Tangakumekuchablog
Muheza, WAKATI
Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Tanga (Tanga Uwasa) ikiwa katika maadhimisho
ya wiki ya Maji, bado wakazi wengi wanaendelea
kuteseka kukosa huduma hiyo muhimu na kulazimika kufunga safari kufuata maji.
Wakazi wa vijiji vya Mkanyageni,
Ngomeni na Kirapura Wilayani Muheza vinavyopakana na jiji la Tanga wamekuwa
katika kero ambayo wamedai kuwa itakuwa ndoto katika maisha yao kupata maji safi
na salama ya mabomba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
Tangakumekuchablog mchana huu, wakazi hao walisema wamekuwa wakiamka saa kumi za usiku kuwahi foleni
kijiji cha Pongwe kilichoko jiji la Tanga ambapo dumu moja huuzwa shilingi mia
tano.
Walisema maji hayo ambayo hutegemewa na wakazi wengi wa Muheza wamekuwa
wakiamka saa kumi za usiku ili kuwahi foleni na kukumbana na vikwazo vingi
vikiwemo gharama za usafiri .
‘Kero hii ya shida ya maji katika
Wilaya yetu ya Muheza imekuwa ya mazoea ambayo inatuumiza-----si usiku wala
mchana muda wote tuko katika kusaka maji na kuacha kufanya kazi za kujiletea
kipato” alisema Asha Mbaraka
“Maadhimisho haya ya wiki ya maji
kwetu hayana faida yoyote kwetu zaidi ya kupigwa vijembe----naweza kuyaita ni
wiki ya masimango” alisema Asha
Asha alisema kero hiyo ya maji
imekuwa ikiwafanya kuwa katika mazingira hatarishi katika majumba yao baada ya
matumizi ya maji kushindwa kukidhi na kutumia kwa tahadhari jambo ambalo
linatishia magonjwa ya miripuko.
Kwa upande wake, mkazi wa Ngomeni
moja, Rukia Abdalla, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiiomba Serikali na
mashirika ya misaada kuwachimbia kisima ili kupunguza kero lakini maombi yao
yamekuwa yakiwekwa kapuni.
Alisema hali hiyo imekuwa ikirejesha
nyuma jitihada za kujiletea maendeleo na nguvu kazi na akili zao kuziweka zaidi
katika kusaka maji ambayo yanahitaji pesa kuweza kuyapata.
“Bila maji watoto hawawezi kwenda
shule na kuwaandalia chai pamoja na chakula cha mchana wanaporejea-----hii
inatufanya kupunguza kasi ya kujiletea maendeleo baada ya kushinda muda mwingi
katika foleni za maji” alisema Rukia
Alisema ili kuweza kumaliza kero
hiyo ni vyema mamlaka ya maji Tanga Uwasa kwa kushirikiana na Serikali kuweka
nguvu za kusambaza maji mjini na vijijini na kudai kuwa ni aibu Wilaya ya
Muheza kukosa maji wakati bwawa linalopeleka maji Tanga linatokea Muheza.
Wakazi wa vijiji vya Mkanyageni, Ngomeni na Kirapura Wilayani Muheza Mkoani Tanga wakiwa katika foleni ya maji kwa kuyafuata zaidi ya kilometa 20 baada ya maeneo yao kutokuwa na maji kwa miaka mingi.
No comments:
Post a Comment