Thursday, March 19, 2015

HADITHI SEHEMU YA (3)


 
NILIJUA NIMEUA (3)
 
ILIPOISHIA
 
Kwa kutaka kumshitua  mimi nikamuuliza.
 
“Simu gani?”
 
“Jamani nilisahau simu yangu kwenye siti. Simu yenyewe niliinunua juzi tu shilingi laki tatu”
 
Nilipoona amehamanika nilimwambia.
 
“Hebu angalia kwenye siti uliyokuwa umekaa”
 
Akasogea  mlango wa nyuma na kuchungulia kwenye dirisha.
 
“Si ile pale!” akasema huku akifungua mlango.
 
Aliingia ndani ya teksi akaichukua ile simu na kutoka.
 
“Asante kaka. Kumbe ulikuwa unanitania!”
 
Sote tukacheka. Huzuni ilikuwa imeshamtoka.
 
“Wewe ni muaminifu sana. Nitakuwa nachukua teksi yako kila siku” akaniambia.
 
“Kwaheri, nakwenda zangu” nikamuaga.
 
“Ulikuwa umeniletea simu yangu. Asante sana kaka, endelea kuwa na moyo huo huo”
 
SASA ENDELEA
 
“Asante bibie”
 
Wakati natia gea niondoe gari sauti yake ikanisitisha.
 
“Nipe namba yako. Nitakuhitaji tena siku nyingine”
 
Nikamtajia namba yangu.
 
Akaijaza kwenye simu yake.
 
“Na mimi nipe yako” nikamwambia.
 
“Ngoja nikupigie. Unaitwa nani?”.
 
“Majombi Teksi”
 
Jina hilo likamchekesha. Alipolijaza kwenye simu akanipigia. Simu yangu iliita. Nikaishika na kuitazama.
 
“Hii ndio namba yako”
 
“Ndiyo hiyo”
 
“Unaitwa nani?”
 
“Mariam” akatamka haraka.
 
Nikahifadhi ile namba pamoja na jina lake kwenye simu yangu. Nilipomaliza nikamwambia “Sawa”
 
Nikaiondoa teksi.
 
Huo ukawa mwanzo wa kujuana na Mariam.
 
Kutoka siku ile akawa ananipigia simmu mara kwa mara kuniita sehemu kwa ajili ya kuhitaji huduma ya teksi yangu. Kulikuwa na siku ambayo alinipigia simu saa tisa usiku. Nilikuwa nimesharudi nyumbani na nilikuwa nimelala. Nikaamka na kuangalia simu iliyokuwa inaita. Nikaona ni yeye aliyekuwa akinipigia. Nikashituka na kujiuliza kwanini alikuwa ananipigia simu usiku ule, alikuwa wapi na alikuwa na nini?
 
“Hallo Mariam …vipi?” nikamuuliza baada ya kupokea simu yake.
 
Nilikuwa nimekereka kukatishwa usingizi wangu lakini nilivumilia.
 
“Majombi uko wapi?”  Sauti ya Mariam ikauliza.
 
“Niko nyumbani” nikajibu.
 
“Ninakuhitaji hapa Habours Club”
 
Habours ilikuwa klabu ya starehe ambayo ilikuwa ikitumiwa kwa maonesho ya miziki hasa miziki ya taarab.
 
“Unataka nikufuate hapo Habours Club?”  nikamuuliza.
 
“Ndiyo”
 
“Nikupeleke wapi?”
 
“Nyumbani”
 
“Ulikuwa kwenye mziki?”
 
“Ndiyo”
 
ITAENDELEA KESHO na usiache kupitia blog hii kwa mengi mazuri na inakupatia habari na matukio ya papo kwa papo na endelea kuperuz www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment