Uchambuzi huu wa stori magazetini unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Kituo kimesajiliwa na NECTE. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Hatimaye mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema “ameshawishika” na kuweka bayana kuwa atachukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa
Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa makada wa
CCM wanaowania urais, lakini hakuwahi kutangaza nia ya kuwania nafasi
hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Lakini jana, alilazimika kufunguka
kuhusu suala la urais ambalo lilimfanya yeye na wenzake watano wafungiwe
kwa kipindi cha miezi 12 kujihusisha na harakati hizo baada ya Kamati
Kuu ya CCM kuwatia hatiani kuwa walianza kampeni mapema kabla ya muda
kufika.
“Nimepata barua za ushawishi kutoka kwa watu wengi, lakini nyinyi nimeshawishika,”
alisema Lowassa nyumbani kwake mjini Dodoma wakati alipokuwa
anazungumza na masheikh wa misikiti ya Wilaya ya Bagamoyo wanaokadiriwa
kuwa kama 50 hivi ambao pia walikuja mjini hapa kwa ajili ya kumshawishi
aingie kwenye kinyang’anyiro cha urais na kumkabidhi mchango wa
Sh700,000 za kuchukulia fomu.
“Lakini bado kuna taratibu za chama za kuheshimu. Nangojea pale watakaposema sasa tuwe, basi itakuwa.”
Lowassa alifungiwa na CCM Februari 18, 2014 pamoja na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Kilimo, Chakula na Ushirika), na January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine waliofungiwa ni Frederick Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu na William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema).
Pamoja na adhabu hiyo kumalizika
Februari 18, CCM imesema Kamati ya Maadili inaendelea na uchunguzi kwa
ajili ya kujiridhisha kama miongoni mwao kuna waliokiuka adhabu hiyo
kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati Kuu ambayo itafanya
uamuzi.
Masheikh waliofika jana nyumbani kwake
wanatoka maeneo ya Mlingotini, Kondo, Kaole, mjini Bagamoyo, Lugoba na
Chalinze wilayani Bagamoyo.
Mbali na kumuomba atangaze nia, masheikh hao pia walimsomea dua ya kumtakia heri katika harakati hizo.
“Nyie
ni special (maalum), mnatoka Bagamoyo na inajulikana kwa historia na ni
nyumbani kwa Rais (Jakaya Kikwete). Namimi nimepata baraka zake na nyie
mmemuwakilisha,”Lowassa.
“Tumetoka
naye mbali sana, lakini Mwenyezi Mungu akinijalia nitaanzia pale
alikomalizia. Amefanya kazi kubwa na ya heshima kwa kweli. Kwa hiyo
kitendo cha kutoka nyumbani kwenu kuja kuniona kwa kweli kimenipa nguvu
kwamba wenzangu wa Bagamoyo wako pamoja na mimi.”
MWANANCHI
Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa
mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.
Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya
nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa
kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia
ubunge.
Akizungumzia uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo atalipwa mafao yake yote.
“Unajua
Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa
yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando.
Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,” Joel.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe
wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa Zitto kabla ya muda wa Bunge la
10 kumalizika huku wakimwelezea ni kiongozi aliyeweza kuwaunganisha
katika kamati bila kujali itikadi za vyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,
wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa familia na
aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
“Alitufanya kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ijayo,”Ismail Aden Rage .
MWANANCHI
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira
aliyepewa jukumu la kuandaa Ilani ya CCM kwa ushirikiano na timu ya
watu 23 wa chama hicho itakayotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka
2015 hadi 2020, amejitokeza na kusema kazi hiyo ipo ukingoni kukamilika.
Kauli hiyo Wasira ameitoka siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
kuwaeleza waandishi wa habari mjini Arusha kuwa Ilani hiyo inasimamiwa
na Wasira na inatarajia kutoa Dira ya Mwelekeo ya chama hicho tawala
katika kutatua matatizo ya wananchi.
Alisema Ilani hiyo itaangazia pia mambo
ambayo yaliahidiwa ndani ya Ilani iliyopita na hayakutekelezwa ipasavyo.
Baadhi ya mambo ambayo hayakufanikiwa ni tatizo la maji, migogoro ya
ardhi na suala la ajira.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu, Wasira alisema: “Unajua
labda ninyi mtakuwa mmechelewa kupata taarifa kuwa tumeanza lini,
lakini sisi tulikwishaanza kazi hii na tuko hatua za mwisho za kutoa
Rasimu ya Ilani yenyewe.”
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda
alisema Ilani hiyo inaandaliwa kwa kuangalia changamoto gani
zilizojitokeza kwa miaka 10 nyuma na ndiyo wanayoipa kipaumbele katika
maandalizi hayo.
“Ukiangalia
uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia saba kila mwaka lakini si kiwango
kikubwa ukilinganisha na maisha ya wananchi yalivyo hivyo Ilani hii
itatakiwa kuja na majibu ya tatizo hilo na kuhakikisha wananchi wetu
wanakuwa na maisha bora,” Wasira.
“Suala
la ajira ukiangalia wanafunzi wengi wanaanza shule za msingi na
wanapomaliza wanaendelea sekondari na baada ya hapo wanakwenda vyuoni
hivyo wahitimu wa vyuo vyetu wanaongezeka jambo hapa ni kuja na mkakati
wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu.”
HABARILEO
Mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta
kwa ajili ya kufua umeme nchini, imetajwa kuwa kikwazo katika maendeleo
ya Taifa, kutokana na kutumia rasilimali fedha za kigeni nyingi katika
kuzalisha nishati hiyo nchini, ambayo ingeweza kutumika katika
maendeleo.
Taarifa za uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Benki Kuu (BoT),
zimebainisha kuwa suluhisho pekee la tatizo hilo, ni kukamilika na
kuanza kazi kwa bomba la gesi kutoka Madimba Mtwara, hadi Kinyerezi, Dar
es Salaam.
Trilioni 1.6 Taarifa ya TPDC kwa umma
iliyotolewa mwishoni mwa wiki kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa
miundombinu ya gesi asilia kutoka Madimba, Mtwara hadi Kinyerezi Dar es
Salaam, imeeleza kuwa ununuzi wa mafuta hayo ya kufua umeme umekuwa
ukigharimu Taifa zaidi ya Sh trilioni 1.6 kila mwaka.
“Itakapokamilika
miundombinu hiyo (ujenzi wa bomba la gesi), itaokoa zaidi ya Dola za
Marekani bilioni moja sawa na Sh trilioni 1.6 kwa mwaka, zinazotumika
kwa sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya kufua umeme kwa kutumia mitambo
ambayo tayari ipo nchini,” imeeleza taarifa hiyo.
Mitambo hiyo ni pamoja na mtambo wa IPTL
uliopo Tegeta Dar es Salaam unaotumia mafuta mazito na mitambo ya
Agreko na Symbion iliyopo Dar es Salaam, inayotumia gesi inayoagizwa
kutoka nje.
Mwingine ni mtambo wa Symbion wa Dar es
Salaam pia, ambao unatumia mafuta ya kurushia ndege na mitambo mingine
miwili ya Symbion ya Dodoma na Arusha, ambayo inatumia gesi inayoagizwa
kutoka nje.
Tanesco inavyonyonywa Taarifa kutoka
Tanesco zimebainisha kuwa kitendo cha mitambo hiyo kutumia mafuta
mazito, mafuta ya ndege na gesi kutoka nje ya nchi, badala ya gesi
asilia kufua umeme, kimekuwa ‘kikitafuna’ shirika hilo, kwa kuwa
wamiliki wa mitambo hiyo huuza umeme kwa shirika hilo kwa bei ya juu,
kuliko bei ambayo Tanesco inalazimika kuuza kwa wananchi.
HABARILEO
Shamba la miwa inayokadiriwa kufikia
tani 6,000 baada ya kuvunwa lenye ukubwa wa hekta 240, limechomwa moto
na watu wasiojulikana na kusababisha hasara ya Sh milioni 280.2, mali ya
wakulima wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi,
wakulima hao walisema kuwa vitendo hivyo vya jamii kuendelea kuchoma
moto hovyo nyikani vimeanza kurejea.
Mmoja wa wakulima hao, Anas Swaibu
alisema uchomaji moto hovyo umekuwa changamoto kuu inayorudisha nyuma
maendeleo ya mkulima na kumsababishia kutotimiza malengo yake.
Alisema kuwa athari ya moto mashambani,
imekuwa ikisababisha mkulima kulazimika kuvuna miwa yake kabla
haijakomaa, huku uamuzi huo ukimuingiza hasara kwani malengo ya mavuno
yake hushindwa kukamilika ipasavyo.
Kutokana na athari zinazoendelea
kusababishwa na vitendo vya uchomaji moto hovyo, mkulima huyo ameuomba
uongozi wa serikali ya wilaya kuangalia upya jinsi gani utawala utaweza
kushirikisha jamii katika kutokomeza majanga hayo.
“Tunaomba
Serikali ifanye utaratibu wa kukutanisha wadau wa maendeleo, wakulima
na jamii kwa ujumla ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza kutokomeza
vitendo hivi kwani kila siku mkulima anazidi kuumia jambo ambalo
linarudisha nyuma maendeleo yake,”alisisitiza.
Alisema kuwa kwa sasa bei inayotolewa na
mnunuzi mkuu ambaye ni kiwanda cha Sukari cha Kagera kilichopo wilayani
humo ambayo ni Sh 46,700 kwa tani moja, kiasi ambacho kiko chini na
hakiendani na gharama za uzalishaji katika kilimo hicho.
Alisema shughuli za kilimo cha miwa
zinachukua gharama nyingi ukilinganisha na bei inayotolewa kiwandani,
japo angalau bei inapaswa kufikia kiasi cha Sh 55,000 kwa tani ili
mkulima aweze kupata faida na kukidhi mahitaji yake ya msingi
ukilingaisha na gharama za kilimo kupanda.
“Mitaji
ya wakulima ni mikopo, hivyo tunalilia bei kwa mnunuzi tukiwa na maana
ya kwamba tuweze kurudisha mikopo ya benki na sisi tunufaike na kilimo
hiki, kuliko kushindwa kurudisha hata mikopo na kufilisiwa na
waliotukopa,” alisema.
Hata hivyo, licha ya kutoridhika na bei
hiyo inayotolewa na mnunuzi wa kiwanda hicho, mkulima huyo ametoa
shukrani kwa uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera Sugar kwa kutoa msaada
mkubwa kwa wakulima vinginevyo kama uongozi usingekuwa karibu na
wakulima hao, hakuna ambaye angelikuwa anaendelea na shughuli za kilimo
hadi sasa.
MTANZANIA
Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda amekimbilia nchini Marekani kuomba hifadhi ya kisiasa.
Chanzo cha kuaminika kutoka Marekani kilisema Banda ameshapewa hifadhi na Serikali ya Marekani ingawa inafanywa kwa siri.
Banda akiwa nchini humo amekuwa
akishiriki hafla mbalimbali anazoalikwa na moja ya hafla aliyoalikwa ni
ile ya utoaji tuzo ya kimataifa ya uongozi ya taasisi ya GB Group Global
ya Marekani ya mwaka 2015 iliyofanyika katika jiji la Washington.
“Ni
kweli Joyce Banda yupo nchini Marekani kwa muda mrefu sasa,na katika
hafla hiyo alisema alipokuwa rais kwa muda mchache alijenga wodi za
wazazi zilizowasaidia wanawake nchini Malawi kujifungua katika mahali
salama” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine kilisema Juni mwaka jana baada ya Peter Mutharika kuapishwa kuwa rais mpya wa Malawi ndipo Banda alipokimbilia Marekani.
JAMBOLEO
CHADEMA imesema aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe angerithi mikoba ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe au Dk. Slaa kama angekuwa na nidhamu na kutokuwa msaliti.
Pia kimesema hakitamsahau Zitto kwa kwani alikuwa na mchango mkubwa ndani ya chama hicho.
Mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani Tundu Lissu
alisema Zitto alikuwa na mazuri yake ndani ya chama hicho na ni
miongoni mwa watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya
viongozi wetu wa ngazi ya juu.
Pia Lissu alifafanua kuwa aliamua
kutompa Ziito mkono wa kumuaga baada ya kutangaza uamuzi huo bungeni kwa
kuwa kufanya hivyo kungemfanya aonekane mnafiki.
Amesema anasimamia anachokiamini kuhusu
kasoro alizozifanya Zitto za kumfanya atimuliwe na aliamua kuondoka kwa
kuwa alijua kinachofuata kwa kuwa alikiuka katiba ya chama inayokataza
mambo ya chama kupelekwa mahakamani.
NIPASHE
Polisi Jijini Arusha wamelazimika
kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananachi wenye hasira waliochoma
nyumba na magari baada ya kijana wao anayetuhumiwa kufumaniwa akifanya
mapenzi na mfanyakazi wa ndani kuuawa na anayedaiwa kuwa bosi wa
mfanyakazi huyo.
Bosi huyo mkazi wa mtaa wa Olasiti Arusha pamoja na wenzake wawili wanatuhumiwa kumuua kijana huyo Melita Mokosio
baada ya kumfumaini akifanya ngono na msichana huyo hatua
iliyosababisha wakazi wenye hasira kuchoma nyumba yake na magari matatu
ya waliohusika na mauaji hayo.
Watu walioshuhudia tukio hilo
lililotokea majira ya saa3 asubuhi walimtaja anayedaiwa kumuua kijana
huyo ambaye anajulikana kwa jina la baba Tony.
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Edward Balele
aliyekuwa eneo la tukio alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na
uharibifu wa mali lakini alisema jeshi lake linafanya uchunguzi wa tukio
hilo kabla ya kutoa taarifa rasmi.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment