Mkusanyiko huu kutoka magazetini unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete
amelikata Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na
vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wapigakura,
upigaji Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Akifunga mafunzo ya maofisa warakibu
wasaidizi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam jana, Rais
Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wenye nia ya
kuhatarisha amani katika matukio hayo.
“Tunayoyasikia
na tunayoyaona yanaashiria kuwapo kwa dalili za wenzetu kukwamisha
shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni
na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa lengo la kuhatarisha amani,” alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa yaliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.
Alisema Serikali itahakikisha kazi ya
uandikishaji katika daftari la wapigakura, upigaji wa kura ya maoni na
uchaguzi mkuu vinafanyika kwa amani na utulivu kwa gharama zozote.
Alisema ili kufanikisha kazi hiyo,
Serikali italiwezesha Jeshi la Polisi ili litekeleze kikamilifu majukumu
yake ya kulinda amani na utulivu.
“Tutawawezesha kwa kuwapa vifaa ili kuhakikisha mnafanya kazi yenu ya kutunza amani kwa umakini zaidi,” alisema Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula miwili ya urais baada ya uchaguzi mwaka huu.
Iwapo mambo yote yatakwenda kama
yalivyopangwa, Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa Aprili
30 wakati Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba.
Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Kikwete,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, “Rais Kikwete yeye
ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa kutangaza tarehe ya kufanyika
kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake na jukumu hilo ni la NEC,
Serikali yake kushindwa kuratibu vyema mchakato wa uandikishaji.
MWANANCHI
Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa
amesema zaidi ya asilimia 80 ya wabunge waliopo kwa sasa bungeni
hawakustahili kuwa wabunge kutokana na baadhi yao kuwa na uwezo mdogo
kiakili na uliolinganishwa na GB moja ya kompyuta.
Msigwa alisema kwa maoni yake ni
asilimia 20 pekee ya Wabunge ndiyo wenye uwezo na vigezo vinavyostahili
kupata nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi katika chombo hicho cha
kutunga sharia.
Alisema wakati umefika kwa taifa kuweka vigezo maalum vya kuwapata viongozi wa kisiasa wakiwemo wabunge na Rais.
“Tatizo la watanzania hatuna vigezo na
uwezo wa tunavyoviweka kwa ajili ya mtu anayetaka kuwa kiongozi, yaani
tujue mtu anayekuja kuomba uongozi anatakiwa awe mtu wa aina gani”
Msigwa.
Alisema kigezo kinachozingatiwa kwa
siasa ili mtu awe Mbunge cha kujua kusoma na kuandika hakitoshi na siyo
sahihi hivyo kinapaswa kitazamwe upya ili kupata wawakilishi watakaoweza
kutimiza wajibu wao ipasavyo.
“Wabunge
wengi hawamuelewi Tundu Lissu kwa sababu vichwa vyao vina GB moja za
ubongo, sasa kukusanya mambo yote yale ya bunge kichwa kinapata moto na
ilikupata majibu rahisi wanasema Lissu kichaa maana hawawezi kufikiria
kiwango kile kutokana na akili zao kuwa ndogo” Msigwa.
MWANANCHI
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi ameziagiza halmashauri zote za wilaya kutenga ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili lijenge nyumba za bei nafuu.
Lukuvi alisema hayo juzi wilayani Babati
mkoani Manyara, wakati akizindua mradi wa nyumba za gharama nafuu
zilizojengwa katika eneo la Mrara.
Katika mradi huo, nyumba 40 zenye vyumba
viwili vya kulala zitauzwa kwa Sh34 milioni, wakati zile zenye vyumba
vitatu, zitauzwa Sh45 milioni.
Alisema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuhakikisha wananchi wanapata nyumba za bei nafuu ili kuishi kwenye makazi bora.
“Tunataka
halmashauri zote zitenge maeneo maalumu, kwani tunatarajia miradi kama
hii iendelezwe mikoa yote nchini,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Naamini,
bei ya nyumba hizi wananchi wa kawaida wanaweza kuzimudu na hivyo
kutimiza ndoto za kuishi kwenye makazi bora yanayokwenda na wakati.”
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu
alisema mpango wa ujenzi wa nyumba za makazi ya gharama nafuu
unaojulikana kwa kauli mbiu; ‘Nyumba yangu, maisha yangu’, ulibuniwa ili
kupunguza uhaba wa nyumba.
Mchechu alisema nyumba nyingine za aina hiyo zinatarajiwa kujengwa katika maeneo 23 katika halmashauri mbalimbali.
“Ujenzi
wa nyumba hizi utawapa fursa wananchi kuishi kwenye nyumba za kisasa,
bora na gharama nafuu. Lakini pia mradi huu unapendezesha mandhari ya
miji na kuongeza wigo wa kodi ya majengo,” Mchechu.
MWANANCHI
Miaka
ya karibuni Jiji la Dar es Salaam limeshuhudia kuporomoka kwa maghorofa
matano katika maeneo tofauti likiwamo tukio la mwaka 2013, ambapo
ghorofa lililokuwa Mtaa wa Indira Ghandi lilianguka na kupoteza maisha
ya watu wapatao 34.
Ajali
zote hizo zimeacha idadi kubwa ya majeruhi, baadhi wakibaki na ulemavu
maisha, lakini hakujawa na taarifa rasmi kutoka tume zilizoundwa au
mamlaka husika zilizochunguza matukio hayo.
Hata hivyo, ukweli unabaki kwamba majanga hayo ya kuporomoka kwa
maghorofa yanahusishwa na ujenzi ulio chini ya kiwango au taratibu
zilikiukwa.
Ujenzi
wa majengo mengi ya sasa, unafanyika kwa kuvunja majengo ya kale yenye
urefu usiozidi ghorofa tano, majengo mapya huwa ni marefu zaidi ya yale
ya awali.
Mbali
na kuendelea kutumia miundombinu ya awali ya maji, umeme na majitaka,
majengo mapya hayana maeneo kwa ajili ya maegesho pengine hata huduma
nyingine za kijamii.
Profesa Kumbwa eli Salewi
anayeiwakilisha taasisi ya makandarasi ya ‘Institution of Civil
Engineers’ (ICE) ya New Zealand nchini anasema ujenzi unaofanyika sasa
wa hadi ghorofa 30 unasababisha kukosekana uwiano wa huduma za msingi.
Anasema
kwamba tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa Dar es Salaam ni jiji ambalo
ujenzi wa majengo mbalimbali unaoendelea sasa hauliweki salama pale
yatakapotokea majanga ya kibinadamu, asili au hata shambulio la kigaidi.
Anasema
kwa bahati mbaya likitokea shambulio, tetemeko la ardhi au kimbunga,
maafa yake huenda yakawa makubwa kuliko inavyofikiriwa na kusababisha
idadi kubwa ya vifo ambavyo vingeweza kuepukika.
Profesa
huyo anasema maeneo mengi ulimwenguni, ujenzi huzingatia uwepo wa
maeneo ya wazi yanayoweza kutumika kuwakusanya majeruhi au waathirika wa
janga lolote linaloweza kutokea.
“Ingawa
mabaya hayaombwi yatokee lakini iwapo itatokea, vifo vitakuwa vingi
kuliko inavyofikiriwa. Itakuwa ni kazi kubwa kulifikia na kuwapo kwa
nafasi kwa ajili ya uokoaji,” anasema.
Profesa
Salewi anasema mitaa ya Azikiwe, Samora, Bibi Titi na Barabara ya
Morogoro ilipaswa kuwa na eneo kubwa la wazi kama ilivyo nchi nyingine,
lakini hali ilivyo ni tofauti, kwani maeneo yote yamejengwa majengo
marefu ya biashara. Anasema nchini sekta ya ujenzi inakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwa pamoja na ukosefu wa uadilifu unaofanya
kandarasi kuzingirwa na rushwa, hivyo ujenzi kuwa chini ya kiwango.
MTANZANIA
Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar
es Salaam zimesababisha watu waliopoteza maisha kwa kufariki dunia
kufikia saba, huku nyumba zaidi ya 200 zikiwa zimezingirwa na maji
katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
umebaini kuwa katika maeneo ya Buguruni Kwa Mnyamani baadhi ya nyumba
bado zimengirwa na maji na kusababisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo
hayo kuhama kwa muda.
Mkazi wa Buguruni kwa Mnyamani, Mussa Abdallah, alisema kuharibika kwa miundombinu ya makaravati kumechangia maji kutuama kwenye makazi yao.
“Hakuna daraja ndiyo maana maji
yametuhama kwenye nyumba zetu, tunaiomba Serikali iweze kuchukua hatua
za dharura kwa kujenga daraja ili tuweze kupunguza hali hii,” alisema
Abdallah.
Alisema kutokana na mvua hizo, wamepata
hasara kubwa ikiwamo kuharibika kwa mali zao vikiwamo vyombo vya ndani
jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira ya umasikini.
“Vitu
vyangu vyote vimeondoka na maji na kubaki masikini, jambo ambalo
limenirudisha nyuma kimaendeleo, kutokana na hali hiyo, ninaiomba
Serikali inisaidie,” alisema.
Alisema licha ya mvua kusomba vitu
hivyo, lakini hawezi kuhama kwa sababu hawana mahali pa kwenda, na
kwamba Serikali imeshindwa kuwasaidia kwa lolote.
“Hadi
sasa hatujapata msaada wowote kutoka serikalini na kwamba hatuna pa
kwenda, jambo ambalo linanifanya nishindwe kuhama kwenye nyumba yangu,” alisema.
Katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole na
Mkunduge, Kigogo Bonde la Mto Msimbazi, Kinondoni Bonde la Mkwajuni,
Jangwani na Magomeni Sunna, pia baadhi ya nyumba bado zimezingirwa na
maji huku wananchi wakiwa wamehama kwa hofu ya kupoteza maisha.
“Nyumba
zetu zimechukuliwa na maji kutokana na mvua zinazonyesha, hali
iliyosababisha kuhamia nyumba za jirani kwa ajili ya kuomba hifadhi,” Juma Hussein mkazi wa Tandale kwa Mkunduge.
Kutokana na mafuriko hayo, wameiomba
Serikali kurekebisha miundombinu ya maji ikiwamo kujenga mifereji ya
kisasa itakayoweza kusafirisha maji kwenda kwenye mkondo wa Mto Ng’ombe.
MTANZANIA
Joto la Uchaguzi wa Rais ndani ya CCM linazidi kupanda huku makada na viongozi wa chama hicho wakipigana vijembe hadharani.
Hali hiyo inatokana na kile
kinachojitokeza sasa, kuibuka kwa makundi ya jamii, wakiwamo wanafunzi
wa vyuo vya elimu ya juu, kuwashawishi makada kadhaa wa CCM wawanie
nafasi hiyo ya uongozi wa nchi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba.
Makada ambao wamekuwa wakishawishiwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wakati baadhi ya makada wengine
wanaotajwa kutaka kuwania urais ndani ya CCM wakimlalamikia Lowassa,
wachambuzi wa siasa wamekuwa wakihoji mpango wa Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alipochapisha
vitabu na kugawa kwa wajumbe wote wa mkutano mkuu, lakini makada wenzake
wamekuwa kimya, hawajalalamikia kitendo chake hicho.
Mbali na hilo, pia anadaiwa kuwa
alinunua simu za Gallaxy Sumsang zaidi ya 140, akazigawa kwa wajumbe wa
Baraza la Vijana la CCM (UVCCM) Zanzibar suala ambalo bado hadi sasa
hajalitolea ufafanuzi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba, ambaye anatajwa kuwapo katika mbio za urais, alikuwa akitembea
na mabango ya kuonyesha watu wakimwomba agombee jambo ambalo lilimfanya
aandikiwe barua na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kusitisha
ziara zake ambazo zilitajwa kuwa za kampeni za kuwania urais.
Wafuasi wa Mwigulu pia wanadaiwa kuandika katika mawe makubwa katika barabara nchi nzima kwamba yeye ndiye Rais 2015.
Jana, Lowassa amejibu mapigo na kusema
hawezi kuwajibu wanaosema anawalipa wanaomshawishi kuwania nafasi hiyo,
kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili na wanachofanya ni
upuuzi na uongo.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana baadhi
ya vyombo vya habari, kumnukuu Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania
urais akisema kuna watu wanatumia vibaya umasikini wa Watanzania kwa
kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza na waandishi wa habari baada
ya kupokea ujumbe wa wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka
sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya
kuwagharamia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi, na kwamba wengi
wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.
HABARILEO
Mwongozo wa ada elekezi utakaondoa utata
wa utofauti wa kulipa ada baina vyuo na vyuo nchini, unatarajiwa
kukamilika na kuanza rasmi kutumika mwezi ujao.
Kwa sasa mwongozo huo umeshaandaliwa na
kinachosubiriwa ni mfumo wa kompyuta utakaosaidia kukokotolea ada
zitakazotumika katika vyuo vikuu nchini ambao ndio utakamilika rasmi
Aprili mwaka huu.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi
(CCM), aliyetaka kujua mchanganuo wa ada baina ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na endapo unaendana na
hali halisi.
Akijibu swali hilo, Kilango alikiri kuwa
kumekuwa na tatizo hilo la utofauti wa utozaji ada katika vyuo
mbalimbali nchini kwa muda mrefu, na kwa sasa Tanzania ina vyuo vikuu 53
na taasisi 21 zinazotoa shahada.
Alisema ada katika vyuo vikuu vya umma
ikiwa ni pamoja na UDSM na UDOM, zinatofautiana kati ya chuo na programu
wanayosomea wanafunzi.
Alisema, mfano programu ya uhandisi UDSM
ada yake ni Sh milioni 1.3 wakati UDOM programu hiyo ni Sh milioni 1.5
na katika programu za Sayansi na Ualimu UDSM inatoza ada Sh milioni 1.3
wakati UDOM unatoza Sh milioni 1.2.
Alisema kwa kuzingatia tofauti za kiasi
cha ada kinachotozwa na vyuo vikuu nchini, Serikali ilifanya utafiti wa
kina kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kupanga ada elekezi
kwa programu zote zinazofundisha katika vyuo vyote vikuu.
“Mwongozo
wa ada elekezi umekwishaandaliwa na kwa sasa Serikali inaandaa mfumo wa
software wa kukokotoa ada zitakazotumika katika vyuo vikuu vyote nchini,” alisema.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment