Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Askari Polisi na wa Magereza, wametiwa
mbaroni mkoani Simiyu kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia ambazo kama
halali zingekuwa na thamani ya Shilingi milioni moja.
Hali kadhalika, askari hao wanadaiwa kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Charles Mkumbo, alisema jana kuwa askari hao walikamatwa juzi saa 9:00 alasiri mtaa wa Old Maswa, kata ya Nyakabindi wilayani Bariadi.
Kamanda Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu H 2420 PC Seleman Juma (25) na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28), wa Magereza wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika katika
kibanda cha kuweka na kutoa fedha cha M-Pesa kinachomilikiwa na Mwalimu
wa Shule ya Sekondari Old Maswa, Cassian Luhende, wakiwa katika pikipiki aina ya Sunlg kwa lengo la kuweka fedha hizo kwenye simu.
Alisema baada ya mwalimu huyo kupokea noti hizo ‘feki’ 10, alizitilia shaka na alipozikagua zaidi aligundua kuwa siyo halali.
Kamanda Mkumbo alisema Mwalimu Luhende
baada ya kugundua kuwa fedha hizo ni bandia, aliwajulisha jirani zake
kwa lengo la kuomba msaada wa kuwakamata askari hao.
Aidha, alisema baada ya mwalimu kutoa
taarifa kwa jirani, wananchi walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao
na ndipo mmoja alipotoa kitambulisho chake kikionyesha ni askari huku
mwingine akijitambulisha ni dereva wa bodaboda.
Aliongeza kuwa wananchi baada ya
kuambiwa hivyo waliwatilia shaka zaidi na kutoa taarifa Kituo cha Polisi
Bariadi na ndipo askari hao walipotiwa mbaroni.
Kamanda Mkumbo alisema baada ya askari
hao kukamatwa, PC Selemani Juma, alipekuliwa katika mfuko wa suruali na
kukutwa na noti nyingine bandia za elfu kumi-kumi ambazo kama halali,
zingekuwa na thamani ya Sh. 1,920,000.
Alifafanua kuwa askari huyo
alipopekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni kaptura
nne, fulana mbili, sare za kivita (combat) jozi moja pamoja na kitambaa
chake.
Kamanda Mkumbo alisema uchunguzi zaidi
unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani
ya mkoa huo huku akielezea baada ya uchunguzi kukamilika askari hao
watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
NIPASHE
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)
imejiondoa katika kesi ya kikatiba iliyoifungua Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam, kupinga utekelezaji wa maazimio nane yaliyopitishwa na
Bunge baada ya kushindwa kupinga mapingamizi yaliyowasilishwa na upande
wa serikali.
Mbali na IPTL kampuni nyingine zilizohusika kupinga maazimio hayo ni Pan Africa Power Solution Ltd (PAP) mmiliki wa IPTL, Habinder Sethi , na mmiliki wa kamapuni VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.
Mbele ya Jaji Stella Mugasha, wakili wa
upande wa utetezi, Gabriel Munyele, akisaidiana na wakili Joseph Sungwa,
aliiambia mahakama kuwa hakuna haja ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo
kwani zuio la muda waliloomba lilikuwa limeshaanza kutekelezwa na Bunge.
Upande wa serikali ukiongozwa na naibu Mwanasheria Mkuu, Gabriel Malata,
ulidai kuwa ulipwe gharama za kesi kutokana na usumbufu uliofanywa na
IPTL kung’ang’ania kupinga maazimio ambayo yalikuwa yalishaanza
kutekelezwa.
Malata alidai kuwa IPTL inatakiwa kulipa
gharama za uendeshaji wa kesi zikiwamo uchapishaji wa majalada na muda
waliotumia kuja mahakamani.
Aidha aliiomba Mahakama itumie vifungu vya sheria vinavyoelezea na masuala ya gharama za kesi kuiamuru IPTL kulipa gharama hizo.
Malata aliiomba mahakama itende haki ili
kukomesha usumbufu unaofanywa na kampuni au watu wanaofungua kesi
wakati wakijua hawawezi kushinda.
Jaji Mugasha aliitaka kampuni ya IPTL
iwajibike kwa kulipa gharama za kesi kwa kushindwa kujiondoa mapema
kupinga maazimio hayo, huku wakijua fika yalishaanza kutekelezwa.
Wakili Malata alisisitiza kuwa upande wa serikali utafuatilia ili kuhakikisha IPTL inalipa gharama za kesi kwa wakati mwafaka.
Desemba 31 mwaka jana serikali
iliwasilisha mapingamizi matano katika mahakama hiyo kupinga maombi ya
IPTL juu ya maazimio yaliyopitishwa na bunge.
Katika kesi hiyo namba 57 iliyosajiliwa
mwaka jana IPTL ilifungua kesi ya maombi kupinga ya maazimio nane
yaliyopitishwa na bunge yakiwamo.
Miongoni mwa maazimio hayo ni Bunge
kuitaka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na
usalama kuwachukulia hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa na
taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)) kuhusika
na kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya
Tegeta Escrow.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetakiwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete,
kusitisha upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa Aprili 30,
mwaka huu, kwa maelezo kuwa kulazimisha suala hilo kutasababisha mpasuko
na hatimaye kuzua vurugu na kuvunja amani ya nchi.
Pia imetakiwa kutokubali kuingiliwa
katika utendaji wake wa kazi ikiwamo kulazimishwa kuendesha mchakato wa
kura ya maoni katika tarehe hiyo.
Matamko hayo yalitolewa kwa nyakati
tofauti na Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) jana.
Wazee hao wakimtaka Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva,
kumshauri Rais Kikwete, kusitisha upigaji kura hiyo, Jukata limeitaka
serikali kuacha kuingilia utendaji kazi wa Nec kuhusu daftari hilo na
kuilazimisha kuendesha mchakato huo katika tarehe hiyo.
Pia wamemwandikia Jaji Lubuva barua kumsisitiza kutekeleza ombi lao hilo.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ester
Samanya, alisema wanamshauri hivyo Jaji Lubuva kwa kuwa wanaamini kuwa
hadi ifikapo tarehe hiyo, uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la
kudumu la wapigakura unaoendelea mkoani Njombe kwa kutumia mfumo mpya wa
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) utakuwa haujakamilika
kote nchini.
Alisema hali hiyo inatokana na nyenzo za
kufanikisha kazi ya uandikishaji wapigakura katika daftari hilo,
ikiwamo muda, vifaa na wataalamu, kutoandaliwa.
Samanya alisema kauli zinazokinzana kati ya Jaji Lubuva na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, juu ya uwezekano wa kura hiyo kupigwa katika tarehe hiyo au la, zinaashiria kuwa serikali inataka mtu wa kufa naye.
Hivyo, alimshauri Jaji Lubuva kutokubali
kuingia kwenye kashfa ya kujivunjia heshima, badala yake amshauri Rais
Kikwete kusitishwa mchakato huo.
“Ili
kuiepusha nchi na uvunjifu wa amani, uandikishaji usitishwe. Hilo siyo
msiba, lazima liandaliwe. Kulilazimisha, ni sawa na kulazimisha jogoo
kutaga. Lubuva asiwe mbuzi wa kafara,”Samanya.
Aliongeza: “Tunachokiona ni fujo inayotaka kutokea, kwani hilo (la kura ya maoni) haliwezi kutekelezeka.”
Kaimu Katibu Mkuu Baraza hilo Taifa, Erasto Gwota,
alisema uandikishaji wapigakura kwa kutumia mfumo wa BVR katika nchi
nyingi umefeli na kwamba, unafanywa nchini ili kuvuruga uchaguzi mkuu
ujao.
“Lubuva amshauri Rais jambo hili lisitishwe. Tukilazimisha hili, wengine watakosa kupiga kura,” alisema Gwota na kushauri kura ya maoni ipigwe baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katika barua yao yenye kichwa cha
habari: “Uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia BVR hapa nchini, ambayo
ilitarajiwa kupelekwa Nec jana, walimtaka Jaji Lubuva kuangalia upya
uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge
na madiwani.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
amesema kuwazuia wananchi kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee
urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni sawa na kuzuia
mafuriko kwa mkono.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake
mjini Dodoma jana wakati alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali
mkoani Mbeya waliokwenda kumshawishi atangaze nia kugombea urais.
Lowassa ametoa kauli hiyo siku moja
baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema kuwa kwa
kuandaa makundi ya kumshawishi, mbunge huyo wa Monduli anajua adhabu
yake na anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea urais kupitia CCM.
“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu jana
kuna watu wamesema maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi
mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo
vya habari. Mnazungumza, mnaelewana mnatoka pale,” alisema.
“Na
utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni vigumu kuuzuia, utazuiaje
mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu nazuia kwa mikono nitaweza
kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema.
Lowassa ambaye hivi karibuni aliweka
bayana kuwa ameshawishika kuwania nafasi hiyo, alisema, “Lakini mambo ya
chama hayawezi kuwa kwenye ma-TV, magazeti na maredio, mara huyu hivi,
mara huyu vipi. Mkiona chama kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari
sana, CCM ninayoijua mimi ni ya vikao.”
“Niseme
mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti nawaiteni, nakupeni fedha,
mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi nikiweka maturubai hapa ni
kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na wanasema nawapeni chakula mambo
ya ajabu sana na yanasemwa na watu wazima wenye heshima zao,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Juzi
walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia chakula nitawaweza? Nyie kwa
wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya unamdhalilisha binadamu
mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria tumbo. Hamna cha kufikiri
isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa
awapeni chakula, ni kudhalilisha watu.”
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunziza
wa Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’
kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo (DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15
hadi 20 ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais
Kikwete kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda
wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda, akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete
alisema, “kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake
kwa wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo
hivyo kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo
zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika,
lakini sasa itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema
Tanzania imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na
bahari. “Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya
kwa haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa
Kati wa Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga
hatua kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji
mizigo kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi
barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi
barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi
vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na
Nyakahura (Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha
kuwajibika katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini,
hivyo ni vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka
bandari ya Dar es Salaam bila tatizo.
MWANANCHI
Mkazi mmoja wa Miembe Saba wilayani
Kibaha mkoani Pwani amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwabaka watoto
wake wawili wadogo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Habari zilizolifikia gazeti hili,
zilisema kuwa katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi na
watoto wenyewe, baba huyo alianza kuwafanyia binti zake vitendo hivyo
mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe ambaye nimama wa wasichana hao hakuwapo
hadi usiku wa Machi 19, mwaka huu. Kwa sasa tunayahifadhi majina ya
familia hiyo.
Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 15
anayesoma darasa la saba na mdogo wake mwenye umri wa miaka 11
aliyeanza kubakwa akiwa darasa la tatu.
Kwa mujibu wa watoto hao, baba huyo
alikuwa anamuita mmoja wa watoto wake chumbani kwake na kumtaka alale na
mdogo wao wa kiume wakati huo akiwa na mwaka mmoja na binti akipitiwa
na usingizi humvua nguo za ndani na kumwingilia huku akimtaka kukaa
kimya na kuvumilia maumivu.
Mke wa mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa
akizimia mara kwa mara kutokana na kulia baada ya kubaini mchezo huo,
alisema aligundua watoto wake wanabakwa Ijumaa iliyopita baada ya mmoja
wa mabinti zake hao kumweleza kuwa baba yake alikuwa amembaka Machi 19,
mwaka huu.
Alisema kabla ya binti huyo kumweleza
hivyo, alimwomba asimpige kwani kuna kitu anataka amweleze, japo ni
kibaya lakini yeye amechoshwa na kimekuwa kikimuumiza kichwa.
“Alisema kila ninapokwenda katika
biashara zangu, anatamani nisiwe ninawaacha hapo, nikamwahidi sitamfanya
kitu ili mradi aseme ukweli tu,” alisema mama huyo.
Baada ya kuhakikishiwa kulindwa, ndipo
binti huyo aliposimulia jinsi ambavyo baba yake amekuwa akiwafanyia na
kuwatishia wakipiga kelele atawaua.
“Niliposikia mwili ulisisimka na ghafla
binti yangu mwingine naye akatokea akilia na kuniambia, ‘hata mimi baba
ananifanyiaga hivyohivyo kila siku unapokuwa umepeleka mboga sokoni
Kariakoo,” alisema mama huyo.
Mwanamke huyo ameomba sheria ichukue
nafasi yake katika tukio hilo kwa kuwa ni la kinyama na pia wataalamu wa
saikolojia wamsaidie binti yake mdogo wa darasa la tano kwani yeye
ameathirika zaidi.
Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.
uu
MWANANCHI
Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye
anaweza kuwa mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa
waliyonayo wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama
wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais
mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja
wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP),
Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna
kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake
kuangaliwa kama kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa
ni zamu yao kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya
urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza,
akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama
gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa
ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile
tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati
wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.”
Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze
kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala
ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania, (TGNP), Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo
ajabu kwani tayari wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali.
Isipokuwa wanahitaji kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
MTANZANIA
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa
ya Binadamu (NIMR),imesema vijana wenye umri wa kuanzia miaka 30 na
kuendelea, wanaongoza kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana,Mkurugenzi wa NIMR,Dk.Mwele Malecela alisema
kwa sasa tatizo hilo ni kubwa ambalo linawakumba vijana wengi hususan
barani Afrika.
Alisema hali hiyo,imesababisha vijana hao kutafuta dawa za kuongeza
nguvu za kiume aina ya Mundex,ili waweze kupunguza ukubwa wa tatizo
hilo.
“Vijana wengi wenye umri wa kuanzia
miaka 30 na kuendelea wana matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume, jambo
ambalo limewafanya kutafuta dawa za kuongeza nguvu ili waweze kuzitumia
na kupunguza ukubwa wa tatizo.
“Tangu tugundue dawa hii, idadi kubwa ya
wanaokuja kununua ni vijana hasa wenye umri wa miaka 30,hali ambayo
inaonesha wazi kuwa tatizo hili linakua kwa kasi,”alisema,”alisema Dk
Mwele.
Alisema kipindi kilichopita, matatizo hayo yalikuwa yanawapata wanaume
wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, lakini sasa hivi ni tofauti
kabisa ambapo vijana wenye umri huo ndiyo wenye matatizo hayo.
“Miaka iliyopita tatizo hili lilionekana
ni la watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea,sasa hivi
ni tofauti kabisa ambapo matatizo hayo yameshamiri kwa vijana, jambo
ambalo limewafanya kutafuta dawa ndani na nje ya nchi ili waweze
kujitibia,”alisema.
Alibainisha kuwa taasisi hiyo kwa
kushirikiana na tiba mbadala walifanya utafiti na kubaini kuwa dawa ya
Mundex inaweza kuwasaidia kupunguza ukubwa wa tatizo.
Taasisi hiyo,pia imebaini idadi kubwa ya wanawake wakiwamo watoto, wana matatizo ya uvimbe tumboni(Fibrous) hasa kwa waafrika.
Alisema dawa hiyo imethibitishwa kisheria na kwamba inaweza kutumika mahali popote kwa sababu haina madhara kwa binadamu.
HABARILEO
Watu watano wamekufa katika matukio
matatu tofauti, wakiwemo watatu waliouawa na miili yao kuchomwa moto na
wananchi wanaojiita wenye hasira, baada ya kutuhumiwa kuiba ng’ombe 40
katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani
Mara, Philipo Kalangi, tukio la kwanza lilitokea Machi 24 mwaka huu,
majira ya saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Kunanga wilayani Bunda.
Alisema watu hao watatu waliuawa kwa
tuhuma ya kuiba ng’ombe 40, mali ya Julius Malima (56), mkazi wa kijiji
cha Kenkombyo Neruma kata ya Neruma wilayani Bunda, baada ya kuvunja
zizi na kuanza kuswaga ng’ombe hao, majira ya saa 10:00 usiku.
Alitaja waliouawa kuwa ni Mayala Buluma
(29) mkazi wa kijiji cha JinivaKyabakari Wilaya ya Butiama na Mukina
Buluma (25), mkazi wa kijiji cha Namhura wilayani hapa, ambao wote ni
watoto wa mzazi mmoja.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment