Uchambuzi huu wa magazeti umeletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi kwa wanaorisiti. Kituo kiko na walimu waliobobea katika fani mbalimbali. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB na kinaendelea kusajili wanafunzi kidato cha nne kujiandaa na mitihani ya Taifa, simu 0715 772746

NIPASHE
Serikali mkoani Kilimanjaro, imetoa saa
48 kwa maofisa watendaji kata, vijiji na mitaa, kufanya zoezi maalum la
uhakiki wa wageni, wanaodaiwa kutumia mwavuli wa dini kuendesha biashara
haramu ya wizi wa watoto.
Agizo hilo limekuja siku chache baada ya
kugundulika mahali walipofichwa watoto 29, wanaodaiwa kupotea kwenye
mazingira ya kutatanisha katika mikoa 13 nchini na kuhifadhiwa kwenye
makazi hayo kinyume cha sheria za nchi.
Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama
alisema unalenga kusaidia kupunguza hofu na hasira ya umma kuhusiana na
usalama wa watoto hao; na mahali wanakopelekwa baada ya kupatiwa
mafunzo maalum ya kujihami pamoja na elimu ya dini.
“Nimeagiza
ndani ya saa 48, kila mtendaji kwenye ngazi za vijiji, mitaa na kata,
wawe wamewatambua watu wote na kuwasilisha taarifa za siri kwa wakuu wa
wilaya zao. Baada ya zoezi hilo nitatoa taarifa rasmi kwa umma, Jumanne
ya wiki ijayo kuhusu hali ya usalama katika mkoa wetu,” Gama.
Watoto walio okolewa hadi sasa, baada ya
kugunduliwa kwa matukio hayo ni wenye umri wa miaka miwili hadi 16,
ambao walikutwa wamehifadhiwa kwenye nyumba moja, iliyopo karibu na
uwanja wa Mandela, Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi, mali ya
mfanyabiashara wa nguo nchini Kenya, Abdelnasir Abdurahaman, maarufu
kama Karata (33), huku watoto wengine 11, wakiokolewa pia katika kituo
cha UMM Sakhail, kilichopo Lyamungo, Wilaya ya Hai.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali namba 280 la mwaka 2002, pamoja na kifungu cha 353 cha Sheria
ya Elimu, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002; mzazi yeyote au mlezi
atakayeshindwa kuhakikisha mwanae anapata elimu ya msingi kwa wakati
husika, atashtakiwa, kulipishwa faini au kupata adhabu ya kifungo, iwapo
atashindwa kutimiza matakwa ya sheria hiyo.
Kufuatia taharuki hiyo kuikumba mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP),
Ernest Mangu, juzi alilazimika kukutana na kutetea kwa zaidi ya saa sita
na timu ya makachero wa makao makuu ya jeshi hilo pamoja na maofisa
wake wa mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni siku tano baada ya kukamatwa kwa
wafanyabiashara wanaodaiwa kuwahifadhi watoto kutoka mikoa mbalimbali
nchini.
Alipoulizwa iwapo watoto hao, wanatokea mikoa ipi ya Tanzania; Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela,
alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watoto hao ni wakazi wa
mikoa ya Tanga, Mtwara, Mbeya, Tabora, Manyara, Arusha, Kagera, Mara,
Kilimanjaro, Dodoma na Shinyanga.
NIPASHE
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewataka wananchi wa Kigoma kuwa wavumilivu wakati akipigania haki za Watanzania hasa anapopambana na mafisadi.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana
katika Kijiji cha Nyarubanda mkoani hapa, baada ya kushindwa kwenye kesi
dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuvuliwa uanachama, Zitto aliwataka wananchi hao kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mgogoro na chama chake.
Aliwataka wananchi kutosononeka kwa kuwa yuko kwenye haki na anatetea maslahi ya watu.
Mapema wiki hii Zitto, alishindwa katika
kesi aliyofungua ya kupinga kujadiliwa na kuvuliwa uanachama na chama
chake kufuatia mgogoro kati yake na Chadema.
“Mimi
nina nia njema na watu wote, niko tayari kuwatetea na ninataka nchi hii
iendelee, ninataka kupambana kwa dhati na ufisadi kama tunavyofanya
bungeni hivi sasa, lakini tunapambana na ufisadi ndani na nje ya vyama
vya siasa na hatutaogopa tutasema ukweli daima uongo kwetu ni mwiko,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki wananchi wawe wavumilivu kwa lolote litakalo tokea na kuwaomba wamuunge mkono.
Alisema kuna watu wanaotumiwa na maadui
zake na kuwaambia suala hilo ni la muda kwani adui akishafanikisha
malengo yake au akishindwa anakaa pembeni.
“Lengo letu ni moja ni maendeleo ya mkoa
wetu, ni maendeleo ya jimbo letu na ni maendeleo ya nchi yetu bila
kujali itikadi za vyama kwa hiyo kesho (leo) nitakuwa na mkutano
nitawaelezea kwa kina zaidi nilitaka niwaaambie haya ili muelewe
msisononeke, msisikie propaganda mimi bado nawahudumia bado nawafanyia
kazi na moja ya kazi ninayofanya ni hii ya kutimiza ahadi yangu ya
kumkabidhi mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma, funguo za gari
aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajiri T 779 DCF kwa ajili ya
kituo cha afya cha Nyarubanda, alisema.
Baada ya kukabidhi gari hiyo, wananchi
walimbeba huku wakiimba “karibu mkombozi wetu, karibu rais mtarajiwa
tunakuombea maisha mema kwa Mungu ili uendelee kutuongoza.”
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Michael Mwandesi,
alimshukuru Zitto kwa kutimiza ahadi yake na kuahidi kwamba gari hiyo
itafanya kazi za kituo cha afya cha Nyarubanda na si vinginevyo.
NIPASHE
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi,
amemsimamisha kazi afisa ardhi msaidizi wa Jiji la Mwanza, Asubuhi
Otieno, kwa udanganyifu wa kubatilisha matumizi ya ardhi kinyume cha
sheria.
Alichukua hatua hiyo kufuatia tuhuma zinazomkabili afisa huyo za kusema uongo.
Alitangaza uamuzi huo katika Halmashauri
ya Jiji la Mwanza ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili ambazo
anadaiwa kuandika barua na kusainiwa na mtu mwingine na alipotakiwa
kuijibu, alijibu kwa kusoma maelezo ambayo hayapo ndani ya barua hiyo.
“Otieno
umenidanganya umesoma kitu ambacho hakijaandikwa katika barua hii,
hivyo kuanzia sasa nakuwajibisha kwa kukusimamisha kazi kwa muda kwa
sababu huna mamlaka ya kubatilisha matumizi ya ardhi kisheria,” Lukuvi.
Hata hivyo, Otieno alipopewa nafasi ya
kujieleza hakuwa na maelezo ya kuridhisha zaidi ya kuinamisha kichwa
chini kabla ya kusimamishwa kazi na kudai aliandika barua kwa niaba
lakini hakubainisha hivyo kwenye nyaraka ya awali.
Hata hivyo, Lukuvi alisema baadhi ya
maafisa wa ardhi wamekuwa wakipima viwanja na kuviuza kiholela bila
kuwashirikisha wananchi na wakati mwingine kuwalipa wamiliki wa ardhi
hiyo fidia isiyo stahiki.
Alisema sheria ya ardhi inabainisha wazi
kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kupima na kugawa kiwanja bila
kushirikisha wananchi na kutambuliwa na uongozi wa serikali ya mtaa.
“Wenyeviti
wa serikali za mitaa andaeni kitabu cha wageni ili maafisa ardhi
wanapoenda maeneo yenu, waweze kusaini na kujitambulisha wamekuja
kufanya nini,” alisema.
NIPASHE
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema iko mbioni kuifungia mitandao ya kijamii, redio na televisheni inayokiuka maadili ya Mtanzania.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungy, alisema kuwa mitandao hiyo ni pamoja na facebook, whatsapp na instagram.
Alisema hayo wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo
kutokana na kuwapo kwa watumiaji wengi wa mitandao hiyo katika kuelekea
Siku ya Mawasiliano duniani inayofanyika Machi 15, kila mwaka.
Mungy alisema kuwa Mamlaka hiyo inafanya
utafiti ili kubaini mitandao inayoongoza kwa kulalamikiwa na wateja ili
hatua zichukuliwe.
“Tangu
TCRA iwezeshe kuwa na wingi wa simu na kuwezesha kuwepo kwa mitandao
mingi ya kijamii changamoto zimeongezeka, maadili yameporomoka tofauti
na miaka ya nyuma wakati kuna redio moja tu maadili yalizingazitiwa, kwa
sasa utasikia lugha za matusi kwenye radio ikiwa ni pamoja na vipindi
visivyofuata maadili na kanuni za habari, tuna mpango wakuifungia
mitandao hiyo na vyombo vya habari visivyokidhi mahitaji,” alisema.
Alisema kuwa Mamlaka hiyo lengo lake ni
kuwezesha Watanzania kwenda na wakati na kuelewa mambo mengi kwa wakati
mmoja ikiwa ni pamoja na kupata habari ndani na nje ya nchi na kuongeza
ajira kwa Watanzania kama ilivyo kwenye makampuni ya simu.
Aliwataka wamiliki wa mitandao kufuata
maadili ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wazazi, kuwafundisha
wananchi na waumini wao kuwa na maadili ili kuondoa upotofu huo ambao
unaweza kugeuza kizazi kisichofuata maadili na wengine kukosa ajira
kutokana na kutumia mitandao vibaya.
MTANZANIA
Serikali imechukua hatua ya dharua ya
kuchangisha damu kwa hiari kutoka kwa wananchi ili kubaliana na tatizo
la upungufu wa damu katika benki ya damu.
Hayo yalibainishwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
na Mpango wa Taifa wa Damu Salama, katika mkutano na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu shughuli hiyo itakayofanyika kwa
siku tano kuanzia Machi 23, mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Michael Mhando,
alisema, mahitaji ya damu salama nchini ni chupa 400, 000 hadi 450, 000
kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa chupa 106,000 za damu kwa robo
moja ya mwaka.
Alisema hadi sasa takwimu zinaonyesha
kuwa kiasi cha chupa 19,000 za damu salama zilikusanywa kati ya Oktoba
na Desemba mwaka jana huku chupa 15,000 zikikusanywa kuanzia Januari
mwaka huu.
“Hili
ni suala la dharura na linahitaji hatua za haraka na ushirikiano
miongoni mwa wadau wa sekta ya afya na wananchi kwa ujumla. Hii
inaonyesha kuwa upo uhaba mkubwa wa damu kulinganisha na uhitaji uliopo
hasa katika vituo vikubwa mfano Muhimbili ambako zinahitajika chupa 50
hadi 60 za damu kwa siku.”
Alisema, NHIF na Mpango huo wa Damu
Salama, wameona vyema kuunga mkono juhudi za serikali katika kipindi
hicho cha uhaba mkubwa wa damu salama kwa kuendesha shughuli hiyo ya
ukusanyaji wa damu kwa hiari kutoka kwa wananchi takriban 6,000.
Aliongeza kuwa, shughuli hiyo pia
itaambatana na upimaji wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza katika mikoa
sita nchini kwa pamoja kwa siku tano tangu Machi 23 mwaka huu.
Alitaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Tabora na Mtwara.
Naye Meneja masoko na uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Rajabu Mwenda,
alisema, changamoto iliyopo ni uhujumu wa damu kwa baadhi ya wahudumu
wa afya wasiowaaminifu hospitalini hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani
na mpango huo.
Hata hivyo, alitoa wito kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi katika maeneo hayo kwa ajili ya shughuli hiyo na
damu salama itakayopatikana iweze kusambazwa nchini kuokoa maisha ya
Watanzania ambao wana uhitaji mkubwa wa damu.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba
ameunga mkono tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kupinga Katiba
Inayopendekezwa, akisema hoja zao ni za msingi kwa kuwa kuna mambo mengi
yanayopingwa na wananchi.
Kauli ya Profesa Lipumba ni mwendelezo
wa kauli tofauti zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu tamko la jukwaa
hilo, wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasiasa
kuhusu hatima ya Kura ya Maoni na muswada wa Makahama ya Kadhi.
Alhamisi iliyopita, jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT)
liliwataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kushiriki
kikamilifu katika elimu ya Kura ya Maoni, na kisha kuipigia kura ya “hapana” Katiba Inayopendekezwa.
Pia, tamko hilo lililotiwa saini na maaskofu Dk Alex Malasusa wa (CCT), Tracisius Ngalalekumtwa (TEC) na Daniel Awet
wa CPCT, lilishauri mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya
kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria
ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya
masuala hayo bila kuihusisha serikali wal
Jana gazeti hili lilimnukuu makamu mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi akisema tayari tamko hilo limeshasambazwa katika majimbo yote ya kanisa katoliki na kwa waumini wa dini nyingine.
Akizungumzia tamko hilo, Profesa Lipumba
alisema ni sahihi kuipinga Katiba hiyo kwa sababu wananchi
walilalamikia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya baada ya kubaini
kuwa mambo mengi waliyoyapendekeza yaliondolewa wakati wa Bunge Maalumu
la Katiba.
“Wananchi
walitaka kuwepo na ukomo wa wabunge wao, viongozi wasifungue akaunti nje
ya nchi na mambo mengine yote hayamo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Hoja yao (maaskofu) ni ya msingi,” Prof. Lipumba aliyeongoza wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge la Katiba na kususia mchakato huo moja kwa moja.
HABARILEO
Akiwa katika maadhimisho ya kuanza mwaka wa pili wa utume wake katika kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis, ametoa kauli kuashiria kuwa huenda asidumu katika wadhifa huo kwa muda mrefu ujao.
Alisema hayo juzi katika mahojiano ya ana kwa ana na kituo kimoja cha televisheni cha Mexico, Televisa News, baada ya kutangaza kuwa Desemba mwaka huu, Kanisa Katoliki litaadhimisha Mwaka Mtakatifu.
Mwaka huo Mtakatifu utaanzia Desemba 8, mwaka huu na kuisha Novemba 20, mwakani.
Inaelezwa kuwa kuzinduliwa kwa Mwaka
Mtakatifu au Jubilee, kunaendana na maadhimisho ya 50 ya kufungwa kwa
Baraza la Pili la Vatican, ambalo hukusanya maaskofu ambao huzungumzia
mambo ya baadae ya kanisa.
Kwa kawaida Mwaka Mtakatifu huadhimishwa
kila baada ya miaka 25. Ukomo wake Katika tamko hilo, Baba Mtakatifu
Francis mwenye umri wa miaka 78, ameweka wazi kuwa hataadhimisha miaka
mingine mitakatifu katika siku zijazo.
“Nina
hisia kwamba utume wangu utakuwa wa muda mfupi, kama miaka minne au
mitano; sijui inaweza hata kuwa miwili au mitatu lakini miaka miwili
imeshapita,” alitabiri katika mahojiano hayo.
Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi kama atafuata nyayo za mtangulizi wake, Baba Mtakatifu mstaafu Benedict XVI,
ambaye ameweka historia ya kuwa Baba Mtakatifu wa kwanza kustaafu
katika miaka 600 iliyopita, baada ya kuchukua hatua hiyo mwaka 2013.
Alipoulizwa swali mahususi kama atafuata nyazo za Baba Mtakatifu mstaafu, Benedict XVI, alijibu; “Huenda Benedict XVI akabakia kuwa Baba Mtakatifu mstaafu pekee kwa miaka mingi ijayo, na huenda akapata mwenzake,” na kuongeza kuwa Baba Mtakatifu mstaafu “ameonesha njia.
” Hii si
mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francis kuzungumzia ukomo wake, kwa
kuwa amewahi kusema kustaafu kwa Baba Mtakatifu Benedict XVI mwaka 2013,
kusichukuliwe kuwa tukio la pekee.
Pia, alisema hakuchukia kuteuliwa kuwa
Baba Mtakatifu, lakini aliweka wazi kwamba katika wadhifa huo, amejikuta
akipoteza uhuru wake.
“Natamani tena kuwa na uwezo wa kutoka
nje siku moja bila mtu yeyote kunifuatilia na kunitambua nikajinunulie
mahitaji yangu,” alisema na kutabasamu. Lengo la mahojiano hayo na kituo
hicho cha Televisa News, lilikuwa kujadili maisha yake ikiwemo
mawasiliano yake na baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakimwandikia barua
kumshirikisha katika huzuni zao na kupata ushauri wake.
MWANANACHI
Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyuo vikuu nchini kuwaandaa vijana kuwa wahadhiri badala ya kutegemea wastaafu.
Kikwete alisema hayo juzi usiku, katika harambee ya kuchangia fedha Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini (Tudarco) iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam ambapo Sh 1.6bilioni zilipatikana.
Alisema kuwa vijana zaidi wanahitajika
kutoa elimu katika vyuo vikuu nchini ili kupunguza uhaba mkubwa wa
wataalamu wa kada hiyo.
“Ajirini wahadhiri wenye damu changa,
tusiwategemee wastaafu peke yao kuwa katika kada hii. Utegemezi wa
wahadhiri wastaafu liwe jambo la mpito tu katika vyuo vyenye sifa,” Kikwete.
Hata hivyo, ushauri huo wa Rais Kikwete wa
kutaka vyuo viajiri vijana zaidi umepokewa kwa hisia tofauti na baadhi
ya wahadhiri. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ProF. Jamidu Katima,
alisema suala hilo lina sura mbili kwani wahadhiri wazee wamefanya
mengi kama tafiti, machapisho na wamekaa muda mrefu katika taaluma
tofauti na wahadhiri vijana.
“Upande
wa pili ni kweli kuwa, ingawa wahadhiri wazee wamefanya mengi, wahadhiri
vijana nao wanahitajika ili kuziba mianya ya uhaba iliyopo,” Prof. Katima.
Alisema wakati mwingine vyuo huona gharama kubwa kusomesha vijana, badala yake huwatumia wahadhiri ambao tayari wamestaafu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema ingawa wahadhiri vijana ni wazuri, ni wachache hapa nchini.
“Serikali
iwekeze katika kuwasomesha maprofesa, ni gharama lakini ni vizuri kwa
sababu kuna uhaba mkubwa wa vijana katika kada hii,” Dk Malya.
Alisema ni vigumu kuwapata wahadhiri vijana
wenye shahada za uzamivu (PhD) na hata hao wenye shahada moja ni
wachache wenye alama nzuri zinazohitajika katika kufundisha.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment