NILIJUA NIMEUA
ILIPOISHIA
Baada ya kusubiri kwa dakika
kumi hivi nikaona wasichana wawili wakifungua milango ya teksi yangu na
kujipakia.
“Habari ya saa hizi?” Mariam
akanisalimia.
“Nzuri” nilimjibu huku
nikiirudisha gari kinyume nyume ksha nikabadili gea na kuondoka.
Wakati teksi ikiwa katika
mwendo Mariam aliniambia.
“Mimi ninakwenda barabara
ishirini na mwenzangu anakwenda Kange. Sijui utaanza wapi?”
Eneo la Kange liko karibu
kilometa tano nje ya jiji. Kwanza niliwaza
gharama ya mwendo wangu hadi huko kisha nikamwambia.
“Nitakupeleka wewe kwanza”
Kwa vile hawakuniuliza
itakuwa kiasi gani sikuona haja ya kuanza mimi kuwaambia. Nikanyamaza kimya.
SASA ENDELEA
Nilimpeleka Mariam barabara
ishirini. Niliposimamisha teksi aliniuliza.
“Ni kiasi gani?”
“Unauliza kiasi cha kukuleta
hapa au cha kwenda mpaka Kange?”
“Kange atakulipa mwenyewe.
Niambie gharama ya kunileta hapa”
“Ni elfu sita”
“Punguza, fanya tano. Mimi ni
mteja wako wa kila siku”
“Haya nipe”
Mariam akafungua pochi na
kutoa noti ya shilingi elfu tano akanipa. Akafungua mlango wa teksi na kushuka.
Aliagana na mwenzake na
kwenda kubisha mlango wa nyumbani kwao. Nami nikaanza safari ya kuelekea Kange.
Nilipofika Kange Nilimuuliza
msichana anakwenda mtaa gani, akaniambia nikate kushoto. Nilipokata kushoto
akanielekeza mtaa ambao anaoishi.
Nilipofika katika mtaa huo
alinionyesha nyumba aliyotaka nimpeleke. Ilikuwa nyumba nzuri kuliko aliyokuwa
anaishi Mariam.
“Unanidai kiasi gani?”
Msichana akaniuliza niliposimamisha teksi.
“Nipe elfu kumi”
Msichana hakubishana.
Alifungua pochi yake akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kunipa. Akafungua
mlango na kushuka.
Alikwenda kwenye baraza ya
ile nyumba na kupiga simu.
Nilimsikia akisema.
“Asiya nifungulie mlango”
Nikaiondoa teksi na kumuacha
hapo hapo.
Wakati narudi jijini nilikuta
gari limeegeshwa kando ya barabara. Taa zake za nyuma zilikuwa zinawaka. Wakati
nalikaribia gari hilo
niliona mtu aliyekuwa kando yake akinipungia mkono kunisimamisha.
Wazo nililolipata kwanza ni
kuwa gari hilo
lilikuwa limeharibika na kwamba mtu aliyekuwa akinipungia mkono ama alikuwa
anataka msaada au alikuwa anahitaji huduma ya teksi yangu.
Kwa vile nilikuwa kwenye
mwendo wa kasi nililipita gari hilo
na kwenda kusimama mbele. Hapo hapo mawazo yangu yakabadilika. Niliwaza kwamba
huenda gari hilo
liliegeshwa kwa hila lionekane limeharibika kumbe ni majambazi wanaosubiri
magari yasimame waanze kupora watu.
Nilikuwa nimechelewa
kufikiria hilo.
Nilikuwa nimeshasimamisha teksi na jamaa aliyenisimamisha alikuwa ameshafika
kwenye dirisha la teksi yangu!
Chini ya siti yangu ya
dereva, siku zote huweka parange (sime ya kimasai) kwa ajili ya kujihami endapo
kutatokea tatizo la kuvamiwa na mtu au watu wenye nia mbaya.
Kwa vile sikuwa na uhakika
kuwa mtu huyo aliyenisimamisha alikuwa na nia mbaya au nzuri, tayari
nilishapeleke mkono wangu wa kulia kuushika mpini wa parange iliyokuawa chini
ya siti niliyokalia.
Nilikuwa nimejiweka tayari, kama atakuwa na nia mbaya niweze kukabiliana naye.
ITAENDELEA kesho na usipitwe na uhondo huu wa kusisimua kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment