kuoa, pengine ni kwa sababu sikuwa na wazazi wa kunipa
msukumo wa kuoa.
Mara tu baada ya kuvaa
nilichukua funguo ya gari nikatoka.
Nilimuamsha mpangaji wangu wa chumba cha mbele na kumwambia afunge mlango wa
mbele.
Teksi yangu ilikuwa barazani
mwa nyumba yangu. Nilifungua mlango wa dereva na kujipakia. Nikawasha gari na
kuondoka.
Nusu saa tu baadaye nilifika
Habours Club ambayo ilikuwa eneo la Bombo. Nilikuta teksi nyingi pamoja na
msongamano wa watu waliokuwa wakitoka katika klabu hiyo. Nilitafuta sehemu
yenye nafasi nikaiegesha teksi na kuwasiliana na Mariam.
“Tayari nimeshafika”
nikamwambia kwenye simu.
“Uko kwa wapi?”
Nakamuelekeza mahali
nilipokuwa namsubiri.
“Tunakuja sasa hivi”
akaniambia.
Baada ya kusubiri kwa dakika
kumi hivi nikaona wasichana wawili wakifungua milango ya teksi yangu na
kujipakia.
“Habari ya saa hizi?” Mariam
akanisalimia.
“Nzuri” nilimjibu huku
nikiirudisha gari kinyume nyume kisha nikabadili gea na kuondoka.
Wakati teksi ikiwa katika
mwendo Mariam aliniambia.
“Mimi ninakwenda barabara
ishirini na mwenzangu anakwenda Kange. Sijui utaanza wapi?”
Eneo la Kange liko karibu
kilometa tano nje ya jiji. Kwanza niliwaza
gharama ya mwendo wangu hadi huko kisha nikamwambia.
“Nitakupeleka wewe kwanza”
Kwa vile hawakuniuliza
itakuwa kiasi gani sikuona haja ya kuanza mimi kuwaambia. Nikanyamaza kimya.
No comments:
Post a Comment