Uchambuzi huu wa magazeti umeletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre.Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi wanaojiunga kidato cha pili hadi cha sita. Pia wanatoa kozi za kiingereza na kufundisha Computer na kutoa cheti. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB, simu 0715 772746
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana,
amewataka wananchi waliowekewa alama ya `X’ katika nyumba zao kwa muda
mrefu bila kulipwa fidia kuzifuta hadi serikali itakapowalipa stahiki
zao.
Kinana alitoa kauli hiyo wakati
akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi
Ngaramtoni Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya
ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Wananchi
wanakaa na hofu kwa muda wote wakati serikali haiwalipi haki zao wala
kuwapelekea maendeleo na matokeo yake wanaishia kudhulumiwa,” Kinana.
Alisema serikali ikitaka kutengeneza
barabara kwanza itafute fedha, kama fedha hakuna basi waondoe alama za
`X’ walizoweka kwenye nyumba za wananchi.
“Haya
mambo ya upembuzi yakinifu, mchakato na tupo mbioni kuleta fedha…ni
mazingaombwe ambayo sasa yafikie mwisho. Mimi nasema kawekeni chokaa
mpaka mtakapolipwa fedha zenu na wakija waambieni tangu miaka mitatu
iliyopita gharama za ujenzi zimeongezeka wawaongeze kidogo,” Kinana.
Alisema haiwezekani mchakato wa kujenga barabara ukae kwa zaidi ya miaka mitatu.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
alisema vyama vya upinzani vimeonyesha dalili ya kufa kutokana na
kukumbatia vurugu na kuwataka wananchi kuingia mitaani hata kwa mambo
yasiyo na maana.
“Mfano
nchi mbili za Libya na Misri, wapinzani waliwahadaa vijana waingie
mitaani kwa ahadi ya maisha bora, lakini kinachotokea sasa hivi katika
nchi hizo ni kinyume chake,”Nape.
NIPASHE
Serikali haijawasilisha kwenye ofisi za
Bunge miswada ikiwamo ya vyombo vya habari ambayo itasomwa na kujadiliwa
kwenye vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa si Ofisi ya Katibu wa Bunge wala wabunge wenye miswada hiyo.
Ofisa Habari wa Bunge, Prosper Minja,
alisema Bunge halijapata nakala za miswada ya sheria ya kupata habari
wa mwaka 2015 na ule wa sheria ya vyombo vya habari wa mwaka 2015,
ambayo yote imepangwa kuwasilishwa Ijumaa ijayo kwa hati ya dharura.
Kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano huu wa
Bunge, miswada hiyo itasomwa kwa mara ya kwanza na kupitishwa kwenye
hatua zake zote siku hiyo hiyo.
Minja alisema bado wanasubiri serikali
iwasilishe miswada hiyo ndipo waandishi wa habari wanaweza kupata
akieleza kuwa haipo hata kwenye idara ya kumbukumbu rasmi za Bunge.
Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
imesema bado haijapata nakala za miswada hiyo licha ya kwamba inapaswa
kuipata ili iweze kuandika maoni ya kambi hiyo kwa mujibu wa kanuni za
Bunge.
Msemaji wa Kambi hiyo katika Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema hata yeye anaitafuta miswada hiyo, lakini hajaipata.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema
hajapata hati za dharura za kuwasilishwa kwa miswada hiyo. Makinda
alilazimika kueleza hayo alipokuwa akimjibu mbunge wa Chonga (CUF), Haroub Muhammed Shamsi, aliyekuwa akiuliza swali kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Miswada hiyo inawasilishwa wakati wadau
wa tasnia ya habari wakiwa na hofu kwa kuwa hawajashirikishwa hivyo
kutoshirikishwa kwao kunaweza kusababisha kutungwa sheria za kuathiri
sekta ya habari.
Wadau wana wasiwasi kuwa miswada hiyo
imekwishakamilika na wadau wa habari hawatakuwa na fursa yoyote ya
kushirikishwa kuutolea maoni kwa lengo la kuuboresha.
Hata hivyo, kuwasilishwa kwa muswada huo
kunaweza kuleta furaha au kiama kwa wadau wa habari kutokana na wadau
kutoshirikishwa katika kuuandaa.
Kulingana na taratibu, kabla ya muswada
huo kuwasilishwa bungeni, wadau wa habari wanatakiwa kushirikishwa
katika mchakato mzima, lakini katika mchakato wa Muswada wa Sheria ya
Vyombo vya Habari wa mwaka 2015 ha wa haki ya kupata habari mwaka 15,
serikali haijafanya jitihada za kushirikisha wadau badala yake,
umeandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
MWANANCHI
Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na
alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga
wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama
wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile
kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka
mmoja uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo
chake cha kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa
mashabiki wake waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa
Chadema.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema: “Hahahaa… tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo
yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu
yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi
tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa
kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa
ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za
siasa.
Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa
naye kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa
uanachama, Mwigamba na Prof. Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na
uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya
uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na
kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba
alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa
kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
MWANANCHI
Serikali imeombwa kuingilia kati mgogoro
unaoendelea baina yake na nchi jirani ya Kenya, kuhusu kuzuiliwa kwa
magari ya Tanzania ya kusafirisha watalii kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Jomo Kenyata ili kuleta usawa na ustawi wa sekta ya utalii
kwa nchi zote mbili.
Akizungumzia athari zinazotokana na mgogoro huo jana, mfanyabiashara maarufu nchini, Vicent Laswai
akipanda Mlima Kilimanjaro alisema, Serikali imekuwa ikipoteza watalii
wengi kutokana na magari yanayotoka nchini kutoruhusiwa kuingia katika
uwanja huo wa ndege.
Alisema suala hilo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kupoteza mapato yanayotokana na utalii pamoja na kudidimiza sekta hiyo.
“Ingawa
kunahitajika tafakuri ya kina kuhusu faida na hasara za mgogoro huo kwa
Tanzania, kuna kila sababu Serikali yetu, ikaamka usingizini kwa kuwa
wenzetu, wanaweza kutumia fursa hii kuendelea kujitanua na kuua
ushindani wa kisekta… Ni vizuri ukatatuliwa haraka ili kutoa nafasi kwa
wadau kuendelea na malengo ya kuvutia kimataifa,” Laswai.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Marenga Investment, Joseph Kimoso alisema mgogoro huo, unahitaji ufumbuzi wa haraka.
Kisomo alisema ni vyema Watanzania
waanze kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuliingizia
taifa kipato, pamoja na mamlaka husika kuanzisha vilabu maalumu vya
utalii.
Mkuu wa Idara ya Utalii ya Hifadhi ya
Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Eva Mallya akitoa taarifa yake,
alisema mkakati endelevu wa Taifa unaolenga kuongeza idadi ya Watanzania
kutembelea hifadhi nchini umeanza kuleta tija.
MTANZANIA
Ifikapo Julai Mosi mwaka huu endapo mwanao atabainika kuwa na silaha bandia (mwanasesere)
atakuwa amefanya kosa la jinai, kwa vile Muswada wa Sheria ya Usimamizi
na Udhibiti wa Silaha na Risasi umepiga marufuku uingizwaji na matumizi
yake nchini.
Muswada huo uliopitishwa na Bunge jana
utaanza kutumika Julai mwaka huu, pamoja na mambo mengine, unalenga
kuziba mianya ya kuingiza silaha bandia nchini.
Mbali na hilo, Muswada huo unasema mtu akibainika kuwa ni mlevi hatakuwa na sifa ya kumiliki silaha.
Pia muswada huo unataja moja ya sifa za
kumiliki silaha kuwa ni mtu na umri wa miaka 25 na kuendelea. Sheria ya
sasa ilikuwa haijaainisha ni umri gani ambao mtu anatakiwa kumiliki
silaha.
Akisoma kwa mara ya pili muswada huo jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, alisema moja ya sababu ya kutungwa kwa sheria hiyo ni kutoainishwa vema silaha zinazoweza kumilikiwa na raia.
Alisema sababu nyingine ni kutobainishwa kwa utaratibu wa kuweka alama kwenye silaha kisheria.
Silima alisema pia kuwa tangu mwaka 2003 hadi 2013 serikali imeteketeza silaha mbalimbali 28,380.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Kapteni John Chiligati, alisema kutokana na ongezeko la uhalifu wa kutumia silaha, adhabu iliyopendekezwa na serikali irekebishwe.
“Kifungu cha 20 (2) kinatoa adhabu ya kulipa faini ya Sh milioni 10 au
kutumikia kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja kwa mtu anayetiwa
hatiani kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria,”alisema.
Naye msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Godbless Lema,
alisema mbali ya kutungwa sheria kali, serikali inapaswa kuzingatia
misingi ya utawala bora, haki, usawa, ukweli na ustawi wa jamii kulinda
amani na utulivu nchini.
HABARILEO
Baadhi ya wabunge wameitaka Serikali
kuona umuhimu wa kuwawekea ulinzi wabunge na viongozi wengine wa
Serikali bila upendeleo, kwa kuwa wanaishi katika maisha ya hofu na
hatarishi.
Pamoja na hayo, wabunge hao pia
wameitaka Serikali kuanza kuchukua tahadhari hasa katika kipindi cha
uchaguzi kwa kuhakikisha inadhibiti matukio yoyote ya uhalifu, ikiwemo
matumizi ya silaha dhidi ya wananchi, wagombea na viongozi.
Wabunge hao walikuwa wakiwasilisha maoni
yao bungeni mjini Dodoma jana wakati wakichangia mjadala wa Muswada wa
Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi wa mwaka 2014.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbelss Lema
(Chadema) ambaye pia ni Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema kutokana na kazi ya kufichua mambo mengi
yanayoigusa jamii, ni vyema Serikali ikafikiria kuweka ulinzi katika
nyumba za wabunge.
Alisema hata Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
aliyeibua sakata la Tegeta Esrow lililowandoa baadhi ya mawaziri na
viongozi wengine wa Serikali madarakani, kwa sasa anaishi kwa hofu
kutokana na kukosa ulinzi.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM)
alisema wakati umefika kwa Serikali kuona umuhimu wa kuwapatia ulinzi
wabunge, ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu kumiliki silaha ili waweze
kujilinda.
Aidha, Ngonyani maarufu kama Profesa
Majimarefu kutokana na shughuli zake za uganga wa asili, aliitaka
Serikali kuanza kuchukua hatua mara moja ya kusajili silaha zote
zinazomilikiwa kwa sasa ili kutambua upya vigezo na uhalali wa wamiliki
wake kwa kuwa vitendo vya kibabe na uhalifu wa kutumia silaha,
vimekithiri mitaani.
“Siku
hizi ni jambo la kawaida kumkuta mtoto wa kiongozi akitishia watu baa
au kwenye maeneo ya starehe pamoja na mitaani na silaha yake,” alisema. Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP)
alisema iko haja kwa Serikali kufanya uchunguzi dhidi ya wamiliki
silaha wakiwemo wawekezaji, kwani kumekuwepo matukio ya kupigwa hovyo
risasi hewani na kutishiana kwa silaha ili tu kuonyeshana ubabe.
HABARILEO
Viongozi wa Afrika wametakiwa kubuni mikakati itakayowawezesha wananchi wote kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa wakati wa mjadala wa Kumbukumbu za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
zilizohifadhiwa kwenye chumba maalumu kilichopewa jina la Kavazi ndani
ya ukumbi wa Costech katika Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Alisema viongozi wa Afrika hawana budi
kubuni miradi inayotoa fursa kwa wananchi wote kushiriki moja kwa moja
katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo kama ilivyokuwa wakati wa
siasa ya ujamaa na kujitegemea hapa Tanzania.
Alieleza kuwa njia mojawapo ya
kufanikisha azma hiyo ni kuwamilikisha ardhi wananchi na kuwawezesha
kuitumia kama rasilimali ya kuzalisha chakula cha kutosha na ziada kwa
ajili ya shughuli za kibiashara.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment