Wednesday, March 25, 2015

HANDENI NI KILIO CHA MAJI KILA KONA

Tangakumekuchablog

Handeni, WAKAZI wa Songe, Misima na Kwagulu Wilayani Handeni Mkoani Tanga, wameitaka Serikali kuchukua uamuzi sahihi wa kulipatia ufumbuzi tatizo la maji Wilayani humo baada ya miaka mingi kuwa wavumilivu wa ahadi zisizotekelezeka.

Wakizungumza na Tangakumekuchablog kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema wakati umefika sasa wa Serikali kulimaliza tatizo hilo ambalo limekuwa likiwaumiza vichwa wananchi  Wilayani humo.

Walisema wakazi wengi wamekuwa wakiugua magonjwa ya matumbo na kichocho baada ya kutumia maji ambayo sio salama kwa matumizi ya binadamu ambapo wengi wao wamekuwa wakitumia maji ya mito na visima visivyo rasmi.

“Kwa miaka mingi tumekuwa wasikivu kwa viongozi wetu kwa ahadi ambazo wamekuwa wakituahidi----lakini sasa ni sisi wananchi tunaomba kusikilizwa kwani tumechoka kutumia maji ambayo ni hatarishi” alisema Sonyo Shetumba

“Watu wengi wanaugua magonjwa ya matumbo na safura ikiwa ni matokeo ya matumizi ya maji ambayo sio salama----kwa kweli sasa wananchi tunaitaka Serikali ituhurumie” alisema

Kwa upende wake mkazi wa Kwagulu, Yussuf  Ramadhani, alisema kukosekana kwa maji katika shule kumekuwa kukihatarisha magonjwa ya miripuko baada ya shule nyingi kutokuwa na visima na badala yake wamekuwa wakitegemea maji msimu wa mvua.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwaweka katika mazingira magumu wanafunzi hasa katika suala zima la usafi wa mazingira jambo ambalo athari zake zimekuwa zikiwakumba majirani wa maeneo ya shule.

“Majirani wanaokaa na shule wamekuwa wahanga wa kuishi  na woga baada ya vyoo wanavyotumia wanafunzi  kutokuwa na maji----hii imekuwa ikiwalazimu kutofanya usafi” alisema Ramadhani

Alisema kwa vipindi virefu viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa ahadi ya kulimaliza tatizo la maji Wilayani humo lakini hakuna utekelezaji na kuiomba Serikali kuu kuliangalia kero hiyo kwa jicho la huruma.

Alisema wakazi wengi wamekuwa wakitegemea maji ya kununua ambapo dungu moja huuzwa kati ya shilingi 2,000 hadi 2,500 na wengi wao husihindwa kutokana na kutokuwa na uwezo.

                                                    Mwisho

No comments:

Post a Comment